Aug 5, 2011

Kampuni ya Steps yaja na mbinu chafu dhidi ya shirikisho la filamu

Jacob Steven (JB)

 Single Mtambalike (Richie)

Habari za kuaminika kutoka kwenye chanzo kimoja zimeupasha mtandao huu kuwa kampuni ya usambazaji wa filamu nchini ya Steps Entertainment imeanza kuandaa mbinu chafu kwa kuwatumia wasanii nyota ambao wapo chini ya kampuni hiyo.

Habari za kuaminika zinasema kuwa majuzi kampuni hiyo iliwatuma wasanii wawili walio chini ya Bongo Movie Club, Jacob Steven (JB) na Single Mtambalike (Richie) kwenda kuonana na Mtendaji Mkuu wa Baraza la Sanaa la taifa (Basata) ili kuweka mambo sawa.

Habari hizo zinasema kuwa mbinu hizo chafu zimeandaliwa hasa baada ya tukio la Jumatatu wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa linaloandaliwa na Basata, ambapo wasanii wa filamu walio watiifu kwa Shirikisho la Filamu chini ya Simon Mwakifwamba, walianzisha vurugu baada ya kutoridhishwa na muongozaji wa kikao, Katibu Mtendaji wa Basata, Ghonche Materego, kuonekana kuwapendelea wawakilishi wa Steps.

Kwa muda mrefu sasa wasanii wameonekana kuilalamikia kampuni ya Steps kwa kusababisha mgawanyiko mkubwa baina ya wasanii kwa kuwabagua wasio maarufu na kuwakumbatia baadhi ya wasanii maarufu huku wakiwalipa kiasi kikubwa cha pesa, kitendo kinachosababisha soko la filamu kuwa gumu kwa walio wengi.

Baada ya mtafaruku wa Jumatatu, kampuni hiyo pamoja na wasanii wake waliona kuwa njia pekee ya kuwapumbaza wasanii walio wengi ambao wameonekana kuwa watiifu kwa Shirikisho la Filamu na Mwakifwamba, ni kuandaa mpango maalum utakaosimamiwa na JB na Richie, ambao wameshapewa kazi ya kuandaa bajeti kwa ajili ya kazi hiyo.

Mbinu hizo ni pamoja na kuvitembelea vikundi karibu vyote vya maigizo na kueneza sumu mbaya dhidi ya Mwakifwamba ili aonekane hafai, mbinu ya pili ni kuchukua kazi za wasanii wachanga na kuzisambaza kupitia kampuni mojawapo iliyo chini ya Steps Entertainment ili kufuta dhana kuwa Steps inawakumbatia mastaa tu. Steps wana kampuni tatu zikiwemo za Splash na Vision One.

Hii ni hatari sana kwa maendeleo ya tasnia hii, hasa inapoonekana kuwa msambazaji anaamua kutumia kiwango kikubwa cha pesa kuhakikisha anawatia mfukoni watendaji wa taasisi za kiserikali zinazosimamia sanaa na mambo ya hakimiliki ili kujihakikishia biashara yake inanyooka bila kujali kama anawanyonya wanyonge.


No comments: