Kama wadau wa filamu tufikirie kutumia Maonesho ya Biashara ya Kimataifa kama haya ya Dar es Salaam ambayo ni njia nzuri sana katika kujitangaza kitaifa na kimataifa
INASEMWA
kuwa sekta ya filamu nchini kwa sasa imerasimishwa, jambo ambalo limekuwa
haliniingii akilini kwa kuwa sijaona mfumo wowote unaotuashiria kwamba sasa
tuko rasmi zaidi ya huu wa kulipa kodi kupitia stika za TRA. Hivi tumerasimishwa
kwa Sera ipi hasa?
Sera
ni hati muhimu inayoelezea thamani na kutokosekana kwa miongozo ya lazima na
visheni. Nimewahi kuandika kabla kuwa bila sera madhubuti ya filamu maendeleo
katika sekta hii yatabaki kuwa ndoto hata kama
viongozi wa serikali watatuahidi mambo makubwa kiasi gani. Lakini kwanini
tuendelee kuongozwa kwa matamko ya viongozi badala ya kupigania uwepo wa sheria?
Tarehe 9 na 10 mwezi huu
tulikuwa na kongamano la kitaifa la wadau wa filamu kuhusu mapendekezo ya Sera
ya Filamu itakayotuongoza katika sekta ya filamu ili tufikie mafanikio. Katika
kongamano hilo lililoandaliwa
na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) mambo mengi yalijadiliwa, lakini leo ningependa
kujikita kwenye jambo moja: Bodi ya Filamu (Tanzania Film Board).
Bodi hii ya Filamu ni tofauti
na Bodi ya
Ukaguzi wa Filamu (Tanzania Film
Censorship Board) iliyopo iliyoundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 4 ya 1976, hii ninayoikusudia ni Bodi Huru ya Filamu itakayowezeshwa
na serikali (an independent government supported board) ikiwa na idara kadhaa
zinazoshughulikia masuala ya filamu ili kupunguza mlolongo wa taratibu ambazo
zimekuwa chini ya sheria na mamlaka mbalimbali (one stop shop).
Hapa pana tofauti kubwa kati ya Bodi ya Ukaguzi wa
Filamu tuliyoizoea na Bodi ya Filamu ninayoikusudia (Independent Film Board),
tofauti hiyo ni katika muundo na majukumu yake. Bodi ya Ukaguzi wa Filamu
iliyopo ni chombo cha Serikali na ina majukumu makubwa ya kukagua na kupanga madaraja ya
filamu na michezo ya kuigiza; kukagua na kutoa vibali kwa maeneo yote
yanayotumika kwa maonesho na usambazaji wa filamu au michezo ya kuigiza;
kuafiki na kutoa vibali kwa shughuli za usambazaji wa filamu na michezo ya
kuigiza; kuafiki na kutoa vibali kwa maonesho ya filamu na michezo ya kuigiza.
Pia kuafiki, kuzuia au kudhibiti maonesho na usambazaji wa filamu na michezo ya
kuigiza.
Bodi hii ya ukaguzi imerithi sheria zilezile za kibaguzi za mkoloni (censorship
laws) zilizotumika kukagua sinema na kuondoa baadhi ya vipande visivyotakiwa
kutazamwa na Waafrika. Yaani tulikuwa tunapangiwa nini cha kutazama na nini
hatupaswi tutazame. Lakini kwa mazingira ya sasa, sisi wote ni Watanzania,
tunaujua utamaduni wetu na tunafanya sinema za Kitanzania kwa ajili ya
Watanzania, kwanini tuwe na chombo cha kutukagua, kutupangia na kutueleza kipi
ni cha Kitanzania na kipi si cha Kitanzania?
Bodi Huru ya Filamu itatusaidia
kuleta ufanisi hasa kwa kuangalia sekta za wenzetu waliofanikiwa. Bodi hii itaongozwa
na wadau wenyewe wa filamu wenye weledi ikifanya kazi kama
zifanyavyo bodi zingine za kitaaluma; mfano Bodi ya Madaktari, Bodi ya
Wakandarasi, Bodi ya Wahasibu na kadhalika ambazo zimekuwa zikiendeshwa na
wadau wenyewe na kusimamia masuala ya kitaaluma katika sekta husika. Ushahidi
nilionao ni kwamba Bodi hizi zimeleta ufanisi mkubwa kwenye sekta hizo.
Bodi ya Filamu itakayosimamiwa
na wadau wenyewe itasaidia kusimamia misingi, sheria na mazingira bora ya
kufanya biashara kwa wawekezaji wa ndani na nje, itapunguza urasimu, itawadhibiti
wadau/wasanii wasiofuata misingi na taratibu zitakazowekwa na kusaidia utambuzi
wa bidhaa hapa nchini.
Pia itasaidia uboreshaji wa
udhibiti wa mfumo wa usambazaji, italinda ubora, usalama na thamani ya kazi
zetu, itarahisisha ujumuishaji wa taarifa nyingi kwa kuwezesha kuitambua sekta,
mfumo wa uzalishaji, ubora, usalama na ufuatiliaji wa bidhaa na masoko (Traceability).
Bodi hii itakuwa na idara
kadhaa kama vile za utoaji wa taarifa za
upatikanaji wa pesa (Funding Information) na kutoa fursa kwa watengeneza
sinema. Idara ya kuandaa takwimu za kina (Data Collection) na kutoa fursa ya
kuzitangaza kazi zetu katika masoko mengine ya Afrika, na duniani na hivyo
kuongeza uwezekano wa kuuza kazi zetu kimataifa na kuigiza pesa za kigeni.
Idara zingine ni ile ya
Uhamasishaji Biashara na Masoko, Idara ya elimu na mafunzo ya weledi
(Professionalism), na Idara itakayosimamia ukusanyaji wa mapato (Revenue Collection)
yatokanayo na filamu kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato (TRA). Pia Idara itakayosimamia
kwa ukamilifu sheria za uharamia (Piracy) wa kazi za sanaa na hivyo kuwafanya
watengenezaji wa kazi hizi kutokuwa na hofu ya kupoteza mapato (Economic
Reward) yatokanayo na kazi zao, Idara itakayopanga madaraja ya filamu (Rating
of Films), Idara ya ukuzaji na utafiti (Research and Development) na Idara ya
ushauri (Consultation Agency).
Katika idara hizi, acha leo
niizungumzie Idara ya Uhamasishaji Biashara na Masoko ambayo itatusaidia kuwa
na soko imara. Pamoja na mambo mengine ipewe jukumu la kusimamia vipaumbele
vifuatavyo: kuandaa, kufuatilia na kupitia sera, sheria na programu zinazosimamia
biashara ya filamu nchini; kuwezesha upatikanaji wa masoko ya ndani, kikanda na
kimataifa kwa filamu za Tanzania; kuandaa mikakati madhubuti ya ujenzi wa
miundombinu ya masoko nchini; kuwajengea uwezo wazalishaji wa filamu ili kazi
zao zifikie viwango vya kimataifa; kuendeleza mfumo sahihi na madhubuti wa
ukusanyaji, uchambuzi, usambazaji na uhifadhi wa taarifa za masoko.
Pia kuongeza uelewa wa
wafanyabiashara juu ya fursa za masoko zilizopo ndani ya nchi, kikanda na
kimataifa ili waweze kunufaika nazo; kuchukua hatua madhubuti za kuwalinda
wazalishaji dhidi ya biashara isiyo halali hususan kutoka nje; na kuendeleza na
kujenga uwezo wa wajasiriamali katika kuibua na kutumia fursa za uzalishaji,
biashara na masoko.
Kwa msaada wa Serikali Bodi
itasaidia juhudi za wasanii katika masoko na usambazaji kwa ajili ya filamu
ambazo ni kwa maslahi ya watazamaji wa Tanzania, pia itazitangaza kazi za
Tanzania kwenye matamasha ya filamu ya kimataifa na masoko ya filamu na
watazamaji wa ndani walio katika maeneo ambayo uwezo wa vyombo vya habari
kupenya ni mdogo.
Uanzishwaji wa Bodi ya aina
hii utawezesha bidhaa zinazozalishwa nchini kutambulika kitaifa na kimataifa
katika uuzaji wake na kuwa na uwezo wa kuuza bidhaa hizo katika soko la
kimataifa.
Katika uhamasishaji wa soko
la ndani, kuwe na juhudi endelevu ya kuhamasisha Watanzania kuwa wazalendo na
kununua kazi halisi (original) za Tanzania .
Hiyo itasaidia kuinua soko la ndani litakalomsaidia mzalishaji wa filamu kupata
kipato cha kutosha kitakachomuwezesha kuzalisha sinema zenye ubora kwa soko la
nje na kuifanya Tanzania
itambulike zaidi kimataifa, tofauti na ilivyo sasa.
Ieleweke kuwa masoko ni
nyenzo muhimu katika maendeleo ya biashara. Taarifa sahihi za masoko zikitolewa
kwa wakati muafaka ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa biashara na hivyo
kuongeza mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi. Bodi hii iwe na kazi ya kubuni
na kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuleta ufanisi katika sekta ya
Masoko ili kuongeza tija katika ukuaji wa uchumi sanjari na kuondoa umasikini.
Hatua hii itawawezesha
Wajasiriamali kutumia Fursa za masoko zitolewazo na Marekani kupitia mpango wa AGOA
(African Growth Opportunity Act). Katika eneo hili, Bodi itakuwa katika nafasi
nzuri ya kutoa elimu kwa wadau kuhusu fursa za soko hilo pamoja na masharti yake na kutumia fursa
za masoko kupitia Vituo vya Biashara vilivyopo duniani.
Kupitia Vituo hivi fursa
mbalimbali zilizopo nchini zitatangazwa. Pia itasaidia uwepo wa ushindani huru
na wa haki utakaoleta ufanisi wa utendaji wa kiuchumi na kukidhi maslahi ya
walaji ambao ndiyo kitovu cha kukua kwa biashara na uchumi. KupitiaTume ya
Ushindani (FCC) na COSOTA, Bodi hii itaweza kuendesha misako katika maeneo
zinakoingilia bidhaa kama vile bandari,
Viwanja vya Ndege, Maduka na Mipakani ili kukagua uwepo wa bidhaa bandia. Aidha
Bodi itatoa elimu kwa wadau kuhusu shughuli zake na athari zinazosababishwa na
bidhaa bandia.
Pia tuangalie namna nzuri
ya kuzitumia fursa kama za Maonesho ya
Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ambayo yamekuwa ya mafanikio makubwa na
kukutanisha Wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi. Maonesho haya yamekuwa
yakiratibiwa na Tantrade na yamekuwepo kwa takribani miaka arobaini sasa. Maonesho
haya yatapanua fursa zaidi kwa wajasiriamali wa sekta ya filamu kubadilishana
uzoefu, kupeana taarifa za masoko na kuuza bidhaa zao.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment