May 25, 2011

Bodi ya Filamu: Wasaidieni wasanii

 Joyce Fissoo

Charles Kayoka

 Ukumbi maarufu wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

BODI ya Ukaguzi wa Filamu Tanzania imewataka watalaam wa tasnia hiyo kusaidia wasanii kuhakikisha wanaandaa kazi nzuri zinazokidhi viwango vinavyokubalika Kitaifa na Kimataifa.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es salaam tarehe 18 Mei, mwaka huu na Katibu wa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu Tanzania, Joyce Fissoo alipokutana na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanaosoma Shahada ya Uzamili katika tasnia ya sanaa za Maonesho na Sanaa za Ufundi.

Alisema hivi sasa baadhi ya wasanii wanaharakisha kufanyakazi bila kufanya utafiti wa kutosha kuhusu kazi wanayotarajia kuzalisha, hivyo kutoa filamu zisizo na utafiti wa kina na nyingine kutozingatia maadili.

Fissoo aliongeza kuwa athari zinazojitokeza kutokana na watengenezaji wa filamu kutozingatia sheria ya filamu ni kuongezeka kwa vibanda visivyo rasmi vya kuoneshea filamu zisizozingatia maadili.

Alisema athari nyingine ni wasanii kutonufaika na kazi zao pamoja na kutumia gharama nyingi za utengenezaji, akitolea mfano kwamba kama filamu haikuzingatia maadili hata kama imeshatengenezwa ni lazima irekebishwe hivyo ni wajbu wa mtengenezaji kufuata sheria kabla ya kutengeneza.

Alieleza ili kuhakikisha kuwa tasnia hiyo inapata usimamizi mzuri nchini mwaka 2009, Wizara ya Habari, Vijana, Utamduni na Michezo imeunda bodi katika halmashauri za wilaya zote hapa Tanzania ambazo makatibu wake ni maafisa utamaduni wa maeneo chini ya usimamamizi wa Bodi ya Taifa ya Ukaguzi wa Filamu.

Naye mwalimu kutoka Idara ya Sanaa za Maonesho na Ufundi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Charles Kayoka alisema ni vizuri wasanii wa filamu wakajenga umoja ili waweze kuwa na nguvu kulinda maslahi yao na ya Taifa kwa ujumla.
 

No comments: