Jun 21, 2011

Filamu ya Maalim Seif yatikisaTamasha la filamu Zanzibar

 Maalim Seif Sharrif Hamad akiwa na Mtayarishaji Kiongozi wa Filamu yake, Javed wakati Filamu hiyo ikioneshwa katika ukumbi wa Ngome Kongwe Zanzibar

 
Maalim Seif Sharrif Hamad akiwahutubia wakazi wa Zanzibar waliofurika katika ukumbi wa Ngome Kongwe kushuhudia uzinduzi wa Filamu yake

Safari ya Makamu wa Rais wa Zanzibar kuelekea Ikulu iliyowekwa katika filamu na kampuni ya ZG na kuzinduliwa katika tamasha la 14 la Filamu visiwani Zanzibar juzi ilikuwa gumzo katika Ukumbi wa Ngome Kongwe na kuzoa umati wa watu kuishuhudia na ilizua upya hisia za kisiasa kiasi cha kumlazimu mhusika mkuu kutuliza hisia za watazamaji hao.

Filamu hiyo maalum inayoelezea maisha na harakati za maisha ya mwanasiasa huyo mkongwe ambaye ni makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad imepewa jina la A Journey to the State House na imetengenezwa na kampuni ya ZG inayojishughulisha na mambo ya filamu visiwani humo.


Filamu hiyo ambayo ilibeba umati mkubwa wa wakazi wa Zanzibar ndani ya ukumbi wa Ngome kongwe ilipokuwa ikioneshwa, wengi wa wakazi hao walionesha kuipenda kutokana na mambo mbalimbali yaliyokuwemo katika filamu hiyo na hasa yale yaliyotokea kwenye uchaguzi wa Urais uliofanyika mwaka jana.

Baadhi ya matukio yaliyogusa hisia za wakazi hao ni pamoja na mikusanyiko ya wafuasi wengi wa chama cha wananchi, CUF, ambapo wananchi hao wengi wao walisikika wakisema kuwa waliibiwa kura zao.

Kwa upande wake, Maalim Seif aliweza kuhutubia umati huo ambapo aliwasihi wananchi wa Zanzibar kufuata yale yote mazuri waliyoyashuhudia kwenye filamu hiyo ya maisha yake mpaka harakati zake za kuingia Ikulu.

Pia Maalim Seif aliishukuru bodi ya ZIFF, kwa kuandaa tamasha hilo kila mwaka na kuiletea sifa Zanzibar kwani ulimwengu mzima unatambua umuhimu wa tamasha hilo.

No comments: