Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akiwa na muigizaji Anti Ezekiel, siku walipotembelea Marekani kutangaza utalii |
SEKTA ya Filamu nchini ikiendelezwa vizuri ni chanzo
kikubwa cha ajira kwa vijana, njia madhubuti ya kukuza utalii na uchumi wa
Taifa na wa wananchi kwa ujumla. Sekta ya Filamu
(kwa kuzingatia kuwa ni sehemu ya habari “media”) inapotumika vizuri, hufanya
kazi kama mhimili huru unaosimamia dola.
Katika nchi ambayo Bunge
linakosa meno dhidi ya udhaifu wa serikali, vyombo vya habari navyo vikawa
kimya, sekta hii inaweza kuwa nyenzo imara zaidi ya kuwasiliana na jamii na
kuieleza jinsi mambo yasivyo sawa. Lakini pia sekta hii ina nguvu kubwa
kiutamaduni, na chanzo kizuri cha kupashana taarifa.
Ni kwa kuwa hatuiangalii sekta hii kwa jicho la tatu. Kuna uchumi mkubwa sana ndani ya filamu. Ni vigumu kuuona au hata kuufikia kama soko lake linakuwa limebanwa. Lazima soko liwe jepesi na huria, wasanii watengeneze fedha na hapo ndipo itakuwa rahisi kuona manufaa mapana ya kiuchumi ndani ya jamii na taifa kwa jumla.
Ukiachana na faida nyepesi ambazo watoto wa shule za msingi hukaririshwa kwamba manufaa ya sanaa (filamu) ni kuelimisha na kuburudisha. Ni wakati mwafaka sasa itambulike kuwa filamu na sanaa kwa ujumla ni fedha, ni uchumi. Inatosha kuwa mkombozi wa bajeti za serikali na kutoa mchango wa thamani katika Pato la Ndani la Taifa (GDP) na jumla katika Pato la Taifa (GNP).
Laiti kila raia angejua thamani ya sanaa, angetamani kuona kila msanii mwenye kipaji na aliye na jitihada za kufanikiwa, basi anafanikiwa na kutengeneza fedha ili kurahisisha mirija mingi ya uchumi kupata mtiririko wenye afya. Sekta hii ni kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa sekta nyingine nyingi. Kwa hiyo, mafanikio ya sekta hii ni msisimko wa uchumi kwa taifa.
Biashara ya filamu ikifanikiwa na kupita kwenye mkondo wake barabara, husisimua uchumi wa sekta ya Utalii na hata Viwanda na Biashara. Huitangaza nchi na kuchagiza kivutio cha wageni kutembea kibiashara au kitalii, hivyo kuipa nguvu sekta ya Utalii. Wasanii wanapotajirika, huwezesha kupanuka kwa sekta ya Uwekezaji na kutanuka kwa sekta za Ajira na Elimu.
Hebu tafakari, ni kwa namna
gani sekta hii imeweza kuitangaza vyema Nigeria? Sekta ya filamu ya Nigeria (Nollywood),
imeweza kuitangaza nchi hiyo kwa kiasi gani? Unaweza tu kupata jibu la haraka
kwamba Taifa la Nigeria limetangazika kwa kiwango ambacho siyo cha kawaida wala
cha chini, hadi kufikia kuonekana ni taifa kubwa.
Kama filamu za Nigeria zimeweza kuteka soko la Afrika na dunia kwa kiasi fulani, haiwezi kukufanya uumize kichwa sana kujua kwamba taifa hilo, limeweza kupata matangazo mengi kupitia sanaa ya maigizo, na zaidi kuvuta watalii kutoka pande mbalimbali za dunia.
Kama filamu za Nigeria zimeweza kuteka soko la Afrika na dunia kwa kiasi fulani, haiwezi kukufanya uumize kichwa sana kujua kwamba taifa hilo, limeweza kupata matangazo mengi kupitia sanaa ya maigizo, na zaidi kuvuta watalii kutoka pande mbalimbali za dunia.
Tanzania
tumebarikiwa kuwa na mandhari mbalimbali za kupendeza, hali nzuri ya hewa na
maeneo mbalimbali yanayoifanya nchi kuwa eneo bora kwa ajili ya biashara ya
filamu na vipindi vya televisheni. Hivyo, ukuaji wa sekta ya filamu na burudani
Tanzania inaweza kuwa na matokeo mazuri kwenye mapato ya utalii.
Sekta
ya filamu kama itathaminiwa inaweza kuzalisha asilimia kubwa ya mapato kwenye
sekta ya utalii. Pia tunapaswa kuelewa kuwa hata ongezeko la watengeneza filamu
wa kimataifa kuja Tanzania na kuitumia kama eneo maalum la upigaji picha za
video, litaongeza nafasi kubwa ya kukua kwa utalii katika nchi.
Serikali
pia inapaswa kuutambua uwezo wa mchango wa sekta ya filamu na kutoa motisha kwa
lengo la kuvutia uzalishaji wa kimataifa ili kusaidia kuongeza ajira, mapato na
kuhimiza utalii.
Nchi hii
kwa sasa inasumbuliwa na ukosefu wa ajira, sekta ya filamu inapigania kukuza
ajira na kuwa na faida kubwa kwa sekta ya utalii ambayo hatimaye itachangia
ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira. Biashara katika sekta ya utalii pia inaweza kushuka zaidi
katika msimu fulani, lakini sekta ya filamu na burudani ni muhimu kupambana na hali
hii.
Hali ya
hewa ya kupendeza ya nchi yetu kwa mwaka mzima kwenye baadhi ya maeneo, inaweza
kuwa kivutio kwa sinema zote maalum zinazohitaji hali fulani ya hewa, kama
maeneo hayo yatatangazwa vyema. Na hakuna njia bora ya kuyatangaza maeneo hayo zaidi
ya sekta ya filamu.
Serikali
inapaswa kuwa na mpango na dhamira ya kufanya kazi na watengeneza filamu wa
ndani ili kukidhi viwango vya kimataifa. Iandae warsha na semina mara kwa
mara zitakazowasaidia watengeneza filamu wa ndani kwenda na wakati na maeneo
mengine ya dunia. Pia tuangalie namna tutakavyoweza kuikuza lugha ya Kiswahili, ambayo inatakiwa ipewe
nafasi kubwa, kwani ni lugha inayozungumzwa na watu wengi zaidi barani
Afrika.
Ili
kufanikisha hili, serikali iangalie uwezekano wa kuziunganisha pamoja Bodi ya
Filamu na Michezo ya Kuigiza (TFCB) na Tume ya Filamu Tanzania (TFC), ili kipatikane
chombo kimoja chenye nguvu zaidi, Mamlaka ya Filamu Tanzania (Tanzania Film Authority),
kwa kujumuisha shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na TFC na TFCB, na hivyo
kuleta ufanisi zaidi.
Bodi
ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ndiyo yenye jukumu la kuisimamia sekta ya
filamu kwa mujibu wa Sheria
ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Na. 4 ya 1976 iliyotungwa na Bunge, ipo chini ya Idara ya
Maendeleo ya Utamaduni katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; na
Tume ya Filamu Tanzania (TFC), iliyoundwa kufuatia Sheria ya Bodi ya Utalii Tanzania,
CAP 364 ya 1962 iliyofanyiwa marekebisho kwa Sheria Na. 18 ya 1992, inayofanya kazi chini ya
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), ipo katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kwa
sasa, japo haionekani, lakini upo muingiliano wa kimamlaka kati ya vyombo hivi
viwili. Naamini lengo la vyombo vyote ni jema, kwani tunahitaji kuwaonesha watengenezaji
wote wa filamu duniani kote fursa za uzuri wa asili. Kikiwepo chombo madhubuti,
watengeneza filamu wa ndani wataweza kuandikishwa katika kanzi data (data base)
ili kuleta urahisi kwa watengenezaji wote wa filamu kuwa chini ya mwavuli
mmoja. Hii ni pamoja na mawakala wa filamu, vipaji vya ndani nk.
Ninazo
taarifa kuwa TFC
kwa sasa inafanya kila iwezalo kuifanya Tanzania kuwa mwanachama wa Chama cha Kimataifa
cha Tume za Filamu (Association of Film Commissions International “AFCI”),
jambo ambalo si baya. Lakini ni jambo linaloweza kuifanya TFC kujiona bora
zaidi ya TFCB kwa kuwa TFCB haitokuwa na uwakilishi ndani ya AFCI.
Tanzania
ni moja ya sehemu bora kabisa ambazo mtengeneza filamu atafurahia kutengeneza
filamu yake, historia, utamaduni na wanyamapori, hali ya hewa nzuri na watu wakarimu
ambao wako tayari kumkaribisha mgeni katika mtazamo wa Kitanzania.
Katika
nchi hii kuna maeneo bora ya upigaji picha, kuanzia Tanzania Bara hadi Zanzibar,
kuanzia kwenye mlima mrefu hadi kwenye maziwa yenye kina kirefu kabisa katika
bara la Afrika. Tanzania ni nchi ya maajabu na vivutio: mlima mrefu
Afrika, Mlima Kilimanjaro, mbuga bora yenye wanyama wa kuvutia duniani ya
Serengeti, yenye stori ya wanyama wanaohama kila mwaka na kurejea.
Nchi hii ina mbuga kubwa na bora duniani, Selous. Mbuga
iliyopewa jina la Muingereza, Frederick Courtney Selous – mhifadhi, muwindaji,
mtalii na mtunzi, ambaye vitabu vyake kuhusu Afrika vimeuzika sana Uingereza.
Pia tuna bonde kubwa Afrika lililotokana na volcano,
Ngorongoro Crater, eneo maarufu duniani, linalofuga wanyama pasipo kuwekwa
fensi (unfenced zoo). Sehemu nzuri ya kuvua samaki na bandari katika Afrika,
labda duniani na mamia ya maili za ufukwe wa Bahari ya Hindi na maziwa yote makubwa, Ziwa Viktoria, Ziwa Tanganyika, na Ziwa Nyasa (hakuna
nchi nyingine zaidi yetu).
Zanzibar pia ni moja ya visiwa vyenye historia ya
kutukuka, iliyokusanya wahamiaji. Zanzibar imeundwa na visiwa vya Unguja
na Pemba, na visiwa vingine vingi vidogo.
Maeneo mengine ya kuvutia ni Amani Forest
Nature Reserve, Mapango ya Amboni,
Bagamoyo,
Isimila Stone
Age Site, Maporomoko ya Kalambo,
Michoro katika mapango ya Kondoa Irangi,
Ziwa Natron, Lushoto,
Mbozi Meteorite,
Hifadhi ya Mkomazi, Mwanza, Ol Donyo
Lengai, Olduvai Gorge,
Mfumo wa Mto Rufiji,
Ukanda wa Pwani ya Waswahili,
Tarangire,
Tendanguru,
Ujiji, na Milima ya Usambara.
Lakini kumekuwepo pia mambo madogo ambayo serikali
inapaswa kuyaangalia upya ili kuvutia wageni kuja kupiga picha za filamu
nchini. Wageni wanalalamikia tozo kubwa wanazotozwa kulinganisha na nchi kama Kenya.
Tozo hizi huhusiana na kupata kibali, kulipia vifaa kama ushuru wa forodha, kibali
cha kufanyia kazi/visa, nk.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment