Dec 1, 2010

HISTORIA YA FILAMU (3): Mwanzo wa Sinema za Sauti (Sound Era)

 Humphrey Bogart, muigizaji anayeshika namba moja ya ubora katika historia

MAJARIBIO ya kuchanganya muziki kwenye sinema kwa kutumia njia mbalimbali hatimaye yalifanikiwa; kurekodi moja kwa moja au kuingizia muziki studio (play back) wakati wa uhariri, ingawa juhudi zilianza tangu kipindi chote tangu mwanzo wa sinema bubu, lakini matatizo makubwa mawili (twin problems) ya kuoanisha (synchronise) na kukuza (amplifiy) sauti katika kiwango kinachostahili yalikuwa kikwazo kikubwa (Eyman, 1997).

Mwaka 1926, studio ya Warner Bros ya Hollywood ilitambulisha mfumo mpya uliojulikana kama ‘Vitaphone’, kwa kutoa sinema fupi zilizotokana na matukio ya moja kwa moja (live entertainment acts) ya wasanii maarufu na baadaye kuongezea sauti maalum (sound effects) na muziki (orchestral scores).

Mwishoni mwa mwaka 1927, Warners ilitoa kazi yake iliyoitwa “THE JAZZ SINGER” ambayo kwa kiasi kubwa haikuwa na muziki lakini ikiwa na mazungumzo (synchronized dialogue) yaliyooanishwa sawia na nyimbo kwenye sinema hiyo. Kazi hiyo ilikuwa ya mafanikio makubwa, ikifuatiwa na kazi nyingine ya “THE LIGHTS OF NEW YORK (1928)”, hizi zikiwa ni sinema za kwanza kabisa (first all-synchronized-sound feature) kuingiziwa muziki na sauti kwa mafanikio.

Mbinu za mwanzo za kuingiza muziki kwenye diski (sound-on-disc processes) kwa mfumo wa ‘Vitaphone’ zilichukua nafasi haraka na kutumika kuingiza muziki kwenye sinema (sound-on-film) zikijulikana kama ‘Fox Movietone’, ‘DeForest Phonofilm’, na ‘RCA Photophone’.

Mwelekeo huo uliwashawishi wafanyabiashara na wenye viwanda walioonekana mwanzoni kutovutiwa na sanaa hii (sinema) kuamini kuwa picha jongefu ziongeazo (talking pictures) zingekuwa na manufaa sana kwa siku za baadaye.

Madhara yaliyoambatana na zama za sauti na muziki:

Kila kitu huwa kina faida na madhara yake.
Mabadiliko makubwa yalikuwa ya haraka sana kuliko ilivyotarajiwa. Mwishoni mwa mwaka 1929, Hollywood ilijikuta ikiwa katika ushindani mkubwa sana kati ya watengeneza filamu katika uboreshaji wa sinema zao, ingawa mabadiliko kama hayo yalikuwa yakienda taratibu sana kwa sehemu zilizobakia za dunia, moja ya sababu kubwa ikiwa ni matatizo ya kiuchumi.

Sababu za kitamaduni pia lilikuwa ni jambo jingine lililochangia, hasa kwa nchi kama China na Japan, ambako sinema bubu (silents) ziliendelea kutawala soko sambamba na zile zenye sauti na nakshi ya muziki (sound) hadi kwenye miaka ya 1930, walitoa sinema ambazo zilitokana na mambo ya asili na ya kitamaduni yaliyoheshimiwa zaidi (revered classics) katika nchi zao, mfano ni kazi ya Wu Yonggang “THE GODDESS (China, 1934)” na ile ya Yasujiro Ozu “I WAS BORN, BUT… (Japan, 1932)”.

turudi kwenye hoja, madhara makubwa ya zama za sauti (sound era) yalipelekea kuanzishwa kwa wingi studio kubwa katika nchi mbalimbali kulikoambatana na kupanda kwa gharama (vast expense) zilizowaghalimu mno (overwhelmed) wenye mitaji midogo (small competitors) kiasi cha kutishia uwepo wao kwenye soko la ushindani, pia upya (novelty) wa mfumo huu uliwavutia kwa wingi (lured vastly) watazamaji wa sinema hizo kiasi cha kuwafanya kujenga imani kubwa kwa waandaaji (producers) waliokuwa wamemudu kubakia kwenye ushindani.

Hapo ndipo ulipoanza mwanzo mpya wa zama za mafanikio makubwa ya sinema za Hollywood (the Golden Age of Hollywood), kipindi hicho kilipelekea mwanzo wa kukua kwa sinema zenye muziki na sauti hadi kwenye miaka ya mwisho ya 1940.
Sinema za Marekani zikafikia kiwango cha juu cha mafanikio ya uzalishaji kimataifa. Waigizaji waliopata chati za juu katika zama hizo ndiyo wanaofikiriwa kuwa waigizaji bora (the classic movie stars) na nyota kuliko wote katika historia ya sinema, waigizaji kama: Clark Gable, Katharine Hepburn, Humphrey Bogart na Shirley Temple.

Ubunifu na ushindani wa zama hizo:

Kiubunifu, kwa hali yoyote kipindi hicho cha mpito kilikuwa kigumu sana, ilifikia wakati sinema zikaanza kurudi (reverted) katika hali ile ya zama za mwanzo.

Kwa miaka 20 ushindani ulisimamisha mambo mengi, jukwaani na mbele ya kamera wasanii walizidisha bidii huku wakikumbana na ukomo (stringent limitations) wa zama za sinema bubu kutokana na upya wa matumizi ya mwanzo (early sound equipment) ya vifaa na jinsi ya kuvitumia.

Ikatokea kuwa wasanii wengi wa jukwaani, waongozaji na waandishi wenye uwezo mkubwa ndiyo waliopata neema kutoka kwa waandaaji walioonekana kutafuta watu wenye uwezo na utaalam wa matumizi ya zana hizo.

Watengeneza sinema wengi wakubwa waliokuwa wamejikita kwenye sinema bubu (silent filmmakers) na wasanii waliozoea sinema hizo hawakuweza tena kuhimili nguvu ya soko.

Kipindi hicho kigumu kilichukua muda mfupi. Mwaka 1929 ulikuwa mwaka wa kazi ngumu na ulibatizwa jina la ‘watershed year’: waandaaji kama William Wellman alitengeneza sinema za “CHINATOWN NIGHTS” na “THE MAN I LOVE”, Rouben Mamoulian alitengeneza “APPLAUSE”, Alfred Hitchcock alitengeneza “BLACKMAIL” (ambayo inasadikiwa kuwa ndiyo sinema ya kwanza nchini Uingereza ya kipindi cha sinema za sauti). Hawa niliowataja walikuwa ni miongoni mwa waongozaji waliofanikiwa sana na kuleta changamoto zaidi (Eyman, 1997).

Kwa maana hiyo, wote walijikuta wakinufaika na kuzama zaidi kwenye matumizi ya vinasa sauti ‘microphones’ na kamera, bila kusahau uwezo wa kuhariri na kuingiza muziki wakati wa uhariri badala ya kurekodi muziki huo moja kwa moja wakati wa upigaji picha.

Kipindi hicho cha sinema zenye sauti na muziki kilitiliwa mkazo sana na kuyafaidisha matabaka (genres) tofauti kuliko ilivyokuwa kabla. Ni wazi kuwa sinema za muziki (music films) zilikuwa zimezaliwa rasmi; kazi ya kwanza ya aina hiyo (classical-type) kutoka Hollywood ilikuwa ni “THE BROADWAY MELODY (1929)”, kazi iliyofanyika chini ya mbunifu wa uchezaji (choreographer) na muongozaji aliyekuwa maarufu, Busby Berkeley.

Nchini Ufaransa, mtu mmoja aliyeitwa Renè Clair alitengeneza vichekesho vyenye mchanganyiko wa ngoma na muziki, mojawapo ya kazi hizo ni “UNDER THE ROOF OF PARIS (1930)” na “LE MILLION (1931)”.
Mfumo wa sinema za aina hiyo ndiyo uliokuja kustawi zaidi India, ambako ushawishi uliochochewa na utamaduni wa ngoma na muziki umekuwa ndiyo mfumo rasmi wa sinema za Kihindi (Cook, 1990); ukweli ambao haukubainiwa na nchi za Magharibi katika kipindi cha muongo (decades) mmoja, sinema hizi za Kihindi zikaanza kuzalishwa kwa wingi sana.

Sinema za Kimarekani za kiharamia (gangster movie) kama ile ya “LITTLE CAESAR” na “THE PUBLIC ENEMY” (zote za mwaka 1931) zilitokea kuwa maarufu sana na kujizolea mashabiki wengi. Mazungumzo katika sinema (dialogue) yakapewa kipaumbele (precedence) katika vichekesho (comedies) vilivyoanza kutengenezwa Hollywood: “THE FRONT PAGE (1931)” au “IT HAPPENED ONE NIGHT (1934)”, pia sinema kama “SHE DONE HIM WRONG (1933)” ya Mae West, na kazi ya Marx Brothers “DUCK SOUP (1933)”.

Mwaka 1939 ndiyo uliokuwa mwaka wa mafanikio zaidi ya sinema za Marekani, sinema kama “THE WIZARD OF OZ” na “GONE WITH THE WIND”.

Kukua kwa biashara ya Sinema Duniani:

Ieleweke wazi kwamba kukua kwa sekta ya filamu kulikoambatana na biashara hakukuanza hivi hivi tu, bali kulitokana na changamoto nyingi sana, kulianza hasa kuonekana kutoka kwa Georges Mèliès wa Paris, Ufaransa aliyepiga picha na kufanya maonesho ya filamu (film exhibitions) mwaka 1896. Kazi zake kama “A TRIP TO THE MOON (1902)”, kazi ambayo inasadikiwa kuwa ndiyo iliyoanzisha vuguvugu na kutia hamasa (potray) kwa wanasayansi kuhusu safari za angani (space travel).

Georges alianzisha mbinu muhimu (fundamental special effects) ambazo zimeendelea kutumika kwenye sinema kwa karne nzima ya ishirini. Kuoneshwa kwa sinema ya ‘A Trip to the Moon’ kuliibua hamasa na juhudi za watu wakitaka waone hali halisi iliyoko mwezini badala ya vitu vya kufikirika kama ilivyokuwa kwenye sinema hiyo (Cook, 1990). Pia Georges aliongoza katika kuelekeza namna ya kuingiza sauti katika matukio mengi mbalimbali (multi-scene) kwenye sinema iliyokuwa na urefu wa dakika kumi na tano.

Itaendelea

No comments: