Ousmane Sembène, gwiji wa filamu barani Afrika
MAMBO ni tofauti kabisa,
kile kinachotokea Nigeria ni
tofauti na kile kinachotokea Afrika Kusini, Tasnia ya filamu ya Misri inaonekana
kuwa na kiwango cha mbali mno ukilinganisha na ile ya Kenya , na nikijaribu kufupisha
mambo, ni kweli soko la filamu barani Afrika ni soko tata kidogo.
Nchini Nigeria, nadhani kilichoanza
kutokea kinaweza kuwa mfano kwa hali ya soko hapo baadaye: Nollywood ilianza
kama aina fulani hivi ya watu mfano wa wazimu/mhemko wa video za bajeti ndogo, zilizotengenezwa
na wafanyabiashara zaidi kuliko watengenezaji wa filamu, na baadaye soko la ushindani
likaanza kudai ubora na ndipo tulipoweza kuona filamu nzuri sana zilizokuja
kuibuka baadaye kama ile ya Kunle Afolayan ya ‘The Figurine’.
Watayarishaji wa filamu Afrika
wameanza taratibu kuelewa haja ya kufanya vizuri zaidi. Nchi za
Afrika zinazozungumza Kifaransa (Francophone) bado zinaonekana kutembeza bakuli
hata kama filamu zinazotengenezwa katika nchi hizo
zinavutia, na za kisanii. Ni nani analipa gharama za kuziandaa (sanaa hizi
za hali ya juu) filamu hizi kutoka nchi makoloni ya Ufaransa? Ni nani anaziangalia?
Nadhani kwa sasa
watayarishaji wa filamu hizi wanaanza kufikiria kuhusu hadithi wanazotaka
kuelezea kwa watu wao, namna gani wataweza kuendelea kugharamia utengenezwaji wake,
na kadhalika. Nimeanza kuiona hatua hii ya Afrika kama ni kipindi cha ‘mwamko wa
kweli’. Sijui, au labda najaribu kuota ndoto ya mchana!
Tukiachana na filamu za
Francophone, hali ya tasnia ya filamu nchini kwa sasa ni ya kusisimua sana . Kuna aina
tofauti za watengenezaji wa filamu na aina mbalimbali za filamu zinazotengenezwa,
ambayo ni kubwa. Nimeanza kuona watu wengi zaidi wakifanya majaribio kwa
kutengeneza filamu fupi, filamu za makala (documentary) na filamu ndefu
(feature films).
Tofauti ya maadili ya
uzalishaji wa filamu, tasnia ya filamu nchini, ambayo ni kama majibu ya Watanzania
kwa tasnia iliyokuwa imeshika kasi nchini mwanzoni mwa miaka ya 2000 - tasnia ya
filamu ya Nigeria (Nollywood)
– imeanza kuwa mahiri lakini kama ilivyo kwa Nollywood,
tasnia ya filamu nchini bado inaendeshwa na wafanyabiashara.
Wafanyabiashara hao ndiyo
wenye kudhibiti mfumo mzima wa usambazaji wa filamu zetu. Wanalielewa soko
lao na wamekuja na mbinu zao za kukabiliana na uharamia wa kazi za sanaa na kwa
namna fulani, wamekuwa wakiwafanya watazamaji wao kuelewa kwamba wanahitaji
kununua kazi halisi – ambazo zinapatikana madukani kwao au kwa mawakala wao.
Wafanyabiashara hao wameigeuza
sekta ya filamu nchini kuwa kitu kingine kabisa. Hawataki kuturuhusu sisi kama wajasiriamali kuamua hatma na mwelekeo wetu wa
kwenda. Siku zote wanataka sisi tufuate nyayo tu!
Filamu hizi zinatengenezwa
kwa bajeti ya chini mno ingawa zimefanikiwa kwa kiasi chake kuliteka soko la
filamu katika nchi za Maziwa Makuu. Kwa upande mwingine, pia kuna filamu
za bajeti kubwa, filamu ambazo hutengenezwa na kupelekwa kwenye matamasha ya
filamu ya kimataifa – kama ‘Tumaini’ ya Beatrix Mugishagwe, ‘Chungu’
ya Vicensia Shule, ‘Chumo’ ya Jordan Riber na kadhalika.
Filamu hizi zinapaswa kuoneshwa
kwenye majumba ya sinema, zimetengenezwa kisinema zaidi, zimetengenezwa kwa
kuzingatia maadili ya utengenezaji filamu, lakini bado ukweli unabaki palepale
kuwa watengenezaji wa filamu hizi hawalielewi soko lao au kuwa na mifumo ya
usambazaji inayoweza kusaidia.
Nadhani soko filamu la kimataifa
siku zote linahitaji filamu mpya zenye kujali masimulizi kutoka Afrika, Asia, India , Korea , na Ulaya ya Mashariki au kwingineko.
Na hii imekuwa ikileta shida kidogo kati ya watazamaji wa ndani na wa nje,
kwani soko la kimataifa linataka ladha tofauti kidogo na ile iliyozoeleka ndani.
Ni mtengenezaji wa filamu wa Tanzania
ambaye anapaswa kuangalia namna nzuri ya kuzalisha filamu zeenye kuzingatia
maudhui mara kwa mara ili tuweze kuliteka soko la filamu ambalo litatusaidia
kupata watazamaji wetu wenyewe wa ndani watakaonunua na kutuunga mkono kwenye
filamu zetu.
Tunapaswa kuwa makini zaidi
kwa kuangalia mahitaji yetu halisi na si mahitaji ya wengine, kwani hatuwezi
kujenga sekta ya filamu kwa kulenga kutosheleza hitaji dogo la kimataifa, kwa
kujifurahisha na kutaka kutambuliwa kimataifa bila kwanza kuanzia nyumbani. Hii
imeleta shida kama ilivyokuwa kwa gwiji wa filamu barani Afrika, Ousmane
Sembene , wa Senegal
ambaye filamu zake zimesifiwa sana
Ulaya na Marekani lakini zimekosa mvuto kabisa nchini kwake na kwa mataifa ya
Afrika.
Mfano mwingine katika
filamu za Kiafrika ni filamu iliyoshinda tuzo za Oscar ya Tsotsi ambayo
pamoja na kukubalika nje ya nchi haikuweza kufanya vizuri na kufikia kiwango
kizuri cha mauzo ya tiketi nchini Afrika Kusini, ukilinganisha na filamu ya Jerusalema ya
Ralph Zimman, ambayo haikuwahi kupata tuzo ya Oscar lakini iliweza kufidia
gharama ya uzalishaji wake kwa kutumia soko lake la ndani ya nchi.
Filamu ya Kunle Afolyan wa Nigeria , ya Figurine ilifanikiwa kurudisha
nusu ya gharama ilizotumia za dola 400,000 kwa kutumia soko la ndani nchini Nigeria
katika wiki chache tu. Filamu za aina hii zinapoingizwa kwenye mfumo wa
DVD, mtengeneza filamu anakuwa katika wakati wa kutarajia kuingiza milioni chache,
kwa sababu Wanigeria wanapenda sinema zao na wana idadi kubwa ya watu ndani ya
nchi na hata ugenini ambayo hununua filamu.
Tatizo kubwa kwa nchi hizi
za Kiafrika bado lipo kwenye upatikanaji wa fedha na usambazaji, mambo haya
mawili ni changamoto kubwa sana kwa watengenezaji wa filamu Tanzania na Afrika
kwa ujumla.
Afrika Kusini imetuonesha
yote jinsi tume ya filamu imara ilivyo muhimu kwa afya ya sekta imara ya
filamu. Mamlaka yao ya filamu inajumuisha pamoja na upatikanaji wa fedha
na mafunzo na watayarishaji wa filamu nchini Afrika Kusini wana fursa nyingi wakiishukuru
tume na sekta ya filamu ambayo imefanya ushawishi mkubwa serikalini na ninaamini
pia sekta binafsi za kibenki zinaitazama sekta ya filamu kama muwekezaji pamoja
na uwezekano wa kutengeneza faida kubwa.
Unapoangalia filamu ndefu
na fupi zilizoshinda tuzo zinazotoka Ulaya, Marekani na Canada mara moja utafahamu jinsi
fedha nyingi zinavyopatikana kwa watengenezaji wa filamu katika nchi zao, hata kwa
nchi zenye tasnia isiyo mahiri.
Hivyo serikali bila shaka ina
jukumu na kufanya mara tu watakapotambua fursa kubwa ya kiuchumi kupitia sekta ya
filamu kwa faida ya nchi na Hazina pia.
Lakini bado tatizo lipo,
hata pale inapotokea fursa ya upatikanaji wa fedha za kutengenezea filamu kama
ilivyokuwa kwa Mfuko wa Utamaduni, mfano inapoelezwa kuwa ni asilimia chache tu
ya maombi yote yaliyotumwa yaliyobahatika kuchaguliwa, utatambua kuwa inaweza isiwe
wale waliopata wamepata kutokana na ujuzi wao kama watengenezaji wa filamu,
lakini imesababishwa na fursa ya upatikanaji wa fedha.
Lakini hebu pia
tujichunguze wenyewe na kipi tunaweza kufanya. Sisi pia, kama
watengenezaji wa filamu tuna jukumu la kufanya kujiunga na kusaidia vyama vya filamu
ili kusimamia na kutetea kila aina ya msaada tunaouhitaji. Serikali zetu hapa
Afrika zinatakiwa kubadilika kutoka kwenye usingizi wa pono na kuamka.
Tunahitaji kuhakikisha kama nchi tunajiamini na kutambua kuwa hatuhitaji tena
kuwa wafuata nyayo, bali tunatakiwa kuongoza pia harakati za kujikomboa. Ili kuongoza, tunapaswa kusoma machapisho mbalimbali ili
kujua njia walizopitia wengine katika kuelekea kwenye mafanikio ya kweli ya
tasnia ya filamu.
Baadhi ya wasomaji wazuri
ulimwenguni ni waandishi na watunzi wa vitabu, na pia watengenezaji wa filamu,
labda tunahitaji kuunda klabu ya filamu kwa ajili ya kubadilishana mawazo na
DVD chache tulizonazo ili tuanze kufurahia kuzungumza pamoja kuhusu filamu na mwelekeo
wa filamu kimataifa, hivyo kuwa sehemu ya udugu wa watengenezaji wa
filamu. Lakini tusisahau kuwa tunahitaji kusoma zaidi pia.
Kusoma kutatuwezesha kupata
taarifa ya mambo mengi - filamu, muundo na kadhalika. Tuna haja pia ya
kuwa na ufahamu zaidi wa dunia na upekee wa hadithi zetu. Tunahitaji kuwa
na imani katika mazingira au juu ya mchezo wetu.
No comments:
Post a Comment