Mkongwe, Dorothy Masuka, akiwa jukwaani katika shoo yake usiku wa Julai 19, katika tamasha la 18, la ZIFF 2015,Ngome Kongwe upande wa Mambo Club |
MATAMASHA
ya filamu duniani ni sehemu nzuri zaidi kwa ajili ya kutengeneza mtandao na
kumfanya mtengenezaji wa filamu au msanii kujulikana si tu katika kanda husika
bali kimataifa.
Mkurugenzi wa ZIFF, Prof. Martin Mhando |
Ukibahatika
kuwa mmoja wa washindi wa tuzo, unakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kujitangaza
na hata kupata msaada wa kipesa (funds) kwa ajili ya kutengeneza sinema bora
zaidi unayohitaji siku zote kwa kuwa utaingia kwenye orodha ya watu
wanaoaminiwa, na hapo ndo’ washindi hujua kuwa wapo katika mstari sahihi.
Hivi
karibuni Tamasha la 18 la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi Zanzibar (ZIFF)
limemalizika katika uwanja wa Mji Mkongwe Zanzibar. Wasanii kutoka ndani na nje
ya Tanzania na pamoja na watalii wamejumuika kwa ajili ya tamasha hilo.
Tamasha
hilo lenye kaulimbiu "Mawimbi na Matumaini" limefanyika kwa siku
tisa, ambapo filamu 99 zilizotengenezwa na waandaaji 65 kutoka nchi 35 zimeoneshwa.
Hatimaye, makundi matano ya waamuzi yakatoa tuzo 22 kwa filamu bora.
Tamasha
hilo lilifunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kwa
niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk.
Ali Mohammed Shein.
Kwenye
ufunguzi huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilibainisha kuwa itaendelea
kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Uongozi wa Tamasha la Kimataifa la
Filamu la Nchi za Jahazi Zanzibar (ZIFF) katika azma yake ya kuijengea
nguvu tasnia ya Filamu Nchini inayoonekana kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia
sekta ya Utalii.
Hayo
yalikuwemo katika Hotuba ya Dk. Ali Mohammed Shein iliyosomwa kwa niaba yake na
Balozi Seif Ali Iddi, wakati akilizindua Tamasha la 18 la Kimataifa la Filamu
la Nchi za Jahazi Zanzibar (ZIFF) hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya
Double Tree By Hilton Shangani Mjini Zanzibar.
Dk. Shein alisema kwamba Tamasha la Nchi za jahazi
limekuwa na mchango mkubwa katika kuitangaza Zanzibar Kimataifa hali ambayo
imetoa ushawishi kwa wageni na watalii wengi kuamua kuvitembelea Visiwa vya
Zanzibar kujionea mazingira na rasilmali zilizopo.
Alisema kupitia Tasnia ya filamu zinazotayarishwa na wasanii
mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa Fani hiyo chini ya Wataalam wa Ziff
wageni na watalii mbalimbali Duniani wamekuwa wakivutiwa na fukwe pamoja na
Utamaduni uliojaa ukarimu wa Watu wa Visiwa vya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi wa ZIFF kuendelea kufanya
juhudi zaidi za kuwashawishi wasanii wa Kimataifa kuzitumia Fukwe na Tamaduni
za Zanzibar katika kutengeneza Filamu mbalimbali kwa lengo la kuitangaza zaidi
Zanzibar Kimataifa.
“Zanzibar ni Visiwa vya maumbile ya Utamaduni ya Ukarimu pamoja
na fukwe za kuvutia mambo ambayo yakitangazwa vyema wasanii wa Kimataifa
wanaweza kushawishika kuyatumia katika kutengeneza Filamu zao”. Alifafanua Dk.
Shein.
Alifahamisha kwamba Tamasha la Kimataifa la Filamu la Nchi za
Jahazi, Tamasha la Iddi, Tamasha la Mzanzibari pamoja na Sherehe za Mwaka
Kogwa zinazofanyika Makunduchi ni Mambo muhimu yanayopaswa kuimarishwa katika
kukuza na kusimamia Utamaduni na Historia ya Zanzibar na Watu wake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
amewapongeza Wasanii wa Maigizo pamoja na Filamu Nchini kutokana na kazi kubwa
wanayoendelea kuifanya ya kuelimisha Jamii sambamba na kuwapatia Burudani.
Alisema mbali ya Tasnia hiyo kutoa ajira pana kwa kundi kubwa
hasa Vijana Nchini lakini pia imepanua soko la filam za nyumbani na kuleta
unafuu kwa kila mtu kumudu kununua na kuangalia kazi za wasanii wa hapa Nchini
hali iliyopelekea kufikia asilimia 80 ya filamu za Kiswahili zinazoangaliwa
tofauti na miaka iliyopita nyuma.
Mratibu
wa tamasha hilo, Prof. Martin Mhando, amesema ameitumia fursa iliyopo kuhimiza
maendeleo ya tamasha hilo.
“Tamasha
la filamu la Kimataifa la Zanzibar ni shughuli muhimu katika historia ya
Zanzibar, ambayo haiwezi kusahauliwa. Kaulimbiu ya mwaka huu ni Mawimbi na
Matumaini. Kama tunavyojua, tunaishi kisiwani Zanzibar, tunakabiliana na
mawimbi yanayotoka kwa pande mbalimbali.
“Natumai
kuhimiza maendeleo ya tamasha ya filamu na nchi yetu kupitia mawimbi ya tamasha
la ZIFF. Leo sote tunavaa mavazi meupe, ambayo yanamaanisha nchi yetu ni nchi
yenye amani na utulivu zaidi barani Afrika na kote duniani. Karibuni ZIFF,
karibuni Zanzibar, asanteni.”
Mwaka huu
siku ya ufunguzi wa tamasha la ZIFF iligongana na sikukuu ya IDD, kwenye hotuba
yake, mwenyekiti wa tamasha la ZIFF, Mahmoud Kombo alisema, kukutana kwa
shughuli hizo mbili kunawavutia watalii wengi zaidi, ambako kuna maana kubwa
kwa ustawi wa utamaduni na uchumi wa Tanzania.
“Leo ni
Julai 18, na ZIFF imetimiza miaka kumi na nane. Na leo pia tunasherehekea
sikukuu ya Idd hapa Zanzibar. Tamasha la ZIFF kila mwaka linawavutia watalii
zaidi ya elfu nne kutoka nchi mbalimbali duniani, leo pia ni sikukuu ya Idd
hapa Zanzibar, nina imani kuwa mwaka huu watalii wengi zaidi watakuja hapa.
“Hivyo
ZIFF inaweza kustawisha utamaduni na uchumi wa nchi yetu, na kuwafanya marafiki
wengi zaidi kufahamu nchi na utamaduni wetu. ZIFF imepita miaka 18, ambayo
inawafanya marafiki wengi kuifahamu Zanzibar yenye mandhari safi na kuipenda.
Nafikiri nyote mtaona uzuri wa Zanzibar”
Baadhi ya
nchi zilizowasilisha filamu kwenye mashindano ni Tanzania, Kenya, Afrika
Kusini, Marekani, Ujerumani na Ufaransa. Mratibu wa tamasha hilo, Prof. Mhando,
amesema filamu zinazohusiana na kupambana na ubaguzi wa rangi zimepewa
kipaumbele katika tamasha hilo. Filamu ya Selma kutoka Marekani, Sarafina
kutoka Afrika Kusini, Samaki Mchangani kutoka Tanzania na Septemba kutoka Kenya
zote zinahusu mada hiyo.
Kati ya
filamu zilizoshiriki kwenye tamasha hilo, 16 zimetengenezwa nchini Tanzania.
Prof. Mhando amefurahia kuona tamasha hilo linastawisha soko la filamu la
Tanzania, kuhimiza maendeleo ya utengenezaji wa filamu Tanzania, na kutoa fursa
nyingi zaidi kwa Watanzania kutazama filamu kutoka nchi mbalimbali duniani.
Katika
ufunguzi, watalii wengi kutoka nchi mbalimbali duniani walikuja hapa, Bibi Rose
kutoka Uholanzi ni mmojawapo ambaye alikuwepo siku ya ufunguzi.
“Naitwa
Rose, natoka Uholanzi. Leo tamasha hili linafunguliwa. Tamasha hili linavutia
sana, kwa sababu linahusu utamaduni na filamu, hapa kuna filamu, muziki na
sanaa kutoka sehemu mablimbali duniani. Naona kuna umuhimu mkubwa wa kufanya
tamasha la filamu ambalo linawashirikisha watu wengi kutoka nchi mbalimbali, na
wengi wao wamekuja kwa ajili ya tamasha hilo.
“Tamasha
la filamu linaunganisha marafiki kutoka Afrika na sehemu nyingine duniani.
Nilikuwa nadhani Afrika ni sehemu maskini, lakini leo mawazo yangu
yamebadilika. Naona tamasha la filamu litawapatia watu wengi ufahamu mpya
kuhusu Tanzania.”
Katika
tamasha hilo, filamu za Tanzania zilizoshinda ni kama ifuatavyo: Mr. Kadamanja
– Chaguo la Watu (People’s Choice Award); Samaki Mchangani – Sinema yenye Sauti
Bora (Best Film in Sound); Daddy’s Wedding – Mpiga Picha Bora (Best
Cinematography); na Kutakapokucha – Filamu Bora (Best Feature Film).
Wasanii
wa Tanzania walioshinda ni Jokate Mwegelo – Muigizaji Bora wa Kike (Best
Actress) kupitia filamu ya Mikono Salama; na Marehemu Adam Kuambiana –
Muigizaji Bora wa Kiume (Best Actor) kupitia filamu ya Mr.Kadamanja. Pia Tuzo
ya Muongozaji Bora (Best Director) imekwenda kwa Honeymoon Mohammed kupitia
filamu ya Daddy’s Wedding.
No comments:
Post a Comment