Jan 11, 2011

Soko la filamu Tanzania linakua? (5)

Tangazo la Sinema ya Aching Heart

Tangazo la vichekesho vya Sharobaro

*Rais anasema linakua kwa kigezo cha filamu zetu kuoneshwa nje ya nchi
*Viongozi wala rushwa wanashirikiana na maharamia wa kazi za sanaa

Nikiwa kama mdau wa filamu na mwanaharakati nalishauri Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff) kuonesha meno katika kupigania haki za wanachama wao ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti wasambazaji wanaochangia kudorora soko letu.

Wadau mbalimbali niliowahi kuzungumza nao wanaamini kwamba kuwa na kampuni tofauti tofauti za kusambaza filamu kunaweza kuleta changamoto na uzalishwaji wa kazi bora na kuleta mabadiliko tofauti na ilivyo sasa ambapo filamu zinauzwa kwa majina na si ubora wa picha au ujumbe uliopo katika filamu, tatizo ni msambazaji mmoja kutaka kulihodhi soko la filamu.

Naamini msambazaji huyu amekuwa sumu kwa tasnia ya filamu kutokana na malipo kidogo anayowalipa wasanii huku akiwa anafahamu fika kuwa uandaaji wa filamu unapaswa kuchukua muda mrefu na kutumia pesa nyingi ili kupata kazi iliyo bora, lakini kwa makusudi na kwa kutumia umaskini wa watayarishaji amekuwa akiwafanyisha mambo bila matakwa yao.
Amekuwa akijali maslahi binafsi bila kufahamu kuwa hali hiyo imekuwa ikichangia kushuka kwa ubora wa filamu nyingi.

Kumekuwepo filamu nyingi zisizo na ubora ingawa tayari Rais Kikwete analitaja soko la filamu Tanzania kuwa lenye kukua katika medani ya kimataifa, kwa kigezo cha baadhi ya filamu zetu kuoneshwa nje ya nchi.

 Sinema ya Babra

Nataka nimhakikishie rais kuwa soko letu halikui kwa maana ya kukua na kuleta tija kwa wadau bali linazidi kudorora na kuparaganyika huku watu wachache wakizidi kuneemeka. Soko hili limefukarishwa makusudi na watu wachache ili waendelee kufaidi jasho la wanyonge walio wengi.

Serikali na shirikisho la filamu Tanzania wanapaswa kuunganisha nguvu za wadau na kusimama imara kwa kupambana na watu hao. Ni wakati sasa wa kuweka mipango ya kuhakikisha msambazaji hajipangii tena bei na kukosa makucha ya kutoa shinikizo la kurekodiwa filamu kwa matakwa yake.

Serikali inapaswa kuiwezesha Idara ya Sanaa na Utamaduni kuwa na jukumu muhimu katika kusaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kazi za sanaa (kama ilivyo kwa NFVF ya Afrika Kusini) kupitia mfuko maalum wa kusaidia filamu.


Hata hivyo, uzoefu wa kimataifa unaonesha kwamba kuwekeza kwa kutoa fedha za utengenezaji filamu bila kuwekeza nguvu kwenye suala la usambazaji ni kufanya kazi bure. Kwa hiyo kuna haja ya serikali kutoa msaada pamoja na kufungua fursa za usambazaji na maonesho ya filamu (distribution and film exhibition). 
 
Serikali inapaswa kuwekeza nguvu kwenye kusimamia usambazaji kwa sababu uwekezaji katika kazi hizi hautoshi kuhakikisha kwamba bidhaa zinalifikia soko la uhakika.
Fursa muhimu zinazopaswa kufunguliwa kama njia za usambazaji ni katika:
-kuwapeleka waandaaji/wasanii kwenye matamasha na masoko ya filamu ya kimataifa kuuza bidhaa zao,
-kuanzisha mawasiliano kati ya waandaaji filamu wa Tanzania na wasambazaji wa kimataifa, na
-kutoa fursa zaidi kwa waandaaji wa Tanzania kukutana na waandaaji wa kimataifa. 
 
Pia kuna hili suala la uharamia wa kazi za sanaa (film pirating) ambalo ni kubwa hapa nchini japo halijafikia kiwango cha kutisha kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya.

Ili kuudhibiti uharamia wa filamu nchini ni muhimu kwa serikali kufanya kazi bega kwa bega na shirikisho la filamu (Taff) na wataalam wa sekta ya filamu kama kweli wanataka kushinda vita hii kwa ajili ya ukuaji wa tasnia ya filamu Tanzania, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku kuingizwaji horera wa sinema feki (DVD) za Hollywood zitokazo China. 
 
Uharamia huu unaacha madhara makubwa katika sekta nzima ya burudani kwa kuwa uzalishaji wa ndani mara nyingi huathirika, kama ambavyo kazi zinaibiwa ndani ya nchi na hazina nafasi ya kuingia katika soko la kimataifa.

Wengi wetu tunayajua madhara hasi tu (the negative effect) ya uharamia wa filamu, hili ni somo kubwa ambalo linapaswa kuangaliwa kwa umakini zaidi. Wanunuzi wa kazi hizi haramu kwa kawaida ni vijana. Katika soko la Bongo, kila filamu hudurufiwa katika DVD nyingi iwezekanavyo - kusambazwa sokoni kupitia maduka yanayouza filamu, wauzaji wa mkononi (machinga) na hatimaye majumbani, wakati mwingine kinyume cha sheria. 
 
Utaratibu huu hutengeneza ajira na kipato kwa watu wanaohusika katika uzalishaji na usambazaji wa kazi. Uharamia wa kazi hizi pia umesababisha kupungua kwa bei za DVD halali. Kama wewe ni shabiki halisi wa kazi za Kitanzania na unapenda wasanii wafaidike na jasho lao, kwa nini usinunue nakala halisi! 
 
Serikali inapotoa takwimu za watu waliokamatwa kutokana na kujihusisha na kazi haramu za sanaa na hatimaye kuishia kutozwa faini isiyozidi laki mbili sio jambo la kujivunia kabisa.
Kuwakamata watuhumiwa na kuwalipisha faini ndogo na wakati mwingine kuharibu mitambo yao bado hakutoshi: Serikali inapaswa kutunga sheria kali zitakazofanikisha wahusika waweze kufungwa kifungo jela na faini kubwa. Ufuatiliaji wa karibu wa maduka yanayouza kazi za sanaa, maktaba zinazokodisha na vituo vya TV pia ni jambo muhimu sana.

Vituo vya Televisheni pia havilipi haki stahiki ili kuwafanya waandaaji waweze kujikwamua na hali duni. Pia kuna hizi televisheni za jamii kwenye wilaya na mikoa yetu ambazo zimeenea Tanzania (cable televisions) zimekuwa zikionesha kazi zetu kinyume cha sheria, takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonesha uwepo wa cable televisions zaidi ya 32.
Na mwisho tishio kubwa ni uharamia wa kisasa kupitia mitandao ya intaneti; sinema nyingi za Kibongo na nyinginezo za Maziwa Makuu zinatazamwa ulimwenguni kote bila malipo kupitia mtandao huu BOFYA HAPA wa intaneti, wahusika wa uharamia huo wanajulikana na hawachukuliwi hatua zozote. 
 
Ni muhimu serikali ikayaelewa mazingira ambayo uharamia huu umejikita kabla ya kutekeleza namna ya kupambana nao. Ingawa kabla ya yote tunapaswa kujiuliza swali, je, ni nini sababu za kuongezeka uharamia wa filamu?

Kutokana na utafiti wangu jibu lake linaweza kuwa ni sababu ya ukosefu wa ajira na mfumo mbovu katika kuwasaidia na kuwawezesha vijana ndiyo umepelekea wengi wao kuuza bidhaa haramu kama njia ya kutengeneza fedha. Kuongezeka kwa uharamia huu kumechangiwa pia na viongozi wala rushwa ambao mara nyingi wamekuwa wakishirikiana na maharamia, kitu kinachopelekea kutotungwa sheria kali dhidi ya uharamia huo.

Mwisho, watu hawana elimu wala ufahamu kuhusu thamani na umuhimu wa kununua kazi halisi na hawajui chochote kuhusu sheria dhidi ya uharamia katika nchi yao.

Tanzania imetajwa kuwa ni nchi yenye kiwango nafuu cha uharamia wa kazi za sanaa, huku nchi tano zinazoongoza katika Afrika kwa kiwango kikubwa cha uharamia wa kazi za sanaa zikiwa ni Nigeria, Cameroon, Togo, Kenya, na Benin, na nchi zenye unafuu sana katika uharamia huu ni Afrika Kusini (kwa sababu imerekebisha sana sheria zake), Namibia, Ghana na Zimbabwe.
Mwisho

No comments: