Wasanii wanaoitwa Mastaa wa lebo ya Steps
Mkurugenzi wa kampuni ya Steps, Dilesh
HIVI karibuni nilikuwa nabadilishana mawazo na mdau muhimu sana katika tasnia ya filamu hapa nchini, Hamisi Kibari, ambaye pia ndiye mhariri wa gazeti hili. Nilivutiwa sana na kisa alichonisimulia kuhusu dada yake, Rehema Kibari (maarufu kama Mama Rashid), ambaye ni hakimu wa mahakama ya mwazo huko Kilwa Kivinje. Kisa hicho ndicho kimenifanya kuandika makala haya.
Dada huyo alimtembelea Kibari nyumbani kwake, Temeke jijini Dar es Salaam na kutaka kujua kama bado anajihusisha na masuala ya filamu. Kibari ambaye kwa mara ya mwisho alitoa filamu ya 'Mtoto wa RPC' mwaka 2007, akaona huo ni wakati mzuri wa kumuwekea dada yake filamu yake mpya ya Naomi (sinema ya mwisho kuchezwa na Tabia wa Kidedea) aliyomaliza kuihariri na inayotarajiwa kuingia sokoni wakati wowote kuanzia sasa, ili kupata maoni.
Hii ni tabia ya watengeneza filamu makini ambao hupenda kuwawekea filamu wadau kwa ajili ya kupata maoni kabla hawajaiingiza sokoni. Dada huyo alionekana kuiangalia kwa utulivu sinema hiyo kwa takribani dakika tano tu za mwanzo, baadaye akaonekana kuikinai na kujishughulisha na usomaji wa gazeti lililokuwa jirani, jambo lililomfanya Kibari kuhoji.
Dada yake alimweleza kuwa amejikuta akianza kujisahau kama anatazama sinema na kujishughulisha na masuala mengine kwa kuwa hakuziona sura za wasanii wakubwa (huku akiwataja kwa majina) katika tasnia, hivyo hakudhani kama sinema hiyo inaweza kuwa nzuri.
Kibari alimweleza kuwa sinema siyo majina makubwa bali ni mtiririko wa hadithi na ubora wa picha, na kumuomba aiangalie hadi mwisho bila kujali kama kuna msanii mkubwa au la, kwani angehitaji kupata maoni yake ili kuiboresha zaidi sinema hiyo. Yule dada, aliachana na gazeti, akaketi vyema kitini na kukubali sasa kuiangalia japo kwa shingo upande. Lakini kadri muda ulivyokuwa ukisogea alijikuta akivutiwa zaidi na hatimaye kuzama kabisa.
Baadaye yule dada alikiri kuwa yeye alikuwa akiamini (na ndivyo wanavyoamini wengi) kuwa sinema ambazo hazikuchezwa na mastaa wa Bongo haziwezi kuwa nzuri, zenye ubora wala mtiririko mzuri wa hadithi. Lakini baada ya kuiangalia sinema hiyo alisema kuwa kajifunza jambo; kuwa uzuri wa sinema siyo majina bali maudhui na ubora wa picha. Kisha akabainisha kuwa sinema nyingi alizopenda kuangalia zilizoshirikisha wasanii wakubwa zilikuwa zinakosa mtiririko mzuri katika hadithi kulinganisha na sinema hiyo ya Naomi.
Hapa ndipo penye shida kubwa, shida iliyosababishwa na msambazaji mkubwa wa filamu hapa nchini, Steps Entertainment, kupandikiza sumu kwa watazamaji kuwa sinema nzuri ni ile iliyowashirikisha wasanii wakubwa, hasa waliopo kwenye lebo yake.
Sikatai, wapo baadhi ya wasanii wakubwa ambao binafsi nawakubali sana, kwani wanaweza kuigiza sehemu yoyote na wakavaa uhusika ili mradi tu wapate muongozo (script) mzuri na muongozaji mzuri. Ila hii sumu iliyopandikizwa kwamba sinema zote zisizowashirikisha wasanii wakubwa ni mbaya kwa maana ya kukosa ubora au kuwa na stori mbaya ni sumu mbaya kabisa kwenye soko letu la filamu.
Si kila anayeitwa msanii mkubwa basi anaweza kuja na stori nzuri ama kuigiza vizuri, kwani wengine umaarufu wao umepatikana kwa kujitengenezea kashfa kwenye magazeti, au kwa kubebwa. Wengi wao hawabadiliki kabisa, kila sinema wanavaa uhusika uleule. Na kuna hili la mtu akitoka kwenye u-miss tayari anakuwa muigizaji nalo ni tatizo kubwa linalowafanya kujisahau juu ya mionekano yao.
Pia kutokana na kukwezwa na msambazaji, wanaojiita mastaa wanajisahau sana, mfano kuna sinema moja ambayo wasanii wakubwa waliigiza eti ni wanafunzi wakati wakiwa wameweka 'wave' kichwani. Sikuelewa kwa nini hawakutafuta wanafunzi au wanaofanana na wanafunzi! Kwani ilikuwa ni lazima wao waigize? Ieleweke kuwa kuna haiba (personalities) ambazo hazifai kwa muktadha fulani, kwa mfano; mtu kuigiza mkurugenzi mkuu wa kampuni tajiri (wakati haonekani hivyo) hata kama filamu ni yake, ni kutoitendea haki taaluma ya filamu.
Sinema nyingi za wasanii hawa hazina mvuto na zimejaa vituko vya walinzi wa magetini tu huku waigizaji wakiwa wanajirudiarudia katika sinema zote. Pia zinakosa mtiririko mzuri wa hadithi. Tatizo hapa ni ubinafsi uliosababishwa na kampuni hiyo ya Steps kuwakweza kiasi cha kujiona siku hizi wao ni watunzi wazuri, waigizaji wazuri na waongozaji wazuri, hivyo wanajichagua wenyewe.
Sinema nyingi za wasanii hawa hazina mvuto na zimejaa vituko vya walinzi wa magetini tu huku waigizaji wakiwa wanajirudiarudia katika sinema zote. Pia zinakosa mtiririko mzuri wa hadithi. Tatizo hapa ni ubinafsi uliosababishwa na kampuni hiyo ya Steps kuwakweza kiasi cha kujiona siku hizi wao ni watunzi wazuri, waigizaji wazuri na waongozaji wazuri, hivyo wanajichagua wenyewe.
Watazamaji wa sinema za Tanzania wanapaswa kuelewa kuwa hali hii imefanywa kuwa hivi kwa makusudi kabisa ili kuwabeba watu fulani ambao wapo chini ya msambazaji huyu mkubwa na kumfanya apate faida kubwa zaidi wakati huohuo ikiwashusha wengine ili kuua soko la wasambazaji wengine wasiokuwa na uwezo wa kuwatumia wasanii hawa wenye majina makubwa.
Lakini kibaya katika hili, kilichonifanya nichukue hatua ya kulipigia kelele jambo hili, ni kile kinachoonekana kuwa ni kuua vipaji vinavyochipukia katika tasnia ya sinema. Nimekuwa nikiona watu wengi kabla ya kununua filamu hupenda kwanza kuuliza imechezwa na wasanii gani wakubwa, endapo wataelezwa kuwa hakuna msanii mkubwa aliyecheza, wengi wao (hata kama watanunua) basi ni kwa shingo upande. Hii ni sumu mbaya katika tasnia ya filamu inayopaswa kuondolewa kabisa.
Ninawalaumu Steps kwa hilo kwani nina ushahidi kwamba kwao uzuri wa filamu unaanzia kwenye majina ya waliohusika wakati hili si suala la kitaalam (professionalism). Kila anayepeleka filamu yake pale huulizwa kama kawahusisha wanaoitwa mastaa na ‘wakiitunuku’ basi humtaka awahusishe mastaa japo kwenye onesho (scene) moja, kitu ambacho pia ni kinyume cha taaluma ya sinema (unprofessional).
Sanaa ya filamu ni kioo (reflection) cha jamii yoyote, kwenye maisha sinema mara nyingi huonekana kama sanaa halisi ya kisasa. Hutufanya tucheke na kulia, na sisi mara nyingi hupenda kuzichukulia sinema hizi kama kielelezo chetu, husaidia kuwa nuru yetu.
Sinema nyingi zinatengenezwa lakini si zote zinazopata nafasi ya kuonekana: baadhi zinapata chati ya juu na kuwafanya walioigiza kujizolea umaarufu kwa kuwa wanaonekana wakati zingine zinaishia kabatini na kuwafanya wengine kutojulikana. Baadhi ya filamu hizi huibua mada na majadiliano ya wakosoaji wakati zingine watu hawana hata taarifa nazo, kwa kifupi tu ni kwamba baadhi ya sinema hizi 'hupewa dole' wakati zingine wala haziongelewi kabisa.
Lakini ni sinema ngapi kati ya hizi, ambazo zimekuwa zikipata mauzo na mrejesho mzuri? Je, hii inamaanisha kuwa ni sinema nzuri? Maswali haya yanaweza yasieleweke vizuri au yaonekane yapo 'too subjective'. Maana kile kinachoonekana kizuri kwa baadhi ya watu kinaweza kisiwe hivyo kwa wengine.
Kile kinachoonekana kufurahisha watu kadhaa kinaweza kusiwafurahishe wengine. Basi sinema nzuri hasa ni ipi? Kiujumla, tunaweza kudhani kwamba sinema hizo, ambazo zinasemwa kuwa zinapendwa na wengi zinaweza kuchukuliwa kama ndiyo sinema nzuri. Lakini hivi ni sifa zipi ambazo zinahitajika kwa ajili ya kuifanya sinema kuwa nzuri? Kwanza kabisa sinema nzuri inapaswa kutoa burudani nzuri.
Inayogusa hisia zetu: Sinema lazima iweze kugusa mioyo yetu na kutufanya kuzungumza au kuifikiria badala ya kuifanya tu kuwa kitu cha kupitisha wakati. Sinema nzuri inapaswa kuwa na uwezo wa kutufundisha, kutuhamasisha na kuteka hisia zetu.
Inayoelimisha: Sinema nzuri inapaswa kuwa na uwezo wa kutujulisha kuhusu kitu kipya. Siku hizi sinema zinachukuliwa kuwa moja ya zana bora zaidi ya elimu inayotumika kufundisha au kuelimisha watu kuhusu masuala fulani. Kwa kifupi sinema nzuri lazima iwe na chembechembe ya mambo yanayoelimisha watazamaji.
Kioo cha jamii: Sinema nzuri lazima pia iweze kutoa chembechembe zinazotia moyo na kuhamasisha watu kushinda vikwazo ili kufikia mafanikio. Sinema zinachukuliwa kama kioo cha maisha kwa kuwa zinaakisi maisha halisi ya jamii. Kila hadithi ya sinema nzuri hutia msukumo fulani kwenye maisha yetu, kwa kile kinachotokea kwenye jamii yetu.
Lakini haya si yote, kuna baadhi ya mambo mengine ambayo pia huchangia katika kuifanya sinema, ichukuliwe kama sinema nzuri.
Mambo hayo ni kama:
Msuko wa hadithi (Plot): Hii ni sehemu muhimu sana ya sinema. Bila msuko mzuri wa hadithi sinema itashindwa kuvutia na kuwabakisha watazamaji waendelee kuitazama. Hata kama walikuwa wanaiangalia kwa sababu ya kutaka tu kuwaona mastaa fulani, watapoteza kabisa hamu.
Wahusika (Characters): Sababu ya pili muhimu zaidi ya sinema yoyote kuwa nzuri ni wahusika wa hadithi. Bila wao hakutakuwa na hadithi na wala msuko mzuri wa hadithi. Wahusika wanapaswa kuwa aina ambayo watazamaji wangewapenda. Kuwa katika uhusika wenye tabia chanya au hasi, na wanapaswa kuwa na sifa fulani ambazo watu wanaweza kuzihusha na maisha yao.
Waigizaji (Actors): Waigizaji wazuri huifanya sinema iwe nzuri. Waigizaji, ambao watavaa uhusika na kufanya kama hadithi inavyowataka na kuwa hai mbele ya watazamaji. Lazima wawe na uwezo mkubwa wa kuonesha uhusika wao vizuri ili watazamaji wadhani kuwa ndivyo walivyo na wala hawakuwa wakiigiza (hapa haimaanishi mastaa kama ilivyopandikizwa, bali wale watakaovaa uhusika kwa kadri hadithi inavyotaka. Kama mwanafunzi aonekane ni mwanafunzi, basi). Wanapaswa kuwa sehemu ya uhusika.
Muswada andishi (Script): Bila kuwa na muongozo uliopangiliwa katika mazungumzo (dialogues) sinema haitakuwa hai. Script ndiyo maisha ya sinema inayowafanya waigizaji kuwa na nguvu ya uwasilishaji mzuri. Wanaweza hata kuwafanya watu kuiangalia sinema hiyo kila mara bila kuchoka.
Mandhari (sceneries): Mandhari nzuri katika sinema, zinazoendana na uhalisia wa maudhui husika na matukio (scenes), pia vinaweza kushawishi na kuwateka watu kuipenda sinema. Lakini kuna tatizo siku hizi la watu kuamini katika majumba ya kifahari na magari hata kama hayajengi uhalisia wa Watanzania walio wengi. Hii pia inaanza kuwa sumu kwa waigizaji na hata watazamaji wa Kibongo na kuna siku nitaizungumzia kwa kina.
Tukutane wiki ijayo kwa ajili ya kujua mwendelezo wa sumu iliyomwagwa na kampuni ya Steps.
1 comment:
Ni kweli kabisa watu wanaojiita watunzi wanakurupuka tu na kuweka script zisizo na kichwa wala miguu. Nakubali Kibari ni mtunzi mzuri hata hadithi zake nyingi ktk magazeti ni za kutumia akili. Natamani ningepata majina ya watu waliocheza filam ya USIKU WA TAABU. Na wapo wapi kwasasa??
Asante.
Post a Comment