Edwin S. Porter - The Great Train Robbery (1903)
George Melies
KAMA nilivyoanza kuelezea issue iliyopita, biashara ya sinema ilianza kujikita rasmi na kuwa ajira kamili iliyowawezesha watu kujipatia kipato halali kutokana na kazi hiyo.
Kukua kwa sekta ya filamu kulikoambatana na biashara hakukuanza hivi hivi tu, kulitokana na changamoto nyingi sana na kulianza kuonekana kwa Georges Mèliès wa Paris, Ufaransa aliyepiga picha na kufanya maonesho ya filamu (film exhibition) mwaka 1896. Kazi zake kama “A TRIP TO THE MOON (1902)”, kazi inayosadikiwa kuwa ndiyo iliyoanzisha vuguvugu na kutia hamasa (potray) kwa wanasayansi kuhusu safari za angani (space travel).
Georges alianzisha mbinu muhimu (fundamental special effects) ambazo zimeendelea kutumika kwenye sinema kwa karne nzima ya ishirini. Kuoneshwa kwa sinema ya ‘A Trip to the Moon’ kuliibua hamasa na juhudi za watu kutaka waone hali halisi iliyoko mwezini badala ya vitu vya kufikirika kama ilivyokuwa kwenye sinema hiyo (Cook, 1990).
Pia Georges aliongoza katika kuelekeza namna ya kuingiza sauti katika matukio mengi mbalimbali (multi-scene) kwenye sinema iliyokuwa na urefu wa dakika kumi na tano.
Baadaye aliibuka Edwin S. Porter aliyekuwa kiongozi wa jopo la waongozaji filamu wa kampuni ya Edison baada ya kubuni mbinu mpya iliyokuja kusaidia sana katika kazi ya uhariri wa filamu, mbinu hiyo ikasambaa duniani kupitia kazi ya “LIFE OF AN AMERICAN FIREMAN”, sinema ambayo inasadikiwa kuwa ndiyo sinema ya kwanza iliyojaa mambo na tamaduni za Kimagharibi, na “THE GREAT TRAIN ROBBERY” zote za mwaka 1903.
Kuanzia wakati huo, Porter akawa amekaribisha ushindani na changamoto kubwa kutoka kwa wadau wa filamu ambao baadaye walielewa kuwa kitu muhimu kwenye sinema kinachoifanya kuwa nzuri na bora wakati wa uhariri ni upigaji (shot) na wala siyo tukio (scene).
Hii ilisaidia sana kuifanya sekta ya filamu iwe maarufu miongoni mwa jamii na kusababisha ongezeko kubwa la kumbi maalum za kuoneshea sinema (nickelodeons).
Ukumbi mkongwe kabisa duniani wa kuoneshea sinema (the oldest cinema in the world) na wa kwanza wa kudumu ambao hadi leo unatumika kwa kazi hiyo unajulikana kama ‘Pionier Cinema’, ulifunguliwa tarehe 26 septemba, 1909 huko Stettin, Ujerumani (kwa sasa panajulikana kama Szczecin, Poland) – hii ni kwa mujibu wa kitabu cha Guinness World Records.
Hadi kufikia mwaka 1908 tayari kulikuwa na kumbi 10,000 za kuoneshea sinema kwa Marekani pekee. (Cook, 1990).
Mwanzo wa sinema ndefu:
Kuibuka kwa sinema ndefu (feature film) kuliifanya sekta ya filamu kukua zaidi na kuwa sanaa kamili; ikumbukwe kuwa urefu wa sinema za mwanzo ulikuwa ni kati ya dakika kumi na kumi na tano tu, hasa katika muongo wa kwanza tangu kuanza kwa historia ya sinema.
Ilikuwa ni filamu iliyotengenezwa nchini Australia “THE STORY OF THE KELL GANG” (ambayo pia ilijulikana kama ‘NED KELLY AND HIS GANG’) ambayo ndiyo sinema ya kwanza ndefu (feature length film) kutolewa. Urefu wa sinema hiyo ulikuwa wa dakika 80 na ilitolewa mwaka 1906.
Walikuwa ni Dan Barry na Charles Tait wa Melbourne, Australia walioiongoza na kuitoa sinema hiyo. Lakini haikuwa hivyo kwa nchi zingine hadi ilipofika mwaka 1911 ndipo nchi zingine zilipoanza kutengeneza sinema ndefu. Katika miaka hiyo, sinema ndefu kama 16 zilikuwa zimetengenezwa nchini Australia pekee.
Sinema ndefu zaidi ya kwanza katika zama za sinema bubu (silent era) ilitengenezwa nchini India na Dhundiraj Govind Phalke (aliyejulikana kwa jina la utani la Dadasaheb Phalke) ambaye ndiye anayeaminika kuwa “baba wa sinema za Kihindi”.
Sinema yake iliitwa “RAJA HARISHCHANDRA” (King Harishchandra, 1913) ndiyo iliyoanzisha msingi maalum wa mifululizo (series) ya kisinema. Katika kipindi cha muongo mmoja uliofuatia sinema za Kihindi zilifikia wastani wa sinema 27 kwa mwaka.
Mafanikio ya sinema za Hollywood:
Tasnia ya filamu ya Marekani au kama linavyojulikana na wengi ‘Hollywood’, jina linalotokana na eneo la kijiografia lililopo katikati ya California, imeweza kufikia nafasi ilipo sasa si kwa bahati tu, bali ilitokana na jitihada kubwa na mikakati ya dhati iliyofanywa kitaifa. Hollywood imefanikiwa kuzalisha na kusambaza sinema zake kwenye nchi zote hadi kufikia kulitawala soko la sinema duniani.
Ieleweke kuwa kukua kwa sekta ya filamu ndiko kulikosababisha uwepo wa nembo mbalimbali katika nchi nyingi zikiwakilisha soko la filamu kwa nchi zao, kama vile: Hollywood (USA), Bollywood (India), Nollywood (Nigeria) na Lollywood (Pakistan).
Pia kuna nembo kama; Tollygunge (Bengali Film Industry), Malluwood (Malayalam Film Industry), Kollywood (Tamil), Sandalwood (Kannada Film Industry) na Tollywood, zote hizi zikiwa katika majimbo mbalimbali ndani ya ardhi ya India.
Ingawa Hollywood ndiyo wameonekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana katika sekta ya filamu duniani lakini hakuna ubishi kuwa ni sinema za Kifaransa na Kiitaliano ndizo sinema zenye nguvu sana (most powerful) duniani.
Kabla ya vita kuu ya kwanza ya dunia, Ufaransa ndiyo waliokuwa wakilitawala soko la sinema duniani. Hollywood walikuja kutumia mwanya wa kuanguka kwa uzalishaji wa sinema nchini Ufaransa wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na hivyo kujijengea mkakati madhubuti (hegemony) dhidi ya nchi zingine katika soko.
Ikumbukwe kuwa Marekani tayari walianza kukua kwa kasi hadi kufikia wakati wa Vita Kuu ya Kwanza (1914-1918) na kusababisha kupungua kasi ya soko la filamu zitokazo bara la Ulaya (Europian film industries).
Baadaye Ujerumani ikawa nchi pekee duniani iliyoweza kutoa ushindani wa kweli kwa Marekani (Hollywood) katika soko la filamu.
Katika miaka ya 1920, Marekani iliweza kufikia kile ambacho hadi sasa kinajulikana kama zama zake za mafanikio makubwa, iliweza kuzalisha wastani wa sinema 800 kwa mwaka, na kuingiza asilimia 82 ya mauzo yote ya filamu duniani (Eyman, 1997).
Sinema za Marekani zikaanza kuwafanya waigizaji wake kuwa maarufu zaidi duniani: vichekesho vya wachekeshaji maarufu duniani, Charlie Chaplin na Buster Keaton, “THE SWASHBUCKLING ADVENTURES OF DOUGLAS FAIRBANKS” na “THE ROMANCES OF CLARA BOW”, ni mifano michache ya sinema hizo jinsi zilivyoweza kufanya sura za waigizaji wa Hollywood kuwa maarufu sana katika kila bara la dunia hii.
Ujio wa Sinema katika bara la Afrika:
Ieleweke kuwa kwa miaka mingi tu Afrika imekuwa ikiwasilishwa katika uwanja wa filamu kama bara la giza na mataifa ya Ulaya na Magharibi.
Matamanio ya kueneza propaganda katika kipindi cha Vita Kuu ndiko kulikosababisha na kuibua upya ari ya mataifa ya Magharibi, kwa mfano nchini Uingereza walitengeneza sinema kama “FORTY-NINTH PARALLEI (1941)”, “WENT THE DAY WELL? (1942)”, na “THE WAY AHEAD (1944)” zote zikiwa zina lengo lile lile la kueneza propaganda kwa mataifa ya Kiafrika.
Miaka ya mwanzo ya kuingia kwa sekta ya filamu Afrika, vitengo vya filamu vya Serikali za kikoloni vilisambaza sinema zilizokuwa zimetengenezwa Ulaya na Marekani kwa lengo maalum, ndiyo maana sinema zilizooneshwa Afrika zilikuwa zinafanyiwa uhariri mara ya pili (re-edited) chini ya uangalizi mkubwa wa watu maalum ili kuhakikisha kuwa Waafrika hawaoni mambo ambayo hayakukusudiwa kwao.
Sekta hii ya filamu ilipoingia katika bara hili, iligawanyika katika makundi manne kulingana na lugha zilizotumiwa kwenye nchi husika:
Anglophone iliwakilisha sekta ya filamu kwa nchi zilizotumia lugha ya Kiingereza au zilizokuwa chini ya Muingereza.
Francophone iliwakilisha nchi zote zilizokuwa chini na Mfaransa, Lusophone iliwakilisha nchi zilizokuwa chini ya koloni la Kireno, na Arabophone iliwakilisha nchi za Kiarabu.
Ukweli unabaki palepale kuwa nchi zilizokuwa chini ya Wafaransa ndizo zilizofanikiwa sana katika tasnia ya filamu. Hili ni somo maalum ambalo nitakuja kulieleza siku nyingine.
Pamoja na yote, Wakoloni walijikita zaidi kwenye kuonesha sinema za kipropaganda zaidi kwa Waafrika. Walitufanya tuamini kuwa matambiko yetu ni ushenzi mtupu, ni kutostaarabika kulikopitiliza!
Hali hiyo imeendelea hadi sasa kwani sinema zao nyingi zimejikita zaidi katika kuonesha matatizo tu ya bara la Afrika na jinsi mtu mweupe akiingia kwenye bara hili anavyokumbana na matatizo na jinsi anavyoyashinda.
Sinema kama: “KING SOLOMON’S MINES”, “TARZAN”, “SAFARI”, “THE APE MAN”, “SNOW OF KILIMANJARO”, “TRADE HORN” na kadhalika. (zote za miaka ya 1980), ni mfano mzuri.
Mwisho
No comments:
Post a Comment