Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, kushoto
na msanii mwenzake maaruf kama Mikogowakijiandaa kwa filamu
Elizabeth Michael (Lulu) katika pozi
Wasanii Irene Uwoya na JB katika moja ya scene
za mapenzi kwenye filamu za Bongo
TUNAPOFIKIRIA juu ya faida na vikwazo vya kutatua matatizo ya uratibu wa jamii kupitia taratibu za masoko ya filamu, ni muhimu kuzitupilia mbali baadhi ya hoja za uongo zinazolazimishwa miongoni mwetu. Ninaposema hoja za uongo nakusudia maneno ambayo kutokana na ukweli ulio dhahiri hupita hivihivi bila hata ya kuwa na haja ya kuhoji au kuhitaji uthibitisho.
Ni maneno unayoweza kuyasikia kutoka kwa watu mbalimbali kuhalalisha kile wanachokiamini au wanachotaka jamii ikikubali kwa maslahi fulanifulani. Maneno ambayo hurudiwarudiwa kana kwamba ndiyo aina mojawapo ya maneno ya hekima. Hatari iliyoko ni kwamba, kwa sababu yameenea sana, hayafanyiwi uchunguzi wa kina. Na hicho ndicho ninachokusudia kukifanya leo.
Mara nyingi, lakini si mara zote, hoja hizi zimekuwa zikienezwa na wale ambao wanahisi kuwa hawana jipya katika tasnia hii au wana hofu ya kutupwa nje ya soko la filamu, hivyo hutumia hoja hizi kujijengea uhalali wa kuendelea kulitawala soko.
Masoko huwafanya watu wafikirie tu kuhusu kupata faida. Hakuna suala la maadili katika ubadilishanaji wa soko, hakuna jitihada za makusudi zinazoelekezwa katika kutambua utofauti wetu kama wanadamu: Uwezo wetu wa kufikiri si tu kitu kilicho na manufaa kwetu, bali kuhusu kilicho sahihi na kisicho sahihi, kinachofaa kulingana na maadili na kisichofaa kimaadili.
Ieleweke kuwa kila kitu katika dunia hii kina hatua zake toka kuzaliwa mpaka kufa kwake, katika kila hatua kuna changamoto mbalimbali ambazo ndizo zinaifanya hatua inayofuata iwe bora zaidi kuliko iliyokuwepo kabla. Ila hili la filamu nyingi za Bongo na kukosa uhalisia katika mavazi bado linatia shaka ukuaji wa tasnia hii.
Hapa siongelei zile skendo zinazotawala kwenye magazeti kila kukicha, ninachojaribu kukiangalia hapa ni mavazi yanayotumika kwenye filamu zetu na uhalisia wake katika kulisapoti soko la filamu.
Suala la mavazi ya aibu wanayovaa wasanii wetu ndani ya filamu wanazoigiza eti linatajwa kuwa ndiyo kivutio kikubwa cha soko la filamu! Mavazi ambayo wakati mwingine hayana umuhimu katika kujenga taswira yoyote!
Sijui waigizaji wetu wanapovaa mavazi hayo yasiyoendana na maudhui wanajaribu kuonesha nini, kuwa wanajua sana kuvaa au vipi? Wasanii hawa wameonekana kuwa na ulimbukeni mbaya sana. Wakiamini kuwa kuvaa nguo zinazoonesha maungo yao ndiyo njia ya kuuza picha na kusahau utamaduni wao kwa kuiga tabia za ajabu zinazofurahiwa na wanaume wakware.
Hoja ya 'biashara ni matangazo' inapofananishwa na mavazi ambayo yanashindwa kutofautisha kati ya mtoto aliyeko katika mikono ya wazazi na changudoa, haina mashiko. Kwani msichana hawezi kuonekana mwenye mvuto hadi avae nusu uchi au sinema haiwezi kuuza hadi wasichana wavae mavazi ya aina hiyo?
Katika uigizaji, kikubwa ni maudhui na kisha fani ambayo ndani yake kuna matumizi ya lugha, mtindo wa uigizaji au wa hadithi yenyewe, muundo, mandhari au eneo ambalo tukio la kifasihi linafanyika na wahusika wenye kuvaa uhalisia.
Vitu hivi vikipangwa na kutumiwa ipasavyo kiasi cha kuifanya hadhira ipate ujumbe kirahisi, iburudike na ielimike kwa wakati mmoja basi ni dhahiri tasnia ya filamu itakuwa imefanikiwa na filamu itauzika. Lakini siyo kuonesha matendo ya kutia aibu kiasi cha kushindwa kutazama filamu pamoja na familia yako.
Sanaa ya filamu ndiyo yenye mwitiko mkubwa kwa vipengele vya sanaa katika nafsi ya mwanadamu, na kwa maana hiyo, haviwezi kuuzwa na kununuliwa kama vile nyanya kwa kisingizio cha kujidhalilisha au kudhalilishana. Kuliacha suala hili hivihivi bila kulikemea ni sawa na kuusaliti utu tuliourithi wa sanaa.
Licha ya hayo, kadiri sanaa hii inavyofunguliwa milango ya kuingizwa kwenye mashindano ya soko la kimataifa, matokeo yake ni kung’olewa kwa misingi yake kwa kuwa, mihimili ya asili hutupwa mbali kwa sababu ya tamaa ya pesa ambazo zina nguvu za kuvuta watu kama za Mungu.
Nikiwa mdau wa filamu za Bongo, natamani sana kuiona tasnia ya filamu hapa nchini ikifika kwenye kilele cha mafanikio na kulitangaza vyema Taifa letu katika medani za kimataifa, lakini hili wingu mbele yetu linalochangiwa na ubinafsi na kujifanya kujua sana linatugharimu.
Sina budi kukiri kuwa nchi yetu imebarikiwa kuwa na watu wenye vipaji vya kuigiza na wenye uwezo wa kuuvaa uhusika inavyotakiwa, endapo tu wanapata muongozaji mzuri, lakini mwenendo wa soko hili unapotosha na kufedhehesha kabisa.
Madai ya uongo kuwa ili sinema iwe nzuri ni lazima iwashirikishe mabinti warembo (na pengine waliopitia umiss Tanzania) ambao watavaa nusu uchi hata kama stori haisemi hivyo, ndiyo magumu hata kuyawaza. Ili mabadilishano yaweze kufanyika lazima pawepo na heshima ya haki.
Hata hivyo, Masoko hayajengwi tu juu ya kuheshimu haki. Hujengwa pia juu ya uwezo wa wanadamu wa kuzingatia sio tu matamanio yao, bali matamanio ya watu wengine, kujiweka kwenye nafasi ya wengine. Mtu mwenye mgahawa asiyejali wanachokitaka wateja wake biashara yake haiwezi kudumu.
Hata hivyo filamu yoyote inayozingatia nguo zinazoendana na uhusika halisi, kwenda na wakati na kuzingatia malezi mazuri huleta mazingira nufaishi mengi, kwa kuwa wengi hupenda kuwaona watu wanavaa vizuri, wenye uhalisia kuhusiana na stori au watu waliolelewa katika maadili mazuri.
Inaeleweka kwamba, msanii anapotaka kucheza nafasi ya kuwa changudoa, basi hana budi kuvaa mavazi fulani hivi yasiyo ya heshima kwa sababu anajiuza, lakini soko letu siku hizi halina tofauti katika filamu kati ya changudoa na mtu mwenye heshima zake. Kwa sababu wote wanavaa vilevile, isipokuwa katika mandhari tofauti.
Uzuri wa filamu hutokana na vifaa bora vya uchukuaji picha, muongozo mzuri wa filamu, wasanii wenye ueledi wa uigizaji na kipaji, na nidhamu kwa muongozaji wa filamu na wala siyo mavazi ya kufedhehesha wala matendo ya aibu ndani ya filamu.
Kuachwa kwa hali hii bila kukemea imefikia mahali ambapo wazazi wanawazuia watoto wao wenye vipaji vya uigizaji kwenda kujiunga na makundi ya uigizaji, kwa sababu mzazi anahofia matendo atakayokwenda kufanya mtoto wake na jamii itakavyomchukulia.
Mzazi anahofia mabadiliko ya kitabia ya mtoto wake pindi atakapoanza kujichanganya na aina fulani ya watu kule kwenye makundi ya uigizaji.
Lengo la filamu ni kufikisha ujumbe kwa jamii, ujumbe ambao utaibadilisha jamii, utaielimisha na maudhui hayo ya kuburudisha. Ujumbe ambao utaleta mabadiliko chanya kwa jamii na siyo mabadiliko hasi, ambayo yanaliengua taifa katika mhimili wa kujisifu kupitia tamaduni zetu wenyewe.
Ili filamu iuze nakala nyingi siyo lazima wahusika wavae nusu uchi au waoneshe matendo ya aibu, bali ni umahiri wao wa kuigiza, kipaji na nidhamu katika uigizaji.
Masoko hufanikiwa zaidi pale ambapo hatua za utekelezaji hubebwa na wale wanaohusika na kutoa maamuzi. Ikiwa watu watanufaika tu bila kuchangia katika mchakato wa jinsi ya kuyafikia hayo manufaa, basi masoko yatashindwa kufanya kazi yake vizuri katika viwango vilivyokusudiwa.
Vilevile, kama watu watapokea 'manufaa hasi', yaani, kama watapata madhara, na hizo gharama kutokuzingatiwa katika maamuzi ya kuzalisha filamu, masoko yatawanufaisha wachache na wengine huishia kubeba gharama kubwa, kwa kuwa mwingine ataishia kulipia gharama tu.
Kutegemea masoko ni jambo zuri pale jamii inapokuwa haina utata, lakini kutokana na ukuaji wa haraka wa uchumi na mitandao ya kijamii, serikali haina budi iiongoze jamii ya wasanii na watengeneza filamu na kuratibu shughuli za tasnia ya filamu. Vinginevyo tutajikuta tukiwa taifa lisilo na maadili kuanzia kwa kiongozi mkuu hadi kwenye jamii nzima.
Naomba kutoa hoja...
No comments:
Post a Comment