Oct 3, 2012

Skendo ya picha chafu, hivi Watanzania tumeingiwa nini?


Wasanii wa filamu Aunt Ezekiel na Wema Sepetu wakiwa jukwaani

INASHANGAZA sana! Katika kipindi cha miaka michache tu iliyopita taratibu kumeingia mdudu mbaya sana katika tasnia nzima ya burudani, huku tasnia ya filamu ikionekana kuongoza. Tumekuwa tukishuhudia jinsi wasanii wa kike wanavyokuwa nusu watupu kitu kinachosemwa eti ndiyo maendeleo (kupiga hatua), na pengine inabainishwa kuwa hiyo ndiyo dalili ya kuwepo kwa mafanikio katika tasnia hii.

Wachambuzi na waandishi wengi wa habari wamekuwa wakiandika makala/uchambuzi kuwaponda wasanii wenye tabia hizi, lakini wakasahau kuwa hata vyombo vya habari (wakiwemo wao wenyewe) haviwezi kukwepa kuwa ni sehemu ya kashfa hizi, kwani vyombo vya habari ndivyo vimekuwa mstari wa mbele kusambaza, japo vyombo hivyo hivyo kwa njia ya ajabu sana vimekuwa pia mstari wa mbele kulaani.

Binafsi, nadhani kuwa haiwezekani nguvu ya kupita tu ikatusababishia mabadiliko tunayoyashuhudia sasa kwa kisingizio cha utandawazi au maendeleo. Ni vyema tukaelewa kuwa aina ya kazi au uzalishaji kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watu na jamii huleta athari katika uundaji wa utamaduni pia.

Mpango wa kutuwekea picha za wasanii walio nusu utupu kwenye kurasa za mbele za magazeti yetu ulianza polepole ukiwa umepambwa na maelezo kuwa hiyo ni njia ya kurekibisha tabia, au mara nyingine ulifanywa kwa kisingizio cha kuonesha jinsi wasanii wetu walivyochanganyikiwa kwa kuiga tamaduni za Magharibi.

Inashangaza sana kuona magazeti yanashupalia kutafuta picha mbalimbali zinazowaonesha wasanii wa kike wakiwa watupu, na wakati mwingine hata video zimekuwa zikitafutwa kwa udi na uvumba na hata kwa matangazo ya hadharani ya kuahidi fedha nyingi, na baada ya hapo kupenyezwa kwenye vyombo vya utangazaji mpaka watoto wadogo wanaweza kupata taarifa hizo bila hata kuhangaika.

Kwa sasa imekuwa ni fasheni kwa wasanii karibu wote wa nchi hii, maarufu na hata wasiokuwa maarufu, kujitangaza kwa njia ya skendo kwa kisingizio cha kutafuta ‘promo’. Bahati nzuri wasanii karibu wote wa nchi hii nawafahamu vizuri sana, wengi ni rafiki zangu na baadhi yao nimefanya nao kazi huku wengine nikiwa nimewasaidia kuingia kwenye fani ya sanaa ya filamu na maigizo.

Naelewa kuwa wengi wao huwa wanajipeleka wenyewe kwenye vyombo vya habari, huwatafuta waandishi na kupiga picha chafu ili kujitengenezea skendo mbaya kwa dhumuni la 'kutoka kisanii', ndiyo maana wengi wao hata wakiandikwa vipi huwasikii kulalamika au kuchukua hatua zozote za kisheria. Si hivyo tu, hata pale wasanii wanapohisi umaarufu wao kuanza kuchuja huwatafuta waandishi wa magazeti na kutengeneza skendo kwa kile wanachodai ‘kuosha nyota!’

Kwa sasa huyu mdudu wa skendo na picha chafu ameenea kwenye sekta nzima ya burudani, hii inatokana na dhana mbaya ya ‘biashara ni matangazo’ ambayo ndiyo imesababisha hatari hii tunayoishuhudia leo. Huu msemo wa ‘biashara ni matangazo’ umekuwa ukichukuliwa vibaya na ni hatari sana si tu kwa uhai wa maadili katika sanaa, lakini pia kwa uhai wa maadili katika vyombo vya habari. Vyombo vya habari pia vimeingia kwenye mkumbo wa ‘biashara ni matangazo’ kwa kutuwekea picha za utupu na skendo feki ili ‘wauze’.

Dhana hii imekuwa chachu ya kuchochea sanaa chafu na inakinzana na tamaduni zetu kwa kisingizio cha kuuza. Hata hivyo ieleweke kuwa dhana ya biashara ni matangazo inakubalika katika biashara zisizohusiana na sanaa, burudani au utamaduni kwa kuwa inapotumika kuhusisha kazi za sanaa husababisha uchafu huu tunaouona.

Wengi wa wanaojiita mastaa wa Bongo waliopata umaarufu kupitia skendo za magazetini, au wanaokubali picha zao za utupu zitumike kwenye vyombo vya habari huwa hawaijui thamani ya ustaa wao. Hata skendo zao za ngono mfululizo tunazoziona kwenye vyombo vya habari ni ujinga mtupu!

Inashangaza kuona mtu akitokea kwenye filamu moja au mbili tu, tena kwa kushirikishwa kwenye sehemu ndogo sana ya sinema hiyo, ataanza kujiita staa na kujiingiza kwenye kujitafutia skendo kwenye magazeti ili asomwe. Ndiyo maana utakuta kila kukicha kunaibuka skendo za aibu kibao!

Hali hii si katika filamu pekee kwani ipo hata katika muziki kupitia video za muziki, hivi inakuwaje vyombo vya habari kuruhusu video za wasanii maarufu duniani kurushwa bila hata kuangalia maadili yaliyomo humo yanaendana vipi na hadhi ya nchi yetu? Tunawaandaaje watoto wetu kwa kuruhusu kurusha sanaa chafu za aina hii kwenye vyombo vyetu vinavyoangaliwa na kila rika? Je, vyombo vya kudhibiti maadili kama Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza na Baraza la Sanaa la Taifa viko wapi katika hili? Mbona kimya?

Hali hii kwa sasa inakuwa ngumu hata kwa watoto kukwepa kupata picha, video na taarifa hizo hata kama tukiamua kuwafungia ndani, TV itawaletea au mazungumzo mazito ya vipindi vinavyoendelea siku hizi katika radio zetu mida ya kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 7 mchana. Bila hata kuwepo na chembe ya staha hali hii imekuwa kubwa kwa kisingizio kikubwa cha uhuru wa kutoa habari.

Hili la wasanii kujitokeza hadharani wakiwa nusu watupu linaendeleza kile ambacho nimekuwa nasisitiza kuwa ‘wasanii ni kioo cha jamii’ japo baadhi ya watu wanadhani kuwa kwa sasa si hivyo tena. Maneno haya yanayotokana na tafsiri ya maneno ya Kiingereza “Artists are the mirror of the society”, usemi uliozoeleka sana katika vyombo vya habari na hata baina ya wasanii wenyewe, na ninaamini kuwa msanii asiyeitafsiri jamii yake hujikuta yuko peke yake akiwa hana wapenzi wala washabiki.

Siku zote wasanii wataendelea kuwa ‘kioo cha jamii’ na haya yote yanayoendelea katika vyombo vya habari, kwenye filamu zao na hata kwenye video za muziki yanaonesha zao halisi la jamii yetu ilivyo kwa sasa. Kitendo chochote cha kuukana ukweli na kuwatupia lawama wasanii peke yao huku tukiwabeza kwa maneno haya na yale ni sawa na kukataa kutumia kioo jambo ambalo si njia ya kubadili ubaya wa sura zetu.

Naamini kuwa tatizo tulilonalo hapa si wasanii kupiga picha za nusu utupu wala kazi zao, kwani wao ni sehemu tu ya jamii hii, tatizo lililopo ni mmomonyoko wa maadili katika jamii nzima, na hili limedhihirishwa na vyombo vyetu vya habari.

Tumeshafika hatua ya wasanii wengine kuamini kuwa jamii haina tatizo na jambo hilo kiasi cha mtu kukaa mtupu katika jukwaa wakati akiangaliwa na maelfu ya watu, na kwa vile teknolojia imekua, wanapokaa katika hali ya utupu ni sawa na kukaa utupu kwenye macho ya ulimwengu mzima!

Imefika wakati, tena nadhani tumechelewa kulisema hili; ni lazima sasa tufungue mdomo na kusema kuwa inatosha. Hata nchi ambazo tunaziiga, huwa zina staha zake kutokana na mila za huko. Picha hizi za utupu zisiwe zinapatikana kiholela hivi, kama ni vipindi vya TV basi zichambuliwe na zihamishiwe vipindi vya usiku wakati watoto wamelala, magazeti yenye picha za aina hii yatafutiwe njia za kuratibu, ikiwezekana picha hizo zisiwekwe kabisa ukurasa wa mbele ambapo hata watoto wanaona mara moja.

Pia tuache unafiki wa kuhubiri tusichotenda na kutenda tusichohubiri, hasa kwa vyombo vya habari ambavyo kila siku ‘vinashadadia’ kutuonesha picha za utupu kwa kisingizio cha kurekebisha tabia. Ni mambo ya ajabu: unapigaje picha ya binti akiwa mtupu usiku wa manane kisha unaweka katika ukurasa wa mbele wa gazeti lako asubuhi na kudai eti unamrekebisha mtu tabia? Hapa sioni kama kuna kurekebishana, bali kiukweli tunasambaza tu yale yaliyokuwa siri usiku na kuyaweka hadharani hata kwa watoto.

Haya yanafanyika huku vyombo vya kuyasimamia vikiwepo na havisemi kitu. Hivi huu Utamaduni ambao kila siku tunauhubiri una picha gani? Hivi viongozi wanaosimamia haya maadili wanajua kweli mila na desturi za jamii zetu? Ndiyo maana sioni ajabu ninapomshuhudia Mkurugenzi wa Utamaduni anapoomba apigiwe Kwaito katika sherehe ya Kitaifa! Najua tumeshapotea sana baada ya miaka 50 ya uhuru, tusisubiri miaka mingine 50 ili kuyarekebisha haya.

Watanzania wote kwa ujumla wetu tuzinduke, tuache unafiki na kufikiria kuwa hatuwezi kufanya biashara bila dhana mbaya ya ‘biashara ni matangazo’ kwa kupiga picha za utupu au kuonesha picha za utupu kwenye vyombo vyetu, huko tunakokwenda si kuzuri. Tunapaswa sasa kwa ujumla wetu tujitambue kuwa sisi ni Watanzania na tunapaswa kuilinda Tanzania yetu na vizazi vyetu kwa kuepuka mambo yanayokwenda kinyume na maadili ya jamii zetu.

Alamsiki.

No comments: