Jul 4, 2013

Umuhimu wa Shirikisho la Filamu Tanzania ni kwenye misiba tu?

Linathaminiwa wakati wa misiba ya wasanii tu na kutupwa katika shughuli zingine za kijamii



Sehemu ya umati wa watu katika Tamasha la Filamu jijini Mwanza

Mmoja wa wasanii wa Bongo Movie, Jacob Steven (JB), 
akigawa vyandarua jijini Mwanza

NI asubuhi tulivu ya Jumatano, siku moja tu baada ya kumalizika kwa ziara ya kiongozi mkuu wa taifa linaloongoza duniani la Marekani, Rais Barack Obama, aliyeondoka nchini baada ya ziara yake ya siku mbili. Nikiwa nimekaa sebuleni nikifuatilia kipindi cha televisheni cha ‘Tuongee Asubuhi’ kinachorushwa na moja ya vituo vya runinga hapa nchini, ambapo kulikuwa na mada iliyosema “Nafasi ya filamu katika soko la kimataifa”.

Katika mada hii, walialikwa wasanii wa jijini Mwanza, Hussein Kim, Prosper Kiri na Anita Kajumulo, na Dar es Salaam kulikuwa na Steve Mengere na Mwakilishi wa TBL wa kinywaji cha Grand Malt, Fimbo Butala. Mada hii ilijikita zaidi kulielezea Tamasha la filamu linaloendelea jijini Mwanza chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji cha Grand Malt.

Tamasha hili linaratibiwa na Mkurugenzi wa Sofia Production, Musa Kissoky, na lilizinduliwa rasmi tarehe 1 Julai katika Uwanja wa Nyamagana, na lilitanguliwa na tukio la wasanii wa Bongo Movie kukabidhi vyandarua kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza pamoja na Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure.

Kilichonishtua zaidi ni kwa TBL, sijui ni kwa makusudi au kutokujua, ilipoamua kuongozana na wasanii wa kikundi cha Bongo Movie na kudharau uwepo wa Shirikisho la Filamu Tanzania ambalo ndilo lenye jukumu la kuwa msimamizi wa shughuli zote za filamu nchini. Sijajua kama tatizo lipo kwa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) kutokutoa mwongozo kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa wengine, tatizo ni TBL kutotambua umuhimu wa Shirikisho, au ni dharau tu kwa Shirikisho!

Kutokushirikishwa kwa Shirikisho ilisemwa kuwa ni kasoro kubwa na ilibainishwa na kiongozi wa waigizaji mkoa wa Mwanza, Hussein Kim, pale alipoelekeza lawama zake moja kwa moja kwa TBL kwa kuwatenga wasanii wa Mwanza waliopaswa kuwa wenyeji wa tamasha hilo na kukumbatia kikundi cha wasanii wa Bongo Movie waliotokanao Dar es Salaam, huku wakidharau hata mamlaka ya Shirikisho kwa kutoambatana na kiongozi yeyote wa Shirikisho.

Kama Katibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu Tanzania, nilibaki najiuliza, mbona ofisi yangu haina taarifa rasmi kuhusiana na Tamasha hili? Upi umuhimu wa kuwa na Shirikisho la Filamu Tanzania kama kila mtu anaweza kujifanyia anachotaka pasipo Shirikisho? Inakuwaje Shirikisho la Filamu Tanzania kupewa kipaumbele/umuhimu wakati wa matukio ya misiba ya wasanii tu na kutupwa katika shughuli zingine za kijamii kama hizi?

Wakati nikiendelea kujiuliza maswali yasiyokuwa na majibu, mfuatiliaji wa filamu na mwanahabari wa muda mrefu, John Hans Badi, kwa kutambua nafasi yangu katika Shirikisho alinipigia simu kuniuliza kuhusu ‘mandate’ ya Shirikisho na jinsi linavyochukuliwa na wadau ambao kwa makusudi wamelidharau na kukumbatia kikundi kidogo cha wasanii. Hii ni baada ya kuguswa na hoja za Kim kuhusu kutengwa na kutoshirikishwa kwa Shirikisho la filamu na wawakilishi wao waliopo jijini Mwanza.

Badi alijaribu kulingalinisha mamlaka ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Akiuliza ni vipi mtu anayejishughulisha na masuala ya mpira wa miguu hata kama ni kwa kuanzisha ligi ya mchangani anavyopaswa kupata kibali/baraka kutoka TFF, lakini hali inakuwa tofauti kwa TAFF kwenye shughuli za filamu. Je, ni kwamba TAFF haina mamlaka ya kuwa msimamizi wa shughuli zinazohusu filamu nchini? Haina meno? Au ni kipi kinachowafanya wasanii na wadau kudharau mamlaka ya TAFF?

Badi alibainisha kuwa kama hali hii itaachwa hivihivi kwa kila mtu kujifanyia atakacho kwenye masuala ya filamu bila uwepo wa chombo cha juu cha wadau kinachopaswa kusimamia shughuli hizi, basi ni wazi tunakoelekea ni kubaya zaidi.

Simu ya John Badi ikanikumbusha matukio yaliyowahi kutokea huko nyuma, matukio yaliyosababisha mgawanyiko wa wasanii na wadau wa filamu nchini yaliyochagizwa na kundi la Bongo Movie dhidi ya uongozi halali wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF).

Nikazikumbuka zile mbinu zilizotumiwa kuwachonganisha wasanii dhidi ya viongozi wao wa shirikisho huku Bongo Movie ikisaidiwa na mfadhili wao anayelimiliki soko la filamu nchini na baadhi ya viongozi wa serikali.

Nikazidi kukumbuka wakati ule mtafaruku wa makundi haya mawili hata serikali ilionekana kuwa kimya ingawa kuna wakati fulani Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa wakati huo, Dk. Emmanuel Nchimbi, alikiri kuwepo matatizo ya kuelewana kwa wasanii wa filamu hapa nchini.

Simu ya John Badi pia ikanikumbusha jinsi nilivyoguswa na mgawanyiko huo ulionifanya kuitaka Serikali itangaze maslahi yake katika mgogoro huo wa wasanii uliokuwa ukiendelea au iwasaidie wasanii kuharakisha kufanya marekebisho si katika sheria tu, bali na taasisi (likiwemo Shirikisho la Filamu) zilizoundwa kwa lengo la kuwasaidia wasanii kusonga mbele kikazi na kimapato.

Ni wazi sanaa ya maigizo na filamu inashika kasi na imetoa ajira za kutosha tu kwa vijana wengi wa Kitanzania, huku pia ikiwa sehemu ya mambo yenye kuchangia katika pato la taifa. Na ni wazi kuwa kwa kasi hii kama tutapata sera madhubuti ya filamu itakayosaidia katika urasimishaji itatuwezesha kufikia mahali ambapo sekta hii itakuwa moja ya sekta zenye kutoa asilimia kubwa ya ajira kwa vijana wa Kitanzania na kuchangia asilimia kubwa katika pato la taifa.

Filamu husaidia kutangaza vivutio vya nchi husika na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utalii wa nchi. Hata utamaduni wa nchi husika huidhinishwa kupitia sanaa, elimu kwa jamii nzima hujumuishwa katika sanaa, maadili ya nchi hubebwa na kusambazwa kwa jamii kupitia sanaa, wanasiasa wote hutengenezwa na kukuzwa kwa kiwango kikubwa sana na sanaa.

Si hivyo tu, mambo mengi katika jamii hubebwa na sanaa ikiwemo kupashana habari ambazo zinaweza kuwafikia wanajamii kwa urahisi zaidi na kuweka kumbukumbu zisizofutika akilini mwao hubebwa na sanaa. Katika nchi zilizoendelea waliligundua hili la sanaa kufanya kila kitu kiwe kama kilivyo, na wakaamua kuiheshimu na si kuidharau kama inavyofanyika hapa kwetu.

Nchi za ulaya zimejikita katika kukuza raslimali watu na kuenzi kile kitokanacho na raslimali watu hawa, mtu yeyote au kitu chochote ambacho kinaweza kuwazuia hawa raslimali watu kutimiza wajibu wao, basi inakuwa jukumu la kila mtu kutatua tatizo hilo, huu ni mfano wa kuigwa.

Sanaa ina uwezo mkubwa sana katika kuongeza pato la nchi, kuongeza ajira kwa vijana kwa kiwango kikubwa kuliko sekta nyingine yeyote, kuitambulisha nchi kimataifa na kutangaza vivutio vya nchi na hivyo kusaidia kuwaleta watalii wengi kuvitembelea vivutio hivyo na kuliingizia taifa pesa nyingi za kigeni kupitia utalii, kujenga uzalendo wa vijana katika kulitumikia taifa lao na hata kuchangia kuijenga nchi kisaikolojia.

Ili kufanikiwa katika haya yote, tutaweza tu kama kweli tutaamua kufuata sheria na kuheshimu mamlaka zilizowekwa kusimamia sekta hii kwa kuzika tofauti zetu ili tusukume gurudumu la maendeleo ya filamu mbele na hatimaye tuwe na soko la filamu lenye nguvu katika Afrika.

Ni umoja pekee utakaotuondoa kwenye huu ugonjwa mbaya wa kumtafuta mchawi: wasanii wanalalamika, wazalishaji wanalalamika, wasambazaji wanalalamika, watumiaji wa kazi za sanaa wanalalamika, wanasiasa wanalalamika pia, serikali inalalamika kukosa ushuru, huku watu wachache wanafurahi, hao si wengine bali wezi wa kazi za sanaa.

Niweke wazi kuwa kutoshirikishwa/ kudharauliwa kwa Shirikisho la Filamu Tanzania kunatokana na tatizo ambalo tayari tunalijua na tunalifanyia kazi. Naamini ni miezi michache tu ijayo tutakuwa na sera ya filamu tunayoipigania sasa ili ipitishwe na Serikali, baada ya kupita ndipo umuhimu wetu utakapoonekana na ndipo tutakapoweza kudhibiti maadili na nidhamu katika sekta ya filamu. Kwani kwa sasa sekta hii imeonekana kuwa kimbilio la kila mtu hata watu walioharibu/kushindwa katika sekta nyingine.

Alamsiki.

No comments: