·
Tuzipitie
upya sheria zetu za Hakimiliki
Maofisa wa Cosoza wakiteketeza CD na Mikanda ya wizi katika uwanda wa Kikungwi, Wilaya ya Kusini Unguja
“MWANAHARAKATI,
kwanza kabisa nakushukuru sana kwa makala yako
wiki hii, pili nakubaliana kabisa na wewe kuhusu ulichoandika kuhusu ‘matumizi
ya muziki ni muhimu sana
kwenye filamu zetu’. Ukweli ni kwamba suala la wasanii wetu kupenda kutumia
nyimbo ambazo wala hawajaomba ruhusa kuzitumia ni jambo baya sana . Huu ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za
Hakimiliki, haina tofauti na ambavyo wao wamekuwa wakilalamika kuibiwa kazi
zao, kwani hata wao ni wezi wa kazi za wengine.
Hebu
fikiria, msanii wa Tanzania
ametengeneza filamu ya Kitanzania kwa ajili ya Watanzania lakini anatumia
nyimbo za West Life, P square, Music Scrol ya Jumong na nyingine kibao za
kudownload ili kunogesha filamu yake, halafu kesho anakuwa wa kwanza kulalamika
eti anaibiwa kazi yake! Ukimgusa kutaka kumweleza ukweli utashushuliwa na kuambiwa
unajifanya mjuaji sana .
Nakushukuru wewe uliyejitoa kimasomaso kuwaeleza ukweli wasanii, maana sisi
wengine imebidi tukae kimya tu”.
Huu ujumbe
ni moja ya nyingine nyingi kutoka kwa wasomaji wa makala zangu, walizoandika
ama kunipongeza au kuongezea katika kile nilichoandika kuhusiana na makala ya
wiki iliyopita. Baadhi ya wasomaji kama huyu hawakusita
kunikumbusha kuhusu suala la ukiukwaji wa sheria za Hakimiliki kwa wasanii wetu.
Msomaji
mmoja aliniambia kuwa ni vema nikaandika kuwakumbusha wasanii wote kuwa wanatakiwa
kujua haki zao zilizoorodheshwa na Sheria ya Hakimiliki na kwamba pale
wanaposhindwa kuzitambua kwa sababu za utaalam wa kisheria, ni bora wakatafuta
wataalam katika eneo hilo
wakawasaidia.
Nakubaliana
kabisa na msomaji huyu, ingawa nadhani suala hili linapaswa kwenda mbali zaidi
na si kuishia kwa wasanii tu, bali lifike hadi upande wa jamii. Ni vizuri
tukaelewa nini thamani ya kazi za wasanii wetu ili siku moja tusiingie matatani
kwa kughushi au kukutwa na kazi ambazo zinavunja hakimilki na hakishiriki za
wasanii wetu na watunzi kutoka pande yoyote ile katika ulimwengu huu wa sayansi
na teknolojia.
Kuwepo kwa sheria za Hakimiliki kuna madhumuni mengi, moja
kubwa ni kuhakikisha kulinda ubunifu wa mtu ili wengine wapate hamasa ya
kutunga/kuandaa kazi mpya badala ya kuendelea kuibiana au kunakiliana, na hivyo
ubunifu kutokusonga mbele. Siku zote penye wizi wa kazi za ubunifu hakuna
ubunifu wala kusonga mbele. Sheria za Hakimiliki humsukuma mtu kukwepa kunakili
au kutumia kazi ya mtu na kutumia ubongo wake kuandaa kazi mpya au kuboresha ya
mwingine kiasi cha kupata kazi bora zaidi.
Lakini katika nchi yetu, wasanii wetu wengi wamekuwa maarufu
kutokana na filamu zisizo na hadithi zao, za wizi na kunakili kutoka kwa wenzao
nje ya nchi, hasa Nigeria , Ghana na India . Na kwa kuwa wameanza kazi
kwa misingi ya wizi huwa hawawezi kufika mbali kwani pale wanapotakiwa kufanya
muendelezo wa kazi zao hushindwa kwa kuwa si wabunifu. Na hata walio wabunifu
wa kweli, watakuwa wamekatishwa tamaa na kuacha kubuni vitu vipya baada ya
kugundua kuwa kazi zao zinaibiwa kirahisi bila kuweko na hatua zozote za maana
zinazoweza kuchukuliwa.
Asilimia kubwa ya filamu zetu zimekuwa zikilalamikiwa kuwa ni
za kukopi na kupesti (copy and paste) kutoka nje, ingawa hata wasanii wetu pia
wanalalamika kuwa kazi zao zinaibiwa. Bahati mbaya sana
jamii yetu imekuwa na tabia ya kukumbatia wahalifu na hata kuwapa sifa na
heshima kwa uhalifu wao, mifano ipo, ambapo wahalifu wanatokea kuwa watu
maarufu katika magazeti na mitandao ya jamii, jambo linalokatisha tamaa sana wale ambao wanataka
kufanya kazi halali.
Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa sheria namba saba ya mwaka 1999, kuna makundi
makubwa mawili ya Haki za Wasanii zinazolindwa na sheria hii, ambazo ni Haki ya
Kiuchumi na Haki za Kitamaduni ambazo mtunzi wa kazi zinazolindwa na sheria hii
ana haki nazo. Lakini pia kuna sehemu inayolinda sheria
za Haki za Maadili. Wakati tukivunja sheria za Haki za Kiuchumi, pia tumekuwa tukivunja
Haki za Maadili za mtunzi mwingine kwa kuiba kisa/hadithi na kutumia kwenye
filamu zetu na kujifanya ni cha kwetu, au kupachika sehemu ya nyimbo kwenye
filamu bila idhini ya mhusika, jambo ambalo ni kosa kubwa kisheria.
Hata
hivyo, haki za kiuchumi na haki za kitamaduni za mtunzi au mmiliki wa kazi ya sanaa
zina mipaka yake kwa mujibu wa sheria hii chini ya kifungu cha 9 na 11 cha sheria
imetoa wakati ambapo mtunzi wa kazi ya sanaa inayolindwa na sheria hii hatakuwa
na mamlaka ya kukataza matumizi ya kazi yake pale itakapotumiwa na mtu
mwingine. Hali hii kisheria inaitwa matumizi yasio ya kibiashara, ikiwa mtu
mwingine zaidi ya mmiliki akiitumia kazi kwa ajili ya kielimu/kitaaluma,
kufanya marejeo, hatahitaji kupata idhini ya mmiliki ili kufanya hivyo.
Lakini pia
tumekuwa na changamoto kubwa kwenye sekta ya filamu nchini kuhusu umiliki wa filamu
kutokana na mazingira ya soko letu yalivyo, ambapo wasanii hulazimika kuuza
haki zao zote, kisha wakajisahau kama wao si
wamiliki tena wa kazi hizo, jambo ambalo limekuwa linaleta kilio kwa wasanii
wetu wengi.
Sasa nirudi kwenye mada, wiki hii nimekusudia kuliangazia
jambo la Mamlaka zinazohusika kusimamia kazi zetu zinapokamata kazi za wizi na
kuziteketeza. Mwishoni mwa wiki iliyopita, Ofisi ya Msajili wa Hakimiliki Zanzibar (Cosoza), ilikamata na kuteketeza CD
na Mikanda ya Video, ambazo ni kazi za sanaa. Kazi ya uchomaji wa kazi hizo za
kiharamia (piracy) ilitekelezwa huku Maofisa wa Idara ya Mazingira na Misitu
wakifuatilia uchomaji huo wa Mikanda ya filamu iliyokamatwa na Ofisi ya Msajili
wa Hakimiliki Zanzibar kutoka kwa wafanyabiashara kadhaa wanaorudufu kazi hizo
bila idhini, hivyo, kuiba umiliki wa miziki na filamu hizo kwa kuuza nakala za
wizi (pirated copies) bila ya ruhusa ya wamiliki wa kazi hizo.
Zoezi hilo la uchomaji wa kazi
hizo limefanyika katika uwanda wa Kikungwi, Wilaya ya Kasuni Unguja mnamo
Jumamosi asubuhi, chini ya uangalizi wa Maofisa wa Cosoza na jeshi la Polisi
Zanzibar.
Kuteketezwa kwa kazi
za wizi za sanaa ni jambo zuri, lakini tunapaswa kuangalia pia na upande wa
pili wa shilingi ili kuona mapungufu makubwa yaliyopo na kuyafanyia kazi, kwani
pamoja na kuteketeza kazi hizo lakini msanii aliyeibiwa kazi yake amekuwa anasahaulika
kwa kuwa mara zote hafidiwi, na hivyo kumkatisha tamaa na kusababisha asiweze
kuzidisha ubunifu zaidi.
Kama nilivyotangulia
kuandika kuwa kuna Haki za Kiuchumi, tabia za uhalifu kama wizi wa kazi za sanaa husababisha kupotea kwa haki za
kiuchumi na nyinginezo, na jamii inapaswa kukemea kwa nguvu zote bila kujali
sifa binafsi za mhalifu.
Pia bado
sheria zetu za Hakimiliki zimekuwa zinatoa mwanya mkubwa kwa wahalifu kukiuka
sheria na kuwa na jeuri ya kuchukua kazi ya msanii yeyote na kuirudufu, kisha
kuiuza mtaani bila woga wowote. Hapa Tanzania ,
baada ya Sheria ya Hakimiliki ya mwaka 1966 kuthibitika kuwa ina mapungufu
mengi, ndipo mwaka 1999 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipotunga Sheria Mpya ya Hakimiliki
na Hakishiriki, namba saba ya mwaka 1999, ambayo ni sura ya 218 ya Sheria za Tanzania (kama
zilivyorekebishwa mwaka 2002). Lengo la Sheria hii ni kutengeneza na kutoa
manufaa zaidi na ulinzi zaidi wa kazi za wasanii wa kazi zinazolindwa na
hakimiliki na hakishiriki na zingine zote zinazoendana na hizo.
Haki hizi
zina msingi katika mkataba wa kimataifa wa Benne wa mwaka 1883 ambao uliridhiwa
na Tanzania tarehe 25 Julai 1994, na hivyo kwa mujibu wa kanuni za sheria za
kimataifa, Tanzania ina wajibu wa kutimiza yaliyomo katika mkataba huu
iliyouridhia.
Uvunjaji
wa hakimiliki umegawanywa katika makundi makuu mawili: kundi ambalo uvunjaji
wake ni wa msingi (primary), yaani mtu anayevunja hakimiliki au hakimiliki ya
mtunzi kwa kunakili, kutengeneza upya au kuionesha kazi hiyo katika hadhara
bila idhini ya mmiliki halali.
Kundi la
pili la uvunjaji wa kiwango cha pili (secondary), ikiwa kama
mtu anayevunja hakimiliki kwa kuitumia kibiashara kazi ya mmiliki halali bila
idhini yake. Hii ni pamoja na kurudufu kazi hiyo bila idhini, kuisamba au kuuza,
ama kutatoa njia za kusaidia hakimiliki kuvunjwa kwa mfano kutoa vifaa vya kurudufia
kazi za sanaa bila idhini ya mmiliki halali.
Tunapaswa
tuzitazame upya sheria zetu za hakimiliki ili zilete ufanisi kwa pande zote,
kwani sekta ya burudani ni chanzo kikubwa cha ajira na inaweza kuchangia pato
kubwa kwenye pato la Taifa, na pengine inaweza kufanya vizuri zaidi endapo itapewa
kipaumbele, kwa kuwa sekta ya tatu kwa ukubwa, baada ya ile ya utalii na madini.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment