Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo |
INGAWA nchini Tanzania
televisheni imekuwapo tangu mwaka 1973 (Zanzibar), Tanzania Bara televisheni
imeanza mwanzoni mwa miaka ya 1990. Hadi 1996 kulikuwa na vituo vitatu tu vya
televisheni: CTN, DTV na ITV. Kupingwa kwa televisheni Tanzania Bara na kuwapo
kwa Radio moja (RTD) tokea miaka ya baada ya uhuru ulikuwa mkakati wa serikali
kujenga utamaduni wa Umoja, Udugu na Utanzania.
Enzi hizo (nilikuwa bado
mdogo) watu walikuwa wanakwenda kwenye majumba maalum ya sinema kuangalia sinema kwa wakati maalum na
masharti maalum. Majumba haya yalikuwepo katika
kila mji-makao makuu ya mkoa na baadaye katika wilaya, na idadi yake ilitegemea
ukubwa wa mji.
Dar es Salaam kulikuwa na
majumba kama Drive Inn (sasa kuna Ubalozi wa Marekani – hili lilikuwa ni
eneo la watu matajiri zaidi, waliruhusiwa kuingia na magari yao kwenye ukumbi,
watu wakikaa ndani ya magari na kuangalia filamu huku wakiburudika na vinywaji), Odeon (sasa kuna DTV/Channel Ten), New Chox (sasa kuna Continental Hotel), Empire (nadhani kuna makao makuu ya NMB), Avalon (lilianza kutumika na madhehebu ya
kilokole kufanyia ibada zao, na sasa ni eneo la
ofisi mbalimbali), Empress (zipo ofisi za BMT), na Cameo (sina uhakika linatumika
kufanya nini kwa sasa).
Baadaye likaibuka jumba la
Starlight (kuna hoteli ya Starlight), lililokuwa na uwezo wa kuingiza
watu wengi sana. Na walalahoi pia walikuwa
na mahali pa kwenda kutazama sinema, Amana Social Hall, eneo la Ilala. Nakumbuka pale Drive Inn, ilikuwa kama huna pesa ya
kuingilia, basi unaangalia sinema bubu – kwani mnalazimika kukaa nje na
kutazama sinema kwa mbali lakini hamsikii sauti.
Tanga kulikuwa na Majestic,
Novelty, Regal na Tanga Cinema. Mwanza kulikuwa
na Liberty na Tivoli, Mji Kasoro Bahari kulikuwa na Shani na baadaye ikaja
Sapna. Arusha ilikuwepo Metropolitan. Vivyo
hivyo na miji mingine.
Enzi hizo, nakumbuka
kulikuwa na mabingwa wa kusimulia sinema hata kama mliiona wote, basi mtaanza
kusimuliana tena na tena, hata kama kimombo hukijui, utasimulia yote waliyokuwa
wanasema kwenye hiyo sinema. Wakati wa sinema yenyewe watu watapiga makelele, “angalia
nyuma wewe… Jamaa anataka kukuua!” Au pale Drive In kwa nje, jamaa anakusimulia
utadhani anasikia vile!
Ilikuwa raha mstarehe,
enzi hizo tukiwa wadogo basi ikatokea kama kuna sinema maarufu mjini wenzako
wanaweza kukusimulia mwanzo hadi mwisho bila kukosea (na kuongezea chumvi
kidogo) ingawa hawajaiona ila wamesimuliwa. Ama kweli siku hazigandi!
Kwa sasa ukiwaona watu
(hasa Dar es Salaam) wakiingia kuangalia sinema pale Century Cinemax–Mlimani
City, Cineplex–Quality Centre, au Century Cinemax–Oyster Bay, unaweza kudhani kuwa huu ni utamaduni mpya. Kumbe kabla
na baada ya Uhuru kwenda Sinema ilikuwa ni jambo la kawaida na kitu kilichoweza
kukuletea mapenzi na heshima kubwa kwa familia yako, rafiki au mpenzi wako, kwa
wakati ule.
Hivi sasa katika ulimwengu huu wa utandawazi na soko huria,
hasa baada ya ujio wa televisheni nchini, majumba ya sinema yamefungwa kutokana
na kukosa wateja – sijui nani kasema mkiwa na televisheni nyumbani basi majumba
ya sinema si muhimu? Badala yake majumba ya sinema yamehamia kwenye nyumba zetu
na vichochoroni kulikochipuka mabanda ya kuonesha video kama uyoga ambayo siyo
rasmi.
Mabanda ya video (maaruf vibanda-hasara) yamechukua
nafasi ya majumba rasmi ya sinema yaliyofungwa au kugeuzwa kuwa ya kufanyia
huduma nyingine za kijamii. Mabanda haya mengi yamejengwa kwa mabati, mbao au
mifuko ya sandarusi na kukosa mvuto, yamekuwa mbadala wa kuonesha sinema
zikiwemo zile chafu maaruf kama ‘Pilau’, ‘Kachumbari’, ‘Kuchikuchi Hotae’,
‘Yale mambo yetu’, ‘Picha la ukweli’, ‘Ubwabwa’ na majina mengine ambayo kwa
mtu wa kawaida si rahisi kujua maana yake.
Mabanda haya (mengi hayastahili kuitwa Kumbi za video) yana
ukubwa tofauti kutegemeana na sehemu lilipo, lakini yenye kuingiza watu 20 hadi
50 kwa wakati mmoja wanaojazana kuangalia sinema. Hutoza kiasi cha shilingi 200
hadi 500 kwa onesho. Baadhi huonesha hadi maonesho 10 kwa siku.
Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 60 ya wakazi wanaoishi
mijini na vijijini wanapenda kuangalia filamu kwenye kumbi za maonesho –
ikiwemo mabanda ya video – ingawa wengi wao, wanawakatishwa tamaa na kutokuwepo
kwa miundombinu sahihi. Takwimu ya waangaliaji sinema inatofautishwa kulingana na umri: Asilimia 50 ya
watazamaji hawa ni wenye umri kati ya miaka 6-24, asilimia 30 ni wenye umri
kati ya miaka 25-34, asilimia 15 ni watu wenye umri wa miaka 35-49 na asilimia
5 tu ya watu wenye umri zaidi ya miaka 50 ndiyo hupenda kuangalia filamu hizi.
Dar
es Salaam ndiyo mji unaoongoza kuwa na idadi kubwa ya watazamaji wa filamu
ikichukua asilimia 35. Hata hivyo, vijana wadogo ndiyo wenye mazoea ya kwenda
kwenye kumbi za video kuangalia sinema.
Kumbi za video zinawavutia vijana wengi hasa wa vijijini.
Filamu za mapigano na mara nyingine hata za ngono (Blue films) zinaoneshwa kwa
viingilio vya bei rahisi kwenye kumbi/mabanda yaliyopo sehemu za vijiweni
karibia kila kitongoji.
Mwaka 2010 Serikali ilipiga marufuku uoneshaji wa sinema
kwenye mabanda ambayo hayajakidhi vigezo vinavyotakiwa kisheria. Kwa mujibu wa
Kanuni za Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza za Mwaka 2011, Sehemu ya V,
kanuni imetamka wazi kabisa masharti ambayo yanatakiwa kutekelezwa ili mtu
aweze kuonesha na kujenga mahali pa kuonesha sinema.
Kwa kuwa kuna uhitaji mkubwa wa watu kutaka kuangalia
sinema (na hapa ndipo panapoonekana umuhimu wa kurejeshwa kwa vituo vya kijamii
“Community Centres” ili kuwezesha wananchi wote nchini kujumuika pamoja na kuweza
kupata habari), hali hii inawafanya wamiliki wa kumbi/mabanda ya video
kufanya shughuli zao kwa njia za wizi, wakiwa hawana leseni na wala hawaingizi
pato lolote kwa Taifa. Wazazi wengi wanakerwa na jambo hili na kuilalamikia
Serikali kwa kushindwa kuyafunga mabanda haya.
Hali hii imewafanya baadhi ya mgambo wa halmashauri na
askari kuyatumia mabanda haya kama sehemu ya kujipatia kipato, kwani huwakamata
waoneshaji video na kuwatisha ili wapatiwe “kitu kidogo”. Kumekuwepo uadui kati
ya waendeshaji wa mabanda haya na serikali kwa upande mmoja, na waendeshaji wa
mabanda na jamii kwa upande mwingine.
Tupende tusipende, mabanda haya yapo na yataendelea
kuwepo, hakuna nanma ya kuyaondosha kabisa. Dawa si kuyapiga marufuku, bali
kutafuta njia nzuri ya kuyarasimisha (kwa yale yatakayokidhi vigezo vinavyokubalika),
ili yaweze kuchangia pato la Taifa, na pia yatumike kama mtandao wa usambazaji
(maonesho ya sinema) kabla hazijatolewa rasmi kwa matumizi ya nyumbani.
Kwa wenzetu, usambazaji filamu huanzia kwenye “Box Office”
– uoneshaji wa sinema ndani ya kumbi za sinema – na baadaye hurushwa kwenye
vituo vya televisheni za kulipia, kwenye mtandao wa internet, kisha katika
televisheni za umma, na hatimaye kutolewa kama bidhaa rasmi (DVDs) kwa matumizi
ya nyumbani.
Ili kupitia mchakato hapo juu Serikali (kupitia Bodi ya
Filamu) inaangalia namna ya kuyarasimisha mabanda haya – yatakayokuwa
yameboreshwa na kukidhi vigezo – ili yatumike kama “box office” zetu (sehemu ya
maonesho/uzinduzi wa sinema). Hii itaongeza kipato kwa wasanii wetu, na hata
kupunguza uchafu huu tunaoushuhudia sasa wa mabanda kutumika kama sehemu ya
maficho ya vibaka na upotoshaji badala ya kuelimisha.
Kwa kuwatumia Maafisa Utamaduni wa Wilaya na Manispaa, kupitia
Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
tutaweza kupata takwimu sahihi za idadi ya mabanda, kuyakagua na kuyapa leseni
yale yote yatakayokidhi vigezo, jambo litakalosaidia pia kuongeza ajira, pato
la wasanii na Taifa, na hata kupunguza uhalifu, kwani yatatumika kisheria
kuliko ilivyo sasa.
Hatuna tena muda wa kulalamikia mabanda bali tuchukue hatua
stahiki, mahitaji ya kumbi za video yameonekana si kwa mijini tu hata vijijini,
licha ya kuwepo kwa utandawazi lakini kuna baadhi ya jamii na hasa za vijijini
bado hazipati taarifa sahihi za mambo mbalimbali yanayoendelea katika ulimwengu
huu. Hii inatokana na njia zinazotumika kutowafikia wengi kama inavyodhaniwa na
hivyo bado kuna haja ya kurasimishwa na kurejeshwa vituo vya kupashana
habari kama ilivyokuwa zamani.
Miaka ya nyuma, nakumbuka kulikuwa na siku na sehemu maalum,
hasa vijijini, watu walikuwa wanakutana na kuangalia sinema mbalimbali ambazo
zilikuwa maalum kwa kufikisha ujumbe fulani kwa jamii. Lakini hayo siku hizi
hakuna, hivyo, nashukuru kwa Bodi ya Filamu kuliona hili na kuangalia namna nzuri
ya kurudisha burudani hizi.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment