Aliyekuwa Afisa Mtendaji wa COSOTA, Yustus Mkinga
SIKU ya Jumanne ya tarehe
26 Machi 2013, ambayo kwangu ilikuwa siku muhimu sana kwani ndiyo siku ya
kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu, siku hii nilipata maliko wa kuitwa kwenye kikao
cha mazungumzo kati ya COSOTA na Viongozi wa Mashirikisho (Muziki, Stadi za
Ufundi, Filamu), niliingia kwenye kikao hiki kwa mujibu wa nafasi yangu ya
Ukatibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu Tanzania.
Mazungumzo yetu yalikuwa na
ajenda kadhaa ikiwemo kumtambulisha Afisa Mtendaji Mkuu mpya wa Cosota, baada
ya aliyekuwepo kumaliza muda wake.
Katika kikao hicho
tulizungumza mengi, mojawapo ikiwa ni mchakato wa mabadiliko ya sheria mpya za
hakimiliki na hakishiriki. Kama kuna mambo yanayowasumbua wasanii wa Tanzania na
watu wengi duniani ni suala la hakimiliki na hakishiriki kwa wasanii na
wabunifu wa sanaa kwa ujumla.
Hapa Tanzania , baada ya sheria ya hakimiliki ya mwaka
1966 kuthibitika kwamba ina mapungufu mengi, ndipo mwaka 1999 Bunge la Jamhuri
ya Muungano lilipotunga sheria mpya ya hakimiliki na hakishiriki, namba saba ya
mwaka 1999 na ambayo ni sura ya 218 ya sheria za Tanzania
(kama zilivyorekebishwa mwaka2002).
Sheria ya hakimiliki na
hakishiriki na 7 ya 1999 ina mapungufu kadha wa kadha. wadau waliyaona hayo
kuanzia muda mrefu, na kuanzia mwaka 2006 kazi mbalimbali zilifanywa ili kupata
mapendekezo ya mabadiliko katika sheria hiyo, mapendekezo yameshapelekwa wizara
ya viwanda na biashara, lakini imekuwa bubu. harakati zilianza na kupelekwa
mabadiliko hayo kwenye Baraza la Mawaziri kisha Bungeni, lakini kumekuwa na
kigugumizi hadi sasa.
Kwa mujibu wa utangulizi wa
sheria hii, imeletwa kutengeneza na kutoa manufaa zaidi na ulinzi zaidi wa kazi
za wasanii wa kazi zinazolindwa na haki miliki na hakishiriki na zingine zote
zinazoendana na hizo.
Chini ya kifungu cha 2(c)
cha sheria hii, ambacho kimsingi kinazungumzia madhumuni ya kutungwa kwa sheria
hii muhimu kwa maendeleo ya wasanii na watunzi na wabunifu wote katika sekta ya
muziki, maigizo na tasnia nyingine nyingi zinazoendana na hizo.
Sheria hii pia ina
madhumuni ya kuinua kazi za fasihi na za kisanii pamoja na nyinginezo
zinazofanana na hizo.
Kwa mujibu wa sheria hii,
kuna makundi makubwa mawili ya haki za wasanii zinazolindwa na sheria hii,
ambazo ni haki ya kiuchumi na haki za kitamaduni ambazo mtunzi wa kazi
zinazolindwa na sheria hii ana haki nazo.
Haki hizi zina msingi
katika mkataba wa kimataifa wa Benne wa mwaka 1883 ambao uliridhiwa na Tanzania
tarehe 25 mwezi wa Julai mwaka 1994 na hivyo kwa mujibu wa kanuni za kisheria
za kimataifa, Tanzania ina wajibu wa kutimiza yaliyomo katika mkataba huu
iliyouridhia.
Kwa mujibu wa sheria hii,
chini ya kifungu cha 3(i) cha sheria hii, kazi zinazolindwa na sheria hii ni
zile ambazo zimetengenezwa na mtunzi wa Kitanzania au zile ambazo mtunzi wake
siyo Mtanzania lakini ana makazi yake ya kudumu hapa nchini au kazi hiyo
iliyotengenezwa kwa mara ya kwanza hapa Tanzania au kazi ambazo ni za kusikika
na kuona (audio-visual) ambazo mtayarishaji wake ni Mtanzania au makao makuu
yake yakutengeneza kazi hizo zipo Tanzania.
Na kwa mujibu wa kifungu
cha 3(3) cha Sheria hii wasanii wanaomiliki kazi za kisanii na wana hakishiriki
pia watapewa ulinzi na sheria hii. Na kwa mujibu wa kifungu cha nne, msanii
ametafsiriwa kama muigizaji, muimbaji,
mwanamuziki, mchezaji (dancer) au mtu mwingine anayeigiza, kuchonga au kufanya
maonesho jukwaani.
Lakini haki hizi
hutofautinana sana
kulingana na aina ya sanaa, kwani zipo sanaa ambazo hujumuisha watu wengi hadi
kukamilika kwake. Kwa mfano; katika tasnia ya filamu kuna hatua tano katika
kukamilisha zao la kazi (filamu) kabla ya kumfikia mlaji. Hatua hizo kwa
kitaalam hujulikana kama Development,
Pre-production, Production, Post-Production na Distribution.
Pia katika uandaaji wa kazi
hizi kuna makundi ya wadau wa aina tofauti: wasanii waigizaji, watunzi wa
hadithi, waandishi wa script, waongozaji, watayarishaji wa filamu, wasambazaji
na kadhalika. Na baadaye kuna vyombo vya urushaji wa matangazo ya filamu na
video kama vile vituo vya televisheni na
kampuni kadhaa za usambazaji kazi kwa njia ya Cable.
Katika kila kundi kati ya
haya niliyoyataja kuna aina mbalimbali za haki kulingana na ushiriki wa mtu
husika. Kwa mfano wasanii waigizaji hulindwa na sehemu ya hakimiliki inayotajwa
kama 'Hakishiriki', na hawa kwa kawaida hulipwa
moja kwa moja kutokana na nafasi walizoigiza katika filamu, au hulipwa kwa
scenes (matukio) kutegemea aina ya mkataba wao na mtayarishaji unasemaje.
Katika kile kinachosemwa
kuwa watu wanaibiwa, utaona kuwa wasanii waigizaji hawana cha kuibiwa kwani
wanakuwa wameshalipwa na watengenezaji wa filamu. Labda tatizo liwe ni malipo
kiduchu wanayopewa na si vinginevyo.
Upande wa watayarishaji wa
filamu ambao ndiyo wana jukumu la kuwalipa waandishi wa script, wasanii
waigizaji, waongozaji wa filamu na washiriki wengine katika filamu. Hawa
hutegemea kupata fedha zao kutokana na malipo wanayopata kwa wasambazaji. Na
hapa ndo' penye ugomvi na kelele za kuibiwa.
Watengezaji wa filamu
nchini wamekuwa wanalalamika kila mara kuwa wanaibiwa au kuwekewa masharti magumu
ambayo yanadumaza tasnia ya filamu ikiwemo kuuza haki zao, kama
nilivyoainisha katika makala yangu ya wiki iliyopita.
Kwa sasa imekuwa ni jambo
la kawaida kusikia kuwa mtayarishaji wa filamu kauza kazi zake kwa msambazaji,
jambo linaloshangaza sana hasa kwa nchi kama hii. Sababu za kushangaza ni nyingi; ya kwanza kubwa
ambayo ni kuwa majukumu ya msambazaji yanajulikana wazi kuwa yeye kazi yake
inapaswa kuishia kwenye kusambaza kazi husika tu, sasa anaponunua haki zote
ndipo inapotia shaka kubwa! Kwa nini anunue haki yako?
Ndiyo maana katika makala
yangu iliyopita niliishauri serikali kuingilia kati na kutoa elimu kwa wasanii
na watayarishaji wa filamu kwa kuwa imeonekana kuwa wengi hawana uelewa wa haki
zao, na wenye uelewa huo wanakwazwa na hali iliyopo sokoni kwa kuwa msambazaji
ndiye anayelimiliki soko na mwenye kauli ya mwisho katika kazi yoyote ya
filamu.
Kile alichotaka ufafanuzi
msomaji wangu kuhusu haki, ambazo nadhani si yeye tu bali kila mdau anapaswa
kuzielewa ili kama ataamua kuuza haki zake
(ingawa siyo busara) ajue anapoteza nini. Pia hii itaondoa malalamiko ya
kuibiwa kazi yanayoendelea kujitokeza. Kwani hata wale ambao kwa sasa
wanaojiona wajanja kwa kuuza haki zao kwa msambazaji na kuishia kupewa gari na
pesa zinazowasaidia kwa miezi michache, siku 'wakichuja' na thamani yao
kupungua nina imani kuwa wataingia kwenye mkumbo wa kulalamikia haki zao.
Kwa kawaida kazi za filamu
(kama ilivyo kwenye muziki) zina haki zipatazo
kumi ambazo zimetajwa katika kifungu na 9(1) cha Sheria ya Hakimiliki na
Hakishiriki ya 1999.
Haki hizo ni: (i) Kurudufu
kazi, (ii) Kusambaza kazi, (iii) Kukodisha, (iv) Kuonesha hadharani, (v)
Kutafsiri, (vi) Kubadili matumizi ya kazi, (vii) Kufanya maonesho ya hadhara,
(viii) Kutangaza kazi katika vyombo vya utangazaji, (ix) Kutangaza kwa njia
nyingine zozote, na (x)Kuingiza kazi nchini.
Kwa hiyo ukiangalia haki
hizo kama zilivyoainishwa utaona wazi kuwa
msambazaji kimsingi anahitaji haki mbili tu za mwanzo; yaani kurudufu kazi na
kuzisambaza basi. Kwani hizi haki nyingine zinamruhusu mwenye mali
(mtayarishaji) aendelee kufaidi matunda ya kazi yake kwa maisha yake yote na
kuwaachia warithi wake miaka hamsini mingine baada ya kifo chake.
Sasa inapotokea mtu akaamua
kuuza haki zake kwa msambazaji basi ajue kabisa kuwa anauza hata zile haki nane
zilizobakia ambazo kimsingi hawezi tena kuzitumia, kwa kuwa tayari atakuwa
ameshazipoteza.
Hivi ukiamua kuuza kazi zako
kwa maana ya kumuachia haki zote msambazaji, unatarajia kuwaachia nini warithi
wako, au unataka kubaki na ile sifa tu ya kuwa uliwahi kuwa na kazi? Lakini,
kwa nini uuze haki yako?
No comments:
Post a Comment