Apr 5, 2012

Maadili ya Watanzania katika filamu ni yepi?


SUALA la maadili ya Mtanzania hasa katika filamu limekuwa linazungumzwa sana, na binafsi limekuwa linanitatiza sana kama nilivyokuwa natatizwa na suala la mila na utamaduni wa Watanzania. Kama moja ya makala zangu nimewahi kuuliza maswali haya na sikuweza kupatiwa majibu japo ni kama nilijijibu mwenyewe: Tunaposema utamaduni na mila za Watanzania tunamaanisha nini kwa Tanzania yenye zaidi ya makabila 120 ambayo kila moja lina mila na utamaduni wake? Na huu utamaduni na mila za Watanzania ni upi hasa?


Ndivyo leo ninavyojaribu kuliangalia suala hili la maadili ya Mtanzania kwenye makabila 123 na kujaribu kujiuliza maswali ambayo ninapata majibu nusunusu tu. Niliwahi kumuuliza kiongozi wa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza tulipokutana kuhusu yepi ni maadili ya Watanzania wanayoyaangalia kwenye filamu zetu?
Lakini nasikitika kusema kuwa alishindwa kunijibu na ‘aliingia mitini’ kama tusemavyo vijana wa leo.


Watetezi wa maadili wanaozilalamikia filamu zetu ndani ya jamii za Kitanzania wanapaswa kutafuta majibu ya maswali haya ili kutuweka sawa sisi tusiokuwa na majibu, vinginevyo watakuwa wakiimba wimbo wasioujua.


Katika machapisho kadhaa nimewahi kusoma kuwa maadili ni wema wa mwenendo au tendo la mtu; ni kule kuhukumiwa kwa mwenendo wa mtu kuwa ni mwema, au tendo la kibinadamu kuwa ni jema. Mwenendo au tendo la mtu ni jema vinapolingana na hadhi yake kibinadamu, yaani vinapoakisi utu wake. Hapa tunasema mtu huyu ni mwadilifu, au tendo hili ni adilifu.


Na mwenendo wa mtu au matendo yake vinapokuwa kinyume na hadhi yake ya kibinadamu, yaani kinyume cha utu wake, tunahukumu kuwa ni mabaya, na huo ni ukosefu wa uadilifu. Kwa kifupi, uadilifu ni wema wa mwenendo au tendo la kibinadamu, na ukosefu wa uadilifu ni ubaya wa mwenendo au tendo la kibinadamu.


Maadili pia ni taaluma juu ya kanuni zinazohukumu mwenendo na matendo ya mtu kulingana na UTU wake. Katika kuhukumu uadilifu wa mwenendo au tendo la mtu (yaani, wema au ubaya wao), dhana ya maadili inazingatia vipengele vifuatavyo:

Sheria ya kimaumbile ya Kimaadili: Hii ni sheria iliyochapwa katika nafsi ya binadamu tangu kuumbwa kwake. Tunaiita ‘sheria’ kwa kuwa hutoa mwongozo na hukumu juu ya uadilifu wa mwenendo na matendo ya mtu kulingana na utu wake; ni ya ‘Kimaumbile’ kwa kuwa mtu aliumbwa nayo, si kitu ambacho mtu anatunga bali iko katika hulka yake ya kibinadamu; ni ya ‘kimaadili’ kwa sababu inahusu wema au ubaya wa mwenendo na tendo la kibinadamu.


Sheria hii inasema: “Tenda wema, epuka ubaya.” Binadamu huitambua na/au huing’amua sheria hii ya kimaadili kwa kutumia vipawa vyake vya akili na utashi. Vipawa hivi ndivyo vinavyomtofautisha mwanadamu na viumbe vingine vyote katika ulimwengu huu, na pia humpa hadhi ya juu na mamlaka ya kuvitawala viumbe hivyo.


Watu wengi kujifunza kanuni za maadili nyumbani, shuleni, kwenye nyumba za ibada, au katika mazingira mengine ya kijamii. Ingawa watu wengi kupata hisia za haki na makosa wakati wa utotoni, maendeleo ya kimaadili hutokea katika maisha ya binadamu na kupita katika hatua tofauti za ukuaji wanapokua.


Kanuni ya kimaadili zipo kila mahali na mtu anaweza kujaribiwa kuziangalia kama maarifa ya kawaida. Kwa upande mwingine, kama maadili hayakuwa chochote zaidi ya maarifa ya kawaida, kwa nini basi kuna migogoro mingi ya kimaadili na katika jamii yetu?


Inaposemwa kuwa mtu hujifunza maadili nyumbani au kwenye mazingira ya kijamii hasa katika jamii mtu anayotoka ndilo hasa linalonivuta kujiuliza maswali haya. Imekuwa inasema sana kuwa filamu zetu hazina maadili kwa kuwa watu wanavaa mavazi ya nusu uchi, lakini nashindwa kuelewa ukosefu wa maadili katika mavazi tunamaanisha nini? Ikumbukwe kuwa mavazi yetu ya asili si haya tunayojivunia leo kuwa ukiyavaa utaonekana umevaa mavazi ya maadili yetu.


Asili yetu ni mavazi yanayoficha sehemu za mbeleni tu kwa wanaume na eneo la kiuno hadi kwenye mapaja kwa wanawake huku yakiacha sehemu kubwa ya mwili yakiwemo matiti wazi. Hivi tunapoongelea maadili katika mavazi tunakumbuka jambo hili au sasa tunadai kwenda na wakati?


Nimejiuliza sana kwa kuwa hivi karibuni nilibahatika kutembelea maeneo fulani hapa nchini ambako nilikuta watu bado wakivaa aina ya mavazi ambayo huacha sehemu kubwa ya mwili ukiwa mtupu. Je, hawa pia hawana maadili? Ikitokea mtu akatengeneza filamu inayohusisha mavazi ya asili tutasemaje? Haina maadili? Mi nadhani hapa tujaribu kuwa wawazi zaidi.


Naomba ieleweke kuwa si lengo la makala haya kutetea kinachofanywa na baadhi ya wasanii, hasa wa kike kuvaa mavazi yanayoacha sehemu kubwa ya mwili ikiwa tupu, hasa pale ambapo hadithi haielekezi kufanya hivyo, lakini pia tunapaswa kuangalia hili kwa mapana yake badala ya kufuata mkumbo tu wa kushabikia mavazi ya Kizungu au yenye asili ya Kiarabu kwa kudai ndiyo mavazi ya maadili yetu.


Ninachoamini ni kuwa sanaa ni zao la matokeo ya juhudi za wasanii katika kutoa ujumbe, kukidhi matumizi na mahitaji ya binadamu kwa kufuata tamaduni zao, jambo hili linaonesha umuhimu wa utamaduni kuwa si kitu kilichoibuka tu.


Hakuna heshima kubwa kama mtu kutambulika kuwa ni sehemu ya utamaduni fulani, utamaduni unaoweza kutupatia urithi usiofutika. Yale tunayoyaonesha katika maisha yetu ya kawaida, hayaishii hapo tu bali yanaathiri hata maisha yetu ya kiimani.


Jambo moja ninalokubaliana nalo ni sanaa yetu ya filamu kusahaulika kabisa, na tumekuwa tukipokea ile ya nje tena kwa fujo, hali hii imesababisha Watanzania kuwa wafuatiliaji na waigaji wa filamu za nje badala ya kuweka nguvu zaidi katika kubadili fikra zetu ili filamu zetu ziende na matakwa ya dunia kwa kuziboresha.


Sasa ni wakati muafaka wa kujaribu kufikiria na kuchambua kila tunapoiga mambo ya kigeni iwapo yana mchango wowote katika makuzi ya tamaduni zetu au yanakuwa chanzo cha kuziangamiza. Hatuna budi kuelewa kwamba kuanguka kwa tamaduni ni anguko letu pia.


Ikumbukwe kuwa mara baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Serikali iliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, mwaka 1962. Mwalimu Julius Nyerere alitamka wazi kuwa Utamaduni ni kiini na roho ya Taifa, na kwamba nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.


Kupuuzwa kwa tamaduni kumekuwa ni suala linalojitokeza katika nyanja mbalimbali hapa nchini. Kati ya mambo ambayo binadamu hana budi kuyazingatia ni uhusiano wake na mila na desturi alizotunukiwa na jamii yake. Ni katika kuzingatia hilo tu ndipo binadamu anapata uwezo wa kukua na kujichotea utajiri mkubwa unaotolewa na tamaduni za jamii yake.


Pamoja na umuhimu uliopo katika suala la utamaduni kwenye jamii yetu lakini bado sera ya utamaduni hapa nchini imekuwa haipewi nafasi katika serikali hii tangu ilipoanzishwa wizara inayoshughulikia masuala ya sanaa. Tangu mwaka 1962 shughuli za sanaa zilipewa nafasi katika mfumo wa kiserikali lakini zimekuwa hazithaminiwi.


Ingawa mimi si mtu wa imani ya kiroho lakini naamini kuwa hali ya mtu kujitenga na tamaduni asilia kunaweza kuwa tishio katika kupokea hata imani ya kidini. Hii inatokana na ukweli kwamba imani ambayo mtu aipokeayo kama zawadi toka kwa Mungu ina msingi wake katika mila na desturi tuziishizo. Hakuna uwezekano wa kuwa na imani ya kidini iwapo mtu hakujengeka katika utamaduni wa kweli. Ni katika tamaduni zetu ndipo tunapata maana ya utu, upendo na kadhalika.


Hatari kubwa ya kupotea kwa tamaduni asilia inatukumba sana vijana ambao bila kujua huwa tunajikuta katika utamaduni hasi unaotusukuma kudharau tamaduni zetu na kujiingiza katika mienendo ambayo kwa kiasi kikubwa si tamaduni ila vurugu zinazotokana na kukosekana kwa tamaduni.


Hii inajionesha hasa katika sanaa zetu na hasa filamu tunazoziandaa ambazo nyingi zinajengwa katika misingi isiyo na maana katika jamii. Uigaji usio na uchambuzi umetupelekea kukosa kabisa vipaumbele katika maisha yetu, na kubaki kuwa bendera kufuata upepo.


Nawakilisha.

No comments: