Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Dk. Emmanuel Nchimbi
ASUBUHI moja naamka na kwenda panapouzwa magazeti ili nipate kujua kinachoendelea hapa nchini na duniani kupitia magazeti, kama kawaida nasoma kwanza vichwa vya habari kwenye magazeti kabla sijajua ninunue gazeti lipi. Mara navutiwa kuangalia picha kadhaa za wasanii wa filamu kwenye ukurasa wa mbele gazeti moja pendwa (la udaku) pamoja na kichwa cha habari: “Hatuibiwi... Haki ya Mungu tunaibiwa”.
Picha zinazopamba ukurasa huu wa mbele wa gazeti hili ni za baadhi ya wasanii wa kundi la Bongo Movie kwa upande mmoja zinazoambatana na neno 'Hatuibiwi', na wale walio watiifu kwa Shirikisho la Filamu Tanzania na maneno 'Haki ya Mungu tunaibiwa', kwa upande mwingine.
Napigwa butwaa kwa sekunde kadhaa nikiukodolea macho ukurasa huu wa mbele wa gazeti hili, huku nikijiuliza faida hasa ya malumbano haya ambayo yamedumu kwa muda mrefu sasa katika tasnia ya filamu. Namfikiria mtu anayedaiwa kuudhamini mgogoro huu, mara naukumbuka ule usemi wa; “vita vya panzi furaha ya kunguru.”
Ingawa wiki iliyopita niliandika makala iliyohusu malumbano haya kwa kuiuliza serikali kulikoni iko kimya katika malumbano haya, lakini sioni kwa nini nisiendeleze mada hii kwa kuwa nahisi mwisho wa malumbano haya unaweza usiwe mwema kwa baadhi ya wadau, hasa kwa kuwa wahusika wameshafikia hatua ya kutishiana maisha.
Kinachonishangaza zaidi ni kwamba katika muda wote tangu kuanza kwa malumbano haya Serikali imeonekana kuwa kimya ingawa waziri mwenye dhamana, Dk. Nchimbi, anajua kila kitu kinachoendelea katika malumbano haya, na sitaki kuamini kuwa ameshindwa kuutatua.
Wiki iliyopita bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, wizara yenye dhamana ya masuala ya sanaa (filamu zikiwemo) ilisomwa huku baadhi ya wabunge wakijaribu kuuelezea mgogoro uliopo katika tasnia ya filamu ya kutaka hatua zichukuliwe, hasa baada ya viongozi wa shirikisho la filamu kwenda Dodoma kukutana na wabunge hao jambo linalotia matumaini.
Lakini kwa upande mwingine hatua ya viongozi wa shirikisho kukaribishwa bungeni imebezwa na baadhi ya wasanii wa kundi la Bongo Movie; nilimsikia mmoja akijisifu kuwa hata kama viongozi wa shirikisho watakwenda kuonana na mkuu wa nchi lakini wao hawababaiki kwani tayari wamekwishaliteka soko, na hata Serikali!
Kwa kauli kama hii ya msanii huyo ambaye namuonea huruma kwa kuwa hana 'future' yoyote na anaponzwa na ulimbukeni, nashindwa kuelewa malumbano haya yameanzishwa kwa faida ya nani? Kwa nini Serikali inapata kigugumizi katika hili au tuamini wanavyosema wenyewe kuwa wameiteka Serikali? Kama serikali haijatekwa, inasubiri nini kuushughulikia mgogoro huu au kwanza inataka machafuko yatokee ndipo iingilie kati?
Ukimya wa Serikali katika mgogoro huu nadhani unatokana na Serikali ya Tanzania kutokuelewa ukubwa wa biashara hii jambo ambalo limekuwa ni tatizo kubwa sana. Laiti wangelijua hili wangejihusisha kwa kiwango kikubwa katika shughuli za aina hii kwani imeonesha kuwa chanzo kikubwa sana cha pato la taifa na nafasi yenye ajira pana kwa vijana na wananchi kwa ujumla.
Kwa kweli malumbano haya hayataisha kama hali hii itaendelea kuachwa kuwa kama ilivyo sasa, ingawa mimi si mtabiri lakini nahisi kabisa kuwa mwisho wa malumbano haya hautakuwa mzuri kwani wasanii walio watiifu kwa shirikisho ambao wengi wao hawana majina makubwa wanaona kuwa kuna wasanii (kambi ya Bongo Movie) ambao wana uhakika wa kuuza kazi zao kwa wasambazaji na pia wana uhakika wa misaada mingi ya kuwaweka katika hali nzuri mbele ya jicho la jamii.
Jambo hili la baadhi ya wasanii kujikuta wanashindwa kusambaza kazi zao, wala kupata mahala pa kuuza kazi zao hata kama zina ubora mzuri kiasi gani, labda pale wanapokubali kuuza kwa pesa 'kiduchu' ambazo hata hivyo hazikidhi hata malipo ya utayarishaji wa kazi, huku wengine kazi zao zikipokelewa bila masharti na wanalipwa pesa nyingi ndicho chanzo cha malumbano haya.
Wasanii hawa wanaolalamika kuibiwa mara nyingi hukutana na masharti ya kulazimishwa kushirikisha wasanii ambao msambazaji anaona kuwa ‘wanauza’, au hata wakati mwingine hulazimishwa kubadili hadithi au kuirefusha ili iweze kutoa namba moja na namba mbili.
Masharti mengine ni kulazimishwa kuingia katika mikataba ambapo filamu nzima (haki ya kumiliki) hununuliwa na msambazaji. Hakimiliki hii humfanya mwenye kuimiliki filamu (msambazaji) kuwa na haki nyingi katika filamu; mfano kurudufu, kusambaza, kutafsiri lugha, kubadili kazi (kwa mafano kutumia kipande katika matangazo), kurusha katika vyombo vya habari, kupeleka nje ya nchi nakala za kazi husika na kadhalika.
Watayarishaji wengi wa filamu hujikuta wakiwa hawana haki yoyote kwenye filamu zao ambazo zimekuwa zikitumika kwa njia tofauti na makubaliano ya usambazaji huku zikioneshwa pia kwenye vituo mbalimbali vya runinga hapa nchini na hata nje ya nchi bila ya wahusika kupata chochote, kwa kuwa tayari wameshalazimishwa kuuza haki zao.
Malumbano ya pande hizi mbili (Bongo Movie VS Shirikisho) yalianza pale shirikisho lilipoanzisha juhudi za makusudi za kuvalia njuga tetesi za kampuni kubwa ya Steps kuamua kuwamaliza wasambazaji wadogo ili ibakie peke yake kwenye soko.
Mbinu za kuwamaliza wasambazaji wengine ni pamoja na kuingia mikataba na wasanii wote maarufu ambao inaaminika 'wanauza' na kuwazuia kufanya kazi na kampuni au watu wengine, kushusha bei ya jumla kutoka shilingi 3000 kwa nakala hadi shilingi 1500 au pengine chini zaidi kwa nakala hivyo kuwazuia wasambazaji wadogo kuweza kufanya kazi.
Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa duniani kote kuna wasambazaji wakubwa (mainstream) na wadogo (indies). Lakini kinachofanyika hapa nchini katika miaka ya karibuni ni msambazaji huyo mkubwa kutumia mbinu hizo na nyingine ambazo zinaidhalilisha hata serikali yetu, jambo ambalo amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani hii imelazimisha kila mtengenezaji kumsujudia yeye ambaye hata hivyo hutoa masharti lukuki, na kudai kuwa hajamlazimisha mtu kuja kwake.
Sitaki kuamini kuwa wasanii hawa waliosainishwa mikataba na msambazaji na wanaouza haki zao hawajui sheria ya Hakimiliki, kuwa hakimiliki hudumu kwa maisha yote ya mwenye hakimiliki, na miaka hamsini baada ya kifo chake. Na kama wanajua, je, wanalipwa kiasi gani kuuza haki zao zenye thamani ya umri huu?
Hivi, msanii anayeingia mikataba ambayo haimruhusu kutengeza filamu nje ya kampuni hiyo ya usambazaji, kwa kupewa malipo ya gari moja kwa kutengeneza filamu zaidi ya mbili na filamu hiyo kuwa mali ya msambazaji, ni kweli anaijua thamani ya kazi yake? Hata kama ni njaa, lakini njaa hii imezidi kipimo!
Mi' nadhani Serikali ingeanzia hapa penye ukosefu wa uelewa wa ukubwa wa biashara hii kwa kutoa elimu kwa wasanii wetu, ukosefu huu wa uelewa unamfanya msanii kukubali malipo duni namna hii na kuona hajaibiwa.
Wasanii wasiendekeze njaa, wachukue muda kwanza kupata elimu kuhusu haki zao ambazo wakizielewa zitawasaidia kuishi vizuri hata pale ambapo umaarufu wao utakuwa umeshuka, au pindi msambazaji wanayejivunia atakapoamua kuwatosa. Wakumbuke kuwa falsafa ya wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia ni “kutokuwa na rafiki wa kudumu bali maslahi ya kudumu”.
Wasifikiri watadumu milele.
No comments:
Post a Comment