- Watayarishaji wa filamu nchini hawana bajeti ya
muziki
- Wengi huokoteza miziki isiyoendana na maudhui
Kwenye nchi zingine wanamuziki kama hawa (John Kitime), wenye ubunifu huwa wanatumika kunogesha filamu kutokana na midundo ya muziki
WIKI hii nilitembelea ofisi
ya watayarishaji wa filamu nchini, John Lister na Paul Mtendah, kwa lengo la
kuwajulia hali, niliwakuta wakikamilisha uhariri wa sinema inayotazamiwa kutoka
hivi karibuni ya ‘Mke Mchafu’, iliyotokana na mwongozo (script) niliouandika. Nikiri
tu kuwa pamoja na kuandika script hiyo, lakini nilijikuta nikiangalia sinema
ambayo ni kama vile sikuwahi kuiona hadithi
yake kutokana na jinsi sauti na miziki iliyotumika kwenye filamu hiyo jinsi
ilivyoleta radha tofauti.
Ingawa nilikuwa na haraka,
nilijikuta navutiwa sana kuiangalia sinema
kutokana na miziki iliyotumika kwenye sinema hiyo kuendana sana na matukio ya sinema na kukoleza mshawasha
wangu wa kutaka kuiangalia hadi mwisho. Niliwadadisi watayarishaji hao kama
miziki hiyo ilikuwa imetungwa maalum kwa ajili ya filamu hiyo au imetokea kama ajali (accidentally) tu.
John Lister alinieleza kuwa
ilitengenezwa maalum kwa ajili ya sinema hiyo kwani amegundua kuwa muziki, hasa
unaoandaliwa maalum kwa kufuata kisa cha filamu huipa filamu yako uzito mkubwa
na kuwavutia watazamaji wako waendelee kuifuatilia hadithi hata kama itakuwa na mapungufu fulani. Kwa kiasi kikubwa mno
nakubaliana na John Lister.
Mimi ni mtazamaji mzuri sana wa sinema, huwa
napenda zaidi sinema zenye hadithi za mikasa au sinema za matukio yanayoduwaza
(suspense movies). Miaka kadhaa iliyopita nilikuwa nikijiuliza kwanini ninapoangalia
sinema hasa za Kihindi zikiwa na maandishi yenye tafsiri (subtitle) za
Kiingereza zenye kuniwezesha kufahamu kinachoongewa, nikiondoa sauti, hasa
muziki, hujikuta hisia zangu zinatoweka kabisa kwenye sinema hizo? Na kwanini
nikiacha sauti isikike hata kama hakuna
‘subtitle’ huwa nakuwa sehemu ya sinema hiyo japo kinachoongelewa sikijui?
Siku zilivyokuwa zikisonga
ndipo nilipofahamu umuhimu wa muziki kwenye filamu. Ukitaka kujua umuhimu wa
muziki kwenye filamu hebu jaribu kuiangalia filamu ukiwa umeminya/umetoa sauti. Unaweza
kuacha ‘subtitle’ zisomeke kama nilivyokuwa
nikifanya ili kujua kinachoendelea, bila shaka utajikuta hisia zote zinatoweka. Mfano
mzuri ni kwenye sinema za kutisha. Ondoa muziki, hata mashaka (suspense)
pia hutoweka!
Matumizi ya muziki ni
muhimu sana
katika filamu yoyote. Muziki unaweza kuwa laini wakuvutia na kusikika kwa
sauti ya chini wakati wa tukio la kimapenzi (romantic scene) kuwafanya wanawake
kutokwa machozi, unaweza kuwa wa sauti kubwa, wenye kuashiria tukio la kutisha,
unaotumika kuhamasisha fikra za mtazamaji katika njia zote – muziki ni muhimu
katika kuweka mazingira fulani (mood) ambayo yatakufanya uzame wakati ukiiangalia
sinema, na kukufanya ujikute ukizama kwenye hisia zaidi kuliko kama isingekuwa
na muziki.
Muziki ni sehemu ya
kichocheo. Muziki hukupa mtazamo wenye mbawa za kuruka hadi mbinguni.
Amini usiamini, muziki huleta tofauti kubwa katika sinema. Muziki hufanya kazi
kama mtengeneza hali ‘mood setter’.
Kwa sinema fulanifulani, muziki hutengeneza mtiririko wa filamu, kwa sinema zingine, muziki upo hapo ili kuwaweka watu katika tahadhari, kutegemeana na hadithi, kwa mfano; matukio ya haraka na ya ghadhabu, msuko wa hadithi unapokosa sifa yoyote ya ukweli, lakini tempo inakuwepo, ikisaidiwa na muziki. Kwa walioziona filamu kama Gladiator,
Hivyo, nadhani kuwa baadhi ya sinema zinahitaji
Muziki hukufanya kuweka kipaumbele
kwenye sinema unayoitazama badala ya kufikiria mambo mengine. Pia inakuwezesha
kujua jambo zuri linaloelekea kutokea na jambo baya linalotokea. Kitu
kingine muziki unachoweza kufanya ni kukufanya ufikiri kuna kitu kibaya kinaendelea
wakati ukweli si hivyo. Hii hukusaidia kuiweka akili yako ililenge moja
kwa moja kwenye sinema (kukuteka katika ulimwngu wa sinema). Muziki pia hukupumzisha
wakati unaangalia sinema.
Hata katika maisha, muziki una
jukumu muhimu sana
na ushawishi mkubwa katika maisha yetu tofauti na jamii kwa ujumla. Kila
mtu anahusiana kwa namna tofauti na muziki, lakini bado humuathiri kila mtu kwa
namna anavyofikiri. Muziki hutumika kwa zaidi ya kusikiliza tu au
madhumuni ya kuburudika, unaweza kukubadilisha katika maamuzi yako, unaweza kukupunguzia
msongo au kukushawishi, hubadili namna mtu anavyoweza kutambua mambo, hutumika kukirihisha,
kutesa na mengine mengi zaidi.
Kuna ushahidi ulio wazi
kwamba muziki una jukumu muhimu katika maisha yetu, lakini jambo la kujiuliza; kwanini
watayarishaji wengi wa sinema wa Tanzania hawana bajeti kwa ajili ya
muziki, au hawadhani kuwa wanauhitaji? Nimekuwa nikishuhudia watayarishaji wetu
wa filamu kuokoteza nyimbo zisizoendana na maudhui na kuzitumia kwenye sinema
zao jambo linalopunguza utamu wa sinema. Ndiyo maana ni jambo la kawaida
kuwakuta watu wakizilalamikia sinema zetu kuwa ‘zinaboa’ mno kuzitazama.
Watayarishaji hawa wa
filamu wanasahau kuwa hata kama tukio la sinema limejengwa vizuri sana na ukawatumia waigizaji wazuri bado kama
hakuna muziki sinema yako itapungukiwa kitu muhimu, muziki huongeza radha ya
tukio. Lakini pia isidhaniwe kuwa nasema muziki ni muhimu katika kila tukio
kwenye filamu. La hasha.
Ni wazi, kuna mifano mingi ya
jinsi ukosekanaji wa muziki unavyoweza kufanya matukio kuwa makubwa zaidi na kuduwaza. Hata
hivyo, ukosefu wa muziki katika filamu nzima unaweza kusababisha kuwepo haja ya
kutafuta kitu cha ziada; kitu cha kuusaidia ujumbe na kuibeba script zaidi
kuliko uigizaji wenyewe.
Muziki unapochukuliwakama kitu kisicho muhimu
au jambo dogo, pia hupunguza soko lako na humsababishia mtengenezaji wa filamu
kukosa fursa kubwa ambayo ingeweza kuifanya filamu yake kutambulika zaidi. Uzoefu
unaonesha kuwa muziki ni moja ya zana muhimu sana kimasoko mtu anaweza kuitumia katika
sekta yoyote. Mtayarishaji wa filamu anapaswa kuweka bajeti kwa ajili ya muziki
kila atengenezapo sinema, ambapo asilimia 10 ya bajeti nzima inapaswa kuwa ya
muziki na sauti zingine maalum.
Muziki unapochukuliwa
Kumbuka, unaweza kuwa na
hadithi nzuri mno na waigizaji wazuri sana , waongozaji,
watayarishaji, wahariri, vikorombwezo muhimu (special effects), nk, lakini kama nakshi ya muziki imekosekana kwenye filamu, basi itaishusha
filamu yako hadi ‘levo’ ya chini, ambayo inaweza kupunguza mafanikio ya filamu
sokoni.
Hapa kuna tofauti kubwa kati ya mtu anayechukua/anayeokoteza vipande vya muziki kutoka maktaba na yule anayemlipa mtunzi ili atunge nyimbo maalum kwa ajili ya sinema fulani, utunzi wa nyimbo huzidisha msukumo kwenye filamu yako, lakini muziki wa maktaba ni kwa kipande cha jina tu (title), lakini huwa tofauti kabisa na mwelekeo wa hadithi yako. Muziki unapotungwa maalum kwa filamu yako, hutengeneza uhusika mwingine zaidi; pamoja na husika zilizotangulia huunda kitu kimoja kilicho kamili. lakini muziki wa kuokoteza siku zote hauna uhusiano wowote na hadithi iliyotumika kwenye filamu.
Ni jukumu la waongozaji wa filamu kuhakikisha wanateka hisia za watazamaji wao. Wana wajibu wa kuhakikisha kunakuwa na watunzi wa muziki wenye ubunifu kwa ajili ya kubuni muziki utakaoongeza radha tofauti katika filamu. Muziki unaweza kutoa tafsiri ya wahusika, kuihamisha hadithi yako kutoka point A kwenda point B, kujenga mazingira ya mvutano (tension), kukoreza uhondo katika mchezo, na kuungisha pamoja dhamira (themes) ambazo humuacha mtazamaji katika hisia kamili zaidi.
Hapa kuna tofauti kubwa kati ya mtu anayechukua/anayeokoteza vipande vya muziki kutoka maktaba na yule anayemlipa mtunzi ili atunge nyimbo maalum kwa ajili ya sinema fulani, utunzi wa nyimbo huzidisha msukumo kwenye filamu yako, lakini muziki wa maktaba ni kwa kipande cha jina tu (title), lakini huwa tofauti kabisa na mwelekeo wa hadithi yako. Muziki unapotungwa maalum kwa filamu yako, hutengeneza uhusika mwingine zaidi; pamoja na husika zilizotangulia huunda kitu kimoja kilicho kamili. lakini muziki wa kuokoteza siku zote hauna uhusiano wowote na hadithi iliyotumika kwenye filamu.
Ni jukumu la waongozaji wa filamu kuhakikisha wanateka hisia za watazamaji wao. Wana wajibu wa kuhakikisha kunakuwa na watunzi wa muziki wenye ubunifu kwa ajili ya kubuni muziki utakaoongeza radha tofauti katika filamu. Muziki unaweza kutoa tafsiri ya wahusika, kuihamisha hadithi yako kutoka point A kwenda point B, kujenga mazingira ya mvutano (tension), kukoreza uhondo katika mchezo, na kuungisha pamoja dhamira (themes) ambazo humuacha mtazamaji katika hisia kamili zaidi.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment