May 16, 2013

KILIO CHA WASANII KUIBIWA: Je, ni kweli msanii muigizaji ana hakimiliki?


Mmoja wa wasanii waigizaji nchini, Issa Mussa maaruf kwa jina la Claude

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema

MAKALA yangu ya wiki iliyopita iliyohusu mikataba ya wasanii imezua maswali mengine kutoka kwa wasomaji wangu, hasa kutokana na maswali kadhaa niliyoyaibua kuhusu ile hoja ya kilio cha wasanii kulia kuibiwa kazi zao. maswali niliyoyaibua ni kama: Je, ni kweli wanaibiwa? Na kama wanaibiwa, huwa wanaibiwaje? Je, ni kweli uharamia (piracy) wa kazi za filamu ndiyo tatizo kubwa kwenye tasnia ya filamu nchini? Kama ni kubwa lipo kwa kiwango gani? Hivi, wasanii wanayafahamu kweli matatizo yao ya msingi?

Baadhi ya wasomaji wamenitaka niyatolee ufafanuzi maswali haya ili hata wao waelewe kwa kina kinachotokea kwani nimezidi kuwaacha gizani. Ndiyo maana wiki hii nimekuja na swali litakalosaidia kutafuta majibu ya maswali haya; je, ni msanii wa filamu ana hakimiliki?

Ukiliangalia swali hili katika hali ya uvivu wa kufikiri litaonekana ni swali lenye jibu rahisi, lakini kama utaacha uvivu wa kufikiri utagundua kuwa ni swali linalohitaji utafiti wa kina kuyajua mazingira halisi ya mtu anayeitwa msanii kwenye tasnia ya filamu nchini. Jibu halisi ni kwamba si kila msanii ana hakimiliki, si yule wa filamu tu bali hata wa fani zingine.

Kwa mfano kwenye muziki, unaweza kuwa mwanamuziki muimbaji lakini si mtunzi, unaimba kazi zilizotungwa na wenzio, wewe utakuwa unalindwa na Hakishiriki na si Hakimiliki. Kwa upande wa filamu, msanii anayeangaliwa hapa ni muigizaji ambaye anaigiza hadithi iliyotungwa na mtu mwingine akifuata script iliyoandikwa na mtu mwingine, chini ya uongozi wa muongozaji wa filamu, pia hana kabisa hakimiliki ya kazi hiyo, bali analindwa na Hakishiriki tu.

Suala hili limekuwa likiwachanganya wengi kwa kushindwa kutofautisha kati ya wasanii waigizaji (actors) na waandaaji wa filamu (producers) ambao kisheria ndiyo wenye kazi. Msanii anapolipwa baada ya kushiriki kwenye filamu maana yake kuwa ameuza haki hiyo ili kumruhusu anayetengeneza filamu aoneshe hadharani au auze kazi hiyo bila kuingiliwa tena na msanii muigizaji.

Tulio wengi tunachanganya sana kwa kudhani kuwa wasanii waigizaji ndiyo wenye sinema, hasa pale tunapowaona wasanii wenye majina makubwa kwenye tasnia ya filamu nchini ndiyo wakiwa waandaaji wa filamu, kumbe tunashindwa kutofautisha kati ya uigizaji na utayarishaji wa filamu. Jambo hili limekuwa likiwakumba hata wasanii wenyewe pale wanaposhindwa kujipambanua, ni wakati gani wanapaswa kuongea kama watayarishaji wa filamu na wakati gani wanaongea kama wasanii waigizaji.

Tukija kwenye suala la Hakimiliki katika filamu kwa kweli lina upana mkubwa kuliko hata katika muziki, kwa msingi ya kuwa filamu huwa na sauti na picha zinazotembea (audio-visual) wakati muziki huwa sauti (audio) tu. Katika filamu kimsingi kuna wengi wenye hakimiliki kama mtunzi wa hadithi, mwandishi wa script, mtayarishaji, wakati msanii muigizaji akiwa analindwa na sehemu ya sheria inayoitwa Hakishiriki. Kwa kawaida mtengeneza filamu hununua au huingia makubaliano na wenye hakimiliki hawa (hii lazima iwe kwa maandishi), ili haki ziwe kwa mtu mmoja au kampuni moja na iwe ni rahisi zaidi kuzifuatilia.

Hakimiliki na hakishiriki ni mambo yanayowasumbua watu wengi duniani si Tanzania tu. Hapa nchini, baada ya sheria ya hakimiliki ya mwaka 1966 kuthibitika kwamba ina mapungufu mengi, ndipo mwaka 1999 Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipotunga sheria mpya ya hakimiliki na hakishiriki, namba 7 ya mwaka 1999, yenye sura ya 218 ya sheria za Tanzania (kama zilivyorekebishwa mwaka 2002).

Kwa mujibu wa utangulizi wa sheria hii, imeletwa kutengeneza na kutoa manufaa zaidi na ulinzi zaidi wa kazi za wasanii wa kazi zinazolindwa na hakimiliki na hakishiriki na zingine zote zinazoendana na hizo, japo hata yenyewe bado ina mapungufu makubwa. Chini ya kifungu cha 2(c) cha sheria hii, ambacho kimsingi kinazungumzia madhumuni ya kutungwa kwa sheria hii ya muhimu kwa maendeleo ya wasanii na watunzi na wabunifu wote katika nyanja za nyimbo, maigizo na tasnia nyingine zinazoendana na hizo. Sheria hii ina madhumuni ya kuinua kazi za fasihi na za kisanii pamoja na nyinginezo zinazofanana na hizo.

Kwa mujibu wa sheria hii, kuna makundi makubwa mawili ya haki za wasanii zinazolindwa na sheria hii, ambazo ni Haki za Kiuchumi (Economic Rights) na Haki za Kimaadili (Moral Rights) ambazo mtunzi wa kazi zinazolindwa na sheria hii ana haki nazo.

Haki hizi zina msingi katika mkataba wa kimataifa wa Benne wa mwaka 1883 ulioridhiwa na Tanzania Julai 25, 1994; na hivyo kwa mujibu wa kanuni za kisheria za kimataifa, Tanzania ina wajibu wa kutimiza yaliyomo katika mkataba huu iliyouridhia. Kwa mujibu wa sheria hii, chini ya kifungu cha 3(i) cha sheria hii, kazi zinazolindwa na sheria hii ni zile ambazo zimetengenezwa na mtunzi wa Kitanzania au zile ambazo mtunzi wake si Mtanzania lakini ana makazi yake ya kudumu hapa nchini au kazi hiyo iliyotengenezwa kwa mara ya kwanza hapa Tanzania, au kazi ambazo ni za sauti na picha zinazotembea (audio-visual) ambazo mtayarishaji wake ni Mtanzania au makao makuu yake ya kutengeneza kazi hizo yapo nchini.

Na kwa mujibu wa kifungu cha 3(3) cha Sheria hii wasanii wabunifu wanaomiliki kazi za sanaa na wasanii waigizaji wanaolindwa na hakishiriki watapewa ulinzi na sheria hii. Katika kifungu cha 4, msanii ametafsiriwa kama mwigizaji, mwimbaji, mwanamuziki, mchezaji (dancer) au mtu anayeigiza, kuchonga au kufanya maonesho jukwaani. 

Hata hivyo, sheria hii kama sheria nyingine nyingi za hakimiliki, imetoa sharti kwa kazi za kisanii kulindwa na sheria hii na kigezo hiki ni kwamba kazi hiyo iwe katika hali ya kushikika, na kwa maana nyingine ni kwamba wazo/mawazo hayatalindwa na sheria hii hata kidogo. 

Tukija sasa kwenye mada yetu, ingawa hakimiliki zina maisha ya miaka mingi, lakini hapa kwetu tumekuwa na utamaduni wa kuuza hakimiliki, na kama ilivyo kawaida ukiuza kitu huna tena amri nacho. Ni kama mtu aliyeuza nyumba yake, je, atarudi baadae kuuliza kwanini wapangaji hawalipi kodi?

Ndiyo maana nimekuwa nikisema kuwa wasanii waigizaji wanaopiga kelele za kuibiwa, ni ama hawajui wanachokililia (kwa kuwa wanalilia haki zisizowahusu) au wanatumiwa na walionunua kazi zao kwa maslahi ya wamiliki wapya wa kazi hizo ili wapunguziwe kodi na TRA. Tutafakari; kwanini walionunua Hakimiliki siyo wanaopiga kelele za kuibiwa ila wale waliouza haki ndiyo wanaolalamika? Ndiyo maana nilisisitiza kwenye makala yangu iliyopita kuwa kuna haja ya kuwepo elimu endelevu kwenye mambo haya.

Pia elimu itolewe kwa jeshi letu la Polisi kuhusiana na Hakimiliki na Hakishiriki kwani inaonekana hawajui kabisa hasa pale unapomfikisha mtuhumiwa wa wizi wa kazi za sanaa katika jeshi la polisi. Polisi wanashindwa kutofautisha wizi wa mali zinazohamishika na zisizohamishika, lakini wanashindwa kuelewa kuwa kuna wizi wa mali aina ya tatu ambayo hata wenye mali mara nyingine hawajui kama ni mali yao, hii ni mali itokanayo na ubunifu na huitwa ‘Milikiubunifu’ au kwa Kimombo inajulikana kama ‘Intellectual Property’.

Mali zinazohamishika ni kama pesa, nguo, magari nk, zisizohamishika ni kama nyumba, mashamba viwanja na mali aina hizo. Sheria za ulinzi wa mali hizi ziko wazi.

Milikiubunifu ni kama mali nyingine na sheria zake za msingi ni zilezile. Mwenye mali ndie mwenye amri kuhusu mali zake. Anaweza akauza, akaazimisha akazibadili matumizi, akamruhusu mtu mwingine kutumia, kimsingi mwenye mali ana haki zote kuhusu mali zake. Tatizo la mali aina ya Milikiubunifu ni kuwa unaweza kuilinda pale ikiwa bado kichwani kwako, lakini ukishaitoa kunakuwa na ugumu wa kuilinda, ukishatoa filamu basi uwezekano wa kutumia kazi zako bila ruksa yako unakuwa mkubwa zaidi hata katika zama hizi za intanet.

Ndiyo maana serikali zimetengeneza sheria zinazoitwa sheria za milikibunifu ili kuwawezesha wabunifu walinde haki zao. Sheria hizi zimegawanywa katika makundi mawili: Industrial Property na Copyright. Industrial Property iko chini ya BRELA, na Copyright inaratibiwa na Cosota. Sheria hizi humpa haki 'mbunifu' ili kulinda haki zake za kiuchumi na za kimaadili.

Takafari…

No comments: