Filamu ya White Chair, moja ya sinema zilizokumbwa na kadhia ya kulazimishwa kuingiza sura zinazodaiwa kuuza
Msanii Issa Mussa maaruf kama Claude
Mtengeneza filamu maaruf, John Riber
SIKU zote naamini kuwa penye ukweli uongo hujitenga. Jumamosi iliyopita, katika kipindi cha Baragumu kinachorushwa asubuhi kwenye moja ya vituo vyetu vya televisheni kulikuwa na mada inayozungumzia changamoto zinazoigusa tasnia ya filamu Tanzania, ambapo kampuni ya usambazaji wa filamu ya Steps Entertainment ilimtuma mwakilishi wake, anayejiita Kambarage, kujibu baadhi ya tuhuma zinazoikabili kampuni hiyo.
Kwa kweli sikutegemea kwa kampuni kubwa inayoaminika kuwa na watu makini kama Steps Entertainment kuwakilishwa na msemaji wa aina ile aliyeishia kujisifia kwa kusafiri kwenda Kenya, Burundi, Rwanda na Kongo, lakini akionekana kutojua mambo mengi kwa jinsi alivyokuwa akibabaika kujieleza, japo mwendeshaji wa kipindi, Fred Mwanjala alionekana kumuuliza maswali ya kumbeba.
Nilimsikia Kambarage akikanusha kuwa kampuni yao haihusiki na mgawanyiko uliopo wa wasanii, alikanusha vikali kuhusu kampuni yao kuchochea mgawanyiko baina ya Shirikisho la Filamu (TAFF) na wasanii waliounda Bongo Movie Club, lakini hapohapo akageuka kuwa msemaji wa Bongo Movie Club kitendo kilichoonesha kujichanganya mwenyewe.
Pia madai kwamba mikataba wanayoingia na wasanii inawakataza kufanya kazi na watu wengine, msemaji huyo alijichanganya pia, kwa kudai kuwa si kweli ingawa alikiri kuwa mikataba wanayoingia wasanii na kampuni hiyo ina masharti magumu ambayo si rahisi kwa wasanii kufanya kazi na watu wengine! Eti kwa kuwa Steps ndiyo wanagharimia pesa (Executive Producer) za kufanyia kazi.
Akijibu tuhuma kuwa kampuni yao inawabagua wasanii wengine alisema kuwa wao kama wafanyabiashara huangalia zaidi biashara kwa kuchagua filamu nzuri inayouza kwa maana ya hadithi (maudhui) na yenye ubora, na kwamba kampuni yao ina watu makini wanaoangalia filamu kabla hazijatoka wakikazia zaidi kuangalia maadili na maudhui.
Jambo la kushangaza ni kwamba kama kweli wanaangalia maadili na maudhui inakuwaje sinema wanazosambaza ndizo zinazolalamikiwa kwa kukosa maadili na kuwa na maudhui mabaya? Ni watu wa aina gani ambao kampuni hiyo inawatumia kukagua sinema hizo? Je, vipi kuhusu weledi wao katika masuala yanayohusu filamu? Haya ni mambo yanayopaswa kujibiwa na mtu makini lakini si msemaji aliyetumwa siku hiyo.
Ni jambo zuri kwa kampuni ya usambazaji kuamua kuzikagua filamu zake kabla hazijaingia dukani hasa kwa kuwa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu imeonekana kulala usingizi, lakini kwa jinsi nijuavyo kampuni hiyo haina watu weledi wa kukagua maadili na hata maudhui ya hadithi zenyewe. Kinachoangaliwa zaidi ni sinema kacheza nani, au imetayarishwa na nani basi.
Msemaji wa steps pia aliendelea kujichanganya pale aliposema kuwa kampuni yao inazipanga sinema katika madaraja (akitumia neno la Kiingereza 'class') kulingana na umaarufu wa wasanii, hii inamaanisha kuwa wao hawaangalii ubora wa kazi husika bali ustaa! Pia alinishangaza pale aliposisitiza kuwa eti wasanii wachanga wanaibuliwa na kina Kanumba akitolea mfano wa muigizaji mdogo, Jennifer aliyeibuliwa kwenye filamu ya This Is It!
Ina maana kuibua vipaji vipya ni hadi wasanii hao washirikishwe na Kanumba, Ray na wengineo waliopo kwenye lebo ya Steps? Kama huo si ubaguzi basi ni nini? Kwao Steps, sinema nzuri ni ile inayoandaliwa na wasanii wanaowaita wakubwa, basi huipitisha moja kwa moja.
Kuna ushahidi wa kutosha kuwa watu wengi wamekataliwa sinema zao kwa kuwa tu hazikuwashirikisha wasanii wakubwa, na hata alipotakiwa kujibu msemaji huyo alijitetea kuwa sinema nyingi wanazozikataa huwapa ushauri watayarishaji wake namna ya kuziboresha, jambo ambalo sio kweli. Ushauri ambao mara zote wanautoa huwa ni kuwataka wawatumie wasanii maarufu japo kwenye scene moja au mbili ili sinema hizo zipate nafasi hapo Steps, kitu ambacho hakiendani na taaluma ya tasnia ya sinema.
Hata ile hoja kwamba wanasambaza sinema za wengine, akitolea mfano sinema ya White Chair bado ni hoja dhaifu sana, kwani sinema hiyo pia ilipewa sharti la kumtumia japo msanii mmoja anayeaminika kuuza wa lebo hiyo. Na ndipo mtayarishaji wa sinema hiyo alipolazimika kuingiza scene mpya na kumtafuta msanii Issa Mussa maarufu kama Claude na kumchezesha kwenye scene moja tu ya kwanza.
Pia ieleweke kuwa sinema yoyote isiyokuwa na wanaodaiwa kuwa 'mastaa wanaouza' ikiwemo hiyo ya White Chair, japo ilimchezesha Claude zimewekewa masharti magumu ikiwa ni pamoja na kulipwa pesa kiduchu, kiasi ambacho ni aibu hata kukitaja.
Msemaji wa Steps pia hakuona aibu kuudanganya umma wa Watanzania kuwa kampuni ya Steps imemleta mtengeneza filamu, John Riber kutoka Zimbabwe kufanya kazi na Steps. Ukweli ni kwamba John Riber na mwanaye, Jordan Riber si Wazimbabwe na wala hawaishi Zimbabwe bali ni raia wa Marekani wanaoishi na kufanyia kazi zao jijini Dar es Salaam.
John Riber ana kampuni inayoitwa Media for Development International (MFDI), yenye maskani yake barabara ya Kimweri, Msasani jijini Dar es Salaam, akiwa anaishi nchini tangu 2004, akitokea Zimbabwe alikoishi kuanzia 1987. Kazi alizotengeneza John Riber ni pamoja na Chumo (2011), Mwamba Ngoma (2009), Yellow Card (2000), Everyone's Child (1996), More Time (1994) na Neria (1993). Pia ndiye producer wa kipindi maarufu cha redio cha Wahapahapa.
Suala la usambazaji wa filamu nchini ni jambo linaloumiza sana kichwa, biashara hii imejengewa mazingira ya kuwa ngumu kuliko biashara nyingine yoyote. Watayarishaji wa filamu wengi ambao wamekuwa wakipeleka kazi zao Steps, kazi ambazo ni nzuri kwa maana ya ubora wa picha na maudhui yanayozingatia mazingira, tamaduni na hali halisi, hujikuta wakikwamishwa na kazi zao kukataliwa kwa sababu tu hawakuwachezesha wasanii ambao ni “lebo” ya msambazaji.
Kampuni ya Steps ndiyo iliyokuja na wazo la kuwalazimisha watayarishaji wa filamu kutengeneza sinema yenye sehemu mbili, maarufu kama Part 1 na 2 hata kama hadithi hairuhusu, kitu ambacho si haki kabisa na kinyume cha taaluma husika.
Kulazimisha sinema iwe na namba moja na mbili kunasababisha kuoneshwa kipande kimoja cha mtu kwa zaidi ya dakika tano akifanya tukio moja, jambo ambalo limekuwa likiwakera watazamaji badala ya kuwaburudisha na kuwaelimisha kama ilivyo dhana nzima ya filamu na uigizaji.
Hata ile hoja kwamba bila wasanii au majina makubwa sinema haiwezi kufanya vizuri sokoni haina mantiki yoyote na ina lengo la kuwakweza watu fulani. Kama ingekuwa kweli kwa nini filamu za hao wanaouza zinafanyiwa promosheni kubwa sana, kuanzia kwenye magazeti, mabango makubwa ya barabarani, magari ya matangazo, hadi kwenye vituo vya redio na televisheni, huku wengine wakiwa hawapati kabisa fursa hiyo ya kutangaziwa kazi zao!
Pia mwakilishi wa Steps aliwaponda wanaodai kwamba kampuni yao iliamua kushusha bei ya mauzo ya DVD na VCD kutoka wastani wa sh. 5000 hadi 1,500 ili kuwaua wasambazaji wengine wadogo (jambo ambalo wamefanikiwa), akidai kuwa walishusha bei ili kupambana na wezi wa filamu (pirates).
Madai yake yaliyosisitizwa na kauli kwamba wanachopata ni faida ya shilingi 100 tu kwa kila nakala, lakini akashindwa kufafanua kuwa kwa kampuni kubwa kama Steps yenye uwezo wa kuagiza DVD tupu nje (ingawa hazina ubora), yenye mitambo ya kudurufu (dubbing) kazi zake na hata kazi za wengine, inapata faida ya shilingi 100, hawa wasambazaji wengine wanaotegemea kununua DVD tupu kutoka kwao na kufanyiwa dubbing watamudu vipi soko?
Pia mwakilishi huyo hakujibu madai kwamba kampuni yao inatumia mwanya wa filamu inazoziuza kwa bei ndogo kwa kuwa inapata faida kwa matangazo yake ya biashara yaliyomo ndani ya filamu hizo, kama vile pikipiki, set za Tv na bidhaa zingine ambayo hata hivyo hayalipiwi kodi!
Katika suala la kununua hakimiliki za wasanii na watayarishaji, mwakilishi huyo alishindwa kabisa kujibu tuhuma za kununua hakimiliki za wasanii kwa kuwasainisha mikataba inayokiuka sheria za hakimiliki, hata pale alipoonekana kusaidiwa kujibu na mwendesha kipindi, Fred Mwanjala. Sidhani kama kweli mwakilishi huyo anaelewa maana ya Intellectual Property.
Katika kipindi cha karibuni kumekuwepo ongezeko la wimbi la kupeleka filamu za Kitanzania kwenye vituo vya televisheni ili zioneshwe. Vituo vya televisheni vya hapa nchini siku hizi vinaonesha filamu za Kitanzania, jambo ambalo ni zuri lakini bado lina utata. Utata huu unatokana na kuwa filamu hizo zinapelekwa huko na kampuni inayozisambaza filamu hizo kutokana na tatizo kubwa la kutokuwa na mikataba sahihi au kutambua maana ya intellectual property.
Msambazaji kazi yake ni kusambaza kazi, na hivyo mkataba wake unatakiwa umruhusu kwa kazi ya usambazaji tu. Haki za kurusha au kuonesha kazi zinatakiwa zibaki kwa mwenye filamu ili aweze kufaidika tena kutokana na kurusha hewani kazi hizo, na si kama inavyofanyika hapa kwetu.
Jana, Alhamisi niliitwa kwenye kikao cha Kamatikazi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao wanaangalia jinsi ya kuiokoa tasnia hii kwa kuangalia miundo ya soko letu na kulifanya Taifa lipate mapato yatokanayo na kazi za sanaa, ikiwemo kuangalia suala la intellectual property.
Hivyo naamini kuwa haki ya mtu haitapotea hata kama utatungwa uongo wa aina gani, na hakuna marefu yasiyo na ncha. Hivi sasa mwanga wa haki unaanza kuonekana na siku za karibuni haki itajidhihirisha.
Naomba kutoka hoja.
No comments:
Post a Comment