Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Dk. Fenella Mukangara
Dk. Fenella Mukangara
Niliwahi kuandika makala hii kuhusu kutumia filamu kuhamasisha uzalendo, nalazimika kuirudia kutokana na sababu fulanifulani ingawa ikiwa imeboreshwa zaidi.
Mwaka huu tarehe 9 mwezi
Disemba tunatimiza miaka 52 tangu tuwe huru, huku tukishuhudia jamii ya
Kitanzania ikizidi kupoteza maadili, mila na tamaduni zake kila kukicha. Baada ya
uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana iliundwa
mwaka 1962, rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alitamka wazi
kuwa Utamaduni ndiyo kiini na roho ya Taifa, na nchi inayokosa utamaduni wake
ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa
taifa kamili.
Miaka hii hamsini na mbili ya
uhuru tunazidi kushuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili huku sekta ya filamu (na
hata muziki) ikiwa haina sera inayoiongoza wala sheria jambo linalotafsiriwa kama kutelekezwa japo serikali inadai imeirasimisha kwa
maana ya kuanza kukusanya kodi kupitia kazi za filamu na muziki. Tasnia hii
imesheheni utajiri mkubwa ambao kama
itaangaliwa kwa jicho tatu itaweza kuliingizia taifa hili mapato makubwa.
Sekta hii ni kubwa kuliko
tunavyodhani, ikipewa umuhimu unaostahili, inaweza kuwa sekta ya tatu kwa
ukubwa baada ya madini na utalii. Lakini kinachoshuhudiwa kwa miaka ya hivi karibuni
ni nguvu kubwa inayotumiwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
kutafuta vazi linaloitwa la taifa utadhani ndiyo suluhisho na mmomonyoko huu wa
maadili na kupotea kwa tamaduni zetu!
Mwanzoni nilidhani kuwa
Sera ya Utamaduni iliyozinduliwa Agosti 23, 1997 mjini Dodoma , ambayo ilikuwa ni hatua ya pili
muhimu baada ya ile ya kwanza ya kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na
Vijana mwaka 1962, ingekuwa jibu la matatizo ya sanaa hapa nchini ikiwemo sekta
ya filamu, kumbe sivyo. Wizara inayosimamia utamaduni ipo lakini hatuoni mipango
yoyote ya kimaendeleo ambayo imekuwa ikibuniwa au kutekelezwa ili kujenga moyo
wa uzalendo kwa jamii. Utamaduni umekuwa haupewi dhima katika uamuzi na
mipango ya maendeleo kwa sababu inadhaniwa kuwa maendeleo ni kuondokana na mambo
ya kiasili pasipo kuchunguza misingi ya mambo hayo na faida zake.
Hili la Serikali kutoipa
umuhimu tasnia ya sanaa/utamaduni ndiyo sababu ya uchafu na tatizo la maadili tunalolishuhudia
katika filamu na nyimbo zetu, kwani kumekosekana uthibiti wa kazi chafu. kwa miaka
ya karibuni wizara imekuwa katika mchakato wa kutafuta vazi ambalo wanaamini
kuwa ndilo suluhisho la maendeleo ya nchi na uzalendo kwa vijana. Na sijui vazi
hilo limeishia
wapi kwa sasa, maana imekuwa kimya!
Kwa kutafuta vazi
linaloitwa la taifa wizara inaamini kuwa ndilo suluhisho la mmomonyoko na kukosekana
kwa maadili katika jamii na kazi za sanaa(filamu na nyimbo zetu).
Kwa nini tunakosa alama ya
mfano wa filamu zetu? Hivi tutaendelea kujidanganya hadi lini kuwa alama ya
filamu zetu ni Kiswahili kinachozungumzwa wakati lugha hii inazungumzwa pia
katika nchi zingine kama Kenya ,
Rwanda ,
Kongo na kwingineko? Na bahati mbaya sana
ni kwamba majina tunayotumia kwenye filamu zetu ni ya Kizungu!
Kwa nyakati tofauti pia nimewahi kuwasikia viongozi wa serikali wakilalamikia kuhusu maadili katika filamu hizi. Kila kukicha ni filamu za mapenzi peke yake zinazotawala kwenye tasnia yetu au hadithi zisizo na asili yetu tulizonakili kwa wenzetu zenye vitendo na maudhui ya jamii za nje. Kwa nini Wizara haijawahi kufikiria kuwa na muongozo (Sera) utakaosaidia kutafuta tiba ili watayarishaji wa filamu na wasambazaji wabanwe kutumia visa vyetu wenyewe na aina ya mavazi yetu hadi tuige kutoka kwa wenzetu?
Kwa kweli haya ni maswali muhimu
na inabidi kila mdau aliye kwenye tasnia ya filamu na sanaa kwa ujumla anapaswa
ajiulize. Tusipokuwa makini tutajikuta
tukipita njia potofu na kukipoteza kizazi chetu kwa kuwa njia tunayoenda nayo
sasa katika filamu zetu ni ile iliyojengwa juu ya msingi wa wimbi la utandawazi
inayoakisi utamaduni wa Kimagharibi. Hata tukisisitizwa kuvaa hiyo nguo
inayotafutwa sasa bado haitatusaidia lolote.
Tutake tusitake, ukweli ni
kwamba fani yetu ya filamu kwa sasa ipo katika hatari kubwa ya kuporomosha
mfumo mzima wa maadili katika jamii zetu kwani watayarishaji na wasanii walio
wengi katika tasnia hii wameshapotea njia kwa kutofuata au kutoijua miiko na
maadili katika hadithi wanazoandaa, mitindo na maudhui ya hadithi yanaonekana
dhahiri kupotosha kulingana na asili yetu, mila, desturi, mapokeo, historia na
urithi tulioachiwa na waliotutangulia.
Kwa hali hii ya serikali
kutoizingatia sekta hii na kukosa udhibiti wa sanaa huku ikituacha tujifanyie
tunavyodhani inatufaa ni ishara ya hatari inayoashiria mporomoka si kwa fani
hii tu bali kwa jamii nzima ya Tanzania .
Hata tukilazimishana kuvaa hilo vazi
linalotafutwa sasa bado haitatusaidia kama
hatutaangalia mambo haya kwa mapana yake. Je, kama ni kweli hatua zipi
zichukuliwe ili kunusuru au kudhibiti tatizo hili?
Ninachoamini ni kuwa sanaa
ya filamu ni zao la matokeo ya juhudi za mtayarishaji, watendaji wengine katika
kazi ya filamu na wasanii katika kutoa ujumbe, kukidhi matumizi na mahitaji ya
binadamu na hii kama tanzu muhimu ya utamaduni
si kitu kilichoibuka tu.
Hivyo jambo muhimu na la
msingi hapa ni kwa Serikali na wadau wote kuzingatia, kuzitambua na kuzilinda
sanaa zetu ili zisipoteze uasili wake pamoja na wimbi la mabadiliko ya wakati
na mazingira ya sasa ya utandawazi na biashara huria. Sanaa ya filamu ni kazi
ya ubunifu yenye ufundi na mvuto, inapaswa kutopoteza ubunifu, uasili na kukosa
mbinu bora ya uwasilishwaji wa ujumbe kwa hadhira.
Wizara ingeliangalia sana suala hili la
mzalishaji wa filamu anayeumiza kichwa kutafuta mtaji na kuandaa bajeti ya
filamu - uandaaji hadi kukamilika - lakini bado hana sauti wala nguvu sokoni,
hili ndilo linalochochea mmomonyoko huu wa maadili, kwa kuwa mtayarishaji anatengeneza
filamu kwa matakwa ya msambazaji ambaye yeye anaangalia soko tu.
Mtayarishaji wa filamu
nchini huwa anafanya kazi kwa shinikizo la woga wa soko! Hana uhakika wa soko lake na
endapo atakuwa jeuri basi kuna hatari ya filamu yake kutosambazwa, hivyo
kinachobaki kwake ni kuweka mikono nyuma awapo mbele ya msambazaji ili filamu
yake isambazwe!
Kwa hali hii maadili
yanazidi kupotea kwa kuwa mnunuzi wa mwisho bado hujikuta anafuata mkumbo wa
nguvu ya msambazaji bila kujali ubora filamu, kuanzia kwa mtunzi wa hadithi,
muigizaji, muongozaji, mazingira na taaluma ya filamu yote! Ananunua filamu kwa
mazoea ya majina na hadithi!
Hadi sasa filamu nyingi za
Kitanzania au michezo ya kuigiza katika runinga ni vitu vilivyopoteza mwelekeo
kwani leo hii inafuata mifumo na mtiririko wa kigeni zaidi kama filamu za Nigeria ,
Philippine na kwingineko. Yote hii inasababishwa na wavamizi kwenye fani hii
waliodhani kuwa mtu akikosa kazi ya kufanya basi kimbilio lake ni
kwenye sanaa hasa filamu. Hapa ndipo wizara ingeunda kamati ya kushughulikia
mambo haya kwa kuwa athari zake ni kubwa kuliko kukosa vazi linaloitwa la
taifa.
Matokeo yake tumejikuta
tukiwa na idadi kubwa ya watayarishaji filamu, waandishi wa miswada, waongozaji
filamu na waigizaji bandia wasio na misingi wala kanuni za fani husika jambo
linalosababisha kazi zetu kuwa sawa na Big G inayoisha utamu kwa muda mfupi, huku
watu wenye taaluma na misingi wakitupwa nje ya soko kwa kuwa sanaa siku hizi
imekuwa ni biashara isiyozingatia na kufuata maadili ya Taifa.
Alamsiki…
No comments:
Post a Comment