Katibu Mtendaji wa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu, Joyce Fisoo
Katibu Mtendaji wa Basata, Ghonche Materego
WIKI iliyopita niliandika makala kuhusu umoja mpya wa wasanii, watayarishaji na wadau wa filamu ulioanzishwa hivi karibuni kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Leaders Club na kuweka historia mpya kwa kuifanya tasnia ya filamu kuzaliwa upya kwa kuwa na kundi moja lenye nguvu na uhamasishaji katika kutafuta maendeleo na pia kupambana na uharamia ambao umekuwa ukiwarudisha nyuma wasanii na kuwanufaisha wachache bila ya wao kutokwa jasho hata kidogo.
Umoja huu mpya umekuja baada ya kuiona serikali ikianza kuitazama tasnia ya filamu kwa jicho la tatu, ambapo kumekuwepo nadharia kwamba Serikali kupitia Mpango wa Kurasimisha Biashara na Rasilimali za wanyonge nchini (Mkurabita) inataka kuirasimisha tasnia hii ili kuwafanya wasanii wafanye kazi kwenye mazingira yaliyo rasmi kwa kuwa hali ilivyo sasa inawafanya wakose fursa nyingi za kukuza kazi zao na kuongeza vipato.
Juhudi za serikali zilianza kuonekana wakati wa vikao vya bunge la bajeti kwa mwaka 2012/13, hasa kwenye hotuba ya Waziri wa Fedha, William Mgimwa, aliyoiwasilisha mbele ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Waziri huyo alieleza hayo wakati akipendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147, huku akitambua kuwepo kwa kilio cha muda mrefu cha wasanii kurudufiwa kazi zao za sanaa na kukosa maslahi kwa kazi wanazofanya. Akabainisha kuwa ili kutatua tatizo hili, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato itaanza kurasimisha biashara ya bidhaa za muziki na filamu kwa nia ya kuhakikisha kwamba uasili wake unatambulika na hivyo kuzuia vitendo vya kurudufu kazi za sanaa (piracy of artists work) hali ambayo inadumaza ukuaji wa sanaa na vipaji hapa nchini.
Baada ya makala hiyo, mdau na mwanaharakati wa siku nyingi wa filamu nchini, Ignas Mkindi, aliandika kuelezea kuhusu mkanganyiko uliopo sasa baina ya taasisi mbili za serikali kuhusiana na mustakabali wa filamu nchini.
Mkanganyiko huu unatokana na hali halisi ambayo hadi sasa wasanii na wadau wote wa filamu bado tupo njia panda kwa kuwa usimamizi wa tasnia ya filamu bado unasimamiwa na Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya mwaka 1976 ambayo ndiyo iliyounda Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza.
Mwanaharakati huyu anabainisha kuwa hata ilipoundwa sheria namba 23 ya mwaka 1984 iliyoanzisha Baraza la Sanaa la taifa (Basata) kwa kuunganisha Baraza la Sanaa la Taifa na Baraza la Muziki la Taifa na kuitambua Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa ya mwaka 1974, bado haikuifuta sheria ya filamu na michezo ya kuigiza ya 1976 wala haikuwa na lengo la kulipa Baraza la Sanaa la Taifa nguvu ya kusimamia filamu kama ambavyo wamekuwa wanajaribu kufanya hivi sasa.
Mwanaharakati huyu anabainisha kuwa hata ilipoundwa sheria namba 23 ya mwaka 1984 iliyoanzisha Baraza la Sanaa la taifa (Basata) kwa kuunganisha Baraza la Sanaa la Taifa na Baraza la Muziki la Taifa na kuitambua Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa ya mwaka 1974, bado haikuifuta sheria ya filamu na michezo ya kuigiza ya 1976 wala haikuwa na lengo la kulipa Baraza la Sanaa la Taifa nguvu ya kusimamia filamu kama ambavyo wamekuwa wanajaribu kufanya hivi sasa.
Hivyo, ukiangalia kwa umakini zaidi, utagundua kuwa pamoja na tafsiri nyingine za kazi za sanaa katika sheria iliyounda Basata kipengele cha 2(a)(iv), kazi ya sanaa inayosimamiwa na Basata imetafsiriwa kama 'Picha ambazo hazikutengenezwa kwenye mashine ya picha za filamu (siku hizi wanapenda itambulike kama picha jongefu)'
Sasa mkanganyiko upo kwenye utendaji kazi wa taasisi hizi mbili, Basata na Bodi ya Filamu, kwa kuwa hadi sasa kunaonekana kuingiliana kwa namna fulani katika maamuzi yao juu ya hatma ya tasnia ya filamu nchini. Hatuelewi ni taasisi ipi inayopaswa kuwa na mamlaka zaidi kwani kumekuwepo mkanganyiko kati yao ambao unawayumbisha wasanii na wadau wa filamu.
Serikali inapaswa kuweka wazi, ipi ni mipaka ya Basata na ipi ni mipaka ya Bodi ya Filamu katika mustakabali wa filamu nchini.
Ninavyotambua mimi, filamu ni zaidi ya sanaa, filamu ni suala mtambuka ambalo linahusisha taaluma nyingi, na waigizaji ambao ni wasanii ni sehemu ndogo tu ya tasnia ya filamu ila huwa wanaonekana kuwa na nguvu sana kwa kuwa ndiyo wanaoonekana.
Kwa kuwa wakati inatengenezwa sheria hiyo ya Filamu na Michezo ya kuigiza ya mwaka 1976 hakukuwa na televisheni, hakukuwa na wasambazaji wa filamu wala hakukuwa na maduka ya kukodisha mikanda ya video maarufu
Katika waraka wake, Mkindi anabainisha kuwa kuliwahi kuwepo juhudi za Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na dhamira aliyokuwa nayo aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Kapteni Mstaafu George Mkuchika, ambapo wizara ilianzisha mchakato wa marekebisho ya sheria hiyo iliyopitwa na wakati ili iwe sheria ya mamlaka ya filamu.
Kwake yeye, huo ndiyo ulikuwa ufumbuzi wa kweli wa matatizo katika tasnia ya filamu. Lakini akabainisha ni nini kilichotokea baada ya hapo. Ni kwamba wadau waliitwa mnamo mwezi Mei, 2009 kujadili marekebisho ya sheria hiyo kwa siku mbili na kutoa mapendekezo
Pia siku ya tatu walifanya uchaguzi wa kamati ya wadau kuangalia namna ya mchakato wa kuunda Shirikisho la Filamu
Baada ya hapo, kulitokea mvurugano mkubwa kati ya Basata, Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza pamoja na wasanii/watayarishaji wa filamu kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa shirikisho la filamu.
Tangu wakati huo hadi sasa mkanganyiko huu umeendelea licha ya kuwa tayari shirikisho la filamu nchini limeshaundwa, na kinachoonekana ni wazi kuwa, kuna baadhi ya watendaji katika taasisi za serikali wanaonufaika na mvurugano wa kisheria uliopo katika usimamizi wa tasnia ya filamu, ndiyo maana wanakwamisha marekebisho ya sheria ya filamu na kuishauri serikali mambo ambayo hayawasaidii wadau wa filamu kwa asilimia kubwa.
Sasa hebu tujiulize, katika mvurugano huu, waathirika ni kina nani? Mkindi anabainisha kuwa wasanii mastaa si waathirika sana katika mvurugano huu, kwa hali iliyopo ni kwamba huwa hawaigizi mpaka walipwe fedha wanazotaka, na hata wakiandaa filamu, wengi wao wanakuwa wameshauza hakimiliki kwa wasambazaji ila wao ndiyo wanapata fursa ya kusikilizwa sana na viongozi wa juu wa serikali kwa kuwa ndiyo wanaoonekana sana kwenye vioo (screen).
Waathirika wakubwa katika mkanganyiko huu ni watayarishaji waliowafanya hawa mastaa wawepo kisha wakawekwa pembeni na mfumo wa wasambazaji kuwapa hela moja kwa moja waigizaji wawatengenezee filamu ambazo wamiliki wanakuwa wasambazaji. Si jambo baya kwa wasambazaji kuwa wawezeshaji wa utayarishaji wa filamu (executive producers), kwa sababu wanafanya biashara kutafuta faida, tatizo lipo kwa watendaji wa serikali ambao wanawafumba macho wasanii wasioelewa na kudhani kuwa maadui wao ni wasambazaji kumbe wao ndiyo maadui.
Na waathirika wengine ni maelfu ya wasanii wachanga/wanaochipukia wanaohangaika kutoka na kuigizishwa kwa malipo kidogo katika filamu hizo za wasambazaji zinazotengenezwa na wasanii mastaa.
Hivyo, kutokana na hali ilivyo, hata hili suala la serikali kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 halina maana ya kutambua uwepo wa kilio cha muda mrefu cha wasanii kurudufiwa kazi zao za sanaa au kukosa maslahi kwa kazi wanazofanya, na hili la kuiagiza Mamlaka ya Mapato kuanzisha stampu halina maana ya kuwakomboa wasanii/watayarishaji, bali ni njia tu ya serikali kutaka kujiongezea mapato yenyewe na sio kusaidia wasanii.
Serikali iondoe kwanza mkanganyiko huu kama kweli ina nia ya dhati ya kusaidia tasnia ya filamu nchini, vinginevyo tutakuwa tunadanganyana.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment