Sep 14, 2012

Tanzania na nchi za SADC bado zina nafasi ya kufanya vizuri


Wakati wa upigaji wa sinema ya Tsotsi, nje ya jiji la Johannesburg

NCHI za kusini mwa Afrika zina nafasi kubwa ya kutoa mchango katika tasnia ya filamu na televisheni duniani. Kumekuwepo makubaliano miongoni mwa wadau na wachunguzi wa tasnia hii, kwamba, utajiri uliopo wa ubunifu miongoni mwa vijana na hadithi zilizopo katika ukanda huu vitumike vyema. Hata hivyo, pia wote wanakubaliana kwamba tasnia ya filamu katika nchi hizi bado iko chini sana na, katika hali halisi, inazidi kushuka.

Utafiti unaonesha kuwa tasnia ya filamu ya nchi za SADC ni ndogo na haijapiga hatua, ingawa inaonekana kutoa fursa nyingi katika kuendeleza miundombinu na hadithi zetu. Makampuni mengi katika sekta hii ni madogo madogo na yanayoonekana kuchangia katika ajira na ukuaji wa uchumi.

Matatizo ya kupata fedha za kutengenezea filamu ni moja ya kikwazo kikubwa kwenye maendeleo ya sekta ya filamu na televisheni katika nchi hizi. Hii inajumuisha ufadhili kwenye sekta ya umma na sekta binafsi. Kazi nyingi ukiiacha Afrika Kusini, mara nyingi hutegemea fedha za wafadhili na vyote; serikali za kitaifa na wawekezaji binafsi mara nyingi huchukulia sekta hii kama sekta isiyo ya uhakika.

Baadhi ya wachambuzi wa utamaduni katika ukanda huu wanasema kwamba nchi za SADC, ukiachia Afrika Kusini, kiukweli haziwezi kujisema kuwa zina tasnia ya filamu, ila zina malighafi za filamu. Ila huu si mtazamo katika makala haya. Kazi nyingi za tasnia hii zinapatikana katika baadhi ya nchi za SADC.

Kuna mtikisiko wa nchi zilizozungukwa na nchi nyingine (enclaves), hata hivyo tasnia ya filamu bado ni ndogo sana, inayotegemea wafadhili na iliyokosa pesa za kutengenezea filamu. Afrika Kusini inaonekana kuwa nchi pekee katika ukanda huu ambapo uwekezaji kutoka sekta binafsi (kinyume na ufadhili) kwa ajili ya uzalishaji filamu unapatikana bila matatizo.

Mwaka 2000, ilikisiwa kwamba ni chini ya asilimia 2 tu ya Wa-Afrika waliotazama filamu za Ki-Afrika. Uzalishaji katika bara la Afrika ulifikia kilele katika miaka ya 1980, wakati ambapo filamu 30 (si hizi homevideo tunazotengeneza na kuziita filamu) zilizalishwa kwa mwaka, zaidi kwa msaada mkubwa kutoka wawekezaji wa nje. Idadi hii imekuwa ikishuka tangu wakati huo. Afrika Kusini kwa sasa inazalisha wastani wa filamu ndefu mbili kwa mwaka na ndiyo mzalishaji mkubwa katika ukanda huu.

Filamu za Marekani zinachangia asilimia 70 ya soko la Afrika, wakati filamu za Ki-Afrika zinachangia asilimia 3 tu ya soko lake. Wakati haya yakitokea yanaonesha tatizo kubwa lililopo katika bara hili ambapo katika miaka 85 iliyopita zilitengenezwa zaidi ya filamu ndefu 600 (na idadi kubwa ya filamu fupi), idadi ambayo si tofauti na ile ya Ulaya (ingawa hili ni soko kubwa la watazamaji wa filamu).
Kwa kusema ukweli, hii inaashiria utawala wa tasnia ya filamu ya marekani (Hollywood), kutokana na ukomo wa fedha za kuitangaza (marketing) tasnia ya filamu ya Afrika, na kushindwa kuwashawishi watazamaji wa filamu wa ndani kuangalia filamu za ndani.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Filamu ya Afrika Kusini (Film Resource Unit): Mashirika ya utangazaji na wamiliki wa majumba ya sinema wamekuwa wakisita kuonesha filamu za Ki-Afrika, kwa sababu wasambazaji wa filamu zilizotengenezwa nje, tamthilia na vipindi vya ucheshi (comedy), ni kazi ambazo haziwagharimu pesa kuzizalisha. Matokeo yake, filamu nyingi zilizokuwa zimepigwa marufuku wakati wa zama za ubaguzi wa rangi bado hazijapata nafasi ya kuonekana hadharani, na filamu mpya za Ki-Afrika bado zina kazi kubwa ya kupigania kuoneshwa.

Miaka kumi iliyopita imeshuhudia kuibuka kwa maeneo ya kupigia picha za filamu. Kabla ya mwaka 1994, Zimbabwe ilikuwa ndiyo eneo muhimu la utengenezaji filamu katika ukanda huu, hii ilitokana na miundombinu mizuri iliyopo na uhusiano mzuri kati ya serikali na watengeneza filamu wa nje. Filamu za kupinga ubaguzi wa rangi kama ile ya ‘Cry Freedom’, ambayo isingeweza kutengenezewa Afrika Kusini, ilitengenezewa Zimbabwe. Baada ya mwaka 1994, Afrika Kusini ilivutia zaidi kwa maeneo na utendaji kazi.

Miundombinu maalum katika filamu inaiwezesha Afrika Kusini katika kutengeneza filamu bora za kiwango cha kimataifa. Hali hii, ukichanganya na maeneo yake mbalimbali na hali nzuri ya hewa imeifanya Afrika Kusini kuwa eneo maarufu la kutengenezea filamu. Katika muktadha wa kidunia, hali hii inayafanya maeneo ya Afrika Kusini, Mauritius na Namibia kuwa maeneo muhimu na yenye gharama ndogo za kutengenezea filamu katika ukanda wa SADC.

Utengenezaji wa filamu za makabila na uuzaji nje wa filamu za ndani (filamu na vipindi vya televisheni vilivyofadhiliwa na kutengenezwa kwa maonesho na kurushwa nchini Afrika Kusini) vimekuwa na kiwango cha mafanikio katika nchi zote za SADC. Changamoto kubwa inazozikumba tasnia za filamu za ndani ni ukosefu wa uwekezaji katika sekta binafsi ambazo zingeweza kutoa fedha kwa ajili ya utengenezaji wa filamu bora ambazo zingewuzwa nje.

Umiliki wa vipindi vya ndani kwa vyombo vya utangazaji na tabia ya uvivu wa kufikiri katika kubuni kwenye tasnia ya filamu katika kuhakikisha maendeleo ya mipango ya kuuza nje inaendelea kuikwaza tasnia.

Utafiti uliofanywa na hata baadhi ya wachambuzi katika tasnia ya filamu wanasema kwamba nchi za Afrika zinazozungumza Kifaransa (Francophone Africa) ziko mbele katika uzalishaji wa filamu ukilinganisha na zile zinazozungumza Kiingereza (Anglophone Africa). Cameron Mackenzie anaandika kwamba nchi za Ki-Afrika zinazozungumza Kifaransa zinapata msaada kutoka serikali ya Ufaransa ili kukuza lugha na utamaduni wake.

Serikali ya Ufaransa inachangia kwa kiasi kikubwa katika kutoa fedha za utengenezaji wa filamu (tazama, kwa mfano, filamu za lugha ya Kifaransa kutoka Senegal, Mali, Ivory Coast na Algeria). Kwa kulinganisha, filamu za lugha ya Kiingereza katika bara hili mara nyingi zinatengenezwa kwa msaada wa watu binafsi.
                                      
Nigeria, kwa mfano, ina tasnia ya filamu yenye nguvu, ikizalisha zaidi ya filamu (homevideo) 500 kwa mwaka, lakini nyingi kati ya hizi hutengenezwa kwa bajeti ndogo sana zikiwa pia zinatokana na script mbovu au vifaa duni visivyoweza kuifanya sinema iwe bora kwa ajili ya kuvutia watazamaji wengi”.

Lakini, Gaston Kabore, mtengeneza filamu anayeinukia Afrika anayetoka Burkina Faso anasema kwamba tasnia ya filamu ya nchi za Afrika zinazozungumza Kifaransa haijaendelea zaidi kama inavyodhaniwa, ni tofauti. Maoni yake ni kuwa, Wizara ya Ushirikiano ya Ufaransa imefanikiwa kudumisha uhusiano kati ya Ufaransa na makoloni yake ya zamani na kutoa usaidizi katika uwasilishaji wa filamu za Ki-Afrika katika matamasha ya filamu duniani kote.

Serikali pia zinahusishwa zaidi katika tasnia ya filamu katika nchi za Afrika zinazozungumza Kifaransa. Kabore anasema: “Kwa filamu yangu ya mwisho, nilikuwa na kila aina ya visaidizi katika kufanikisha kazi yangu, kama miundombinu, watendaji, vifaa na magari – ila kiukweli unachoweza kuambulia ni vitendea kazi tu na msaada wa kisiasa, basi.”

Katika nchi za kusini mwa Afrika, kwa wakati huu, hasa nchi za Kiafrika zinazozungumza Kiingereza ziko mbele katika matumizi ya video na utengenezaji wa filamu za makala (documentary-making).

Hata hivyo, nchi za Kusini mwa Afrika zina kiwango kizuri cha miundombinu ya utengenezaji wa filamu na vipindi vya televisheni ukilinganisha na nchi zingine za Afrika nje ya ukanda huu. Miundombinu hii ikiwa ni pamoja na vitendea kazi vya uzalishaji na uhariri, vitenda kazi vya kutolea mafunzo na vifaa. Hata hivyo, filamu zinazozalishwa kutoka nchi za Afrika Magharibi mara nyingi zinachukuliwa kama filamu bora kuliko zinazozalishwa Kusini (ukanda wa SADC).

Sababu moja inayodhaniwa kwa tofauti hii katika ubora ni kwamba kiwango cha mabadiliko katika nchi za kusini mwa Afrika kimekuwa cha haraka sana hivyo watengeneza filamu hupata shida kutokana na matatizo ya kufahamika (kuwa na nembo).

Ni wazi kwamba watengenezaji wa filamu wa Ki-Afrika barani kote wanaweza kujifunza kutoka miongoni mwao, na ni muhimu zaidi, kuzishawishi serikali zao kwa ajili ya kuwapa misaada ya hali na mali katika kuwa wazalishaji wenza (co-productions) na ushirikiano unaovuka mipaka. Ushirika kati ya watengenezaji wa filamu wa Ki-Afrika na makampuni ya filamu kutoka sehemu mbalimbali za Afrika ni jambo zuri kwa kuanzia ili kutoa msaada wa lazima katika kujitegemea ili kuondokana na utegemezi wa wafadhili wa nje.

Alamsiki.

No comments: