Robert Nesta Marley (Bob Marley)
Steven Charles Kanumba
SEKTA ya filamu nchini ni sekta kubwa sana , yenye nguvu kubwa na ushawishi mkubwa mno, lakini ndiyo sekta isiyopewa kipaumbele kama sekta muhimu inayoweza kuchangia pato kubwa kwa maendeleo na ukuaji wa uchumi wa taifa letu. Sekta hii imefukarishwa makusudi na watu wachache, ndiyo maana wajasiriamali wa soko la filamu wanafanya kazi kwa nguvu zote lakini hawapati kile wanachostahili.
Ukitaka kujua kuwa sekta hii imefukarishwa hebu mtazame mtayarishaji wa sinema za Tanzania (achilia mbali msanii), hana kabisa hadhi ya kuitwa mtayarishaji wa sinema, hana kipato wala ushawishi ukilinganisha na sekta nyingine, wakati sinema ndiyo nyenzo kuu ya kupashana habari na kuelimishana.
Soko la filamu nchini limeachwa mikononi mwa watu wachache wakilimiliki watakavyo. Serikali haipati kitu, haina kitu wala haitegemei kitu, huku watayarishaji wa filamu na wasanii kwa ujumla wao wakionekana kama walalamishi tu na wasiostahili kusaidiwa.
Majuzi kamati kuu ya mazishi ya aliyekuwa msanii mashuhuri wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba, imedai msanii huyo amefariki dunia akiwa maskini, kinyume kabisa cha umaarufu mkubwa aliokuwa nao wakati wa uhai wake. Kanumba alishiriki kwenye filamu zaidi ya 40.
Ikumbukwe kuwa kwa miaka mingi sasa, wasanii na watengenezaji wa sinema miongoni mwa wadau wengine wa sanaa wameendelea kutoa sinema hapa Tanzania ili kujipatia riziki kutokana na kazi yao bila mafanikio. Ingawaje sekta ya filamu ni sekta yenye thamani ya mabilioni ya fedha, lakini wengi wameishi na kufa maskini.
Tusidanganyane, hali itaendelea kuwa hivi na taaluma hii haiwezi kukua kama viongozi wataishia kusema tu bila kutekeleza walichoahidi huku kukiwa na mambo mengi yanayoirudisha nyuma. Haki za wasanii na watayarishaji wa filamu zitaendelea kuporwa, kwa kutumia unyonge wao na umasikini wao wataendelea kutumika kwa maslahi ya wachache, na mwishowe watakufa wakiwa masikini lakini wenye majina makubwa, tena bila hata kuwaachia wategemezi wao urithi unaoeleweka.
Binafsi nimetumia miaka kadhaa kujifunza na kufanya tafiti mbalimbali kuhusu historia ya filamu, matatizo makubwa katika tasnia hii, mfumo unaofaa kutumika katika tasnia ya filamu na mambo mengine mengi, kutokana na haya, naamini kabisa kwamba sekta ya filamu Tanzania ina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 300 ya pesa za Tanzania katika biashara, kama tu serikali itatilia mkazo na kutoa msaada unaohitajika na si kama ilivyo leo ambapo wanasubiri msanii maarufu afe ili waende kuuza sura na kutoa ahadi.
Niliwahi kumwandikia Rais Kikwete wakati fulani kuwa kama kweli kadhamiria kuiokoa tasnia hii; serikali yake inapaswa kuelekeza nguvu nyingi katika suala la utoaji wa mafunzo kwa wasanii na watengeneza filamu. Kutafuta gharama za mafunzo kwa watengeneza filamu lingekuwa jambo la kwanza kabisa kwa serikali yake katika kuutambua mchango wa sekta ya filamu.
Bado naamini kuwa Serikali kama kweli wameazimia kwa dhati kusaidia tasnia ya filamu, inapaswa kuandaa mwongozo (roadmap) utakaotuongoza kwenye mafanikio ya soko letu. Tunahitaji kuwa na vyombo madhubuti katika kusimamia kazi zetu. Vyombo kama; Chama Cha Hakimiliki Tanzania (Cosota), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na kadhalika, vinahitaji kuangaliwa upya ili viweze kwenda na wakati na kusimamia kazi zetu kikamilifu.
Kwa wenzetu pesa inatengenezwa hata pale mtu anapokuwa amefariki dunia, hii ni kutokana na nchi hizo kuwa na sheria nzuri za hakimiliki, serikali kuwasimamia watu wake na viongozi kutimiza wajibu wao ipasavyo.
Wasanii kumi wanaoendelea kuvuna pesa japo walishafariki dunia ni: Kurt Cobain, Elvis Presley, Charles M. Schulz, John Lennon, Albert Einstein, Andy Warhol, Dr. Seuss (Theodor Geisel), Ray Charles, Marilyn Monroe, Johnny Cash, J.R.R. Tolkien, George Harrison na Bob Marley.
Michael Jackson ingawa hayumo kwenye orodha hii na ingawa kifo chake kimesababisha hasara kubwa kwa ulimwengu wa muziki, lakini takriban miezi 18 baada ya kifo chake, Mfalme huyo wa Pop duniani ameendelea kuiingizia familia yake pesa.
Wasanii kama Elvis Presley, anayeshikilia nafasi ya pili ameendelea kutengeneza fedha nyingi japo amefariki miaka mingi sana iliyopita. Whitney Huston, ambaye aliripotiwa kufilisika na hatimaye kupata mfadhaiko wa akili kuhusiana na matatizo yake ya kifedha kabla ya kufariki, sasa anatarajiwa kutengeneza pesa lukuki baada ya kifo chake!
Kanumba kafa akiwa na miaka 28 tu, na tayari alishatoa zaidi ya filamu 40, je, sinema zake zina thamani gani? Serikali inalijua hilo ? Mi’ nadhani walipaswa kulijua kabla hawajafikiria kujazana kwenye msiba wake pale Sinza, au kujigamba kugharamia mazishi yake ingawa tunaambiwa tena kuwa kumbe kamati ya mazishi nayo imetumia milioni 60 kwenye mazishi!
Kwa mtu aliyefanya kazi nzuri, kufariki siyo mwisho. Anaweza kuendelea kuishi hata baada ya kifo, kwani kazi zake, pamoja na nembo zake zinaweza kuendelea kuvuna mashabiki ambao wanamkumbuka, na wale waliozaliwa muda mrefu baada ya kufa, na kuingiza mapesa kibao kama inavyotokea kwa mastaa niliowataja hapo juu.
Wasanii hao japo wengi wao wamefariki miaka mingi sana iliyopita lakini kwa pamoja wamechuma dola milioni 247 katika miezi 12 tu iliyopita. Wameendelea kukusanya fedha katika mikataba ikishirikisha vyote; kazi zao na haki za kutumia majina yao kibiashara na kampeni za masoko.
Vipi kuhusu Tanzania ? Serikali ina mpango gani kuhakikisha wasanii kama Kanumba na wengine waliofariki wanaendelea kuvuna pesa na kuzifaidisha familia zao na wategemezi wao waliobakia? Au ndo’ ule msemo wetu wa ‘Asiyekuwepo na lake halipo ?’.
Watengezaji wa filamu nchini wamekuwa wanalalamika kila mara kuwa wanaibiwa au kuwekewa masharti magumu na wasambazaji ambayo yanadumaza tasnia ya filamu ikiwemo kuuza haki zao, lakini wamekuwa wakionekana wendawazimu.
Kwa sasa imekuwa ni jambo la kawaida kusikia kuwa mtayarishaji wa filamu kauza kazi zake kwa msambazaji, jambo linaloshangaza sana hasa kwa nchi kama hii inayoanza kupiga hatua katika tasnia ya filamu. Sababu za kushangaza ni nyingi; ya kwanza kubwa ni kuwa majukumu ya msambazaji yanajulikana wazi kuwa yeye kazi yake inapaswa kuishia kwenye kusambaza kazi husika tu, sasa anaponunua haki zote ndipo inapotia shaka kubwa! Kwa nini anunue haki ya msanii? Kwa nini msanii amuuzie haki yake? Je, Serikali iko wapi kwenye hili?
Katika makala yangu moja niliwahi kuishauri serikali kama inataka kufuta umasikini kwa vijana waliojiajiri kupitia sanaa inapaswa kuingilia kati na kutoa elimu kwa wasanii na watayarishaji wa filamu kwa kuwa imeonekana kuwa wengi hawana uelewa wa haki zao, na wenye uelewa huo wanakwazwa na hali iliyopo sokoni kwa kuwa msambazaji ndiye anayelimiliki soko na mwenye kauli ya mwisho katika kazi yoyote ya filamu.
Kanumba alikuwa mmoja wa wale ambao walikuwa wanaojiona washindi kwa kuingia mikataba inayowafanya kuuza haki zao kwa msambazaji na kuishia kupewa gari na pesa zinazowasaidia kwa miezi michache, masikini hakujua kabisa kuwa atakapoaga dunia haki yake itakuwa imeishia hapohapo, na hawa waliobaki wanapaswa kujifunza kupitia yeye kwani siku 'wakichuja' na thamani yao kupungua watarudi kwenye msoto kwani haki zao tayari zitakuwa zimeshapotea.
Sheria ya Hakimiliki ya nchi yetu inasema wazi kuwa hakimiliki hudumu kwa mwenye haki kwa maisha yake yote na miaka hamsini baada ya kifo chake. Kwa nchi kama Marekani wameongeza hadi miaka sabini. Ndiyo maana utaona kuwa kuna kazi nyingi ambazo zinaendelea kuwa maarufu miaka mingi baada ya wenye kazi kufariki, huku zikiwanufaisha warithi wao.
Kwa kawaida kazi za filamu (kama ilivyo kwenye muziki) zina haki zipatazo kumi ambazo zimetajwa katika kifungu na 9(1) cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya 1999.
Haki hizo ni: (i) Kurudufu kazi, (ii) Kusambaza kazi, (iii) Kukodisha, (iv) Kuonesha hadharani, (v) Kutafsiri, (vi) Kubadili matumizi ya kazi, (vii) Kufanya maonesho ya hadhara, (viii) Kutangaza kazi katika vyombo vya utangazaji, (ix) Kutangaza kwa njia nyingine zozote, na (x) Kuingiza kazi nchini.
Kwa hiyo ukiangalia haki hizo kama zilivyoainishwa utaona wazi kuwa msambazaji anahitaji haki mbili tu za mwanzo, haki nyingine zinamruhusu mwenye mali (mtayarishaji) aendelee kufaidi matunda ya kazi yake kwa maisha yake yote na kuwaachia warithi wake miaka hamsini mingine baada ya kifo chake.
Inapotokea ukauza haki zako kwa msambazaji basi ujue unauza hata zile haki nane zilizobakia ambazo kimsingi huwezi tena kuzitumia, kwa kuwa tayari utakuwa umeshazipoteza. Hivi ukiamua kuuza kazi zako kwa maana ya kumuachia haki zote msambazaji, unatarajia kuwaachia nini warithi wako, au unataka kubaki na ile sifa tu ya kuwa uliwahi kuwa na kazi?
No comments:
Post a Comment