Jun 6, 2013

KUELEKEA 1 JULAI 2013: Hivi tuna uhakika na mfumo wetu wa urasimishaji?

Sina hakika kama kuna nia ya dhati kumkomboa msanii


Wadau wa sanaa wakichangia mawazo yao kwenye Jukwaa la Sanaa linaloendeshwa kila Jumatatu na Basata

FILAMU zimeibuka kuanzia karne ya ishirini na baadaye kuwa kishawishi kikubwa na mawasiliano ghali katika karne ya ishirini na moja. Hakuna aina nyingine ya sanaa ambayo imesambaa kwa ufanisi na kuonekana kuvuka mipaka ya kiutamaduni katika mataifa mengi.


Katika karne hii, teknolojia ya televisheni na maonesho mbalimbali ya wajasiriamali vimeitangaza sana tasnia ya filamu kwa watu wote; watazamaji wa mijini na vijijini katika nchi nyingi zinazoendelea. Hata hivyo, filamu nyingi zinazosambazwa kimataifa na kupenya soko la nchi nyingi ni zile zinazozalishwa nchini Marekani na baadhi ya nchi za  Ulaya. Ukweli huu, pamoja na kutambua nguvu ya filamu “inayoyumbisha mioyo na akili za watu” unaamsha wasiwasi kwa walio wengi.


Kama inavyoeleweka kuwa kwa sasa serikali yetu imeamua kuutambua mchango wa filamu na muziki na hivyo sasa tunashuhudia nchi ikiingia kwenye mfumo rasmi kwa kurasimisha Sekta ya Filamu na Muziki, ambapo mchakato wa urasimishaji wa sekta hizi ulioanza rasmi tarehe 1 Januari 2013, utaanza kufanikishwa zaidi ifikapo tarehe 1 Julai 2013, kwa kuhakikisha kuwa hakuna kazi yoyote ya Filamu na Muziki itakayoingia sokoni bila kuwa na stamp ya TRA.


Jumatatu ya wiki hii, tarehe 3 Juni 2013, Baraza la Sanaa la Taifa lilizikutanisha taasisi nne zinazohusika na urasmishaji wa sekta za filamu na muziki kwenye Jukwaa la Sanaa ambalo hulifanya kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz), kila Jumatatu kuanzia saa 4 asubuhi kwenye ukumbi wake ulioko makao makuu ya Baraza hilo, Ilala Sharif Shamba.


Katika Jukwaa la Sanaa linalohusisha wadau wote wa sanaa, hoja nzito na motomoto kuhusu tasnia ya Sanaa na Utamaduni zimekuwa zikijadiliwa na kujibiwa.


Lengo la kuzikutanisha taasisi zote nne: Baraza la Sanaa la Taifa lenyewe, Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza, Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki Tanzania (Cosota) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) lilikuwa ni kutoa elimu kwa Wasanii, wadau na wakuzaji sanaa, na pia kuwakumbusha kuwa tarehe 1 Julai mfumo rasmi wa stempu za TRA utaanza. Wadau wa sekta ya sanaa nikiwemo mimi tulialikwa ili kupeleka michango na hoja zetu ili kuleta mustakabali utakaojenga sekta ya sanaa.
Nasikitika kuwa sikuweza kufika siku hiyo kuwasilisha maoni yangu kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu, lakini hata hivyo, maoni ambayo ningeyatoa hayatofautiani na yale ambayo nimekuwa nikiyasema mara kwa mara pindi ninapopata nafasi ya kukutana na watendaji wa taasisi hizi zinazohusika na urasimishaji, pia hayatofautiani na yale ambayo nimekuwa nikiyaandika kwenye makala zangu, ambayo hata leo japo nataka kuelezea jambo jipya lakini siwezi kuyakwepa kuyaeleza.


Haya ni mambo ninayodhani kuwa kama hayatarekebishwa au yakiendelea kupuuzwa basi yatazidi kuwa kikwazo kikubwa katika kufikia ufanisi wa kile kinachosemwa kuwa ni urasimishaji wa filamu na muziki.


Niweke wazi kwamba binafsi siamini kama mfumo huu walioamua kuutumia ni urasimishaji, bali ninachokiona ni mfumo wa ukusanyaji mapato kupitia kazi za filamu na muziki, kwa kuwa mfumo unaotumika kufanikisha zoezi hili ni mfumo mpya kabisa duniani, haupo popote (nina uhakika na hili) na haueleweki si kwa wadau na wasanii tu, bali hata kwa watendaji wenyewe umeonekana kuwakanganya.


Nijuavyo mimi, mfumo wa urasimishaji wa sekta yoyote ile duniani, huanza kwanza kwa kuandaa SERA. Hivi ni lini tutaacha kufanya kazi ‘kibongobongo’ ili tupate tija kwenye kazi zetu? Hivi serikali wameamua kurasimisha sekta hizi kwa sera ipi hasa? Nani anaweza kunihakikishia kuwa tuna sera ya filamu/muziki? Je, sera ya filamu/muziki nchini ni ipi?


Kama kweli tunaamini kuwa tasnia ya filamu na muziki ni moja ya sekta zenye nguvu na zenye kuchangia kwa kiwango kikubwa katika ajira kwa vijana, kwa nini hatuna sera inayotuongoza? Au tunadhani tutaendelea kuongozwa na matamko ya viongozi hadi lini? Ieleweke matamko si sheria, ndiyo maana kila kiongozi anayeingia anakuwa na matamko yake ambayo atakayefuata baada yake halazimiki kuyafuata.


Hivi hatuoni kama huu ni muda muafaka wa kuwa na sera ya filamu itakayotuongoza katika kutenda kazi zetu? Hatujui kuwa nchi yoyote iliyoendelea kwenye tasnia ya filamu ina sera madhubuti?


Inawezekana wengi wetu hata hatujui sera ni nini, na upi umuhimu wa kuwa na sera. Kwa ufahamu wangu natambua kuwa Sera ni mfumo, ni mwongozo thabiti unaotamkwa, unaoandikwa au unaoashiriwa na kuanzisha mipaka na maagizo ambayo kwayo hatua za usimamizi thabiti zitafanyika. Hutoa muundo ambao ndani yake waamuzi wanatarajiwa kufanya kazi wakati wakifanya maamuzi.


Sera huzingatia katika kuwatambua wadau na wote wanaofanya kazi katika sekta husika, kuzitambua taasisi na mamlaka zote zinazosimamia sekta husika, kutambua ubora wa elimu inayopatikana au wanayoitaka (wadau) katika nchi, kiwango na ushawishi wa utamaduni katika mafunzo, utafiti, mafunzo na maendeleo, miundombinu ya masoko, upatikanaji wa takwimu sahihi, na mwisho ndipo ukusanyaji wa kodi hufanyika.


Katika mfumo ulioanzishwa hapa nchini, inaonekana wazi haya yote yameonekana si muhimu kabisa isipokuwa suala la kukusanya kodi.


Sera itatuondolea huu mkanganyiko ambao hata watendaji wenyewe wa mamlaka (TRA) wameonekana kutojua washike kipi na waache kipi. Hivi inawezekanaje mimi kama mmiliki wa kampuni ya kutengeneza filamu ambaye imefanyiwa makadirio kulipa kodi na Mamlaka ya Mapato na kutakiwa kulipa laki sita kwa mwaka (kwa mfano) kwa kazi hii, nitakiwe tena kulipia sh 54/- za stempu kwa kila kazi ninayotoa? Inakuwaje nitoe kodi mara mbili? Hii imekaaje?


Pili, inaposemwa kuwa kazi zote zilizopo dukani zinatakiwa ziwe na stempu za TRA, haijafafanuliwa ni nani wa kuzibandika stempu; mwenye duka, msambazaji au mmiliki wa kazi hizo? Itakuwaje pindi mmiliki asipopatikana (kwa mfano alishafariki na hakuacha mtegemezi, yupo nje ya nchi, hajulikani alipo au baada ya kuingia mkataba na msambazaji akaachana na biashara hiyo)? Kwanini abebeshwe mzigo mwenye duka au msambazaji ambaye yeye alinunua kazi hizo wakati sheria hizi zilikuwa hazijatungwa? Mimi nadhani suala hili lingeangaliwa upya.


Ieleweke kuwa thamani ya sera inaonekana kutokosekana kwa miongozo ya lazima na visheni, kwa hiyo ni dhahiri kwamba akili zinazoweka pamoja sera zinakwenda na wakati na huwa zina maono. Hata hivyo, hali ya sasa inaonekana kutoendana na hisia zinazojionesha. Hali ya utengenezaji wa filamu na matumizi inahitaji kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa. Bila sera madhubuti hili litabaki kuwa ndoto.


Inaweza isiwe muhimu sana kushiriki katika mapitio ya sera ya filamu au hata miundombinu isiyokuwepo au fedha za kujikimu na utaratibu wa mitaji ya fedha za uzalishaji filamu nchini kama itafanywa kuwa mada tofauti. Kwa kweli, inahitajika semina nzima kutathmini fedha na masoko ya filamu nchini.


Jambo moja ambalo linaonekana kwa haraka ambalo liko kati ya rasilimali watu ni tofauti na elimu ya asili. Kwa hiyo inapaswa kuangalia kuwa ubora wa elimu ya filamu inapatikana katika nchi. Je, kuna mwelekeo wa wazi na kiwango na ushawishi wa utamaduni katika mafunzo? Tuwe na sera ya filamu ambayo itahusika na mafunzo, utafiti na maendeleo kama nilivyodokeza hapo juu.


Hakuna haja tena ya kuangalia uhalali au dosari ya taasisi inayojishughulisha na filamu katika kipindi hiki cha uchumi wa kweli katika taifa letu. Tunachoweza kuzingatia ni jinsi ya kuangalia namna elimu inavyoweza kutolewa kwa walioikosa katika shule za filamu na jinsi ya kuanzisha taasisi za mafunzo ya filamu ambazo kwa sasa hazipo, jambo linaloweza kutumiwa na hali yetu ya sasa ambapo hakuna tena busara kiuchumi ili kuwekeza katika filamu. Sababu ya kuamua ni majibu mazuri ya soko kwa filamu zinazozalishwa kwa mitaji midogo.


Katika mafunzo yatakayotolewa kwenye Taasisi za filamu, mtaala lazima uzingatie pamoja na jinsi ya kupenyeza vyote, teknolojia na utamaduni ili kuzalisha kazi zenye viwango vya kimataifa katika masuala ya ubora wa mada.


Kama dhana nzima ilivyo hatuwezi kuendelea kulalamika tu bila kutafakari cha kufanya, kinachoweza kujadiliwa kitakuwa na uwezekano wa kutatuliwa kwa mtazamo mpana zaidi.


Alamsiki…

No comments: