Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Dk. Fenela Mukangara
SERIKALI imekuwa ikijinadi
kuwa inawajali wasanii ndiyo maana imeamua kuutambua mchango wao kwa
kuirasimisha tasnia ya burudani - hasa filamu na muziki – ili wasanii wafaidi
jasho la kazi yao, na imekuwa ikionesha kwa vitendo kuwa karibu na wasanii
pindi kunapotokea msiba wa msanii maarufu, ingawa bado kuna maswali kadhaa
ambayo yanajitokeza na kuleta maswali makubwa zaidi kama kweli inawajali.
Inashangaza kuona kuwa Wasanii
ambao Serikali inajigamba kuwajali hadi leo tunapojigamba kuingia kwenye
urasimishaji bado hawana sera (ya filamu kwa waigizaji au ya muziki kwa
wanamuziki) inayowaongoza katika kufikia mafanikio ya tasnia yao . Pia inashangaza kuona kuwa Idara muhimu
ambayo ndiyo uti wa mgongo wa sanaa nchini, ya Utamaduni limekuwa tatizo
jingine kubwa kwa mustakabali wa maendeleo ya sanaa nchini.
Idara hii imekwishahama
Wizara zaidi ya kumi toka nchi hii ilipopata Uhuru wake mwaka 1961. Kwanini? Sidhani
kama hali hii inatokea tu kwa bahati mbaya. Mwaka 1995 na pia mwaka 2010, Idara
hii ilisahauliwa kutajwa wakati wa kutangaza Baraza la Mawaziri baada ya
Uchaguzi Mkuu, mwaka 2010 tulipewa taarifa kuwa jambo hilo lilitokea kwa bahati
mbaya ingawa mwaka 1995 hapakutolewa maelezo yoyote, ila kimya kimya ikaelezwa kuwa
Utamaduni utaendelea kuwa chini ya Wizara ya Elimu.
Kuanzia kipindi cha miaka
ya 90, Serikali ilifuta ngazi kadhaa za uongozi katika Utamaduni,
kulikuweko na nafasi ya Kamishna wa Utamaduni ambayo leo hii haiko tena,
kulikuweko na nafasi ya Afisa Utamaduni wa Mkoa, nayo haiko tena. Na Maafisa
Utamaduni tulionao leo hii, wa Wilaya na Manispaa, hawawajibiki katika Wizara inayohusika
na Utamaduni, bali wako chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambayo ni wizara tofauti kabisa na ile inayohusika
na Utamaduni. Kwa wenye uelewa watagundua kuwa hapa pana tatizo kubwa
linatokea.
Wakati tukiwa katikati ya
kipindi ndipo lilipoibuka suala la Maafisa Utamaduni walioonekana kusahaulika
katika mfumo huu wa urasimishaji uliopo sasa. Lawama zilishushwa kwa wasanii kwamba
wao hupenda kwenda moja kwa moja Wizarani (kwenye Bodi ya Filamu) na
kulithamini Baraza la sanaa La Taifa (Basata) huku wakiwaacha Maafisa Utamaduni
ambao ndiyo wako karibu na wasanii na jamii kwa ujumla.
Katika mazungumzo hayo
yaliyoibua ukinzani fulani wa mawazo na hoja, nilijaribu kuelezea uelewa wangu
kuhusu Maafisa Utamaduni na majukumu yao , ndipo
Afisa Utamaduni wa Manispaa moja jijini Dar
es Salaam alipopaza sauti akinialika kuwa nimtembelee
ofisini kwake kwa mazungumzo zaidi. Sikujivunga, nilimtembelea ofosini kwake siku
mbili baadaye.
Nikiwa ofisini kwake
tuliongea mambo mengi sana ,
na alijitahidi kunielezea namna Maafisa Utamaduni wanavyofanya kazi zao na kusisitiza
kuwa hizi taasisi zingine zimeamua kupora mamlaka ya Maafisa Utamaduni. Hapa
hakumumunya maneno, alikuwa akizilenga Bodi ya Filamu na Basata. Nikakumbuka
kuwahi kumsikia Afisa huyo huyo wakati fulani akitamba kuwa yeye hababaishwi na
Basata. Nilijiuliza sana
wakati ule, kumbe alitamba kwa kuwa hayuko chini ya Wizara ya Utamaduni!
Kwa hali hiyo, shughuli za
pamoja za Kitaifa zinazohusu Utamaduni ni ngumu kuzifanya katika mazingira ya sasa,
ndiyo maana hata Mashindano ya Kitaifa ya kazi za sanaa hayasikiki tena, hata
shughuli zinazohusika na maslahi ya pamoja ya wasanii kama vile ulinzi wa haki
za wasanii (Hakimiliki) umekuwa wa shaghalabaghala, maana hakuna ajenda ya
pamoja kwa viongozi hawa wanaotegemewa kuwa karibu kabisa na wasanii.
Kwa mujibu wa Afisa wa
Utamaduni niliyeongea naye, upokaji huo wa mamlaka kwa Maafisa Utamaduni wa
Wilaya umewafanya wao kuwa wakusanyaji wa pato la Wilaya bila kuwa na mchango
kwa wadau waliomo katika tasnia mbalimbali za Utamaduni wilayani mwao jambo
ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya sanaa, kwa kuwa wao ndiyo walio karibu na
wananchi. Pia wamekuwa wakikumbukwa nyakati za Mwenge tu kwa kupewa fedha za
kukamilisha shughuli hiyo, jambo ambalo ni tofauti na majukumu yao halisi.
Pia hali iliyopo sasa ya
Maafisa Utamaduni kuwa chini ya Idara ya Elimu na Mafunzo iliyo chini ya Afisa
Elimu wa wilaya inawafanya wakose gawio la kutosha la bajeti kwa ajili ya
maendeleo ya sekta ya utamaduni badala ya wao kuwa na bajeti maalum kwa ajili
ya kushughulikia sekta hiyo muhimu.
Nakumbuka miaka ya nyuma sana , wakati huo nikiwa
mdogo, Maafisa Utamaduni walikuwa kimbilio la wasanii, waliweza kutafuta vifaa
vya muziki kwa wanamuziki, kutafuta maeneo ya kufanyia mazoezi kwa wasanii
wasio na nafasi. Hata yale majumba yaliyojengwa karibu kila wilaya maarufu kama Community Centres yalikuwa chini ya Maafisa
Utamaduni na kuwa mahala ambapo serikali ilipajenga maalum kwa ajili ya shughuli
za sanaa.
Community Centres hazipo
tena baada ya kugeuzwa aidha kuwa ofisi za Manisipaa au kukodishwa kwa watu
binafsi kuongeza pato la serikali za mitaa bila kujali vijana waliomo katika Manispaa
wanapewa sehemu maalum kufanya shuguli zao za sanaa.
Kwa kukosa sera nzuri ya
filamu/muziki, kukosekana kwa Community Centres na mkanganyiko katika Idara ya
Utamaduni ni mambo ambayo, tupende tusipende, yanadidimiza sanaa nchini japo
serikali inajidai kuwathamini wasanii. Pia ukiangalia Bajeti ya Tamisemi unajiuliza
ni asilimia ngapi ya bajeti hiyo huenda katika shughuli za Utamaduni?
Tunasahau kuwa Utamaduni
ukilelewa vizuri ni chombo chenye nafasi nyingi sana za ajira, huweza kuongeza
pato la eneo husika kwa kuhamasisha maendeleo, huleta uzalendo, ubunifu wa
mambo mbalimbali ya Utamaduni, huweza kuhamasisha Utalii katika Utamaduni, na
huwa ni sehemu ya Utalii ambayo kwa bahati mbaya sana haijatumika kikamilifu
katika kuongeza kipato cha nchi hii kwa ujumla.
Mkanganyiko huu umeifanya sekta
ya sanaa kuyumba kwa kuwa inashughulikiwa na wizara tatu tofauti; Wizara ya Viwanda
na Masoko, Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, hali ambayo imekuwa
ikisababisha migongano ya kiutendaji na ukosefu wa usimamizi wa moja kwa moja
wa sekta hii katika wizara moja.
Hali hii imekuwa
ikisababisha hata Sera ya utamaduni iliyozinduliwa mnamo Agosti 23, 1997 mjini Dodoma , ikiwa ni hatua ya
pili baada ya ile ya kwanza ya kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na
Vijana mwaka 1962 kuonekana kupuuzwa, si hivyo tu, bali hata huo utamaduni
wenyewe unapuuzwa…
No comments:
Post a Comment