Elizabeth Michael maaruf kwa jina la Lulu katika pozi
IJUMAA ya
wiki iliyopita nilialikwa kwenye ofisi za Bodi ya Ukaguzi wa Filamu kwa ajili
ya mazungumzo ya kiofisi, kuhusu mustakabali wa sekta ya filamu nchini, hasa
ikizingatiwa kuwa mimi ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu Tanzania, chombo
cha juu cha wadau wa filamu nchini, kinachopaswa kufanya kazi kwa ukaribu na
Bodi ya filamu.
Hapo
kwenye ofisi za Bodi, niliongea mengi na watendaji wakuu wa ofisi hiyo, chini
ya uenyekiti wa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, yaliyotufikisha katika suala
la maadili katika filamu zetu ambapo aliwataja baadhi ya wasanii wanaokiuka
maadili na hawako tayari kujikosoa hata pale wanapoelekezwa njia sahihi.
“Kwa mfano
(anamtaja jina msanii mmoja), unapomwelekeza jambo kwenye kazi zake hujifanya
kukusikiliza kwa makini lakini ukweli huwa ana-pretend tu, na akitoka hapa
huyafanya yaleyale. Lakini kuna wasanii wengine unaona kabisa wana nia ya dhati
ya kutengeneze filamu nzuri zenye maadili na hukubali makosa pale unapowakosoa.
Mfano Elizabeth Michael (Lulu), huyu ameonekana kubadilika kabisa. Tulimwita baada
ya kuikagua sinema yake ya ‘Foolish Age’, jinsi alivyotoa ushirikiano mkubwa
katika kuupokea ushauri wetu kwa kweli ameonekana kubadilika sana …”
Haya ni
baadhi ya yale tuliyojadili ambayo yalinifanya kukumbuka mjadala mmoja niliokuwa
nao na rafiki yangu mmoja raia wa nchi jirani, ambaye huwa tunakutana kwenye
mtandao wa facebook, mjadala ulihusu maadili na utengenezaji wa sinema katika
nchi zinazoendelea, na athari wanazozipata wale wanaoigiza na hata kwa jamii
nzima.
Ukweli ni
kwamba filamu ni mojawapo ya sanaa na nguzo muhimu ya Utamaduni. Filamu zimeibuka
kuanzia karne ya ishirini na baadaye kuwa kishawishi kikubwa na mawasiliano
ghali katika karne hii ya ishirini na moja. Hakuna aina nyingine ya sanaa
ambayo imesambaa kwa ufanisi na kuonekana kuvuka mipaka ya kiutamaduni katika
mataifa mengi.
Rafiki
yangu huyo alizisifu sana filamu za Tanzania na akabainisha kuwa anatuonea sana wivu kwa fursa
tuliyonayo, lakini akakiri kuwa kwa miaka ya karibuni filamu zetu zimeanza kukosa
mwelekeo, na zinatupeleka kusikojulikana. Akaniuliza kupata maoni yangu, je, ni
kwanini kila kukicha ni filamu za mapenzi tu ndizo zinazotawala kwenye soko letu?
Je, kwanini hadithi zetu nyingi si za asili yetu bali tunanakili kwa wenzetu
zenye vitendo na maudhui ya jamii za nje? Kwa nini hatutaki kutumia visa vyetu
wenyewe hadi tuige kutoka kwa wenzetu?
Maswali
hayo yakanikumbusha wakati nafanya utafiti, nilijiuliza sana maswali haya, na wakati natafuta majibu
yake yakazaliwa maswali mengine: Je, filamu zetu zilivyo leo zinaweka
kumbukumbu nzuri itakayorithiwa na vizazi vijavyo? Au kizazi chetu kinaweka
kumbukumbu potofu ya filamu na sanaa zetu na utamaduni kwa vizazi vijavyo?
Kwa kweli haya
ni maswali muhimu na inabidi kila mdau wa filamu ajiulize. Tusipokuwa
makini tutajikuta tukipita njia potofu na kukipoteza kizazi
chetu kwa kuwa njia tunayoenda nayo sasa katika filamu zetu ni ile iliyojengwa
juu ya msingi wa wimbi la utandawazi inayoakisi utamaduni wa Kimagharibi.
Kwa
tafsiri rahisi, filamu ni aina ya mawasiliano yanayotumiwa kutolea hadithi au
kuwafundisha watu kuhusiana na fikra au mitazamo mipya katika jamii kupitia video/skrini.
Wafuatiliaji wa filamu huangalia filamu ambazo zinaelezea hadithi fulani kama njia mojawapo ya kuburudika, kujifunza au kwa sababu
ya upenzi tu.
Filamu ni
njia bora ya kuongeza uelewa na kuteka umakini wa watu katika mada fulani au
suala fulani. Hata hivyo, kabla ya kuandaa filamu, kuna masuala mengi ya kimaadili
ambayo lazima yazingatiwe.
Katika
karne hii teknolojia ya televisheni na maonesho mbalimbali ya wajasiriamali
vimeitangaza sana
tasnia ya filamu kwa watu wote; watazamaji wa mijini na vijijini katika nchi
nyingi zinazoendelea. Filamu pia zimeweza kutumika kama
njia muhimu ya uchumi.
Hapa ieleweke kuwa mapokeo ya kazi za sanaa katika jamii yoyote hufuata utaratibu wa kurithisha mfumo, mtindo, muundo, maudhui na hivyo hubaki kuelezea juhudi, matatizo au mafanikio ya jamii husika.
Tutake
tusitake, ukweli ni kwamba fani yetu ya filamu kwa sasa ipo katika hatari kubwa
ya kuporomosha mfumo mzima wa maadili katika jamii zetu kwani watayarishaji na
wasanii walio wengi katika tasnia hii wameshapotea njia kwa kutofuata au
kutoijua miiko na maadili katika hadithi wanazoandaa, mitindo na maudhui ya
hadithi yanaonekana dhahiri kupotosha kulingana na asili yetu, mila, desturi,
mapokeo, historia na urithi tulioachiwa na waliotutangulia.
Maswali
haya yana majibu mbalimbali, kulingana na hali ilivyo, lakini yana utaratibu
tofauti. Yanaweka uzito tofauti wa wajibu wa watengenezaji wa filamu ambao hupenda
kuwaonesha wengine badala ya kuonesha uhusika wa uvumbuzi wao wenyewe. Masuala
haya huongeza kiwango cha kuzingatia maadili kwa maandishi ambayo si maarufu sana katika utengenezaji
wa filamu.”
Hivyo,
watengenezaji wa filamu wana wajibu wa kuwalinda waigizaji, na wanapaswa
kujitahidi kutowadhalilisha au kuwasababishia madhara. Hata hivyo, mara nyingi
kuwalinda waigizaji huleta msuguano na tamaa ya watengenezaji filamu kuandaa
filamu inayolazimisha.
Mbali na
kuzuia madhara kwa waigizaji wa filamu, watengenezaji wa filamu lazima wajitahidi
kuwa na muongozo wenye sifa za wahusika wote (character description) ili kuwafanya
waigizaji wawe na ufahamu wa jinsi watakavyowakilishwa katika filamu na jinsi
filamu itakavyotumika. "Maadili huwepo kuongoza mwenendo mzima sehemu
ambayo mambo magumu na haraka, kanuni au sheria pekee hazitoshi.
Wakati wa
kutengeneza filamu, kuna chaguzi nyingi kwa watengenezaji wa filamu. Watengenezaji
wa filamu lazima waamue kipande kipi wakijumuishe, waigizaji gani, na jinsi ya
kuwawasilisha washiriki katika filamu. Kwa hiyo, ni muhimu kwa watengenezaji wa
filamu kutambua madhara ya maamuzi yao .
Watengenezaji wa filamu wanapaswa kujitahidi kutowadhalilisha au kuwasababishia
madhara wanaowapiga picha, na wanapaswa kujitahidi kuwawasilisha katika njia
bora, au vinginevyo kuwajulisha jinsi watakavyowasilishwa. Aidha, ingawa watengenezaji
wa filamu kawaida huandaa filamu kuwakilisha maoni yao , hawapaswi kutumia sauti moja au mtazamo mmoja
tu kuiwakilisha jamii nzima.
Kinachotokea
hapa kwetu ni mtayarishaji wa filamu kufanya kazi kwa shinikizo la woga wa
soko! Hana uhakika wa soko lake
na endapo atakuwa jeuri
basi kuna hatari ya filamu yake kutosambazwa, hivyo kinachobaki kwake ni kuweka
mikono nyuma awapo mbele ya msambazaji ili filamu yake isambazwe. Na hii ni
hatari sana kwa
mustakabali wa tasnia nzima ya filamu!
Kwa hali
hii maadili yanazidi kupotea kwa kuwa mnunuzi wa mwisho bado hujikuta anafuata
mkumbo wa nguvu ya soko lililoamuliwa na msambazaji bila kujali ubora wa
filamu; kuanzia kwa mtunzi, muigizaji, muongozaji, mazingira na taaluma ya
filamu yote! Ananunua filamu kwa mazoea ya majina na hadithi!
Ndiyo
sababu filamu nyingi za Kitanzania au michezo ya kuigiza ni vitu vilivyopoteza
mwelekeo kwani leo hii zinafuata mifumo na mtiririko wa kigeni zaidi. Yote hii
inasababishwa na wavamizi kwenye fani waliodhani kuwa mtu akikosa kazi ya
kufanya basi kimbilio lake
ni kwenye sanaa hasa
filamu.
Tumejikuta
tukiwa na idadi kubwa ya watayarishaji filamu, waandishi, waongozaji na waigizaji
bandia wasio na uelewa jambo linalosababisha kazi zetu kuwa sawa na Big G
inayoisha utamu kwa muda mfupi, wakati huohuo wenye taaluma wakitupwa nje ya
soko kwa kuwa sanaa siku hizi imekuwa ni biashara isiyozingatia na kufuata
maadili ya Taifa.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment