Dec 15, 2010

Soko la filamu Tanzania linakua?

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitafakari

TASNIA ya filamu hapa Tanzania kwa miaka ya karibuni imeonekana kupata mwamko mkubwa sana, lakini kwa bahati mbaya (au kwa makusudi) mara nyingi kumekuwa hakuna takwimu au taarifa sahihi kuhusu mwamko na maendeleo ya tasnia hii ya filamu hapa Tanzania.

Miaka michache iliyopita asilimia kubwa ya Watanzania walipendelea kutazama filamu zilizotoka nje ya nchi, hususan sinema za Nigeria na India, lakini hivi sasa hali imekuwa tofauti kidogo. Tofauti hiyo imesababishwa na ujio wa hizi filamu za Kibongo za kizazi kipya (new generation films), kutoka kwa wasanii na waandaaji wa Kitanzania ambao mpaka sasa wamechangia kwa kiasi kikubwa kuitambulisha tasnia ya filamu Tanzania ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Tasnia hii hapa Tanzania imeripotiwa kukua huku ikipitia dhoruba la mahitaji na hali. Mgongano umeiweka tasnia hii njia panda baada ya kuibuka kwa teknolojia na mahitaji halisi ya watazamaji. Ipo haja kwa watayarishaji wa filamu kutafuta ufumbuzi wa misingi ya ubunifu katika teknolojia mpya.

Inasemwa kuwa fani ya uigizaji na filamu hapa Tanzania sambamba na viwango vya ubora wa filamu zetu imekuwa ikikua kila siku kama ilivyothibitishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, katika hotuba yake ya kuzindua Bunge la Kumi mjini Dodoma hivi karibuni.

Kikwete alisema kuwa filamu za Tanzania zimeanza kuitangaza vyema Tanzania katika medani ya kimataifa kutokana na kuonekana katika kituo cha runinga cha Africa Magic. Na hivi sasa TV za hapa nchini zinaonesha filamu hizi za Kitanzania kwa kasi, ingawa kuna utata unaoambatana na wasanii husika kuonesha mshangao kuhusu filamu zao kuoneshwa bila ruhusa yao.

Nakubaliana na rais Kikwete kuwa filamu hizi zinaitangaza Tanzania duniani, lakini rais anapaswa aelewe kuwa bado tasnia ya filamu hapa nchini inakabiliwa na changamoto kubwa sana ya kukua kwa soko la filamu linalopaswa kwenda sambamba na kufaidika kwa waandaaji na waigizaji wa kazi hizo.

Anti Ezekiel

Kabla ya miaka ya 2000 Tanzania ilikuwa haivumi katika medani ya filamu, ingawa fani ya sanaa hii ilikuwa ikifanya kazi kupitia wasanii na waandaaji mbalimbali tena kwa kiwango kizuri kabisa. Filamu za sasa zimeonesha kuwa na mchango kwa kiasi fulani wa kutoa elimu katika jamii, ikiwa ni pamoja na kuitambulisha Tanzania kwa kuitangaza lugha ya Kiswahili ambayo ndio inayotumika kwa kiasi kikubwa katika filamu hizo.

Pia fani hii hadi sasa imewawezesha vijana wengi kujipatia mkombozi wa ajira na kuwawezesha kujitimizia mahitaji yao ya kimaisha, na kama alivyowahi kuandika mchambuzi mmoja kuwa hata wale walioonekana watukutu ama kushindikana katika jamii sasa wameonekana kukubalika na kuwa watu waadilifu.

Sanaa ya maigizo ni njia rahisi na muhimu kwa kufanya kazi hizo muhimu, kama Rais Kikwete alivyoonekana kuutambua mchango wa filamu za Tanzania kwenye hotuba zake nyingi ingawa bado huwa ninapata shaka kidogo kama kweli ana taarifa sahihi kuhusu tasnia hii, changamoto zake na matatizo yaliyopo.

Najua kuwa rais ana nia nzuri ya kutaka tasnia ya filamu ifikie kiwango cha juu na kuwa mkombozi wa ajira kwa vijana wengi, lakini kabla serikali yake haijaanza kusaidia katika kuiboresha tasnia hii ni bora kwanza akafahamu ni mkondo gani anadhani tasnia ya filamu Tanzania inafaa iuelekee ili kufika huko anakodhani kunafaa.

Kutambua mkondo unaofaa ni jambo zuri zaidi, isije ikawa hadithi ya mgombea fulani aliyekwenda kuomba kura kwa wananchi halafu akawaahidi kuwajengea daraja la kisasa ili waweze kuvuka mto kirahisi. Wananchi wakamwambia kuwa hawana mto, akaona kuwa amepatikana kwa kuwa hakuwa akiyajua matatizo yao halisi, akaamua kuwaahidi kuwapelekea na mto pia...

Kama nilivyowahi kuandika huko nyuma kuwa, ipo haja kubwa kwa Rais kuifahamu kwanza nguvu ya soko letu la filamu (dynamics of the home video industry) kabla hajataka kusaidia. Ni muhimu pia kwa rais kuufahamu msingi imara unaohitaji mipango madhubuti na ya lazima katika kuiwezesha (empower) sekta ya filamu hapa Tanzania.

Tasnia ya filamu duniani imegawanyika katika mikondo mikuu miwili; mainstream film ambayo pia hujulikana kama major movies studio, na independent film au huitwa kwa kifupi Indies.

Independent film ni mkondo wa filamu zinazotengenezwa kwa bajeti ya kawaida kutoka kwa watengeneza filamu huru (independent filmmakers) na kusambazwa bila msaada kutoka studio na makampuni makubwa. Mainstream ni mkondo wa filamu zinazotengenezwa kwa bajeti kubwa sana kwa msaada wa studio kubwa ambazo huwa ziko tayari kumsapoti mtengeneza filamu yeyote.

Kama ningetakiwa kumshauri rais katika nia yake ya kutaka tasnia ya filamu ikue, ningemshauri ajiulize kwanza maswali yafuatayo ili kujiridhisha; je, ni kwa namna gani watayarishaji na wasanii wanafaidika na kazi za kisanii wanazozifanya licha ya kuwa ni zenye umuhimu mkubwa katika jamii? Swali jingine ni je, wasambazaji wa filamu hizi wanazingatia umuhimu wa kazi za wasanii na wanashauri masuala muhimu ya kitaalam kwa lengo la kukuza soko la filamu?

Je, kuna madhara gani yanayotokana na uharamia wa kazi za filamu, yepi madhara hasi na yepi madhara chanya ya uharamia hapa Tanzania? Je, nini kifanyike kukabiliana na uharamia huu? Nini sababu za uharamia huu wa filamu?

Halafu malipo kwa wasanii yakoje? Yanazingatia kweli hali halisi ya ugumu wa kazi na umuhimu wa kazi?

Pengine kabla sijazama katika uchambuzi huu ingefaa kwanza tukajikumbusha kuhusu historia ya filamu Tanzania ambayo inaonesha kuwa ilianza miaka mingi iliyopita; ilikuwa ni mwaka 1929 ambapo sinema ya kwanza kabisa iliingia Tanganyika (sasa Tanzania).

Kati ya mwaka 1935 na 1936 raia wawili wa Uingereza, Major L.A. Notcutt na Geoffrey Latham waliingia Tanganyika na kuifanya kituo maalum kwa ajili ya mradi wa majaribio ya elimu kwa njia ya sinema “Bantu Education Cinema Experiment”. Mradi ulioanzishwa kama heshima, tuzo na imani ya utawala wa Kiingereza katika makoloni yake kwa ajili ya kuinua na kuendeleza sekta ya filamu hasa kwa Waafrika walioonekana ni mbumbumbu (illiterate Africans).

Elimu iliyotokana na “Bantu Education Experiment” iliwezesha kutengenezwa kwa sinema ya “GUMU”, sinema iliyokuwa ikielezea matatizo na ugumu wa maisha ya mjini, lengo kubwa likiwa kuwafanya vijana wabakie vijijini badala ya kukimbilia mjini.

G. C. Latham, aliyekuwa mkurugenzi wa mafunzo wa “Bantu Education Experiment” aligundua kuwa mazingira na tamaduni za Kiafrika yalikuwa ni mandhali nzuri sana kwa sinema za kuburudisha (entertaining), hivyo alishauri kuwa baadhi ya sinema zingeweza kutengenezwa kwa kutumia baadhi ya hadithi za mapokeo zilizowahusu mashujaa wa Kiafrika, moja ya sinema iliyokuja kutengenezwa kutokana na ushauri huo ni ile ya ‘The Wakalindi Saga’.

Jumla ya sinema 35 zilitengenezwa hapa Afrika Mashariki katika maeneo tofauti zikiwa katika lugha ya Kiingereza, pia lugha zingine nane za asili zilitumiwa ambazo ni Kiswahili, Kisukuma, Kikikuyu, Kijaluo, Kiganda, Kinyanja, Kibemba, na Kitumbuka. Mambo yaliyotiliwa mkazo sana katika sinema ni pamoja na Benki ya Posta (Postal Bank), Mmomonyoko wa udongo (soil erosion), Malaria kwa watoto wachanga (Infant Malaria), Safura (Hookworm), Soko la kahawa (coffee), kodi (tax), n.k.

Walisafiri maeneo mengi ya Afrika Mashariki na Kati kwenye miaka ya 1936 na 1937 na kufanikiwa kuzionesha sinema hizo kwa zaidi ya watu 100,000.

Notcutt na Latham walipofika mwisho wa mradi wao waliishauri Serikali ya wakati huo ianzishe kitengo maalum cha filamu kitakachofanya kazi za kueneza propaganda kwa maelekezo maalum kutoka London, Uingereza.

Wizara ya Habari ya Uingereza (British Ministry of Information) ikaanzisha kitengo cha sinema kilichojulikana kama “Colonial Film Unit (CFU)” mwaka 1939 kwa ajili ya kutengeneza na kusambaza sinema za kipropaganda. Wizara hiyo pia iliandaa magari maalum (mobile cinema vans) kwa ajili ya kuoneshea sinema hizo na zingine za kuburudisha kwenye maeneo ya vijijini katika Afrika Mashariki.

Serikali ya Uingereza ilianzisha matawi yake katika sehemu zote Afrika yalipo makoloni yake: Afrika Mashariki matawi hayo yalikuwa Kenya, Tanganyika (sasa Tanzania), na Uganda. Afrika ya Kati matawi yalikuwa Rhodesia (sasa Zimbabwe), na Nyasaland (sasa Malawi), na Afrika Magharibi waliweka matawi yao Nigeria na Gold Coast (sasa Ghana).

Serikali ya Uingereza ilianzisha vitengo hivi vya filamu ili iweze kuwapata vijana wa Kiafrika kwa urahisi zaidi kwa ajili ya kushiriki kwenye Vita Kuu ya Pili ya Dunia (Rouch, uk. 390).

Vita Kuu ya Pili ya Dunia ilitoa msukumo zaidi kwa sekta ya filamu; Serikali ya Uingereza iliichukulia sekta ya filamu si kwa ajili ya kuwaburudisha tu, lakini pia kama wazo zuri la kueneza propaganda, hasa kwa watu ambao hawakwenda shule (illiterate audiences).

Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kitengo cha filamu cha Posta “British General Post Office Film Unit” kilionekana kuzidiwa na kupoteza mwelekeo, hivyo shughuli zake kuhamishiwa kwenye kitengo kingine cha “Crown Film Unit”, kilichofanya kazi kubwa ya kuwapatia mafunzo Waafrika na baadaye kuvigawa vitengo vya filamu katika kila koloni ili vijiendeshe.

Itaendelea 
 

No comments: