Mmoja wa wasanii mjini Iringa akikabidhiwa cheti cha kuhitimu mafunzo na Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba
ILIONEKANA kama masikhara, wengi waliwabeza, hata rafiki zao waliona
kuwa walichokuwa wakikifanya ulikuwa ni upuuzi mtupu. Hatimaye siku zikaanza
kujongea taratibu, mara wiki, mbili, hadi ukatimia mwezi tangu waanze kuchukua
mafunzo yaliyobeba dhana nzima ya kujitambua, kujifunza misingi ya uigizaji,
uandishi, uongozaji na utayarishaji wa filamu.
Mafunzo haya ya mwezi mmoja
yaliandaliwa na Taasisi Isiyo ya Kiserikali ya Tanganyika Center for Development
and Advocacy (TCDA) ya mjini Iringa na kufadhiliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Fredrick Mwakalebela. Taasisi hii ni
matokeo ya vijana wawili waliomaliza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika fani
tofauti na kukumbana na changamoto za ajira baada ya kurudi mtaani. Moja ya
malengo ya Taasisi hii ni kuwaelimisha vijana umuhimu wa kujiajiri kwa kutumia
fursa zilizopo.
Walianza kwa kuwakusanya
vijana kutoka kwenye vikundi vya sanaa vilivyoonekana kama
ni vya vijana waliokosa kazi ambao hukutana katika kumbi mbalimbali kufanya
mazoezi kidogo na kupiga porojo pasipo manufaa yoyote.
Wasanii wa Iringa
walipopata taarifa njema kuhusu ujio wa mafunzo hayo, waliamua kuchangamkia
fursa hiyo, japo wengi waliwabeza.
Ilionekana kama ni vijana
wenye ndoto za alinacha, wanaotaraji makubwa wakati uwezo huo hawana, lakini
mwisho wake, waliocheka sasa wanatamani fursa kama
hiyo iwashukie wao pia. Hatimaye mafunzo yalifungwa na Rais wa Shirikisho la
Filamu Tanzania (TAFF) kwa kutoa vyeti maalum vinavyotambuliwa na Shirikisho hilo .
Vijana na wasanii hawa wa
Iringa ni kama walishaliona tatizo kubwa katika filamu zetu la kukosa watu
wenye weledi nchini wasio na mafunzo ya msingi (nitty-gritty) ya namna ya kutengeneza au kuongoza kazi zao
katika kiwango kinachokubalika ambacho kinaweza kuwasaidia kuzifanya sinema zao
angalau zifikie kiwango chenye kuridhisha, tangu wakati huo wakaanza kuonesha
nia thabiti ya kuhitaji mafunzo miongoni mwao ili waweze kujikosoa wenyewe
kabla ya kukosolewa na wengine.
Mafunzo haya yaliendeshwa
na vijana wawili wanataaluma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , na Shule Kuu ya Uandishi wa
Habari na Mawasiliano (IJMC). Baada ya kumaliza mafunzo hayo, vijana hawa sasa
wanahitaji mafunzo ya kina zaidi katika fani mbalimbali zikiwemo uandishi wa
miongozo ya filamu, uongozaji, utayarishaji wa filamu, uigizaji na fani
zingine. Na wanasema kuwa wako tayari kulipia gharama za mafunzo hayo.
Ndiyo maana ninasema kuwa
vijana hawa wa Iringa wanapaswa kuigwa na wadau wote wanaopenda maendeleo ya
sanaa. Wanapaswa kuungwa mkono kwani kumekuwepo changamoto kubwa ya kubezwa,
kutelekezwa, kutoungwa mkono na watu waliopaswa kuwasapoti. Kiukweli kwa sisi
wenye kupenda maendeleo ya sanaa, vijana hawa wanatia moyo sana na wanaweza kuifikisha mbali tasnia hii
ya filamu.
Inaaminika kuwa kukosekana
kwa mafunzo na kutojielewa ni sababu kubwa ya filamu zetu kuwa ni kitu
kisichozingatia au kuhitaji taaluma yoyote. Wengi wamekuwa wanalipua kazi na
wanafanya mambo bila kuzingatia utaalam kwa kuwa tu hawajitambui. Wanafanya
mambo ili mradi wanajua watauza na kupata pesa, basi. Hali hii imekuwa
ikiwakatisha tamaa hata wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika tasnia hii.
Pia kukosa mafunzo
kumewafanya walio wengi kujawa na ubinafsi (kwa kuwa hawajiamini) ambao umekuwa
ni sababu kuu ya kuufanya uwanja wa filamu wa Tanzania kuwa ni sehemu
inayoongoza kwa kutokuwa na mgawanyo wa majukumu. Si ajabu kuona mkurugenzi wa
kampuni ya kutengeneza filamu, ndiye aliyeandika skripti, ndiye muongozaji
mkuu, ndiye muigizaji mkuu na kadhalika! Na mwisho wa siku hawapendi
kukosolewa.
Siku za karibuni nilikuwa
na kikao na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Prof. Elisante ole Gabriel, aliyetuita viongozi wa Shirikisho la
Filamu Tanzania
ili tujadili changamoto zilizopo zinazopaswa kufanyiwa kazi.
Niliiomba Serikali kuwa,
kama kweli wamedhamiria kutusaidia basi wanapaswa kuanzisha mpango maalum wa
mafunzo kwa wasanii na watendaji wengine wakiwemo waandishi wa miongozo,
waongozaji, wapiga picha, wahariri na wengineo kama uliopo nchini Afrika Kusini
kupitia taasisi yao ya National Film
and Video Foundation (NFVF), mpango unaoweza kuwasaidia wajasiriamali
katika tasnia ya filamu nchini kutengeneza kazi nzuri zitakazokidhi ubora wa
soko letu na hata nje ya mipaka yetu.
Kwa mpango huu wa wasanii
wa Iringa kuamua kuchangamkia mafunzo wakishirikiana na Taasisi ya TCDA
itasaidia sana kuwaongezea ufahamu na
kujitambua, kitendo ninachoamini kitapunguza matatizo ya filamu zetu ambazo si
ajabu kumuona mwigizaji akiigiza analia lakini uso wake umebeba tabasamu la
chati kama ambavyo msomaji mmoja aliwahi
kuniomba nitoe ufafanuzi. Au yale matukio ya utekaji nyara katika filamu huku
mtekwaji akionesha dalili zote za kukaa tayari kwa kutekwa!
Kwa kuwa nilibahatika
kukutana na wasanii hawa siku ya kuhitimu kwao, niliombwa niseme nao maneno
machache kama usia wangu kwao, nami
niliwaeleza wazi kuwa wasivunjike moyo kwani jambo waliloamua kulifanya lina
changamoto zake, wasitarajie njia ya mkato kuwafikisha kwenye mafanikio bali
wanahitaji kufanya maamuzi magumu kwenye baadhi ya mambo ili kufikia mafanikio.
Niliwapa moyo kuwa
wasijione wanyonge kwa kukosa elimu ya darasani, kwani kuna njia nyingi za
kupata mafunzo ikiwemo njia waliyoitumia wao, ambayo naamini kama
watayazingatia waliyofundishwa yatawasaidia mno katika kazi zao. Kukosa elimu
ya darasani si mwisho wa kujifundisha, kwani hata Hollywood kuna waigizaji na
waongozaji ambao hawakupata elimu rasmi katika vyuo vya filamu lakini wameweza
kuwa waongozaji wazuri na wanaoheshimika sana
duniani.
Waongozaji hao ni pamoja
na; Steven Soderbergh, Robert Rodriguez, Quentin Tarantino, Richard Linklater,
Spike Jonze...
Kwa njia kama hizi nakubaliana
na mwalimu wangu, Dk. Urassa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule ya Biashara
(UDBS) kuwa ili ufanikiwe unahitaji kupitia kipindi kigumu chenye changamoto.
Mwalimu huyu aliwahi kunisimulia kisa cha ndege tai (the story of the eagle).
Tai ni ndege anayeishi
maisha marefu kuliko ndege wengine wa aina yake. Lakini ili kufikia umri huo
anatakiwa kuchukua maamuzi magumu. Ana uwezo wa kuishi hadi miaka 70. Kwa
kawaida akifikia umri wa miaka 40 makucha yake hurefuka na kupinda na hivyo
hayawezi tena kunyakuwa au kubeba chakula. Mdomo wake huota gamba gumu na
kupinda, mabawa yake huota manyoya mengi na kuwa mazito, hunasia kwenye kifua
chake na kumpa ugumu wa kuruka. Sasa anapofikia hatua hii huwa ana njia mbili
za kufanya; asubiri kufa au afanye maamuzi magumu kwa kupitia kipindi kigumu
chenye mateso kwa siku 150.
Kipindi hiki hukitumia
kwenda milimani na kukaa kwenye kiota chake, hapo hugonga mdomo wake kwenye
miamba au kitu kigumu hadi gamba lililoota litoke. Baada ya kutoka tai husubiri
hadi gamba jipya liote kisha ataanza mchakato wa kuhakikisha anagonga magamba
yaliyoota kwenye kucha zake hadi yatoke, baada ya kucha mpya kuota ataanza
mchakato wa kuhakikisha anapiga mbawa zake kwenye miti na miamba hadi manyoya
ya uzeeni yapukutike.
Miezi mitano baada ya
kupita kipindi hiki kigumu tai huwa amezaliwa upya na huwa ana nafasi ya kuishi
miaka mingine 30. kisa hiki kinatufundisha kuwa ili kufanikiwa tunapaswa kuwa
tayari kwa mabadiliko, mabadiliko ambayo hayaji kirahisi kama tunavyotarajia.
Tunahitaji wakati mwingine kuachana na mambo ya kufanya kazi “kibongobongo”,
tuachane na kufanya kazi kwa mazoea na kuchangamkia fursa zilizopo.
Wasanii wa Iringa kama
watakuwa na uelewa wa kina wa jinsi sinema inavyotengenezwa, kuwa na ubunifu
mkubwa (creative vision),
ufahamu wa namna ya kuandika miongozo ya filamu na kujitoa kwa dhati (commitment) katika kufanikisha kazi
nzima huku wakikubali kupitia kipindi kigumu cha mabadiliko ya kweli, naamini
watafanikiwa mno.
Ni matumaini yangu kuwa
wasanii hawa wa Iringa waliohudhuria mafunzo haya ya mwezi mzima watakuwa
wamepata msingi mzuri sana na kuwa mfano mzuri kwa wale waliokuwa wakiwabeza au
ambao hawakupata fursa kama hii muhimu popote nchini, na ninaamini kuwa
wataendeleza yale mazuri waliyofundishwa na wakufunzi wao.
Sitegemei kuwaona wakirudia
makosa yaleyele hata baada ya kupata ufahamu kuhusu utayarishaji wa filamu.
Alamsiki...
No comments:
Post a Comment