Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mkoa wa Mara,
Ester Bulaya
Ili kukomesha vitendi vya wizi wa kazi za wasanii nchini, Serikali imetenga kiasi cha Sh. milioni 470 ili kufanikisha mpango wa utengenezwaji wa stika maalumu (Haki gramu) zitakazowekwa kwenye kanda za sauti (kaseti), video na CD ili kukomesha wizi wa kazi za wasanii. Serikali imesema kuwa itashirikiana na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na nchi za SADC katika kuandaa stika maalum kwa ajili ya kudhibiti uharamia huo.
Mpango huo wa serikali ulielezwa bungeni mjini Dodoma jana (Jumatano) na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalumu (CCM), Ester Bulaya, aliyetaka kujua ni vipi serikali imejipanga kukomesha wizi wa kazi za wasanii.
Malima alisema kuwa kazi ya uwekaji wa stika hizo itafanywa na Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota) ambapo msanii ataingia mkataba maalum na msambazaji kwa ajili ya kusambaza idadi fulani ya nakala ya kazi zake kabla ya kusambazwa.
Alisema kuwa baada ya mpango huo kuanza rasmi nakala ambazo hazitakuwa na stika zitaondolewa sokoni sambamba na wahusika watakaokutwa nazo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Malima alisema kuwa kimsingi wigo wa kazi za wasanii wa Tanzania ni mkubwa ambapo utafiti umebaini kuwapo kwa zaidi ya nakala milioni 20 halisi na bandia zilizosabazwa nchi jirani ikiwemo Kenya, Rwanda, Uganda na Burundi.
"Soko la kazi za wasanii wa Tanzania ni kubwa mno, utafiti unaonesha kuna zaidi ya nakala milioni 20 zilizosambazwa nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi lakini wasanii wenyewe hawafaidiki na serikali kukosa mapato yanayokadiriwa kufikia Sh. bilioni 20," alisema Malima.
Aidha, alisema wizi wa kazi za wasanii ni kosa la jinai na yeyote atakayejihusisha nalo atachukuliwa hatua za kisheria. Pia alibainisha kuwa serikali ilifanya tathmini na kubaini ukubwa wa soko la kazi za wasanii kupitia mauzo ya kanda za sauti video na CD, ambao ulifikia nakala milioni 20 kwa mwaka.
"Utafiti huo pia ulibaini kuwa kanda nyingi zilikuwa zinauzwa kinyemela na ni bandia kwa wakati huo, bei ya mkanda wa sauti iliuzwa shiling 1000/-, mkanda wa video shilingi 1500/- na CD shilingi 3000/-, biashara hiyo ingeweza kuingiza shilingi bilioni 20 kwa mwaka," alisema.
No comments:
Post a Comment