Mtendaji Mkuu wa Cosota, Yustus Mkinga, akifafanua jambo mbele ya wadau wa sanaa wakiwemo waigizaji wa filamu hapa nchini, kuhusiana na suala la hakimiliki za wasanii
“NASHUKURU sana kwa makala yako ambayo imenielimisha mambo mengi kuhusu tasnia ya filamu ingawa nina wasiwasi unaposema kuwa Serikali ya Tanzania haielewi ukubwa wa biashara hii, kama haielewi mbona Rais Jakaya Kikwete aliwahi kutamka bungeni kuwa tasnia ya filamu Tanzania inakua na akaahidi kuwasaidia wasanii...?”
Huu ni ujumbe nilioupata kutoka kwa msomaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Jonas Komba, mkazi wa Iringa aliyeonekana kunishangaa nilipoandika kuwa serikali haijui ukubwa wa biashara ya filamu.
Ningependa kumhakikishia msomaji wangu na wengine wenye kujiuliza kama yeye kuwa nilichokiandika ndiyo hali halisi na kimethibitishwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pale alipoongea na viongozi wa mashirikisho ya sanaa walipomtembelea bungeni wakati Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo ilipokuwa ikiwasilisha bajeti yake.
Waziri Mkuu aliwaomba viongozi hao wa mashirikisho kuandaa kongamano la kitaifa na kuwaalika viongozi wa serikali ambapo wataieleza serikali kuhusu umuhimu wa sanaa na jinsi ilivyoisaidia nchi katika miaka hii hamsini ya uhuru, kwa kuwa (Pinda) anaamini kuwa viongozi wa serikali (walio wengi) akiwemo yeye hawajui chochote kinachoendelea kwenye tasnia ya sanaa.
Sina haja ya kuanzisha mjadala mwingine kuhusu kauli ya Waziri Mkuu bali nimetumia kauli yake kumuelewesha msomaji wangu kuwa kile nilichokiandika kina mantiki, hasa pale inapotokea kiongozi wa ngazi ya juu katika serikali yetu anapoamua kusema ukweli wake wa kutojua kinachoendelea kwenye tasnia hii, sasa hapo tunatarajia nini?
Pia kuna msomaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Elias aliyetaka ufafanuzi kuhusu haki nilizosema kuwa watayarishaji wa filamu na wasanii wanaziuza kwa msambazaji, hasa ameguswa na kauli kuwa hakimiliki hudumu kwa maisha yote ya mwenye hakimiliki, na miaka hamsini baada ya kifo chake.
Ieleweke kuwa katika tasnia ya filamu kuna hatua tano katika kukamilisha zao la kazi (filamu) kabla ya kumfikia mlaji. Hatua hizo kwa kitaalam hujulikana kama Development, Pre-production, Production, Post-Production na Distribution.
Pia katika uandaaji wa kazi hizi kuna makundi ya wadau wa aina tofauti: wasanii waigizaji, watunzi wa hadithi, waandishi wa script, waongozaji, watayarishaji wa filamu, wasambazaji na kadhalika. Na baadaye kuna vyombo vya urushaji wa matangazo ya filamu na video kama vile vituo vya televisheni vya ndani na nje ya nchi na kampuni kadhaa za usambazaji kazi kwa njia ya Cable.
Katika kila kundi kati ya haya niliyoyataja kuna aina mbalimbali za haki kulingana na ushiriki wa mtu/ kampuni husika. Kwa mfano wasanii waigizaji hulindwa na sehemu ya hakimiliki inayotajwa kama 'Hakishiriki', na hawa kwa kawaida hulipwa moja kwa moja kutokana na nafasi walizoigiza katika filamu, ambapo wengine hulipwa kwa scenes (matukio) walizocheza kutegemea aina ya mkataba wao na mtayarishaji unasemaje.
Katika kile kinachosemwa kuwa watu wanaibiwa, utaona kuwa wasanii waigizaji hawana cha kuibiwa kwani wanakuwa wameshalipwa na watengenezaji wa filamu. Labda kama malalamiko yao yawe ni kutokana na malipo kiduchu wanayopewa na si vinginevyo.
Upande wa watayarishaji wa filamu ambao ndiyo wana jukumu la kuwalipa waandishi wa script, wasanii waigizaji, waongozaji wa filamu na washiriki wengine katika filamu. Hawa hutegemea kupata fedha zao kutokana na malipo wanayopata kwa wasambazaji. Na hapa ndipo penye ugomvi na kelele za kuibiwa.
Watengezaji wa filamu nchini wamekuwa wanalalamika kila mara kuwa wanaibiwa au kuwekewa masharti magumu na wasambazaji ambayo yanadumaza tasnia ya filamu ikiwemo kuuza haki zao, kama nilivyoainisha katika makala yangu ya wiki iliyopita.
Kwa sasa imekuwa ni jambo la kawaida kusikia kuwa mtayarishaji wa filamu kauza kazi zake kwa msambazaji, jambo linaloshangaza sana hasa kwa nchi kama hii inayoanza kupiga hatua katika tasnia ya filamu. Sababu za kushangaza ni nyingi; ya kwanza kubwa ni kuwa majukumu ya msambazaji yanajulikana wazi kuwa yeye kazi yake inapaswa kuishia kwenye kusambaza kazi husika tu, sasa anaponunua haki zote ndipo inapotia shaka kubwa! Kwa nini anunue haki yako? Na kwa nini umuuzie haki yako?
Ndiyo maana katika makala yangu iliyopita niliishauri serikali kama inataka kufuta umasikini kwa vijana waliojiajiri kupitia sanaa hii kuingilia kati na kutoa elimu kwa wasanii na watayarishaji wa filamu kwa kuwa imeonekana kuwa wengi hawana uelewa wa haki zao, na wenye uelewa huo wanakwazwa na hali iliyopo sokoni kwa kuwa msambazaji ndiye anayelimiliki soko na mwenye kauli ya mwisho katika kazi yoyote ya filamu.
Na kuhusu ufafanuzi alioutaka msomaji wangu kuhusu haki, kitu ambacho nadhani si yeye tu bali kila mdau anapaswa kuzielewa ili kama ataamua kuuza haki zake (ingawa siyo busara) ajue anapoteza nini. Pia hii itaondoa malalamiko ya kuibiwa kazi yanayoendelea kujitokeza.
Pia ieleweke kuwa hata wale ambao kwa sasa wanaojiona ni washindi kwa kuingia mikataba inayowafanya kuuza haki zao kwa msambazaji na kuishia kupewa gari na pesa zinazowasaidia kwa miezi michache, wajue kabisa siku 'wakichuja' na thamani yao kupungua nina imani kabisa wataingia kwenye mkumbo wa kulalamikia haki zao ambazo tayari watakuwa wameshazipoteza.
Kwa kawaida kazi za filamu (kama ilivyo kwenye muziki) zina haki zipatazo kumi ambazo zimetajwa katika kifungu na 9(1) cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya 1999.
Haki hizo ni: (i) Kurudufu kazi, (ii) Kusambaza kazi, (iii) Kukodisha, (iv) Kuonesha hadharani, (v) Kutafsiri, (vi) Kubadili matumizi ya kazi, (vii) Kufanya maonesho ya hadhara, (viii) Kutangaza kazi katika vyombo vya utangazaji, (ix) Kutangaza kwa njia nyingine zozote, na (x) Kuingiza kazi nchini.
Kwa hiyo ukiangalia haki hizo kama zilivyoainishwa utaona wazi kuwa msambazaji kimsingi anahitaji haki mbili tu za mwanzo; yaani kurudufu kazi na kuzisambaza, basi. Kwani hizi haki nyingine zinamruhusu mwenye mali (mtayarishaji) aendelee kufaidi matunda ya kazi yake kwa maisha yake yote na kuwaachia warithi wake miaka hamsini mingine baada ya kifo chake.
Kama inavyoeleweka, Sheria ya Hakimiliki ya nchi yetu inasema wazi kuwa hakimiliki hudumu kwa mwenye haki kwa maisha yake yote na miaka hamsini baada ya kifo chake. Kwa nchi kama Marekani wameongeza hadi miaka sabini. Ndiyo maana utaona kuwa kuna kazi nyingi ambazo zinaendelea kuwa maarufu miaka mingi baada ya wenye kazi kufariki, huku zikiwanufaisha warithi wao.
Sasa inapotokea mtu akaamua kuuza haki zake kwa msambazaji basi ajue kabisa kuwa anauza hata zile haki nane zilizobakia ambazo kimsingi hawezi tena kuzitumia, kwa kuwa tayari atakuwa ameshazipoteza.
Hivi ukiamua kuuza kazi zako kwa maana ya kumuachia haki zote msambazaji, unatarajia kuwaachia nini warithi wako, au unataka kubaki na ile sifa tu ya kuwa uliwahi kuwa na kazi? Lakini, kwa nini uuze haki yako?
Naomba kuwasilisha...
No comments:
Post a Comment