Inye, moja ya sinema zilizoonja makali ya kudhibitiwa na Bodi ya Ukaguzi wa Filamu nchini
MAKALA ya wiki iliyopita iliyoonesha kupinga waziwazi uwepo wa Bodi ya sasa
ya Ukaguzi wa Filamu kwa kuwa imerithi sheria za kibaguzi za mkoloni
(censorship laws) zilizotumika kukagua sinema na kuondoa baadhi ya vipande
visivyotakiwa kutazamwa na Waafrika, imepokelewa kwa mitazamo tofauti sana na wasomaji wangu
wengi. Wapo ambao walibainisha kuwa hawajaelewa namaanisha nini hasa na wengine
wameonesha kutofautiana nami kabisa katika jambo hili.
Kauli ya: “…Lakini kwa mazingira ya sasa, sisi wote ni Watanzania, tunaujua
utamaduni wetu na tunafanya sinema za Kitanzania kwa ajili ya Watanzania,
kwanini tuwe na chombo cha kutukagua, kutupangia na kutueleza kipi ni cha
Kitanzania na kipi si cha Kitanzania?” imeonekana kutumiwa na wasomaji wangu kama
reference ya kupinga vikali kuwa nataka wasanii waachiwe kufanya watakavyo bila
kudhibitiwa jambo linaloweza kuzidisha mmomonyoko wa maadili kwenye jamii.
Lakini pia wapo wengi
walionipongeza kwa kuliona hili, hasa katika kile nilichoandika kuwa tunahitaji
bodi huru ya filamu chini ya wadau wenyewe kama ilivyo kwa Bodi ya Madaktari,
Bodi ya Wakandarasi, Bodi ya Wahasibu na kadhalika ambazo zipo chini ya wadau
wenyewe na kusimamia masuala yao
ya kitaaluma.
Msomaji mmoja amenitumia
ujumbe kunipongeza akisema kuwa hata yeye amekuwa haelewi mantiki ya kuwa na
Bodi ya Ukaguzi wa Filamu ambayo ni kitengo kidogo kwa ajili ya ukaguzi na
udhibiti tu wa filamu ndani ya Idara ya Utamaduni, badala ya kuwa na Bodi ya
Filamu yenye ‘mandate’ kamili katika kusimamia mambo yote ya filamu nchini.
Pia ameshangaa kuwa kama kweli hatuna sera ya filamu tumekuwa tukiendesha
vipi shughuli za filamu nchini, kwa sheria zipi, kwani pasipo sera humaanisha
hata sheria pia hakuna.
Nawashukuru walioliona hilo na kuelewa
nilichomaanisha, lakini pia nawaeleza waliopingana nami kuwa nilichoandika wiki
iliyopita ndicho nilichomaanisha. Na leo nauendeleza mjadala kwa ufafanuzi
zaidi. Sitaki kuuma maneno; hatuhitaji
sheria za kutudhibiti katika filamu zetu bali kutupima. We don’t need to be
censored, we need to be rated.
Udhibiti unapaswa ufanywe kwa
vipindi vya TV, hii ni kwa sababu watoto wasikumbane na baadhi ya mambo
yaliyopaswa kuoneshwa kwa watu wazima tu: mambo kama
unyama wa wazi uliokithiri, vurugu, ngono, na mambo mengine yenye ukakasi
(profanity) ambayo yanapaswa kuzuiwa (kudhibitiwa) yasioneshwe kwenye
televisheni hasa wakati ambapo watoto huangalia TV.
Lakini kwenye filamu ni suala
tofauti kabisa. Kwenye filamu hakuna ‘censorship per se’. Filamu zinahitaji
kupimwa na kupangiwa daraja kulingana na maudhui, kwa kuwa mzazi ana ‘option’
ya kuamua kama atainunua kwa ajili ya familia
yake au la. Suala la kwamba watoto wanaangalia filamu zenye ukakasi kwenye
mabanda ya kuoneshea video si suala la mtayarishaji wa filamu, ni suala la
waliopewa dhamana kushindwa kufanya kazi zao sawaswa.
Mfumo wa upimaji filamu umewekwa
maalum kuainisha aina za filamu zinazofaa kuoneshwa kwa makundi tofauti ya watazamaji. Upimaji
huo unaweza kuitwa Uainishaji, Tathmini au Upangaji Madaraja. Upimaji na
upangaji madaraja ya sinema huwapa wazazi taarifa muhimu kuhusu maudhui ya
sinema husika, na hatimaye ni juu yao kuamua kama sinema hiyo inafaa kwa familia zao.
Ieleweke kuwa ubongo wa
mtoto mdogo ni kama kaseti tupu inayosubiri kurekodi matukio, hivyo, sinema
huumba ulimwengu mpya kwa watoto kuchunguza na kujifunza, na unaweza kuwasaidia
kwa kuhakikisha safari yao ina mtazamo chanya. Wasaidie watoto wako kuchagua
sinema za kuangalia na jadiliana nao kuhusu maudhui. Imarisha na jenga maadili
mazuri kupitia sinema kwa kukaa chini na watoto wako baada ya kuangalia na
mjadili kile walichokiona. Wakati mwingine tumia sinema kama
misaada ya kielimu na kubadilishana mawazo mapya.
Sinema zinaweza kuwafumbua
macho watoto wetu kwa maeneo mapya, utamaduni na mawazo, na wazazi wana jukumu
muhimu katika kuhakikisha kwamba wanajifunza mambo chanya yatakayowasaidia
watoto wao. Hivyo wazazi wanahitaji kuamua iwapo sinema ni nzuri kwa watoto wao
kuiangalia. Kutokana na kuelewa jinsi madaraja yanavyowekwa husaidia wazazi
kutafuta sinema sahihi kwa watoto wao.
Mfumo wa kupanga madaraja
kwa ajili ya makundi tofauti ya watazamaji ulianza kutumika Marekani mwaka
1968, kama mbadala wa Kanuni za Uzalishaji
Filamu za Hays (William Harrison Hays, Sr. aliyekuwa mkuu wa Chama cha
Watayarishaji Filamu Marekani “MPPDA”, 1922 hadi 1945). Kanuni za Uzalishaji
Filamu za Hays zilitumika tu kutoa kibali cha ama kuikubali au kuikataa filamu,
bila hata kupima maudhui ya filamu.
Kuwasilishwa kwa rufaa mara
kwa mara za filamu zenye ukakasi kulikifanya Chama cha Picha Jongevu Marekani (MPAA),
kwa kushirikiana na Chama cha Taifa cha Wamiliki wa Kumbi za Kuoneshea Sinema
(NATO) na Waagizaji na Wasambazaji wa Kimataifa wa Filamu Marekani (IFIDA),
kubuni mfumo mpya wa kuzipima na kuzipa madaraja ili kuwasaidia wazazi
kuwalinda watoto wao. Mfumo huu ulihusisha madaraja manne ingawa sasa yapo
matano.
Bodi ya Filamu ina wajumbe
wa kudumu wanane hadi 13 na ni sehemu ya Uainishaji madaraja (Classification)
na Upimaji (Rating). Hii ni Bodi Huru inayosimamiwa na wadau wenyewe (si
ya serikali), ambapo Rais wa MPAA huteua mwenyekiti wa Bodi ingawa baadaya ya
kuteua hana mamlaka yoyote juu ya maamuzi yatakayotolewa na bodi. Wajumbe wa Bodi
hutoka katika maeneo mbalimbali, lakini wenye uzoefu katika mambo ya malezi ya
watoto ili waweze kuziangalia sinema kwa mtazamo wa mzazi/mlezi. Wajumbe wa Bodi
huangalia kila filamu iliyowasilishwa kwao kwa umakini, huitathmini kwa usahihi
kila mmoja kwa nafasi yake (individually), kisha hujadiliana na kupiga kura juu
ya daraja gani filamu inapaswa kupewa.
Kisha Bodi humpa mtayarishaji
wa filamu hiyo majibu ya uamuzi wao pamoja na maelezo, endapo atayahitaji. Kama mtayarishaji hatafurahishwa na daraja iliyopata
filamu yake, anaweza kuihariri upya na kuiwasilisha tena kwenye Bodi, au
anaweza kukata rufaa juu ya uamuzi wa bodi. Katika kesi hii, Bodi ya
Rufaa, ambayo ina wataalam 14 hadi 18 wa sekta ya filamu, watasikiliza hoja za pande
zote na kupiga kura kama wanaweza kubadili
uamuzi wa Bodi. Maamuzi yanaweza tu kubadilishwa kwa theluthi mbili ya
kura.
Mchakato wa upimaji filamu
kwa kiasi kikubwa ni wa upande mmoja (subjective). Bodi hupima na kutoa
madaraja yenye alama za G, PG, PG-13, R na NC-17 kama
ilivyoainishwa:
G - "General Audience”
– Imekubalika kwa watu wote: daraja hili hutumika pale sinema inapokuwa haina
matukio yoyote ya unyama wa wazi uliokithiri, utupu, ngono au mambo mengine
yenye ukakasi. Au kama matukio ya vurugu ni machache na maudhui yanafaa
kwa watoto wadogo. Lakini daraja G halimaanishi kuwa ni filamu ya watoto.
PG - "Parental
Guidance” – Mwongozo wa Wazazi: Ni daraja linaloelezea kuwa baadhi ya picha zinaweza
zisifae kwa Watoto wadogo: Bodi hutumia daraja hili wakiamini kuwa filamu
ina maudhui ambayo pengine wazazi watapima wenyewe kama
yanafaa kwa watoto wadogo. filamu inaweza kuwa na baadhi ya vipande vyenye
lugha chafu, vurugu na kadhalika, lakini katika kiwango kidogo mno.
PG-13 "Parents
Strongly Cautioned” – Onyo kwa Wazazi kuwa baadhi ya matukio kwenye sinema si
Muafaka Kwa Watoto Chini ya Miaka 13. Daraja hili limeongezwa na MPAA mwaka
1984 kuashiria kuwa filamu ina matukio ya vurugu, lugha chafu au maudhui yasiyofaa
kwa watoto chini ya umri huu, ambapo wazazi wengi wasingependa kuyaonesha kwa
watoto wao wadogo, lakini si yenye ukakasi mkubwa kiasi cha kupewa daraja R.
R - " Restricted” – Bodi
hutumia daraja hili ambalo wajumbe wake wanaamini sinema ina matumizi makubwa
mno ya maudhui yenye ukakasi. Katika baadhi ya majimbo ya Marekani, umri wa
chini ya kuangalia sinema yenye daraja R ni miaka 18.
NC-17: "No One 17 and
Under Admitted": daraja hili asili yake ni daraja X, hutumika kwa
filamu ambazo si muafaka kabisa kwa watoto. Huonesha kuwa maudhui yake ni
ya ukakasi zaidi kuliko katika daraja R. haipaswi kuoneshwa kwa watu chini ya miaka
18.
Sasa utaona kuwa filamu bado
inatoa ‘option’ kwa wazazi na watazamaji, Bodi tuliyonayo imekuwa ikikagua na
kuzuia maonesho ya filamu za Kitanzania tu kwa kisingizio cha utamaduni wetu
lakini imekosa ‘meno’ kwenye filamu na tamthilia za nje zinazorushwa kwenye
vituo vya televisheni jambo ambalo ni hatari zaidi kwa watoto wadogo.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment