Lucas Mhuvile (Joti)
Ramadhani mwinshehe (Kingwendu)
NAKUMBUKA kabla ya teknolojia hii ya televisheni kuingia nchini mwetu kwenye miaka mwishoni mwa tisini, tulizoea kusikiliza michezo ya kuigiza na vichekesho kupitia redio, michezo kama vile Mahoka, Pwagu na Pwaguzi, Twende na Wakati na kadhalika. Wakati huo kituo cha redio kikiwa kimoja tu, yaani Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD).
Ndipo miaka ya tisini vituo vingine vya redio vilipojitokeza na kuanza kutoa burudani huku vikimaliza ukiritimba wa RTD wa kuhodhi matangazo yote na kutulazimisha kusikiliza hata vile vipindi ambavyo hatukuvihitaji. Kuingia kwa redio zingine kulisababisha baadhi ya vituo hivi vipya kuwanyakua baadhi ya watangazaji waliokuwa RTD.
Mwanzoni mwa matangazo ya redio hizi tuliburudika sana kwa kupata burudani ya muziki mfululizo, jambo lililokuwa adimu kulipata wakati ule wa redio moja tu ambapo vipindi vingi vilikuwa vya Mkulima wa Kisasa, Shambani, Ukulima wa Pamba, Kahawa, Mtu ni Afya, Ushirika, Mikingamo na mambo kama hayo. Burudani ya muziki ilipatikana kwa nadra sana hasa kwenye vipindi kama Mchana Mwema, Club Rahaleo Show, Salamu za Wagonjwa...
Ajabu ilikuwa pale mnapojikuta wote; madaktari, wanasheria, wachumi na kadhalika mkilazimika kusikiliza kipindi cha kilimo cha pamba! Hata hivyo enzi hizo sasa hivi zimebakia historia.
Ujio wa redio zingine ulikuwa kama neema kwetu si tu kwa kupata burudani bali hata kuona ubunifu ukiongezeka, lakini vituo hivi vilipoanza kurusha vipindi vingine visivyo vya burudani tulishangazwa kuona vikija na vipindi kama vilevile vilivyokuwa RTD ingawa ni kwa majina tofauti.
Haikuishia hapo tu kwani hata muda wa urushaji vipindi hivyo uliendelea kuwa ni uleule kama ulivyoasisiwa na RTD, kwangu mimi hapa ndipo tulipoonekana kuanza kukosa kabisa ubunifu na kuishia kunakiri na kubandika kila kitu kama kilivyo (totally copy and paste).
Hali hii imeendelea kuwepo hata kwenye vituo vya televisheni kwa miaka nenda miaka rudi huku tukiongopewa kwa kubadilishiwa majina ya vipindi, lakini maudhui, muundo na muda kuendelea kuwa uleule kwa vituo karibu vyote vya televisheni.
Hali hii ya Watanzania kuwa ni watu wa kusubiri kwanza ajitokeze mtu mmoja wa kuanzisha jambo na apate mafanikio ndipo tujitose kuliendeleza imekuwa ni sababu ya kutufanya kuendelea kuwa nyuma siku zote, tukizidiwa na jirani zetu Kenya na Uganda. Mfano mzuri angalia hata biashara zetu tunazofanya, si jambo la kushangaza kukuta mtaa mzima ukiwa na grosari zilizojipanga, eti tu kwa sababu aliyeanzisha alipata mafanikio makubwa katika mtaa huo.
Au kukuta mtaa mzima una vibanda vya kuuza mitumba, kisa tu muuzaji wa kwanza mtaani hapo alifanikiwa sana, hivyo imeonekana kuwa mtaa huo unafaa kwa biashara ya mitumba!
Nimeamua kuandika makala hii kwa kuwa Alhamisi ndo imekuwa siku ya vichekesho vinavyorushwa na televishani zetu hapa nyumbani ambavyo kwa sasa vinaonesha kuchukua nafasi kwa kuteka watazamaji, huku kila kikundi kikiwa kinapata mafanikio kupitia maigizo hayo.
Kabla ya vichekesho hivi kuteka watazamaji, tulizoea kupata burudani kupitia vituko vya kina Majuto, Mzee Small, Onyango na wenzake na baadaye Mizengwe. Vichekesho hivi vilikuwa vikiruka kwenye vituo tofauti, kwa staili tofauti, siku tofauti na nyakati tofauti.
Baadaye liliibuka kundi la Ze Comedy lililokuwa likirusha vichekesho vyake EATV (Channel 5) na kujizolea umaarufu mkubwa kwa aina ya uwasilishaji wake wa vichekesho kwa kutumia mfumo wa taarifa ya habari. Hivi sasa kuna makundi manne makubwa yanayorusha vichekesho katika runinga nne tofauti, lakini kwa siku moja na katika muda unaofuatana!
Baada ya Ze Comedy kusitisha mkataba na EATV na kusababisha mgogoro na mmiliki wa kituo hicho kwa kugombea jina, waliibuka hawa jamaa wa Futuhi, actually kipindi hiki kikapata umaarufu mkubwa wakati Ze Comedy wakiwa bado ndani ya mgogoro na EATV, yaani jamaa waliibukia juu ya mgongo wa Ze Comedy na kupiga bao! Waswahili wanasema kufa kufaana! Kipindi cha Futuhi kinarushwa hewani na Star TV siku ya Alhamisi saa tatu hadi saa nne usiku.
Hata hivyo mgogoro wa Ze Comedy ulisababisha kuzaliwa kwa kundi la Orijino Komedi lililohamishia vichekesho vyake katika kituo cha televisheni cha TBC1. Orijino Komedi wanaendelea kuonesha vichekesho vyao TBC1 siku ya Alhamisi, saa moja hadi saa mbili usiku.
Ndipo likazaliwa upya kundi la Ze Comedy lililoasisiwa kwa mara nyingine baada ya lile la kwanza kujitenga. Kundi hili liliibuka baada ya kufanyika mchakato wa kuwapata wasanii wapya kwa kuendeleza kipindi hicho cha ucheshi, kupitia kile kilichoitwa 'Ze Comedy Starsearch'. Kipindi hiki cha ucheshi cha Ze Comedy hurusha vichekesho vyake EATV siku ya Alhamisi, saa moja hadi saa mbili usiku.
Ndipo likazaliwa upya kundi la Ze Comedy lililoasisiwa kwa mara nyingine baada ya lile la kwanza kujitenga. Kundi hili liliibuka baada ya kufanyika mchakato wa kuwapata wasanii wapya kwa kuendeleza kipindi hicho cha ucheshi, kupitia kile kilichoitwa 'Ze Comedy Starsearch'. Kipindi hiki cha ucheshi cha Ze Comedy hurusha vichekesho vyake EATV siku ya Alhamisi, saa moja hadi saa mbili usiku.
Na mwisho kuna kipindi kingine ambacho kwa sasa kinajizolea umaarufu mkubwa cha Vituko Show, kinachorusha vichekesho vyake kwenye televisheni ya Channel Ten na kukusanya wachekeshaji wengi maarufu (comedian all stars). Kipindi hiki pia hurusha michezo yake siku ya Alhamisi, saa mbili na nusu hadi saa tatu na nusu usiku!
Sasa, swali linakuja; kuna nini siku hii ya Alhamisi? Kwa nini iwe ni siku ya Alhamisi tu na si siku nyingine? Kwani ukiweka kipindi cha ucheshi siku nyingine tofauti na Alhamisi kitakosa watazamaji? Au kuna sheria iliyotungwa kuwa kipindi cha ucheshi lazima kiwe Alhamisi tu? Na mbaya zaidi kuna makundi mawili yanaonesha vichekesho vya aina moja katika muda mmoja!
Na ifikapo saa tatu siku hiyo hiyo ya Alhamisi, vipindi vingine tena hugongana kwa kuwa hurusha vichekesho vyao katika muda huo, na kuwafanya watazamaji kushindwa kujigawa kuangalia vipindi vyote. Watazamaji wamekuwa wanajiuliza kuna sababu gani muhimu kwa vituo hivi vya televisheni na hata vikundi husika kushindwa kuachiana siku na muda ili watazamaji wawe na uhuru wa kupata burudani zote kwa nyakati tofauti na kutoa tathimini?
Kwani ukionesha vichekesho vyako Jumatano, Ijumaa au Jumamosi utapungukiwa nini? Tatizo ni siku au ubunifu zero? Binafsi nadhani kukosa ubunifu ndiyo chanzo cha yote haya, kuamua kubanana siku moja na kuwanyima watazamaji uhondo kutoka upande ambao wenyewe wataona kuna ubunifu na burudani nzuri ni jambo baya sana.
Kukosa ubunifu limekuwa ni tatizo kubwa miongoni mwa Watanzania ambao wamekuwa ni watu wa kusubiri kwanza mtu fulani afanikiwe ndipo kila mtu aanzishe biashara kama yake, sehemu hiyohiyo na akitegemea wateja walewale badala ya kubuni kitu kingine kitakachowavutia, ambacho kinaweza kuwa na tija zaidi na ufanisi.
Watayarishaji wetu wa vichekesho katika vituo vya televisheni, na hata wa filamu wanatakiwa kutayarisha kazi zao kulingana na matakwa ya mashabiki na wapenzi wa kazi hizo, ambao ndiyo mabosi wao wakuu. Wanapaswa waache kukurupuka katika ufanyaji kazi. Wanatakiwa kuzingatia kwamba wanaandaa kazi ya aina gani na kwa ajili ya nani bila kujali itarushwa siku na muda gani.
Bahati mbaya siku hizi watayarishaji wa vichekesho hivi hawazingatii tena namna ya kukidhi matakwa ya wapenzi na mashabiki wao, bali wanatazama nani kafanikiwa nini na siku gani. Mfano, ina maana hakuna namna nyingine ya ucheshi isipokuwa kutumia mfumo wa taarifa ya habari?
Mbona Mizengwe wanarusha vichekesho vyao Jumapili na wanapata mashabiki wengi mno? Kwa mtazamo wangu hawa jamaa wa Mizengwe ndiyo wanaofanya vizuri sana kuliko wengine kwa kuwa hawaonekani kushindana na mwingine, bali wanachekesha kulingana na ubunifu wao.
Tatizo kubwa ninaloliona hapa wachekeshaji walioanzisha mfumo huu wa taarifa ya habari (Ze Comedy phase 1) walikuja na ubunifu wa hali ya juu sana na watu wakategemea kuwa utazidi kuongezeka, kinyume chake umepungua kwa kasi ya ajabu na watu wanaiona tofauti hii.
Bahati mbaya tu ni kwamba hata walipotokea wachekeshaji wengine wameshindwa kuja na mpya kwa kushindwa kufikia viwango vile vya mwanzoni, achilia mbali kuzidi. Ni kama vile mtoto ambaye alipoanza shule alikuwa anapata alama sabini kwa mia (70%), tulipotegemea aongeze bidii yeye akashuka na sasa yupo kwenye alama arobaini kwa mia (40%). Huku wengine wanaoibuka nao wanaangukia kwenye kundi hilohilo!
Napenda kuwaambia kuwa kurusha vichekesho Alhamisi siyo dawa bali wajitahidi kuwa wabunifu, vinginevyo wameshaliacha soko walilolikusudia bila wao kujua!
Ukweli upo wazi, familia yangu na jirani zangu huku kwetu Uswahilini walikuwa hawakosi vipindi vyao, walikuwa wanaitana kwenda kuangalia lakini siku hizi utashangaa kipindi kinaendelea wao wapo barazani wakipiga stori, hata wakiitwa hakuna anayenyanuka.
Jana Alhamisi nilimsikia jirani yangu mmoja akimwambia mwanaye mdogo, “ukiona kuna kitu cha maana niite niangalie...” Hali hii inaonesha kuwa mvuto unapungua kutokana na kukosekana ubunifu. Ndiyo maana nimekuwa najiuliza, “kwa nini Alhamisi?”
Naomba kuwasilisha...
No comments:
Post a Comment