Jan 4, 2011

Filamu za This is it na Huba kuoneshwa tamasha la Fespaco- Ouagadougou

 Steven Kanumba
 Ahmed Ulotu maaruf kama Mzee Chilo
Filamu mbili za Kitanzania: “This is it” ya Steven Kanumba na “Huba” ya Ahmed Olutu, zimefanikiwa kutwaa tuzo ya filamu bora katika tamasha dogo (Min Ziff) la nchi za jahazi Zanzibar, lililomalizika kisiwani juzi.
Mwenyekiti wa Ziff, Hassan Mitawi aliwapongeza wasanii na waandaaji wa filamu hizo kwa kutumia uwezo mkubwa kwa kuwa filamu hizo zimeonekana kuwa na mvuto wa kipekee na ana uhakika filamu zilizoshinda zitaenda kuwakilisha vyema Tanzania kwenye tamasha la Fespaco. Aidha, tuzo ya muigizaji bora wa filamu wa tamasha hilo,
ilienda kwa muigizaji mdogo kuliko wote katika tasnia ya filamu, Anifa Daud ‘Jenifa’ aliyeigiza katika filamu ya ‘This is it’.

Ingawa baadhi ya watu waliohudhuria tamasha hilo walitoa rai na kusema kuwa Tanzania bado ina safari ndefu kutengeneza sinema zinazokidhi kiwango cha kimataifa kama waandaaji wa filamu hawatabadilika na kufuata kanuni zinazotakiwa. Mmoja wa wadau hao alisema kuwa huwezi kuwa na sinema katika mwendelezo wa sehemu ya kwanza na ya pili na ukadhani kwamba utaweza kupenya katika matamasha ya kimataifa.

Alisema kwamba hakufurahishwa namna ambavyo Watanzania wanatengeneza sinema zikiwa na namba mbili mpaka tatu ya simulizi moja. Filamu zilizooneshwa katika ukumbi wa wazi wa Ngome Kongwe ambazo ni This is it na Huba hazikumaliza simulizi ambapo ilikatika na kuendelea sehemu ya 2.

Katika hali ya kawaida sinema hizo si hasa sehemu 2 bali ni mwendelezo wa hadithi ileile ya mwanzo wakati sinema zenye mwendelezo zinaweza kubeba jina moja lakini simulizi hugeuka kabisa na wakati mwingine hata washiriki. 

Filamu nane zilishiriki katika tamasha hilo dogo la Ziff na kupitiwa na wadau mbalimbali sambamba na kuoneshwa katika runinga kubwa ndani ya Ngome Kongwe katika muda wa siku tatu.

Filamu hizo ni pamoja “Divorce” ya Vicent Kigosi (Ray), “Briefcase” ya Mtunis, “This is it” ya Steven Kanumba, “Nani” ya Baby Madaha, “Huba” ya Ahmed Olutu, “Don’t Cry” ya Haji Adam na “Black Sunday” ya Pilipili Entertainment.

Tamasha hilo dogo la Ziff lilikuwa la siku tatu na maalum kwa ajili ya kuoneshwa filamu za Kitanzania pekee ili kupata filamu mbili bora zitakazoshiriki katika tamasha hilo la Fespaco.

No comments: