Moja ya mafunzo ya filamu yaliyotolewa hapa nchini.
Hapa washiriki wakibadilishana mawazo nje ya
Kituo cha Utamaduni cha Ujerumani (Goethe Institut).
Kulia ni mwandishi wa makala hii, Bishop Hiluka
Hapa washiriki wakibadilishana mawazo nje ya
Kituo cha Utamaduni cha Ujerumani (Goethe Institut).
Kulia ni mwandishi wa makala hii, Bishop Hiluka
MWISHONI mwa wiki iliyopita Tamasha la Filamu za Nchi za Majahazi (ZIFF 2010), lilihitimishwa huku kukiwa na mambo kadhaa yanayozidi kuitia doa tasnia ya filamu nchini. Katika tamasha hilo filamu zaidi ya 100 zilioneshwa sambamba na wasanii mbalimbali kutoka nchini Tanzania, Afrika na nje ya Afrika kuonesha burudani ndani ya Visiwa vya Zanzibar.
Tamasha hilo la filamu la Zanzibar lililoanza Juni 18 ndani ya Ngome Kongwe Zanzibar, likiwa linafanyika kwa mara ya 14 tokea lilipoanzishwa, limekuwa na mchango mzuri sana katika tasnia ya filamu na linapaswa kuchukuliwa kama somo muhimu sana na waigizaji, waandaaji, waongozaji na watunzi wa filamu wa Tanzania.
Katika filamu zilizooneshwa waandaaji wameweza kuonesha ujuzi na umahiri wao mkubwa juu ya kufikisha ujumbe kwa njia ya filamu ambazo zilikonga nyoyo za watazamaji waliofika kujionea. Tamasha hilo pia liliambatana na semina iliyotolewa bure ambapo wasanii na watayarishaji wa filamu wa Tanzania wangepata nafasi nzuri sana ya kujifunza kutoka kwa magwiji wa filamu duniani.
Semina hiyo ingesaidia sana kuleta mafanikio japo kwa kiasi fulani kwa wasanii na watengenezaji wa filamu wa Kitanzania, ambapo kwa mwenendo wao wa sasa, kama ilivyowahi kusemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Gonche Materego, inawezekana kwa maendeleo yanayokuja Tanzania, vyanzo vya maendeleo vitakosa kazi za sanaa.
Kutokana na kukosa mafunzo ya taaluma ya filamu Watengenezaji wa filamu na wasanii wa Tanzania wamekuwa ni watu wanaolipua kazi, wasiojali ubora, wanaoshindwa kubuni na kujikuta wakiishia kunakiri kazi za nje na hata kazi zao nyingi hazizingatii mambo muhimu kwa kisingizio cha bajeti hata kwa yale ambayo hayahitaji kuwa na bajeti kubwa.
Pia wengi wao wamekuwa hawana uthubutu kwa sababu wamejawa na woga, jambo ambalo limekuwa linarudisha nyuma maendeleo ya tasnia hii. Wasanii wa Tanzania wamekuwa wakikwepa kuhudhuria makongamano, warsha na semina mbalimbali za filamu nadhani kwa hofu tu ya kutokujiamini.
Nimekuwa nikiandika kuwa nchi yetu imekosa mfumo mzuri ambao ungesaidia kumuendeleza msanii wa Tanzania ambaye hakupata nafasi ya kusomea taaluma na hatuna vyuo vinavyotoa mafunzo ya filamu kama ilivyo kwa jirani zetu Kenya au Afrika Kusini, lakini bado siamini kuwa kuendelea kuitegemea serikali itusaidie au elimu ya darasani ndiyo suluhisho pekee katika kupata mafunzo ya weledi.
Kuna njia nyingi za kupata elimu kama hizi zinazojitokeza ambazo hutolewa kwa njia ya semina, warsha au makongamano ambazo zinaweza kuwa suluhisho japo kwa kiwango fulani na kuwafanya wasanii kufanikisha maendeleo ya tasnia ya filamu nchini na kuitangaza Tanzania ipasavyo nje ya mipaka yake.
Binafsi, japo nimebahatika kupata elimu ya filamu kwa maana ya kuketi darasani, lakini niseme wazi kuwa ni kwa kupitia makongamano, warsha na semina mbalimbali ambapo nimeweza kupata ufahamu mkubwa zaidi kuhusu filamu na namna ya kuandaa kazi, kitu ambacho kimekuwa kikinifanya kujiamini.
Wakati Watanzania wakiendelea kujipa moyo kwamba soko la filamu za Kibongo limekuwa likikua kwa kasi kubwa, waigizaji na waandaaji wa filamu hizo ni kana kwamba wameridhika na kuvimba kichwa kutokana na hali hii.
Wamejisahau sana kiasi cha kudhani kuwa hawahitaji tena kujifunza ingawa ukweli ni kwamba msanii wa Tanzania bado hana mafanikio! bado ni ombaomba! Wengi wenye maisha mazuri kidogo ni kutokana na mafanikio ya familia zao au pengine wanapata kipato kingine nje ya filamu, si kutokana na filamu kama wanavyotaka Watanzania waamini!
Watayarishaji wa filamu wa Tanzania kila siku wanaumiza kichwa kutafuta mtaji na kuandaa bajeti ya filamu, uandaaji wa filamu ambao hadi kukamilika kwake ni kazi ngumu na inayohitaji moyo, lakini bado watayarishaji hawahawa eti hawana sauti wala nguvu sokoni bali kuna mfanyabiashara fulani ndiye anayeamua hatma ya kazi zao!
Watayarishaji wanafanya kazi kwa shinikizo la woga wa soko, kwa sababu tu wamekosa kabisa mafunzo ya msingi (nitty-gritty) ya namna ya kutengeneza kazi zao katika kiwango kinachokubalika! Hawana uhakika wa soko lao! Kinachobaki ni wao kutegemea fadhila ya msambazaji huku wakishindana kupeleka majungu kwa msambazaji ili filamu zao zisambazwe. Haijalishi wanalipwa kiasi gani!
Faida kubwa ya kupata mafunzo ya taaluma ya filamu ni pamoja na kumfanya msanii/mtayarishaji aitambue filamu na kujitambua awapo ndani ya filamu.
Msambazaji anapaswa awe mdau wa mwisho kabisa kwa mapato ya mzalishaji wa filamu za Kitanzania! Tofauti na ilivyo sasa, ambapo mzalishaji ni lazima akampigie magoti msambazaji hata kwa kazi iliyomtoa jasho! Hii ni hatari kubwa katika tasnia ya filamu!
Tamasha la filamu linalofanyika kila mwaka mjini Zanzibar ni moja ya somo kubwa sana kwa tasnia ya filamu ambapo waliobahatika kutembelea tamasha hilo na kuziona kazi zinazowakilishwa na watayarishaji kutoka nchi zilizobobea, ni dhahiri watakuwa wamejifunza jambo na kupata ujuzi utakaowawezesha kupiga hatua.
Katika tamasha hilo, waandaaji na waongozaji wa filamu ambao walitoka nchi zaidi ya 70 duniani kote waliweza kuendesha semina na midahalo ili kuinua tasnia ya filamu kwa nchi zinazojikongoja ikiwemo Tanzania, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba wasanii wa Tanzania ambao walialikwa katika tamasha hilo hawakuweza kuhudhuria kwenye semina hizo zaidi ya kuonekana mitaani 'wakiuza sura'!
Inasikitisha kuona wasanii wetu ambao wamekuwa wakilalamika kila siku kukumbwa na changamoto nyingi ikiwemo kukosa elimu na waliotakiwa kushukuru kwa changamoto wanazopewa ikiwemo kukosolewa kutokana na upungufu uliomo kwenye filamu zao, wamekuwa wakichukulia mambo haya kimzaha namna hii.
Nathubutu kusema kuwa watayarisaji/ wasanii wetu wa nchini bado hawajaweza kukubali kujifunza kwa namna moja ama nyingine, kwa sababu tu wanadhani kuwa tayari wanajua na wamefika, hata kwa jambo ambalo ni la msingi kwao na jamii nzima, na hawajui kwamba kazi zao zinaiwakilisha tasnia ya filamu ya Tanzania katika nchi zingine na hivyo aibu yoyote itokanayo na filamu zao ni ya Watanzania wote.
Wasanii wetu wamevimba kichwa kutokana na mafanikio ya kufikirika pale wanapoona kazi zao zikiwa zimejaa sokoni na kununuliwa kwa wingi japo si wao wanaofaidika bali msambazaji, na wao kuambulia umaarufu huku wakipewa pesa kidogo za kusukuma maisha kwa siku kadhaa na kukopeshwa magari, kiasi cha kukacha hata kuhudhuria mafunzo maalum ya sanaa kama hayo yaliyoandaliwa katika tamasha la filamu Zanzinzar!
Hatua ya wao kukacha mafunzo hayo imewasononesha sana waandaaji wa tamasha ambapo Ofisa Mtendaji Mkuu anayemaliza muda wake, Profesa Martin Mhando, alisema kwamba badala ya Watanzania kuchangamkia mafunzo hayo maalumu ili kuongeza upeo wao wamebaki wakiishutumu ZIFF kwamba haiwasaidii!
Katika tamasha hilo la 14 mwaka huu, ZIFF waliandaa mafunzo mengi yakiwamo ya matumizi ya kamera HD, uandishi wa miongozo ya sinema (scriptwriting), mambo ya muziki, uongozaji wa makala (documentary) na utengenezaji wa filamu.
Binafsi sikushangazwa sana na taarifa za wasanii/ watayarishaji wa filamu wa Tanzania kukacha mafunzo, kwani nchi hii imeshuhudia mafunzo mbalimbali yakitolewa kwa njia ya warsha, semina na makongamano ambapo hakuna msanii hata mmoja ndani ya soko la filamu za Bongo aliyewahi kuhudhuria japo walikuwa wanapata taarifa.
Nasema hivyo kwa kuwa mimi nimeshahudhuria warsha nyingi za filamu zikiwemo za ujasirimalia wa filamu, uandishi wa miongozo (screenwriting), upigaji wa picha (cinematography), ubunifu wa sauti (sound designing), ubunifu wa uzalishaji (production design), uongozaji (directing) na uhariri (editing), sijawahi kuwaona, zaidi ya watu ambao hawapo kwenye soko la filamu.
Kwa mtindo huu, tasnia ya filamu nchini itaendelea kuwa sekta ya kuganga njaa ambayo haizingatii taaluma huku tukijigamba kupiga hatua.
Mungu ibariki Tanzania
No comments:
Post a Comment