Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein |
Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itaendelea kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Uongozi wa
Tamasha la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi Zanzibar (ZIFF) katika
azma yake ya kuijengea nguvu tasnia ya Filamu Nchini inayoonekana kusaidia
ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya Utalii.
Kauli hiyo imetolewa na Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohammed
Shein, katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, wakati akilizindua Tamasha la 18 la
Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi Zanzibar (ZIFF) hafla iliyofanyika kwenye
ukumbi wa Hoteli ya Double Tree By Hilton Shangani Mjini Zanzibar.
Wageni waalikwa wakimsikiliza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (hayupo pichani), wakati wa ufunguzi wa Tamashala |
Dk. Shein alisema
kwamba Tamasha la Nchi za jahazi limekuwa na mchango mkubwa katika kuitangaza
Zanzibar Kimataifa hali ambayo imetoa ushawishi kwa wageni na watalii wengi
kuamua kuvitembelea Visiwa vya Zanzibar kujionea mazingira na rasilmali
zilizopo.
Alisema kupitia Tasnia ya
filamu zinazotayarishwa na wasanii mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa Fani
hiyo chini ya Wataalamu wa Ziff wageni na watalii mbalimbali Duniani wamekuwa
wakivutiwa na fukwe pamoja na Utamaduni uliojaa ukarimu wa Watu wa Visiwa vya
Zanzibar.
Rais wa Zanzibar aliushauri
Uongozi wa ZIFF kuendelea kufanya juhudi zaidi za kuwashawishi wasanii wa
Kimataifa kuzitumia Fukwe na Tamaduni za Zanzibar katika kutengeneza Filamu
mbalimbali kwa lengo la kuitangaza zaidi Zanzibar Kimataifa.
“Zanzibar ni Visiwa vya
maumbile ya Utamaduni ya Ukarimu pamoja na fukwe za kuvutia mambo ambayo
yakitangazwa vyema wasanii wa Kimataifa wanaweza kushawishika kuyatumia katika
kutengeneza Filamu zao”. Alifafanua Dk. Shein.
Alifahamisha kwamba Tamasha
la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi, Tamasha la Iddi, Tamasha la
Mzanzibari pamoja na Sherehe za Mwaka Kogwa zinazofanyika Makunduchi ni
Mambo muhimu yanayopaswa kuimarishwa katika kukuza na kusimamia Utamaduni na
Historia ya Zanzibar na Watu wake.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amewapongeza Wasanii wa Maigizo pamoja na
Filamu Nchini kutokana na kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kuelimisha Jamii
sambamba na kuwapatia Burudani.
Alisema mbali ya Tasnia hiyo
kutoa ajira pana kwa kundi kubwa hasa Vijana Nchini lakini pia imepanua soko la
filam za nyumbani na kuleta unafuu kwa kila mtu kumudu kununua na kuangalia
kazi za wasanii wa hapa Nchini hali iliyopelekea kufikia asilimia 80 ya filamu
za Kiswahili zinazoangaliwa tofauti na miaka iliyopita nyuma.
Mapema Meneja wa Taasisi ya
Kimataifa inayosimamia kukuza vipaji vya wasanii katika ukanda wa Afrika
Mashariki (ZUKU), Bibi Maud Roger, aliahidi kwamba Taasisi yake itaendelea
kukuza vipaji vya wasanii kwa lengo la kufikia kiwango kinachokubalika
Kimataifa.
Bibi Roger alisema hatua hiyo
muhimu itaweza kuwajengea uwezo wa kiajira badala ya kusubiri kutegemea zile za
Serikali ambazo kwa sasa upo upungufu mkubwa hata katika Mataifa yaliyoendelea.
Meneja wa Taasisi hiyo ya
Zuku alifahamisha kwamba mpango maalum umeandaliwa na Uongozi wa Taasisi hiyo
baina ya miaka sita na kumi kwa kuwadhamini Vijana wapatao Kumi wanaopata
Mafunzo ya msingi kuweza kutengeneza Filamu zitazokubalika Kimataifa.
Wakitoa salamu zao kwenye
uzinduzi wa Tamasha hilo la 18 la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi Msanii
Gwiji Duniani kutoka Nchini Afrika Kusini, Leleti Kumalo, aliyeigiza
filamu maarufu ya Sarafina pamoja na msanii mkongwe wa nchi hiyo, Doroth Masuka,
wameelezea faraja yao kutokana na Serikali kupitia taasisi za kijamii
zilivyojikita katika kusaidia vijana kwenye fani ya sanaa.
Akimkaribisha mgeni rasmi
katika uzinduzi wa Tamasha la 18 la Ziff, Mwenyekiti wa Bodi ya Tamasha hilo,
Mahmoud Thabit Kombo, alisema Ziff itaendelea kushirikiana na wadau wote wa
ndani na nje ya nchi katika kuona Taasisi hiyo muhimu inazidi kuimarika.
Mahmoud Thabit Kombo alisema
uimarikaji huo utawapa nguvu na ari Vijana walioamua kujiajiri kupitia Tasnia
ya Filamu inayoonekana kupata umaarufu siku hadi siku hapa Duniani.
Uzinduzi wa Tamasha hilo la
18 la Kimataifa la Filam la Nchi za Jahazi Zanzibar (ZIFF) limekwenda
sambamba na siku yake lililoasisiwa rasmi Tarehe 18 Julai Mwaka 1997 likitimiza
umri wa miaka 18 sasa.
No comments:
Post a Comment