Apr 11, 2012

Mazishi ya Kanumba yahudhuriwa na maelfu ya watu na kuliza wengi

Steven Kanumba enzi za uhai wake

Elizabeth Michael (Lulu) anayehusishwa na
kifo cha Kanumba







Picha zote hapo juu zinaonesha jinsi watu walivyojitokeza
kwa wingi kwenye mazishi ya Msanii wa filamu
Steven Kanumba, kuanzia viwanja vya Leaders hadi
kwenye makaburi ya Kinondoni

Si watu wengi waliotaka kuamini kwamba aliyekuwa mcheza filamu maarufu nchini Tanzania Stephen Kanumba hatunaye tena duniani mpaka pale walipouona mwili wake ukiagwa.

Ilikuwa ni siku ya kipekee, yenye majonzi, simanzi na machozi mengi wakati mamia ya watu wakifurika Jumanne asubuhi kwenye viwanja vya Leaders Club jijini Dar es salaam kuuaga mwili wa aliyekuwa mcheza filamu maarufu nchini Steven Charles Kanumba.

Makamu wa Rais wa Tanzania Mohamed Ghalib Bilal ndiye aliyoongoza umati wa wapenzi wa msanii huyo kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuhitimisha harakati za mazishi ya Marehemu Kanumba. Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania bwana Benald Membe, mke wa rais mama Salma Kikwete na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa nao walihudhuria sherehe za kumuaga msanii huyo maarufu. Wasanii wa Tanzania nao walionesha mshikamano mkubwa kwa kujitokeza kwa wingi kumuaga mwenzi wao.

Katika makaburi ya Kinonondoni watu walifurika huku huduma za afya kama shirika la Msalaba Mwekundu likiwa limejiandaa kusaidia watu watakaoathiriwa na mshtuko wa kifo cha Kanumba. Inasemekana watu wengi walizimia hasa pale mwili wa marehemu ulipowasili katika pumziko la milele kwenye makaburi ya Kinondoni. Tukio hilo liliumiza mioyo ya watu na kuona kwamba “ sasa kweli Kanumba hatunaye tena”.

Wakati hayo yanafanyika  imebainika kwamba chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania, -TAMWA kimetaka ufanyike uchunguzi huru, wa haki na wa kina kufuatia kifo cha msanii huyo wa filamu nchini, ili kumtendea haki Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu ambaye anadaiwa kuwa alikuwa na marehemu Kanumba kabla mauti kumfika.

Hata hivyo maswali ni mengi kuhusu hatma ya msanii Lulu lakini jeshi la polisi nchini Tanzani limesema limeshapeleka jarada la upelelezi wake katika ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka – DPP. Limewataka ndugu jamaa na marafiki wa mcheza filamu huyo kuwa na subira wakati uchunguzi zaidi unaendelea.

Wakati huo huo jopo la madaktari kutoka hospitali ya taifa ya Muhimbili linatarajiwa kutoa ripoti ya uchunguzi wa kifo cha marehemu Kanumba jumanne baada ya kukamilisha uchunguzi rasmi ulioanza jumatatu.

No comments: