Ingawa jamii na viongozi wa nchi yetu hawawezi kukwepa lawama kwa maendeleo hafifu ya sekta ya filamu na burudani kwa ujumla wake, wasanii, waandaaji na watendaji wengine katika sekta hii walistahili kulaumiwa zaidi kwa kutokufanya jitihada za kutosha katika kuungana na kuwa na umoja madhubuti, kuelimisha na kuwaelewesha wananchi juu ya dhana ya burudani (filamu), mchango wake katika uchumi, ajira na umuhimu wake katika kusimulia hadithi zetu.
Siku zote nimekuwa naamini kabisa kuwa misuguano ya wasanii na watayarishaji nchini imekuwa inawafanya wawekezaji waliokuwa tayari kuwekeza katika tasnia ya filamu kusita kuingia kwa sababu kukosekana kwa umoja ni tatizo kubwa linaloweza kuathiri sekta ya filamu kwa ujumla na kufanya utendaji kazi kuwa mbovu. Utengano ni tatizo ambalo hata aliyekuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi aliwahi kuthibitisha kulijua. Hili tatizo mara nyingi huchangiwa kwa kiasi kikubwa na kutokuwepo malengo, kuwa na mipango mibovu na uchoyo usiokuwa wa lazima.
Pia husababishwa na kutojiamini kwa wasanii na watayarishaji wa filamu nchini ambao wamekosa kabisa mafunzo ya msingi (nitty-gritty) ya namna ya kutengeneza kazi zao katika kiwango kinachokubalika. Hali hii imekuwa ikisababisha watayarishaji wengi wa filamu nchini kuwa wabinafsi na wanaowekeza kidogo na kutarajia wavune mara dufu.
Lakini ukweli ni kwamba watu wachache walikuwa wakifaidika kutokana na mgawanyiko huu, na kusababisha soko letu kuparaganyika na watu walioko sokoni kujaribu tu kupata faida iliyo kubwa zaidi bila kuangalia upande wa pili unafaidikaje. Kwa maana hiyo, mgawanyiko ulikuwa unachochewa zaidi na uchoyo na ubinafsi.
Lakini hivi karibuni kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Leaders Club umejaribu kuweka historia mpya kwa kuifanya tasnia ya filamu kuzaliwa upya kwa kuwa na kundi moja lenye nguvu na uhamasishaji katika kutafuta maendeleo na pia kupambana na uharamia ambao umekuwa ukiwarudisha nyuma wasanii na kuwanufaisha wachache bila ya wao kutokwa jasho hata kidogo.
Nataraji kuwa umoja huu utakuwa ni mwanzo mpya wa tasnia ya filamu na hautaishia kwenye vita dhidi ya uharamia tu bali utakwenda mbali zaidi, hasa baada ya makundi mawili hasimu, Bongo Movie Unity chini ya Jacob Stephen (JB) na Tanzania Film Federation (TAFF) chini ya Simon Mwakifwamba, kuamua kufuta tofauti zao na kuanzisha mwanzo mpya.
Katika mkutano huo, MC mashuhuri katika tasnia ya filamu Tanzania, Susan Lewis (Natasha), alimwita JB, ambapo JB alielezea furaha yake kwa kukutana na wasanii ambao pengine wanahitaji kushiriki katika filamu lakini wamekuwa wakikosa nafasi hiyo kulingana na hali ya soko ilivyo.
JB alibainisha kuwa ana furaha kubwa sana katika moyo wake kuwa pamoja na Rais wa TAFF, na kusema kuwa waliwahi kuwa pamoja toka nyuma na walimpokea katika sanaa na kuwa naye na sasa wapo pamoja tena, na anafikiri ni Ibilisi tu aliwaingilia lakini kwa sasa hana nafasi tena, wao ni kitu kimoja na watapambana na maharamia wa kazi zao, na hawataruhusu tena mtu kuwagombanisha.
Baada ya kuongelea suala la maharamia ikiwa pamoja haramia mashuhuri aliyekamatwa hivi karibuni katika mitaa ya Likoma na Magila, alihimiza wasanii kupendana na kuwa kitu kimoja, kisha Simon Mwakifwamba Rais wa Shirikisho la Filamu alibainisha furaha yake na kuwaomba msamaha wasanii na watu ambao aliwahi kutofautiana nao.
Mkutano huo umechochea kiu ya ukuaji wa soko la filamu, naamini kuwa wasanii hawa watasimamia kauli zao na kuwa kitu kimoja ili kuleta ushindi katika mustakabali wa tasnia ya filamu, kwani sasa sioni jambo lolote linaloweza kuwakwamisha kwa kuwa tofauti na kama ilivyokuwa hapo awali.
Nakubaliana na kauli ya Mwakifwamba kuwa mgawanyiko uliokuwepo uliosababishwa kuzaliwa kwa kundi la Bongo Movie ilikuwa ni chachu ya maendeleo kwa tasnia kwa kuwa walitoa changamoto nyingi sana ambazo zililifanya Shirikisho la Filamu kufanya kazi kwa nguvu sana na kufanikisha mambo mengi yenye maslahi katika tasnia ya filamu Tanzania.
Hata ukiangalia katika tasnia za filamu zenye nguvu kubwa ya soko duniani utagundua kuwa wamefika hapo walipo baada ya kukumbana na vikwazo vingi na hatimaye kugundua kuwa njia bora ya kuwafanya kuthaminiwa na kuwa na soko la uhakika ni wao kuwa na umoja madhubuti. Filamu ni utamaduni, filamu husimulia hadithi zetu, huelezea mila na desturi za jamii husika.
Filamu pia husaidia kutangaza vivutio vya nchi husika na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utalii wa nchi. Hata utamaduni wa nchi husika huidhinishwa kupitia sanaa, elimu kwa jamii nzima hujumuishwa katika sanaa, maadili ya nchi hubebwa na kusambazwa kwa jamii kupitia sanaa, wanasiasa wote hutengenezwa na kukuzwa kwa kiwango kikubwa sana na sanaa.
Si hivyo tu, mambo mengi katika jamii hubebwa na sanaa ikiwemo kupashana habari ambazo zinaweza kuwafikia wanajamii kwa urahisi zaidi na kuweka kumbukumbu zisizofutika akilini mwao hubebwa na sanaa. Katika nchi zilizoendelea waliligundua hili la sanaa kufanya kila kitu kiwe kama kilivyo, na wakaamua kuiheshimu na si kuidharau kama inavyofanyika hapa kwetu.
Nchi za ulaya zimejikita katika kukuza raslimali watu na kuenzi kile kitokanacho na raslimali watu hawa, mtu yeyote au kitu chochote ambacho kinaweza kuwazuia hawa raslimali watu kutimiza wajibu wao, basi inakuwa jukumu la kila mtu kutatua tatizo hilo , huu ni mfano wa kuigwa.
Sanaa ina uwezo mkubwa sana katika kuongeza pato la nchi, kuongeza ajira kwa vijana kwa kiwango kikubwa kuliko sekta nyingine yeyote, kuitambulisha nchi kimataifa na kutangaza vivutio vya nchi na hivyo kusaidia kuwaleta watalii wengi kuvitembelea vivutio hivyo na hivyo kuliingizia taifa pesa nyingi za kigeni kupitia utalii, kujenga uzalendo wa vijana katika kulitumikia taifa lao na hata kuchangia kuijenga nchi kisaikolojia.
Haya yote yatawezekana kama kweli tutakuwa tumezika tofauti zetu na kuamua kukubaliana kutokubaliana hata kwa yale mambo tosiyoyapenda, ili mradi tusukume gurudumu la maendeleo ya filamu mbele na hatimaye tuwe na soko la filamu lenye nguvu katika Afrika.
Ni umoja pekee utakaotuondoa kwenye huu ugonjwa mbaya wa kumtafuta mchawi: wasanii wanalalamika, wazalishaji wanalalamika, wasambazaji wanalalamika, watumiaji wa kazi za sanaa wanalalamika, wanasiasa wanalalamika pia, serikali inalalamika kukosa ushuru, huku watu wachache wanafurahi, hao si wengine bali wezi wa kazi za sanaa.
Sasa ni wakati wa kuhakikisha wasanii wanafaidika na jasho lao na tusimamie kwenye misingi imara itakayorudisha tena hadhi ya msanii ili isionekane tena kuwa kazi ya sanaa ni kazi ya watu walioshindwa sehemu nyingine.
Ifike mahali yale matangazo tuliyozoea kuyaona ukutani na kwenye vibao sehemu mbalimbali tunazopita “Tunabani CD na kuweka nyimbo kwenye flash, memory card nk” yasiwepo tena. Maktaba za filamu maarufu kama video library pia zifuate taratibu na sheria ili wasanii na watayarishaji wafaidike, na kusiwepo ujanja ujanja tena. Itambulike kuwa kufanya haya kinyume cha sheria ni wizi kama wizi mwingine.
Huyu msanii, mzalishaji au msambazaji atalipwa vipi? Tukumbuke kuwa sanaa ndilo jembe lake, wakati wengine wanapoibia mali zao polisi na jamii kwa ujumla huambua kupambvana na wizi huo, lakini hii imekuwa tofauti sana kwa wasanii kwani wao wanaibiwa hadharani: ukienda mbele ya ofisi za Cosota wapo hapo nje, mbele ya vituo vya polisi utakuta CD na DVD feki zinatembezwa hadharani bila woga na hakuna mtu anayeonekana kujali kabisa.
Tuache kulalamika, tuchukue hatua sasa.
No comments:
Post a Comment