Ukurasa wa facebook unaweza kutumika kutangaza sinema
Pia unaweza kutumia ukurasa katika mtandao wa Youtube
TASNIA ya filamu nchini ni
sawa na mtoto yatima lakini hali hii isiwe sababu ya kutufanya kulipua kazi
zetu, bali tunapaswa kuangalia namna iliyo nzuri itakayotuwezesha kuboresha
kazi zetu na kufanikiwa katika soko la ndani na hata nje ya Tanzania . Nimewahi kudokeza katika siku za nyuma kuhusu
vigezo muhimu viwili vinavyoweza kutuongoza katika dhana nzima ya mafanikio hasa
tunapolifikiria soko la filamu: Maudhui/Mahitaji ya Watazamaji na Jukwaa la
Uwasilishaji.
Tunapaswa kwanza kuwaelewa watazamaji
wetu kabla ya kufanya chochote, kwani ni hatua muhimu sana katika mchakato wa biashara ya filamu.
Tunapaswa kubainisha maudhui ya kazi zetu ili yaendane na matarajioyao . Kama hatuwezi kuambatanisha maudhui yetu yaende sambamba
na mtazamo wa watazamaji, basi, filamu zetu zitaendelea kupuuzwa na tutaendelea
kuwa watu wa kulalamika.
Tunapaswa kubainisha maudhui ya kazi zetu ili yaendane na matarajio
Kwa miaka kadhaa, sekta ya
filamu Tanzania imeshuhudia utofauti mkubwa kati ya maudhui katika
hadithi zetu na kile watazamaji wanachokihitaji, na matokeo yake yameendelea
kuyumbisha mikakati ya soko na sera za usambazaji. Watazamaji wamekuwa
wakinunua kazi zetu si kwa kuwa wanazipenda, hasha, bali kwa kuwa hawana
mbadala. Tusitegemee hali hii kuendelea kutubeba siku zote, tunapaswa sasa kuzingatia
suala la maudhui ambayo lazima yahusishwe moja kwa moja na mahitaji ya
watazamaji ili kuwe na nafasi ya mafanikio kwenye soko.
Maudhui yanayofaa katika
kizazi cha leo ni yale yanayokwenda sambamba na watazamaji ndani ya akili zao na
kuihusisha jamii moja kwa moja. Kitu ambacho mtayarishaji/ mwandishi anapaswa
kujua kuhusu watazamaji wake ni muhimu sana kwa mafanikio katika biashara ya usambazaji.
Kujenga maudhui bila uelewa mkubwa na ufafanuzi kwa walengwa, ni kama kufunga safari ya kwenda mahali bila kufikiria jinsi ya kufika huko. Kama maudhui tunayoandaa hayakushikamana na aina ya maisha au matarajio ya
watazamaji wetu, ni dhahiri tunawapoteza.
Watayarishaji wa filamu
wayafahamu kwanza makundi ya watazamaji wetu, na kundi la kwanza la watazamaji
wa filamu zetu ni la akina mama wa nyumbani, wafanyakazi wa ndani, na vijana
wasio na ajira. Kundi la pili ni la watazamaji linalotokana na matokeo ya moja
kwa moja ya vituo kama Africa Magic kuonesha filamu kwenye familia za watu
wa tabaka la kati na la juu wenye uelewa mpana.
Na bila shaka kuna kundi la
tatu linalotokana na watazamaji Watanzania walio nje ya nchi na Waafrika (wanaojua
au kukipenda Kiswahili) katika bara la Afrika na maeneo waliko. Ni muhimu
kuelewa kwamba kila moja ya makundi haya ya watazamaji yana muundo na mawazo
ambayo ni tofauti sana na kundi jingine.
Katika utazamaji filamu
zetu, kuna dhana ambayo huendana na mitazamo ya watazamaji (matamanio, maadili,
na mtazamo wa mtu binafsi kulingana na uzoefu wake katika kuangalia kazi
mbalimbali) na vitu hivi huathiri namna watazamaji wanavyohusiana na dunia
inayowazunguka, ikiwa ni pamoja na maudhui.
Kabla hadithi zetu hazijawafikia
watazamaji, tayari mtazamaji atakuwa na picha ya kipi anataka kukiamini na kama hadithi zetu zimeandaliwa katika mtazamo mzuri, mtu wa aina hiyo
huamini na hununua kazi bila kusita kama ilivyo kwa
kazi za wenzetu. Kama hadithi itaifikia jamii ya watazamaji ambao mtazamo
wao utalingana na visa vyetu, wigo wake utapanuka, watu watapeana taarifa kwa
njia ya neno kwa neno (ambayo ni njia ya ufanisi zaidi kwa mkakati wa soko) na
hujenga nidhamu ya utazamaji wa filamu.
Vizuri tu kama , tutaambatanisha ubora wa kiufundi wa filamu zetu uendane na ubora wa
watazamaji wetu waliouzoea. Tusidanganyane, watazamaji wa leo wameelevuka na
wanaujua ubora wanaouhitaji, hivyo tusitegemee kuendelea kufanya biashara - kwa
mfano, kuwapa filamu yenye kiwango hafifu watazamaji ambao wamezoea kuangalia
sinema za kigeni, ambazo zimetengenezwa kwa kiwango cha juu cha ubora.
Pia tusisahau kuwa
watazamaji wetu wanahitaji majukwaa ya habari kama wanavyojali kuangalia maudhui. Falsafa hii ni muhimu wakati tunaposhughulikia
maudhui yanayowafaa watazamaji. Jukwaa la uwasilishaji katika dunia ya kisasa
ya filamu haliishii tu kwenye kazi ya usambazaji, linakwenda ndani zaidi ya
kile hasa soko la filamu lilivyo leo. Jukwaa litasaidia kuwasilisha mawazo kwa
watu katika njia itakayojumuisha mitazamo yao .
Ufanisi katika uwasilishaji
unachangia utoaji haki ya kuchagua; kuyaleta maudhui kwa watazamaji katika
dunia yao wenyewe. Kulingana na uwezo mkubwa wa soko la
Tanzania kama litawezeshwa (ndani na nje ya bara la Afrika), jukwaa muafaka
litamfanikisha kwa urahisi mtengenezaji wa filamu kuendana na ushindani wa
soko.
Mustakabali wa biashara ya
usambazaji wa filamu na masoko Tanzania unatokana na watazamaji vijana. Watoaji filamu
wanatakiwa kuandaa kwa uangalifu takwimu ya watazamaji na kukutana nao katika
dunia yao .
Katika hatua hii itakuwa
vizuri pia kuuchunguza mfumo wa usambazaji ili kupata ufumbuzi wa kutangaza na
kusambaza ambao umesaidia kurekebisha tasnia katika nchi nyingine, ili uigwe
katika sekta ya filamu Tanzania . Filamu ni bidhaa, kama zilivyo bidhaa nyingine, kuzitangaza na kuzisambaza ni vitu vyenye
umuhimu sawa.
Lazima tuweke mkakati wa
kujitangaza kwenye mitandao ya intaneti. Hii itaongeza mipaka katika
utekelezaji wa kampeni ya kuzitangaza kazi.
Lakini tuna tatizo kubwa
hapa kwetu kwamba Tanzania bado haina kiwango kikubwa cha watu wanaotumia
intaneti ukilinganisha na nchi zingine katika Afrika, ni asilimia ndogo sana ya wananchi wanaotumia mtandao.
Hayo ni maeneo ambayo watu
wanaotembelea wanaweza kupata habari zaidi, kushiriki katika mijadala, kujiunga
na majarida, na kubadilishana ujuzi na mawazo na watu wengine, kwa lengo la
kupanua wigo mkubwa wa watazamaji.
Katika miaka michache
iliyopita, mitandao imesaidia sana kufanya uwepo wa gharama nafuu katika kutangaza na
kuuza kazi kwa watengeneza filamu na hata kwa studio. Katika baadhi ya nchi
zilizoendelea, ni nadra na kosa kubwa kutokuwa na wavuti (website) ya kutangaza
filamu kabla haijaoneshwa kwenye majumba ya sinema.
Hii inawapa mashabiki fursa
ya kupata habari kuhusu maudhui/hadithi, wasifu wa waigizaji, na kuchangia
maoni yao na matamanio yao katika filamu na husaidia kuenea kwa taarifa au
tetesi za filamu. Mbali na kuwa na wavuti ya kujitolea, kuweka filamu zetu
kwenye mitandao ya kijamii iliyopo ni njia nyingine nzuri ya kuongeza jamii ya
watazamaji/wafuatiliaji wa filamu.
Siku hizi, facebook,
Twitter, Youtube ni njia nzuri za kujitangaza kwa haraka, kama watayarishaji lazima tuangalie namna ya kuongeza wavuti zetu na
kuongeza matangazo na taarifa zetu muhimu. Matangazo ya kulipia kwenye
televisheni, radio, magazeti, majarida, na majarida ya kitaaluma (professional
journals) ni muhimu pia.
Pia tuhakikishe
tunaziingiza filamu zetu kwenye matamasha ya filamu ili zionekane. Kuzionesha
filamu kwenye matamasha ya filamu ni jambo zuri sana ambalo linaweza kusaidia kuongeza wigo wa taarifa.
Matamasha ya filamu husaidia kueneza taarifa miongoni mwa wakosoaji wa filamu
na watazamaji, na inaweza kuongeza umaarufu wa filamu na watazamaji kuwa wengi kama mapitio yake yalikuwa ya kuvutia.
Wakati sisi tukiendelea
kukaa katika ulimwengu wetu wa 'uvivu wa fikra' sehemu nyingine ya dunia
inasonga mbele kwa kasi zaidi kuliko tunavyodhani.
Pamoja na ongezeko kubwa la
idadi ya mitandao na kunyonya filamu (film downloads) ambapo mauzo na
usambazaji wa DVD na video yanaendana na mahitaji ya teknolojia yatabadilisha
mkondo wa mapato, watengeneza filamu wataweza kupanua njia yao ya wigo wa
usambazaji kwa idadi kubwa ya watazamaji, hasa vijana, ambao wameonekana kuwa
na msisimko mkubwa na teknolojia hii.
Kumbuka kuwa: Hivi sasa,
mipango ipo njiani kwa nchi kuhama kutoka matangazo ya kizamani ya Analogia ya
televisheni kwenda kwenye mfumo mpya wa digitali – kunakoongeza mahitaji
makubwa ya vituo vya televisheni; hii inatoa nafasi kubwa ya kuingia.
Alamsiki…
No comments:
Post a Comment