Jengo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Aliyekuwa Naibu Wizara wa Habari Utamaduni na Michezo,
Joel Nkaya Bendera akisisitiza jambo
*Watazamaji wa kazi za Kiswahili walihamasika zaidi baada ya ITV kurusha mchezo wa Tausi
*Serikali imekusanya sh. Bilioni 2 kwa mwaka 2005 hadi Mei 2009.
BURUDANI nchini Tanzania imepitia mabadiliko makubwa hadi kufika hapa ilipo. Kipindi kile, enzi za kina Black Moses, Maneno Ngedere, Bob Tiger na wengine wengi burudani ya disko ndiyo iliyoshika hatamu. Kipindi hicho ndipo hata zile sinema za kwenye majumba ya sinema (Avalon, Drive Inn Cinema, Empire, Starlight na kadhalika) zilikuwa zimeshika hatamu.
Miaka iliposogea, muziki wa taarabu ukashika hatamu. Mipasho ya kina Nasma Kidogo na Khadija Kopa ikawa gumzo kila mahali. Kisha zikaja enzi za muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Flava.
Bongo Fleva ikiwa bado haijapotea zikaibuka filamu za Kitanzania, tena za Kiswahili kutoka kwa waigizaji wa Kitanzania. Kwa maana nyingine hizi ni zama za Bongo Fleva na Filamu za Kitanzania.
Vituo vya televisheni hapa Tanzania (ukiacha Zanzibar) vilianza rasmi mwaka 1994, na taratibu vilianza kujizolea watazamaji ambao mwanzo walizoea kwenda kwenye majumba ya sinema. Kituo cha kwanza cha televisheni kilikuwa cha ITV (Independent Television Limited) kilichoanza kurusha matangazo yake mwaka 1994.
Ujio wa televisheni ya ITV ukawaleta watu kama Richard Ndunguru, Anna Costantine (Waridi), Tecla Mgaya (Aisha), Philip Njaidi (Sumbi) na Paschal (Bocha), na baadaye wakaibuka Raymond Allen (Bishanga Bashaija) na Single Mtambalike (Richie).
Wakati huo walikuwa wakirusha michezo mifupimifupi kupitia kundi la Mambo Hayo.
Baadaye wasanii nguli waliokuwa wamejizolea umaarufu kupitia michezo ya redio, akina marehemu Mzee Jongo, Rajab Hatia, na watu kama Bakari Mbelemba (Mzee Jangala), Issa Joseph (Onyango), Mzee Kipara wakaanza kuigiza kwenye televisheni na kuwa mwanzo wa tasnia hii kupiga hatua.
Baadaye wasanii nguli waliokuwa wamejizolea umaarufu kupitia michezo ya redio, akina marehemu Mzee Jongo, Rajab Hatia, na watu kama Bakari Mbelemba (Mzee Jangala), Issa Joseph (Onyango), Mzee Kipara wakaanza kuigiza kwenye televisheni na kuwa mwanzo wa tasnia hii kupiga hatua.
Hata hivyo, watazamaji wa maigizo na filamu za kiswahili walianza kuhamasika zaidi kufuatia kituo hicho cha ITV kuanza kurusha mchezo mrefu wa Tausi kutoka Kenya, na hivyo kuwafanya watazamaji waanze kupenda zaidi michezo na filamu za kiswahili.
Baadaye, kwenye miaka ya 2000 M-Net iliichagua Tanzania kushiriki katika mpango wake uliojulikana kama “M-Net New Directions Africa”. Moja ya zao la mpango huo ni Marehemu Kiiza Kahama kwa kazi yake ya “SURRENDER”, na baadaye aliibuka Amri Bawji aliyeandika kisa cha kusisimua “A TEST OF BEANS” (Ladha ya Maharage).
Ukiachia kazi hizo chache za Watanzania zilizowezeshwa na kupata mafanikio, siku hizi soko la ndani kwa kiwango fulani limedorora (ingawa linasemwa kuwa limekua) kutokana na mambo kadha wa kadha nitakayoyaeleza baadaye.
Filamu katika zama hizi zilizoanza kuwatambulisha Wabongo kuwa wanaweza japo mazingira yalikuwa magumu ni filamu ya “Shamba Kubwa (1995)” iliyotungwa na kuongozwa na Mwl. Kassim Al Siagi wa Tanga.
“Shamba Kubwa” ni filamu iliyowaibua wasanii ambao baadaye walikuja kuwa mahiri katika ulimwengu wa filamu, kama Hassan Mwinyi (Hassan Master), Juma Mponda (Jimmy Master), Kaini na Amina Mwinyi, ni filamu iliyoteka wengi kwa wakati ule japo teknolojia ilikuwa bado ndogo na vituo vya televisheni ndo kwanza vilikuwa vimeanza. Wakati huo kama sikosei kulikuwa na vituo viwili au vitatu tu, ITV, CTN na DTV.
Baada ya Shamba Kubwa, zilifuatia sinema nyingine kama “Love Story Tanganyika na Unguja (1998)” iliyotengenezwa na Amri Bawji, “Kifo Haramu” kazi iliyotengenezwa na Jimmy Master, “Dunia Hadaa (2000)” chini ya muongozaji Mwl. Kassim Al Siagi, “Augua (2002)” iliyotengenezwa na Amri Bawji kwa udhamini wa Mfuko wa Utamaduni na kadhalika. Hii inaonesha kuwa Tanga ndiyo waasisi wa filamu hizi za kizazi kipya.
Filamu hizi zilitengenezwa katika mfumo wa analogia (VHS), hata uhariri wake ulitumia akili zaidi kutokana na teknolojia wakati huo kuwa ya kiwango kidogo.
Ndipo ukaja wakati ambapo Wabongo wengi wakapata mwamko kwa sinema za nyumbani baada ya sinema ya “Girlfriend”, sinema inayoaminika kuwa ndiyo iliyoamsha chachu kubwa na kuwafanya Watanzania kuzipenda filamu za nyumbani.
Mimi ni mfuatiliaji mzuri sana wa habari zozote zinazohusu sanaa hasa filamu, kwa maana hiyo naikumbuka pia tarehe 23 June 2009, wakati Martha Mosses Mlata, Mbunge wa viti maalum (CCM) alipouliza swali (namba 88) kwa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo.
Swali lake lililokuwa katika sehemu tatu za (a),(b) na (c) aliuliza kama Serikali inatambua kuwa, sheria ya mwaka 1999 ya Hatimiliki ya kazi za sanaa haijaweza kutatua tatizo la uharamia wa sanaa? Pia aliuliza kama Serikali inajua ukubwa wa biashara hii na imekusanya kodi kwa kiwango gani? Na mwisho alitaka kujua ni kazi ngapi za sanaa zilizokwishakamatwa na kufikishwa mahakamani na hukumu yake ni nini?
Majibu yalitolewa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Joel Nkaya Bendera kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo; aliyesema kuwa si kweli kwamba, Sheria Na. 7 ya mwaka 1999 ya Hakimiliki na Hakishiriki, inayohusiana na kazi za sanaa haijaweza kutatua tatizo la uharamia wa sanaa. Ukweli ni kwamba, sheria hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kutatua tatizo hilo hapa nchini.
Alisema kuwa sheria hii imewezesha wasanii na watengenezaji wa kazi za sanaa kutambua haki zao kama wamiliki au pale wanaposhirikishwa katika kuandaa na kuzitengeneza. Na kwamba kazi nyingi za sanaa zinafanyika kwa kuwekeana mikataba mbalimbali.
Pia alisema Serikali inajua ukubwa wa biashara ya kazi za sanaa kama vile muziki ambapo biashara ya CD, VCD na DVD, inafanyika. Ukubwa wa biashara hii, unatokana na kukua kwa sekta ya utamaduni, kuongezeka kwa wasanii na wapenzi wa muziki na filamu mbalimbali zikiwemo za Kitanzania na za nje ya nchi na hivyo kulifanya soko la bidhaa hiyo kuongezeka.
Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi 2009, Serikali imekuwa ikikusanya kodi mbalimbali kutokana na biashara ya kazi za sanaa: tangu mwaka 2005, makusanyo kutokana na kodi ya mapato ya kazi za sanaa kwa watu binafsi yaliongezeka kutoka sh. milioni 14/- hadi kufikia sh. milioni 90.9/- mwezi Mei mwaka 2009.
Makusanyo kutokana na kodi ya mapato kwa makampuni, yaliongezeka kutoka sh. milioni 26.6/- mwaka 2005 hadi kufikia sh. milioni 342.5/- mwezi Mei mwaka 2009.
Kodi ya mirahaba, sh. milioni 53/- mwaka 2006 hadi sh. milioni 146.2/- mwezi Mei mwaka 2009, wakati mapato ya kodi ya maendeleo ya ujuzi au utaalam yaliongezeka kutoka sh. milioni 2.52/- mwaka 2005 hadi kufikia sh. milioni 323.6/- mwezi Mei mwaka 2009.
Pia alibainisha kuwa jumla ya kodi iliyokusanywa kutokana na biashara ya kazi za sanaa nchini kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi Mei 2009, ni sh. bilioni 2/-.
Pia katika kipindi cha kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 jumla ya kesi nane zinazohusiana na kazi za sanaa, zimekwishafikishwa mbele ya vyombo vya dola katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Kati ya hizo, kesi tano zilisikilizwa katika mahakama ya Kisutu, Jijini Dar es Salaam, moja Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na mbili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Musoma.
Kesi hizo zinahusu kutumia picha za sinema bila kibali, utengenezaji CD na Kaseti na utoaji wa nakala za CD kwenye kompyuta bila kibali cha mwenye kazi. Naibu Waziri huyo aliendelea kubainisha kuwa wale waliopatikana na makosa katika kesi zilizosikilizwa walitozwa faini ya kati ya sh. 20,000/- hadi 200,000/-.
Takwimu za kukusanya sh. bilioni 2 kwa miaka 4 (kwa sekta nzima ya burudani) si jambo la kujivunia hata kidogo kwani hicho ni kiasi kidogo sana kulinganisha na takwimu halisi zinazohusu sekta ya filamu peke yake.
Serikali ilipaswa kushirikiana na wadau halisi ili kupata takwimu sahihi na ione jinsi inavyopoteza mabilioni ya pesa kutokana na kutokuwepo kwa takwimu sahihi kwenye sekta hii.
Katika makala zangu nimewahi kuishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha chombo kitakachoitwa; “Film and Video Promotions Board”, na nikashauri kuwa katika chombo hicho viwepo vitengo vitano; kimojawapo kikiwa ni kitengo cha kuandaa takwimu za kina na kutoa fursa ya kuzitangaza kazi zetu katika masoko mengine ya Afrika, na duniani, na pia kitengo kitakachosimamia mapato (revenue generation) yatokanayo na filamu.
Bila chombo cha aina hii hatuwezi kusimama na kujigamba kuwa serikali imefanikiwa kukusanya mirahaba na mapato yatokanayo na filamu kwa ukamilifu, tutaendelea kuwa kichekesho.
Itaendelea...
No comments:
Post a Comment