Katibu Mtendaji wa Basata, Ghonche Materego
Baraza la Sanaa la Taifa
(Basata) limewaagiza viongozi wa Mashirikisho ya sanaa hapa nchini kufuatilia
kwa karibu matukio ya ukiukwaji wa maadili yanayoendelea katika Sanaa hivi sasa
na kuchukua hatua kwa wanaobainika kufanya hivyo.
Mbali na Basata kuwakemea vikali wasanii wanaotumia majukwaa kwa kuidhalilisha Sanaa wao
wenyewe na Watazamaji pia limeyataka mashirikisho kushirikiana na vyama vyao
kuwaita wale wote watakaohusika na uvunjwaji wa maadili ili kuwakanya katika
hatua ya kwanza na kama wasipoacha tabia hizo Baraza litawafungia
kujishughulisha na kazi ya Sanaa hapa nchini.
“Shirikisho la Muziki
limeagizwa kuangalia tungo za wanamuziki zenye maneno yenye lugha isiyofaa,
Shirikisho la Sanaa za Ufundi limeagizwa kuwachukulia hatua wasanii wachoraji
na wachongaji wanaotengeneza Sanaa zinazokiuka maadili. Aidha Shirikisho la
Sanaa za Maonyesho wameagizwa kufuatilia wasanii wote wanaocheza bila staha
majukwaani. Na mwisho Shirikisho la Filamu limeagizwa kuwaita, kuwaonya na
kuwachukulia hatua wasanii wote katika fani ya Filamu wanaovaa nusu utupu bila
kuzingatia husika katika kazi za Sanaa,”
Aidha Baraza limewaagiza wamiliki wa
kumbi zote za burudani kuzingatia maadili pale ambapo Sanaa zitakuwepo jukwaani
na kwamba Baraza halitasita kuufungia ukumbi wowote utakaokiuka agizo hilo . Pia vyombo vya
usalama vimeombwa kuhakiki muda wa vibali vya maonyesho na bila kuchelewa
kuwachukulia hatua stahiki wasiozingatia muda wa maonyesho.
Na wamiliki
wa vyombo vya Habari na Wahariri wamekumbushwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa
na wasimamizi wa sanaa kwa kutokurusha wala kutangaza maonyesho ambayo kwa njia
yoyote yanachangia mmomonyoko wa maadili ya Taifa letu. Kwa suala hili,
Baraza linaziomba mamlaka zinazohusika na usimamizi wa uendeshaji wa vyombo vya
habari nchini kuingilia kati na kuvichukulia hatua vyombo vya habari ambavyo
kila siku vimekuwa mstari wa mbele kueneza wimbi la mmomonyoko wa maadili hapa
nchini na kushusha hadhi ya Tasnia/Sekta ya Sanaa nchini.
Sanaa ni kazi na
Sanaa ni kioo cha Jamii.
No comments:
Post a Comment