May 30, 2012

Ubora ndiyo suluhisho kwa kazi zetu kung’ara kimataifa


Filamu ya Senior Bachelor iliyopata tuzo katika
tamasha la filamu la Zanzibar (ZIFF) kupitia
kipengele maalum cha filamu za Tanzania.

Filamu ya Fake Pregnant

CHANGAMOTO kubwa ambayo imekuwa midomoni mwa wengi katika soko la filamu za Tanzania na hata Afrika kwa ujumla ni ile ya kuzalisha sinema zisizo na ubora unaoridhisha. Changamoto hii ambayo ni sehemu ya mambo ambayo yameonekana kuwa magumu kutatuliwa (crux) na ndiyo mjadala wangu wa leo, ni suala ambalo tuko nalo kwa muda mrefu sasa tangu sekta hii ya filamu nchini (Bongo movies) iwepo. 

Katika hatua hii, ni muhimu kutambua kuwa nakusudia kuelezea kwa kiasi kikubwa kutokana na mtazamo wa wangu kuhusu sekta ya filamu ya Tanzania, ambalo ndilo soko la filamu ninalolijua vizuri na nililolifanyia utafiti wa kutosha.


Nadhani mtakubaliana na mimi kwamba kwa kusema kwamba lengo au furaha ya kila mtengenezaji wa filamu ni kuona filamu yake/zake zinashinda tuzo na kupata utambulisho kimataifa, na hili liko wazi kabisa. Nina uhakika kabisa kwamba hakuna mtayarishaji wa filamu, muongozaji wa filamu, au mwigizaji ambaye hapendi kuwa sehemu ya filamu iliyofanikiwa au iliyojizolea tuzo.

Pia mtakubaliana na mimi kwamba ubora ndiyo sababu kubwa ya kuzalisha filamu ambayo uwezekano wa kushinda tuzo yoyote ni mkubwa. Wakati sisi (Tanzania na Afrika) tunakazania kujadili kuhusu ubora, marejeo muhimu hujumuisha kila eneo linalohusika katika uzalishaji wa filamu, kuanzia hadithi, muswada andishi (script), taa, mandhari (set), ubora wa sauti, mavazi, upigaji picha, na hata uhariri pia hujumuishwa. Kwa hiyo swali hapa linalojitokeza: basi kwa nini tuna asilimia kubwa ya kazi zisizo na ubora ambazo haziwezi kujitangaza katika eneo la kimataifa? Jibu la swali hili lipo katika ukweli kwamba masoko katika nchi nyingi za Afrika hayajawa katika utaratibu unaoeleweka.

Kuifanya sekta hii iwe katika mtazamo mzuri zaidi, hebu tuangalie kwa makini. Uwekezaji katika utengenezaji wa filamu nchini unahitaji ujasiri mkubwa, na mara nyingi zaidi kuliko, kiwango cha mtaji ndiyo huamua ubora wa kinachozalishwa. Sasa, mitaji ni tatizo kubwa kwa watengenezaji wa filamu nchini. Kwa ufafanuzi, tatizo la kifedha halitokei kwa sababu eti hakuna mitaji inayowekezwa katika sekta hii. Kinyume chake, kwamba kuna wawekezaji tayari wenye fedha ili kuboresha uzalishaji katika sekta tofauti nchini. Hata hivyo, wengi wa wawekezaji, kama si wote hawaigusi kabisa sekta ya filamu. Kwa nini hali hii iko hivi? Jibu ni rahisi: Kanuni - au ukipenda – mazingira.

Serikali yetu (hata katika nchi nyingi za Afrika) haitaki kabisa kushiriki katika sekta ya filamu. Kwa Tanzania kwa mfano, mbali na udhibiti (kupitia Cosota na Bodi ya Filamu), hakuna popote ambapo serikali inahusika katika sekta hii. Hapa naomba nisieleweke vibaya katika hili. Sisemi kuwa serikali ijihusishe moja kwa moja ama ishiriki katika ufadhili au mchakato mzima wa uzalishaji wa filamu - hata kama sioni ubaya katika jambo hili. Badala yake, kinachohitajika hasa kutoka serikalini ni uratibu wa kitaasisi - si vikwazo, na utoaji wa mazingira mazuri ambayo yataruhusu sekta nzima ya burudani kustawi zaidi na kuwa ya kuvutia kwa ajili ya wawekezaji binafsi wa kutosha watakapokuwa na uhakika kwamba wanaweza na watapata faida katika uwekezaji wao.

Hili si suala kwa wakati huu, kwa sababu kwa kila filamu inayotengenezwa nchini watengenezaji wa filamu wanapata asilimia ndogo sana ya mapato yanayotokana na filamu wakati maharamia huvuna kwa wingi. Hapa tunazungumzia uwiano wa 25:75 katika kuangalia suala la uharamia, na hii ni takwimu ya muda mrefu, katika hali halisi uwezekano ni mbaya zaidi. Kwa hali hii hatuwezi kusema kwamba wawekezaji wataendelea kuwa na tamaa ya kutaka kuwekeza. Katika kiini cha tatizo hili ipo haja ya kuanzisha muundo sahihi wa usambazaji ambao mwekezaji yeyote katika sekta hii atakuwa na uwezo wa kurejesha fedha zake na kujipatia faida nzuri kupitia uwekezaji halali wa filamu.

Kwa kuwa ni muda mrefu hili halipo, itakuwa vigumu kufikia kiwango cha ubora wa uzalishaji ambao unaweza kutufanya kushinda tuzo katika jukwaa la kidunia. Hata hivyo, ufanisi wa mtandao wa usambazaji tayari unafurahiwa nchini Afrika Kusini, ambako uchambuzi unaonesha kwamba mfumo wa usambazaji umefanikiwa mara dufu na kwa kweli katika baadhi ya maeneo mapato ya filamu yameongezeka mara tatu kwa filamu zinazozalishwa nchini humo. 

Hivyo ni dhahiri kwamba kuondoa au kuzuia uharamia kupitia mfumo wa usambazaji wenye ufanisi husaidia kuongeza mapato na hivyo kuongeza fedha kwa kuhamasisha wawekezaji kuingiza fedha zao katika sekta hiyo.

Muundo wa upatikanaji wa fedha uliopo kwa sasa ni ule ambao wazalishaji wengi hugharamia filamu zao ama kwa pesa kutoka kwenye mifuko/akaunti zao binafsi au mikopo yenye masharti kutoka kwa wasambazaji wa filamu.

Katika nchi zilizoendelea zaidi za magharibi, hususan Marekani, kuwepo kwa studio kubwa ambazo zina mtaji wa kutosha kuwekeza katika uzalishaji wa filamu huruhusu taaluma na utekelezaji wa uzalishaji filamu za ubora wa juu. Jambo hili halipo hapa kwa sababu kama nilivyoeleza hapo juu wawekezaji hawawezi kuwa na uhakika wa uwekezaji wao. Hii inasababisha katika hali ambapo watu wenye biashara ndogo ambao wana mtaji midogo ndiyo wanaowekeza kwenye sekta ya filamu, angalau kwa kiasi kikubwa.

Matokeo ni kwamba, kwanza (wafanyabiashara) si wataalam na hawajali sana kuhusu taaluma. Lengo lao la msingi litakuwa jinsi ya kupata faida katika uwekezaji wao, ambao – tusisahau - ni rahisi kwa aina ya filamu bora tunazoziona kutoka Marekani na India. Pili, kwa sababu ya kukosekana kwa mitaji ya kutosha mambo mengi huonekana yamefukarishwa. Mambo ya ufaraguzi ni marefu sana kama nitataka kuyataja hapa. Lakini kwa kutaja tu napenda kuuliza, ni mara ngapi katika filamu zetu tumeshuhudia maeneo ya kupigia picha yakijengwa kikamilifu kulingana na hadithi tangu mwanzo kabisa wa upigaji picha.

Sithubutu kusema chochote. Suala hili la faraguzi pia huathiri ubora wa miongozo (scripts). Katika matukio mengi sinema zetu hutokana na maandiko yaliyoandikwa na watu ambao si wataalam wa uandishi wa script.

Naweza kuendelea, kuanza kutaja masuala ambayo huathiri ubora wa uzalishaji wetu katika tasnia ya filamu na kwa kweli katika nchi nyingi za Afrika, lakini hili halihusu mjadala huu. Suala hapa ni kuangalia jinsi gani na kwa nini tunapaswa kuzalisha filamu kwa ajili ya kushinda tuzo kwa soko la Afrika na duniani. Lakini nimeibua masuala yote haya kwa sababu ya uwekezaji mdogo wa fedha uliopo, kukosekana kwa msaada muhimu wa serikali kwa njia ya miundo na ufanisi wa mfumo wa usambazaji ambao unadhoofisha uwezo wa kuzalisha aina ya kazi bora ambazo tunaweza kuzalisha.

Na jambo hili limeendelea kuathiri vibaya sekta ya filamu nchini. Na hii ndiyo sababu pamoja na ongezeko la umaarufu wa filamu za Tanzania katika bara hakuna filamu ya Tanzania (Bongo movies) iliyowahi kushinda tuzo zaidi ya kushuhudia tuzo za kupeana za ZIFF zilizowekwa katika kipengele cha upendeleo ili kutubeba. Filamu zetu zimezidi kuwa maarufu nje ya Tanzania na waigizaji wetu kwa sasa wanazidi kuwa maarufu nje ya Tanzania. Lakini jambo moja ambalo tunaweza kulikabili ni suala la ubora wa kiufundi (huu ni msisitizo ni wangu).

Kwa wale wanaoanza kupoteza matumaini nadhani bado wanapaswa kuwa na imani kwamba kuna matumaini. Jinsi soko la Tanzania linavyokua, naamini kutakuwa na ongezeko la mahitaji ya si hadithi nzuri tu, lakini filamu bora pia, hivyo, hii itaongeza ufanisi katika filamu zetu, na hatimaye kuchochea ushindani katika bara la Afrika.

Kwa sasa tunaweza tu kuota ndoto kuwa siku hiyo yaja.

Alamsiki...

No comments: