Wasanii wakifuatilia jambo kwenye moja ya vikao
MAJUZI nilijikuta nipo
kwenye kikao kimoja cha wadau waliojiita wenye uchungu na tasnia ya filamu
nchini, nilikuwepo hapo si kama mchangiaji bali kama msikilizaji wakati baadhi ya wadau hao walipokuwa wakijadili kuhusu mfumo
unaofaa kwa ajili ya kusambaza na kuuza filamu zetu. Katika kikao hicho ambacho
naamini hakikuwa rasmi bali kilichokuja baada ya mjadala mrefu ulioibuliwa
kuhusu makato ya kodi ya asilimia tano wanayodai kukatwa na msambazaji wa
filamu kwa kisingizio kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeagiza kukwatwa
kwa kodi hiyo.
Kikao hiki kimekuja siku
mojua tu baada ya mkutano mkubwa wa wadau wa filamu na muziki uliofanywa na TRA
ukizihusisha pia taasisi zingine kama Bodi ya Filamu,
Baraza la Sanaa la Taifa, Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki Tanzania , Shirikisho la Muziki Tanzania na Shirikisho la Filamu Tanzania . Mamlaka ya Mapato nchini walitola ufafanuzi kuwa
asilimia tano haikupaswa kukatwa kwenye bidhaa kama ambavyo watayarishaji hawa wa filamu wamekuwa wakikatwa, bali kusudio lake ni kukatwa kwa ajili ya huduma.
Baada ya kupewa ufafanuzi
huo ndipo lilipoibuka kundi la wadau linalotaka kumfikisha kwenye vyombo vya
sheria msambazaji huyo mwenye tabia ya kuwakata asilimia tano ili arudishe pesa
zote alizokuwa akiwakata, na pia wadau hao walikuwa wakijadili kuhusu mfumo
mzuri unaoweza kuwasaidia katika kusambaza kazi zao, hasa baada ya kuonekana
wakitishiwa kunyimwa mikataba ya kusambaziwa filamu kwa kisingizio kuwa
msambazaji huyo anapata hasara kutokana na uharamia wa kazi za sanaa kukithiri.
Ndipo wadau hao
walipojaribu kuja na wazo la kufikiria kusambaza kazi zao wenyewe kwani
kuendelea kuwategemea wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia ambao kiukweli
wamekuwa wakiwanyonya imeonekana ni sawa na kutegemea jua lichomozee magharibi.
Japo sikuwa nimealikwa
kwenye kikao hicho, lakini niliomba kutoa maoni yangu yaliyojikita kwenye kujaribu
kuzitazama fursa za masoko ya filamu zetu si ndani ya nchi tu bali hata nje ya
nchi. Kwani watayarishaji wengi wa filamu nchini wamekuwa wakiliangalia soko
moja tu, linalomilikiwa na wafanyabiashara hao wenye asili ya Kiasia, na
kushindwa kuziangalia fursa zingine.
Siku za hivi karibuni
uzalishaji kwa kutumia kazi za sanaa nchini, hususani filamu umekuwa
ukichukuliwa kama kimbilio kwa wasiojiweza au walioshindwa katika
fani zingine kama njia ya kujikwamua kiuchumi na kuendeleza
utamaduni. Jambo hili limekuwa likisababisha kuwa na watendaji wasio na taaluma
na hatimaye kuzalishwa kwa kazi mbovu zisizokidhi viwango.
Niliwakumbusha wadau hao wa
filamu kuwa hata pale tunapojadili kuhusu mfumo wa usambazaji wa filamu zetu
tujaribu pia kujikita katika kuangalia ni fursa zipi za masoko ya filamu nje ya
nchi. Lakini nikatoa angalizo kuwa kazi mbovu haziwezi kuuzika hata kama tutaandaa mfumo mzuri kiasi gani.
Kuboresha mfumo wa
usambazaji tunahitaji pia kuboresha kazi zetu sambamba na kubadili mtazamo/
dhana iliyojengeka miongoni mwetu kuwa sanaa ya filamu ni kimbilio la
wasiojiweza kiuchumi. Tunapaswa kutambua kuwa sanaa hii ni kazi kama kazi
zingine ambayo inahitaji ubunifu, akili, maarifa na ni muhimu katika kuinua
pato la mtu husika na taifa kwa ujumla kwani inatoa fursa mbalimbali kama vile:
Ajira na kuendeleza biashara ndani na nje ya nchi na kukuza pato la taifa kwa
ujumla.
Hali ya uzalishaji wa
filamu nchini umekuwa ukiongezeka siku hadi siku na kuwavutia wengi ingawa bado
kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia hii. Pamoja na umuhimu mkubwa
uliopo wa kazi za filamu, bado soko la bidhaa za filamu za Kitanzania
limeendelea kuwa duni/ dogo kwa walio wengi katika soko la ndani kiasi cha
kutokuwa na tija ya kuongeza kipato cha wasanii na watayarishaji wa filamu, na
hata maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Hata hivyo, kuna changamoto
mbalimbali zinazosababisha soko la ndani kwa bidhaa za sanaa, hususani filamu
kuwa duni na kusababisha wanaojihusisha na kazi hizo kuendelea kuwa na kipato
duni kinachodidimiza maendeleo binafsi na jamii kwa ujumla. Miongoni mwa
changamoto hizo ni kama zifuatazo: kukosa fursa za kupata mikopo kwenye
asasi za kifedha, kukosa sera zinazosimama katika misingi ya utendaji, kukosa
elimu, ubinafsi na kutokuwa na malengo.
Ukosefu wa fursa za kupata
mikopo kwenye asasi za kifedha pia ni tatizo kubwa mno, kwa kweli serikali
inapaswa kuyasaidia mashirikisho ya sanaa ili kuinua ubora wa kazi za sanaa na
kufikia malengo katika suala la masoko na usambazaji maana ndipo lilipo tatizo.
Wazalishaji wa filamu na wasambazaji wa ndani wapewe nafasi ya kuomba ufadhili
kutoka kwenye taasisi ya serikali kama misaada au
mikopo kwa ajili ya soko na kutangaza bidhaa.
Serikali
inapaswa kusaidia juhudi za wasanii katika masoko na usambazaji kwa ajili ya
filamu ambazo ni kwa maslahi kwa watazamaji wa Tanzania . Iwekwe maanani kuwa watakaotuma
maombi wawezeshwe ili kuzitangaza kazi za Tanzania kwenye matamasha ya filamu ya
kimataifa na masoko ya filamu na watazamaji wa ndani walio katika maeneo ambayo
uwezo wa vyombo vya habari kupenya ni mdogo.
Wakisaidiwa naamini
wataboresha kazi zao kwani filamu nyingi zimekuwa hazina ubora unaohitajika na
watumiaji wa bidhaa hizo. Wazalishaji wengi wamekuwa hawaangalii watumiaji
wanahitahi nini, bali wamekuwa wakizalisha filamu na kupeleka sokoni bila
kujali ubora wa bidhaa yenyewe. Hii inasababisha filamu kukosa soko la
kimataifa kwa sababu wazalishaji hawafanyi tafiti za masoko na kujua ni bidhaa
ya ubora gani ipelekwe sokoni kwa wateja waliokusudiwa (targeted market).
Wazalishaji wengi
wameshindwa kuongeza ubunifu zaidi na badala yake wameendelea kuzalisha vitu kwa
kuiga. Ubunifu unasaidia kumtofautisha mzalishaji mmoja na mwingine, hivyo
inamfanya mzalishaji kuwa wa pekee katika soko na kuwafanya watumiaji wa bidhaa
kuwa tayari kupokea bidhaa za kipekee kutoka kwa mzalishaji hivyo kumsaidia
kuwa mshindani katika soko.
Siku zote nimekuwa
nikiamini kuwa mafanikio ya filamu yoyote nzuri hutegemea ubunifu katika masoko
na promosheni. Sote tunapaswa kuangalia ni namna gani tunaweza kupata msaada
watengenezaji filamu na wasambazaji waweze kutangaza bidhaa zao kwa ufanisi
kwenye masoko ya filamu na hata matamasha.
Kuwe na taasisi za fedha
zinazotoa mikopo yenye masharti nafuu hasa riba nafuu, na kusiwe na mlolongo
mrefu katika suala zima la kutoa mkopo ili kumrahisishia mzalishaji kufanya
kazi kwa haraka kutokana na muda na soko kwa ujumla kwani mahitaji ya soko
yanabadilika mara kwa mara na kwa haraka sana. Pia hii itasaidia kuzalisha kwa
wingi na kutumia vifaa bora vya uzalishaji.
Katika uhamasishaji wa soko
la ndani, kuwe na juhudi endelevu ya kuhamasisha Watanzania kuwa wazalendo na
kununua kazi halisi (original) za Tanzania . Hiyo itasaidia kuinua soko la ndani
litakalomsaidia mzalishaji wa kazi za sanaa kupata kipato cha kutosha
kitakachomuwezesha kuzalisha bidhaa nyingi na zenye ubora zitakazomsaidia kuwa
na uwezo wa kuuza hata katika soko la nje na kuifanya Tanzania itambulike kwa uzalishaji wa bidhaa bora kimataifa.
Kabla sijaanza kuandika
makala hii nilifanya utafiti mdogo kwenye baadhi ya taasisi za fedha ili
kujiridhisha, ambapo nimegundua mambo kadhaa na nadhani tunapaswa kuyatatua
kwanza kabla hatujakimbilia kuyalalamikia mabenki kwamba hayatukopeshi.
Inaeleweka kuwa hakuna
ambaye anaweza kuwekeza pesa zake mahala ambapo hana data sahihi japo anasikia
ama anaamini kuwa anaweza kufanya biashara inayolipa. Katika utafiti wangu
nilikutana na maswali ambayo benki yoyote ingehitaji kupata majibu yake kabla
haijajitumbukiza katika kusaidia sekta ya filamu nchini:
• Tasnia ya filamu nchini ina thamani kiasi gani kwa sasa?
• Je, gharama kiasi gani inatosha kuzalisha filamu nzuri?
• Je, nini wastani wa mauzo ya kila mwaka ya uzalishaji wa filamu?
• Je, makampuni ya filamu katika sekta ya filamu yana dhamana gani kwa ajili ya kupata mikopo?
• Je, hesabu za makampuni ya filamu katika tasnia ya filamu zinafanyiwa ukaguzi?
• Je, makampuni ya filamu katika tasnia yana miundo rasmi?
Pia mabenki kwa kawaida hayawezi kuwa na uhusiano wa kibenki na makampuni au wasaniikama hawatakuwa rasmi na wanaotambulika kisheria. Sekta
ya filamu Tanzania inapaswa kuboreshwa zaidi, na kuanza kudumisha
kumbukumbu sahihi na akaunti, kushiriki huduma ya wakaguzi na kuwa na miundo
rasmi ya shirika.
• Tasnia ya filamu nchini ina thamani kiasi gani kwa sasa?
• Je, gharama kiasi gani inatosha kuzalisha filamu nzuri?
• Je, nini wastani wa mauzo ya kila mwaka ya uzalishaji wa filamu?
• Je, makampuni ya filamu katika sekta ya filamu yana dhamana gani kwa ajili ya kupata mikopo?
• Je, hesabu za makampuni ya filamu katika tasnia ya filamu zinafanyiwa ukaguzi?
• Je, makampuni ya filamu katika tasnia yana miundo rasmi?
Pia mabenki kwa kawaida hayawezi kuwa na uhusiano wa kibenki na makampuni au wasanii
Mambo haya yanaweza
kutusaidia katika:
• Kujifunza kuhusu mienendo ya sekta ya filamu;
• Kuwatambua watu wanaoendesha sekta ya filamu,
• Kupewa mikopo kwa urahisi katika mfumo wa mikopo kwa sekta ya filamu;
• Kupewa huduma za ushauri wa kifedha na kadhalika.
• Kujifunza kuhusu mienendo ya sekta ya filamu;
• Kuwatambua watu wanaoendesha sekta ya filamu,
• Kupewa mikopo kwa urahisi katika mfumo wa mikopo kwa sekta ya filamu;
• Kupewa huduma za ushauri wa kifedha na kadhalika.
Naomba kuwasilisha.
No comments:
Post a Comment