Msanii Aunt Ezekiel akiwa kwenye pozi
Miriam Jolwa (Kabula) na Jacky Pentezel
HAKUNA ubishi kwamba, miongoni mwa fani mbalimbali za sanaa katika jamii ya Kitanzania kwa zama hizi, ni sanaa ya maigizo, hasa filamu ndiyo inayoonekana kutesa zaidi. Pamoja na sanaa ya filamu, pia sanaa ya muziki, hasa wa kizazi kipya imeonekana kutingisha miongoni mwa vijana.
Sanaa ya filamu hapa nchini imetokea kujitwalia wapenzi kibao kiasi cha kuwa kimbilio la vijana wengi, wake kwa waume, watoto kwa wakubwa na hivyo kuonekana kuwa mkombozi wa ajira kwa vijana hao huku wengi wakiwapongeza waigizaji wake kuwa, wameweza kuipa jamii ya Kitanzania kitu kipya.
Siyo siri, kwa nchi za Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, uchunguzi umeonesha kuwa ni Tanzania iliyo mstari wa mbele katika nyanja ya tasnia ya filamu ambayo imeonekana kuwa na mchango mkubwa kwa jamii yetu, licha ya kuwepo mapungufu mengi kiutendaji.
Filamu (Movie au Motion pictures) ni mfululizo wa picha zinazoonesha mwendo wa watu au vitu na kuonekana mbele ya watazamaji kwenye skrini. Ni aina ya mawasiliano yanayotumiwa kutolea hadithi au kuwaelezea watu kuhusiana na kujifunza fikra au mitazamo mipya katika jamii. Watu katika kila pembe ya dunia huwa wanaangalia filamu ambazo zinaelezea hadithi fulani ikiwa kama kiburudisho, au njia mojawapo ya upenzi.
Katika duru nyingi za kimataifa, nchi yetu ilipata kusifiwa kwa jitihada zake za kushughulikia ukuzaji wa utamaduni, filamu zikiwemo. Hata hivyo, kwa hali ilivyo sasa na kama hatua za dhati hazitachukuliwa, kazi iliyofanywa miaka ya nyuma, hasa mara baada ya uhuru hadi miaka ya 90, itapotea na tutajikuta tukiwa taifa lenye raia wasio na mwelekeo, wasiojifahamu au heshima mbele ya mataifa mengine.
Hivi karibuni kuliitishwa mkutano wa wasanii na wadau wa filamu kwenye viwanja vya Leaders Club na shirikisho la filamu Tanzania, ambapo pamoja na mambo mengi yaliyokemewa ni suala la mahusiano ya kingono miongoni mwa wasanii, jambo ambalo limekuwa likifanywa waziwazi huku likipamba vichwa vya habari vya magazeti.
Hemedi Suleiman na Jacky Pentezel
Uwepo wa tungo za kimapenzi katika kazi nyingi za sanaa (filamu na muziki) ni changamoto kubwa katika utamaduni wetu kwani imezifanya kazi za wasanii kuwa za kusisimua na kuamsha utendaji ngono miongoni mwa wanajamii na kuwaacha wao wakiwa waathirika wakubwa. Wasanii wanapaswa wajiulize, kwa nini filamu na nyimbo zetu nyingi ni za mapenzi peke yake au zisizo na asili yetu bali zilizonakili vitendo na maudhui ya jamii za nje?
Cha ajabu wasanii wamekuwa mstari wa mbele kutoa elimu dhidi ya Ukimwi kwa jamii na kujisahau wao binafsi kwamba wako katika mazingira hatari ya kupata maambukizi.
Ieleweke kuwa wasanii wa Kitanzania ni mojawapo ya kada ya wasanii ambao wanatajwa kuwa hatarini kuambukizana virusi vya Ukimwi kutokana na umaarufu walionao na kujikuta wakishawishika kuingia katika vitendo mbalimbali vya hatari kwa afya zao hasa vya ngono.
Imekuwa ikielezwa kuwa umaarufu, ushawishi na kutojitambua miongoni mwao kimekuwa chanzo kikubwa cha wao kuwa hatarini kupata maambukizi hayo. Kutojitambua huwafanya wawe hatarini kuathiriwa na ugonjwa wa Ukimwi kwani hufuatwa na kundi la watu na mara nyingi kujikuta wakishawishiwa kufanya ngono katika mazingira yasiyo salama.
Kada ya wasanii imekuwa ikiathiriwa sana na ugonjwa huu toka umegunduliwa kwani katika nchi zilizoendelea kumekuwa na taarifa za vifo vya wasanii wengi vinavyotokana na Ukimwi, ambapo kutumia vibaya umaarufu kumekuwa kukichanganywa na matumizi ya vilevi.
Kada ya wasanii imekuwa ikiathiriwa sana na ugonjwa huu toka umegunduliwa kwani katika nchi zilizoendelea kumekuwa na taarifa za vifo vya wasanii wengi vinavyotokana na Ukimwi, ambapo kutumia vibaya umaarufu kumekuwa kukichanganywa na matumizi ya vilevi.
Yote haya ni sababu ya kupotea kwa utamaduni wetu kwani utamaduni ndiyo “kidhibiti mwendo” kinachoongoza mwenendo na tabia za watu katika jamii. Ndiyo msingi wa maisha ya mtu binafsi. Humuwezesha kujitambua, kuwa na mwelekeo na kujichagulia falsafa sahihi ya maisha yake. Ndiyo msingi wa maendeleo na ubunifu katika jamii. Maendeleo ya uchumi katika maana yake pana ni matokeo na sehemu ya utamaduni wa watu. Maendeleo yasiyojengwa katika misingi ya utamaduni wa jamii ni maendeleo yasiyokuwa na maana kwa jamii hiyo.
Swali la kujiuliza, je, sanaa zetu zilivyo leo zinaweka kumbukumbu nzuri itakayorithiwa na vizazi vijavyo na kuashiria Historia inayolingana na mila na desturi nzuri za kizazi husika? Au kizazi hiki kinaweka kumbukumbu potofu ya sanaa zetu na uasili wake kwa vizazi vijavyo?
Sanaa kama nguzo mojawapo muhimu ya Utamaduni hukua na pia huweza kufa. Je, kutokana na hoja hii sanaa zetu zinakua au zinakufa au zipo katika chumba cha wagonjwa mahututi? Nadhani kwa hali halisi ilivyo kila mtu atakuwa anayajua majibu sahihi ya maswali haya.
Kuwepo madai au tuhuma za mara kwa mara kwamba, baadhi ya watayarishaji na waongozaji wa filamu wana tabia ya kuomba penzi kutoka kwa wasanii wa kike, ndiyo wawape nafasi ya kushiriki katika filamu zaao au msanii huyo anaweza kuanza kushiriki filamu halafu baada ya muda unasikia yeye na mtayarishaji au muongozaji wake wana mahusiano! Habari hizi zimekuwa zikiripotiwa sana kwenye vyombo vyetu vya habari, hasa magazeti.
Kuna ulazima gani kwa msanii eti kwa sababu kapewa kushiriki filamu halafu baada ya muda anakuwa na mahusiano na mtayarisahji, nini kinasakwa hapa? Ni kweli watayarishaji wanawalazimisha wasanii wa kike au wasanii wenyewe wanajilegeza kwao? Na kama hawakubaliani na mambo hayo kwa nini hawakatai? Kama hawakubaliani na hali hii si wanajua majibu yake?
Kuna ulazima gani kwa msanii eti kwa sababu kapewa kushiriki filamu halafu baada ya muda anakuwa na mahusiano na mtayarisahji, nini kinasakwa hapa? Ni kweli watayarishaji wanawalazimisha wasanii wa kike au wasanii wenyewe wanajilegeza kwao? Na kama hawakubaliani na mambo hayo kwa nini hawakatai? Kama hawakubaliani na hali hii si wanajua majibu yake?
Miaka ya nyuma waliokuwa wakiingia kwenye sanaa wengi wao walisukumwa na vipaji walivyonavyo na waliipenda sanaa bila kujali kama watapata umaarufu au la, na waliongozwa na maadili ya utamaduni wao tofauti na siku hizi, ambapo wengi wanaokimbilia kuigiza (hasa wasanii wa kike) wanasukumwa na lengo la kutaka umaarufu ili wapate 'mapedeshee'. Kwa maana nyingine sanaa ya filamu ni sawa soko la kutafuta mabwana.
Msanii makini huwa anajiwekea malengo makubwa katika maisha yake, ambapo atakuwa makini zaidi na daima atajiepusha na tabia zinazoweza kumpelekea kutofikia malengo yake. Hali hii haina maana kwamba hatajihusisha na starehe zinazoambatana na ujana! La hasha. Ila hata kama anakwenda 'club' au kwenye starehe yoyote basi atatambua lengo lake na atajua dosari inayoweza kumpata endapo atajilegeza na kufuata vishawishi.
Diamond na Wema Sepetu
Mi' nadhani jamii yetu imepotoka na inahitaji msukumo mpya kuirudisha katika maadili ya kweli. Maadili yamepotoshwa tangu kwenye ngazi ya familia tunazotoka, hali hii humfanya kijana kujiona hafai kwa chochote katika familia anamotoka au katika jamii ya watu inayomzunguka.
Hisia hii inampelekea kujichukia na kupata msukumo wa kutaka kutafuta thamani ya nafsi yake kirahisi. Njia mojawapo ya kufanya hivi ni kujaribu mambo ya mapenzi. Kwa msichana wa hali hii ni rahisi kufikiri thamani yake inatokana na tendo hili la ngono kwani linaambatana na lugha nzuri wanazotumia wavulana na ahadi au zawadi anazoweza kupewa.
Ni wakati sasa wa Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia wasanii ambao ndiyo kioo cha jamii, hasa jamii ya vijana kwa kuandaa semina zinazohusu kujitambua na kuwasaidia kuanza safari ya kutafakari, “Mimi ni nani?,” na “Thamani yangu inatokana na nini?” Hii itawasaidia kutambua kwamba thamani ya mtu haitegemei watu wengine wala wanavyosema, hata si umbo alilo nalo, bali ni hali ya ndani. Thamani ya mtu ipo ndani ya utu wake, yaani nafsini mwa mtu mwenyewe.
No comments:
Post a Comment