UONGOZAJI wa filamu ni
zaidi ya kujua “standby... action... cut!” Uongozaji wa filamu ni tatizo kubwa mno
kwenye tasnia ya filamu nchini, ni tatizo kwa kuwa waongozaji wetu wa filamu hudhani
kuwa kazi ya uongozaji wa filamu ni kujua “standby... action... cut!” na
kusahau kuwa muongozaji wa filamu anapaswa kuwa mbunifu na kiungo muhimu kati
yake na timu ya uzalishaji.
Muongozaji wa filamu anawajibika
kuutafsiri muongozo wa filamu ulioandikwa kwenye karatasi na kuuhamishia katika
picha halisi na sauti kwenye skrini – na anapaswa kuiona taswira halisi na
kutafsiri mtindo na muundo wa filamu hiyo, na hivyo kufanya kazi zote mbili
kama kiongozi wa timu na msimulizi kwa kutoa picha halisi. Pia anapaswa
kuangalia mtu anayefaa kuigiza, ndiyo maana mojawapo ya majukumu ya muongozaji
ni pamoja na kufanya usaili (casting).
Wakati masuala muhimu
katika utayarishaji wa filamu, kama vile fedha
na masoko, hubakia mikononi mwa mtayarishaji wa filamu (producer), muongozaji wa
filamu anapaswa kuwa na ufahamu wa bajeti inayotumika kwenye filamu
anayoiongoza na kujua ratiba. Katika baadhi ya filamu, waongozaji huhodhi
majukumu mengi kama Muongozaji/Mtayarishaji au Muongozaji/Mwandishi, jambo
ambalo halikatazwi kama atakuwa na uwezo wa
kuyatenda kwa ufanisi.
Pia muongozaji wa filamu anapaswa
kuwa na uelewa wa kina wa jinsi sinema inavyotengenezwa, kuwa na ubunifu mkubwa
(creative vision), ufahamu wa namna ya kuandika script na kujitoa kwa dhati
(commitment) katika kufanikisha. Yeye anahusika moja kwa moja kwenye mafanikio
yoyote ya kisanii, mafanikio ya kibiashara au kushindwa kwa filamu katika soko.
Kwa maana hiyo ndiye
anayepaswa kumtengeneza mhusika kwa kutegemea muongozo wa filamu (script) unasemaje.
Kama muigizaji atashindwa kuuvaa uhalisia, hilo sio kosa la muigizaji mwenyewe bali ni
kosa la muongozaji wa filamu kwa kushindwa kuongoza vyema na hutafsiri uwezo wa
muongozaji ulipokomea.
Hivi umewahi kuona filamu (hasa
za nje) ambayo mhusika mkuu katika filamu hiyo ni mtoto mdogo, ambaye huonekana
amefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana
kuigiza na kuuvaa uhalisia kiasi kwamba unaweza kudhani hakuwa akiigiza bali
yalikuwa ni matukio halisi? Kama uliiona
sinema ya aina hii, je, umewahi kujiuliza inamaana huyu mtoto ana akili nyingi
kuwazidi waigizaji watu wazima waliopo kwetu? Au hapa tofauti ni nini hasa?
Kwa vyovyote jibu ni moja
tu; muongozaji wa filamu hiyo kafanikiwa kumtengeneza, kitu ambacho
kinakosekana kwa waongozaji wetu wa filamu wanaodhani ukijua kusema “action...
cut...” utakuwa umefuzu kuwa muongozaji wa filamu.
Ninalazimika kuyaeleza haya
niliyowahi kuyaeleza hapo nyuma baada ya matukio makubwa mawili ya kusikitisha yaliyotokea
katika tasnia hii yakiashilia kuvamiwa kwa nafasi ya uongozaji wa filamu na
watu wasiokidhi vigezo vya uongozaji wa filamu na kusababisha madhara makubwa
kwa waigizaji. Kama mwanaharakati na kiongozi
wa taasisi inayosimamia masuala ya filamu nawajibika kuyasemea.
Tukio la muigizaji Maulidi
Mfaume, maarufu kama Gado Balotel, aliyevunjika
miguu yote miwili pamoja na kuteguka nyonga baada ya kudondoka toka ghorofa ya
nne alipokuwa akiigiza filamu ya msanii mwingine aitwaye Joseph Mteme ‘Baga’
limesaababishwa na aliyekuwa muongozaji wa filamu hiyo kushindwa kumudu nafasi
ya uongozaji wa filamu.
Gado Balotel alikutwa na
balaa hilo
akiwa Location ndani ya hotel ya Con Way, Magomeni Kagera wakati akiigiza. Kuna
scene iliyomtaka mtu aigize anajirusha ghorofani, muigizaji huyu kwa maelekezo
ya muongozaji wake akaruka toka ghorofa ya nne na kutua chini (ambako hakukuwa
na kizuizi chochote cha kumlinda na madhara) kwa kufikia miguu ambapo alihisi
moto unawaka miguuni mwake huku harufu ya damu ikimtoka puani na mdomoni na
baada ya kujiangalia aliona visigino vyake vikiwa vimepasuka vyote huku tumboni
kukiwa na maumivu makali sana, kumbe wakati huo nyonga ilikuwa imeachia huku
miguu yake ikiwa imesogea tumboni.
Wasanii wenzake walimchukua
na kumkimbiza Hospitali ya Mwananyamala ambapo ilishindikana na baadaye kukimbizwa
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Tukio jingine ni la majuzi,
ambapo msanii mwingine (hadi tunakwenda mitamboni nilikuwa sijapata jina lake)
alimwagiwa mafuta ya taa mwilini na kuunguzwa moto wakati wakiwa location kwa
ajili ya upigaji picha ya sinema. Lengo lilikuwa eti kuonesha mtu anayeungua
moto kwenye filamu hiyo.
Vitendo kama hivi si tu
havipaswi kufumbiwa macho, bali vinapaswa kukemewa na kulaaniwa kwa nguvu zote,
ndiyo maana nimekuwa nikipigania uwepo wa mamlaka kamili ya Shirikisho la
Filamu nchini ili kuwadhibiti waongozaji wa aina hii. Chama cha Waongozaji wa
Filamu nchini kimekuwa kikiendesha mafunzo mara kwa mara kwa wanachama wake kuongeza
ufahamu na kujitambua kitendo kitakachopunguza matatizo kama haya, kwani kwa
sasa katika filamu zetu si ajabu kumuona mwigizaji akiigiza analia lakini uso
wake umebeba tabasamu la chati, au yale matukio ya utekaji nyara huku mtekwaji
akionesha dalili zote za kukaa tayari kwa kutekwa!
Hii inasababishwa na
waongozaji wa filamu wa aina hii waliokosa mafunzo ya msingi (nitty-gritty) ya
namna ya kuongoza kazi zao katika kiwango kinachokubalika. Kukosekana kwa
mafunzo na kutojielewa ni sababu kubwa ya filamu zetu kuwa ni kitu
kisichozingatia au kuhitaji taaluma yoyote. Watu wamekuwa wanalipua kazi na
wanafanya mambo bila kuzingatia utaalam kwa kuwa tu hawajitambui. Wanafanya
mambo ili mradi wanajua watauza na kupata pesa, basi. Hali hii imekuwa
ikiwakatisha tamaa hata wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika tasnia hii.
Pia kukosa mafunzo
kumewafanya walio wengi kujawa na ubinafsi (kwa kuwa hawajiamini) ambao umekuwa
ni sababu kuu ya kuufanya uwanja wa filamu wa Tanzania kuwa ni sehemu
inayoongoza kwa kutokuwa na mgawanyo wa majukumu. Si ajabu kuona mkurugenzi wa
kampuni ya kutengeneza filamu, ndiye aliyeandika skripti, ndiye muongozaji mkuu,
ndiye muigizaji mkuu na kadhalika! Na mwisho wa siku hawapendi kukosolewa.
Nitaendelea kusema bila
kigugumizi, tasnia yetu imebarikiwa kuwa na waigizaji wengi wazuri, wapigapicha
wengi wazuri, wahariri wengi wazuri, na hata baadhi ya waandishi lakini inakosa
kabisa waongozaji wazuri wa filamu. Hii haimaanishi kuwa hakuna kabisa
waongozaji wazuri, wapo wengi wenye uzoefu na elimu ya kutosha katika uongozaji
wa filamu, tatizo ni mfumo mbovu unaowafanya kutupwa nje ya ulingo wa soko la
filamu kwa kuwa hawathaminiki, hawatumiki na wala hawapewi heshima
inayostahili.
Tunasahau kuwa muongozaji
wa filamu ana mchango mkubwa sana
katika kufanikisha kazi nzima ya utengenezwaji wa filamu kwa kuwa ndiye
mtendaji pekee anayeshiriki kwenye hatua zote za uandaaji wa filamu; kuanzia
kwenye wazo hadi kwenye uhariri wa filamu.
Matatizo ya uongozaji kama
haya niliyoyaeleza hapa kwetu wala hayatokei kwa kuwa eti waongozaji wa filamu
nchini hawakusoma, kwangu mimi hii inaweza isiwe sababu ya msingi sana, kama
waongozaji hao watajitambua na kujiendelea kwa kupata mafunzo japo ya muda
mfupi wataweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa. Kukosa elimu ya darasani si
mwisho wa kujifundisha. Hata Hollywood kuna waongozaji ambao hawakusoma kabisa
katika vyuo vya filamu lakini wamepata wamekuwa waongozaji wazuri na
wanaoheshimika sana
duniani.
Waongozaji hao ni pamoja na
Steven Soderbergh, Robert Rodriguez, Quentin Tarantino, Richard Linklater, na
Spike Jonze...
Uongozaji wa filamu ni
zaidi ya elimu ya darasani, unakwenda pamoja na creative vision, commitment na visualization,
sifa zingine zinazoongezeka kwa muongozaji wa filamu ni uwezo wa kuandika
script au kusimamia uandikwaji baada ya rasimu ya awali ya script kukamilika. Pia
baada ya kupata waigizaji, muongozaji wa filamu anapaswa kusimamia masuala ya
kiufundi ya sinema, ikiwa ni pamoja na kamera, sauti, taa, ubunifu na
kadhalika.
Wakati wa uhariri
(post-production), muongozaji wa filamu hufanya kazi kwa ukaribu na Wahariri
katika mchakato wa kiufundi wa uhariri, hadi kufikia mwisho wa kazi. Katika
hatua zote, muongozaji wa filamu anawajibika kuhamasisha timu yake kutayarisha
kazi bora. Muongozaji wa filamu pia anapaswa kuyafahamu mahitaji na matarajio
ya soko la filamu.
Mwisho, muongozaji wa
filamu anapaswa kuwa na uwezo wa kufanya mawasiliano (communication skills) na
watu wengine katika kufanikisha kazi iliyo mbele yake.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment