Oct 10, 2012

Mtalalamika na kuponda kazi zetu hadi lini?


Cover ya filamu ya handsome wa Kijiji

WIMBI la wanaojiita wakosoaji wa filamu nchini limeibuka kiwa kasi ya ajabu, wengi wamecharuka kuandika maoni na ujumbe mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii wakiponda sinema za Kitanzania kila kukicha pasipo hata kutoa ufumbuzi wa nini kifanyike ili kuboresha kazi zetu.

Mojawapo ya ujumbe maaruf unaotumika kuponda sinema za Kibongo katika mitandao kama facebook, Jamii Forums na twitter ni huu:
Utajuaje ni Bongo Movies: Jini akifika barabarani anaangalia pande zote ndo avuke barabara; Matajiri majumba yao yana askari badala ya electric fence & gates; Trailer inachukua dakika 40; Part 2 ya movie ukiiona mwanzo unajua part 1 ilikuwaje; Madem wanaamka wana makeups usoni na hereni kabisa; Wakifika hotelini imezoeleka ni juice inaagizwa au wine isiyofunguliwa; Nusu saa mtu anatembea,anafanya mazoezi, anakimbizwa ananunua vitu; Wimbo wa malavidavi unaimba mpaka unaisha; Mtu yupo village, life gumu ana wave kichwani; Wote wanaouwawa kwa bunduki hupigwa kifuani au tumboni sio kichwani; Jambazi lazima awe anavaa miwani nyeusi na mvuta sigara; Tajiri anakuja kumpenda maskini.

Tangu kuanza kwa karne ya 21 nchi yetu imeshuhudia ongezeko kubwa sana la utengenezaji na utoaji wa sinema kila kukicha, hali inayoambatana na malalamiko kutoka kwa wadau, wasomi na wakosoaji kuwa sinema zetu zinakosa kabisa ubora na hazikidhi matakwa ya jamii.

Ieleweke kuwa ukosoaji wa filamu duniani ni uchambuzi na utathmini wa filamu, iwe kwa mtu mmoja mmoja au kwa pamoja. Kwa ujumla, kazi hii ya ukosoaji wa filamu inaweza kugawanywa katika makundi mbalimbali kama vile mapitio ya filamu yanayofanywa na waandishi wa habari ambayo huonekana mara kwa mara katika magazeti, na njia nyingine maarufu, kupitia maduka ya usambazaji, au ukosoaji wa kitaaluma ambapo wasomi na wanataaluma katika filamu hutoa taarifa na nadharia ya filamu na kuchapishwa katika majarida.

Wapitiaji wa filamu hufanya kazi kwenye magazeti, majarida, vyombo vingine vya habari, na machapisho mengine kwenye mitandao, hasa hupitia kazi mpya zilizotoka karibuni au zilizo mbioni kutoka ili kuuhabarisha umma. Kwa kuichambua filamu kitaaluma na kuweka wazi mapungufu na hata mazuri yake hasa kwa filamu ambazo zipo karibuni kutoka inaweza kuwa na impact kubwa katika kile ambacho kama mapitio hayo yatakuwa yenye tija watu wataamua kuitafuta filamu.

Kwa vyovyote vile upitiaji mbovu (poor review) wa filamu au kutafuta makosa tu (kuponda) bila kuangalia mazuri unaweza kusababisha hasara kwa waandaaji husika wa filamu na kuathiri mauzo ya filamu husika, na ndiyo chuki binafsi zinapoanzia.

Katika siku za hivi karibuni, mapitio na ukosoaji wa filamu nchini yamekuwa yakizua mjadala mkubwa, hasa pale wapitiaji na wakosoaji hawa walio wengi wanapoonekana kulenga zaidi katika kuponda tu na kushindwa hata kuyaona mazuri machache yaliyopo kwenye kazi husika jambo linalowachukiza waandaaji wa kazi hizo.

Kwa kawaida, kama ni mpitiaji au mkosoaji wa filamu, kabla hujaanza kutoa makosa ni lazima kwanza ueleze yale mazuri (hata kama ni moja) uliyoyaona, kisha ndipo ueleze makosa uliyoyaona na kuelekeza namna nzuri ya kuyarekebisha ili mtayarishaji, msanii au muongozaji husika asije akayarudia tena. Hii ni aina nyingine nzuri ya kupeana darasa na inaweza kuwasaidia wasanii ambao hawakubahatika kukaa darasani.

Badala yake tumekuwa tukishuhudia kuongezeka watu wanaojiita wakosoaji ambao kiukweli hawakosoi bali wanaponda, inawezekana kwa chuki au kwa kutokujua pia. Ndiyo maana hushauriwa kuwa mkosoaji wa filamu lazima awe na elimu ya filamu ili iwe rahisi kwake kuitazama filamu kitaaluma zaidi badala ya kuvutwa na shabiki.

Kuna wale wanaofikiria kuhusu soko la filamu, kwa kutumia utamaduni na vyombo vya habari vya kijamii pamoja na njia za jadi za matangazo, jambo ambalo limekuwa likiwafanya wapitiaji hawa katika ukosoaji kujijengea uhalali ambao hata hivyo hauwafikii wahusika walio wengi.

Ni kweli kuwa watunzi wa filamu nchini hawana mafunzo maalum ya uandishi wa miongozo ya filamu na michezo ya kuigiza (Script), nddiyo maana tatizo kubwa lililopo kwenye filamu (nyingi) za Kitanzania ni uwezo mdogo wa uandishi wa miongozo, kitu ambacho kinasababisha filamu na michezo mingi ya kuigiza kuonekana kuwa haina muelekeo.

Pia waigizaji wa Kitanzania wengi ni wazuri katika uigizaji lakini si katika kuandaa miongozo ya filamu, na kwa kuwa lengo ni kuzifanya filamu za Kitanzania kuwa na ubora, hawa wanaojiita wakosoaji kwa pamoja wangehimiza katika kuwataka waandaaji kupata mafunzo ya sanaa na uandishi wa miongozo.

Sisiti kusema kuwa nina mashaka sana na uwezo ama mbinu wanazozitumia hawa wanaojiita wakosoaji katika kufikisha ujumbe wao, nina shaka kama kweli wanafanya tafiti za kutosha kuhusu sekta hii, na kama wanafanya basi zitakuwa ni za juujuu tu. Huwezi kukosoa sinema za Kitanzania kwa kuzilinganisha na za Hollywood, vinginevyo utakuwa na matatizo ya uelewa.

Kama kweli hawa wanaoponda wana nia ya dhati ya kutaka kazi za Kitazania ziboreke basi wanapaswa kwanza kufanya tafiti za kina kabla hawajakimbilia kuziponda filamu za Kitanzania kwenye mitandao, wao pia wanapaswa kusoma ili kuondokana na pazia la uzuzu linalowafunika usoni wakashindwa kuyaelewa mazingira halisi ya tasnia ya filamu. Baada ya kuelimika na pia kujiridhisha na tafiti zao ndipo waanze kutafuta njia sahihi za kuwasaidia watengeneza sinema na si kuishia kuponda tu.

Ni kweli kuna makosa katika filamu za Kitanzania, kati ya hayo yapo ambayo hayahitaji uwe na bajeti kubwa bali ni ufahamu na ujuzi, na kuna makosa yanayosababishwa na ufinyu wa bajeti na mfumo mbovu uliopo nchini.

Tuelewe kuwa kila fani ina elimu yake, sio mtu unakurupuka tu kwa kuwa umezoea kuangalia sinema za Hollywood na Ulaya basi unajiona wewe ni mkosoaji wa filamu. Elimu ya filamu umeipata wapi? Au na wewe uko kwenye ule mkumbo ule ule wa hao unaowaponda wa “usanii upo kwenye damu!” Sijui ukosoaji nao ni kipaji? Au kwa lugha nyingine “ukosoaji upo kwenye damu!”

Katika elimu ya filamu hufundishwa nidhamu (academic discipline) inayohusu mambo mbalimbali ya kinadharia, historia, na njia bora za uhakiki makini wa sinema (critical approaches to the cinema).

Sekta ya filamu ni sekta pana sana inayojitegemea kwa kila idara, huwezi kuifananisha na soka au sanaa nyingine. Sekta ya filamu hapa Tanzania imeachwa tu kama mtoto yatima asiye na mlezi na anayejitafutia chakula chake mwenyewe huku akibezwa, kuchekwa na kusimangwa na jamii inayomzunguka ambayo ilipaswa kumsaidia ili aondokane na hali duni.

Wote sisi ni mashahidi jinsi mabenki yetu, wawekezaji na makampuni makubwa hapa nchini yanavyokimbilia kuwekeza kwenye soka (ambalo hata hivyo bado halina mwelekeo), kwenye mashindano ya urembo (yanayoendeleza tamaduni za Kizungu) na kukumbatia tamthilia za nje.

Wakati sasa umefika kwa serikali na wadau wote (wakiwemo hawa wanaoziponda filamu za Kitanzania) kuwekeza nguvu nyingi katika kuhakikisha elimu kwa waandaaji wa filamu inatolewa. Nampongeza sana dada yangu, Vicensia Shule (Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) kujitoa na kuandaa sinema ya Chungu ambayo kiukweli ni somo tosha kwa watengeneza sinema wa Kibongo.

Wakati sasa umefika kwa serikali, wadau na wenye taaluma ya fani hii kufanya kwa vitendo kile wanachokiongea kila siku katika kuhakikisha kuwa sekta hii inakua na kutengeneza sinema na michezo ya kuigiza iliyo bora na siyo kusubiri vijana wasio na taaluma, mitaji na wala hawajawezeshwa wanapojitoa mhanga kutengeneza filamu na kukosea ili nyinyi muwe wa kwanza kuwatupia mawe.

Hata hivyo, juhudi na nguvu zaidi zinahitajika katika kufanikisha mapambano ya kuwakomboa wasanii, watengenezaji sinema na wasambazaji wa kazi za sanaa hapa nchini ili wapate malipo/mapato stahiki kutokana na kazi zao kitu kitakachopelekea kuboreka kwa tasnia hii hapa nchini.

Kwa kufanya hivyo na kuwawezesha wasanii na watengeneza filamu, sekta hii itakua mara dufu na kufikia kiwango kinachokubalika.

Vijana wa taifa hili tutajisikia fahari kuitwa Watanzania na hatimaye kuwa taifa ambalo vijana wake ndoto zao si kuzamia “Majuu” kama ilivyo sasa bali kuutangaza utamaduni, utalii, na historia za mashujaa wetu kupitia filamu.

Naomba kutoa hoja.

No comments: