May 4, 2011

HAMMIE RAJAB: Gwiji wa filamu na simulizi aliyetabiri kifo chake

 Marehemu Hammie Rajab akitoa maelekezo kwa baadhi ya wasaniii wakati wa utengenezaji wa filamu ya simu ya Kifo mjini Tabora

SAID K. RAJAB
Dar es Salaam

NINA 'projects' nyingi bado sijamaliza... sasa nimeanza kuandika 'script' ya kitabu changu, Ama Zao Ama Zangu. Nataka iwe filamu. Mwenyezi Mungu akiniweka hai, InshaAllah, itakuwa moja ya filamu bomba sana!”

Ni maneno ya mwisho kabisa ambayo Hammie Rajab aliniambia, wakati nilipokwenda kumuona nyumbani kwake, Magomeni Mwembechai, siku tatu kabla hajafariki dunia. Alikuwa amelala kitandani, akiwa na maumivu makali sana ya tumbo.

Pamoja na maumivu aliyokuwa nayo, Hammie Rajab aliweza, walau kuzungumzia kitu tofauti na maumivu yake. Kwa kawaida, binadamu anapokabiliwa na maumivu makali, hicho ndiyo kipimo halisi cha kumfahamu yeye ni mtu wa aina gani na anafikiria nini.

Hammie Rajab aliweza kuzungumzia filamu, akiwa amebakiza siku tatu tu za kuishi hapa duniani, jambo linalothibitisha kwamba sanaa ya filamu ilikuwa ndani ya damu yake. Kwa hiyo, si jambo la kushangaza mzee huyu kuitwa gwiji la filamu na simulizi hapa Tanzania.

"Katika Tanzania hakuna aliye na fani ya juu zaidi ya uongozaji filamu kama Hammie Rajab"
Hayo ni maneno ya Hashim Kambi, msanii maarufu wa filamu hapa nchini, ambaye amefanya kazi nyingi sana na Hammie Rajab. Nilizungumza na Hashim mjini Morogoro, wakati wa mazishi ya mkongwe huyo wa filamu Tanzania:

"Ana kiwango cha juu sana. Anafuata sheria na kanuni za taaluma ya uongozaji wa filamu siyo uzoefu tu", anasema Hashim Kambi:
"Mfano Ndotoni. Mzee Hammie aliitunga na akaandika script yeye mwenyewe, kisha akapewa jukumu la kuiongoza. Lakini walitokea watu wakafanya fitna kwa producer aliyenunua ile script, ili fedha iende kwao".

"Ikafikia mahala yule producer, kwa sababu ya fitna, alikataa kumpa Hammie ile kazi na akaanza kumponda. Lakini baada ya mabishano marefu, hatimaye aliamua kuwaita wote, ili kujua ukweli uko wapi", anafichua Hashim Kambi:

"Mzee Hammie alikuwa rafiki yangu sana..." anasita kidogo kuzungumza, machozi yanamlengalenga, na kuyapangusa:
"Aliniambia, uncle nakutaka uwepo kwenye mkutano, tunakutana makumbusho Dar es salaam. Katika mkutano ule, ndipo Hammie alipoonesha uwezo wake. Alichambua taaluma ya uongozaji filamu katika upeo wa juu, kiasi kwamba hakuna aliyefungua mdomo. Wote walikosa hoja na ile kazi akapewa tena yeye na producer," anasema Hashim Kambi.

Hiyo ilikuwa mwaka 2008, na filamu yenyewe ambayo awali iliitwa Ndotoni, sasa imebadilishwa jina, inaitwa Visa na itatoka hivi karibuni.

Lakini si hivyo tu, Hammie Rajab, kama muongozaji wa filamu mkongwe hapa nchini, alikuwa anajua jinsi ya kumchukulia msanii. Kila wakati anamtia moyo, na hata anapokosea, Hammie hakasiriki na kufoka, kama walivyo waongozaji wengine. Sana sana atamnunulia kinywaji!
Huo ni upande mmoja tu wa Hammie Rajab, kama muongozaji mahiri wa filamu. Lakini ukweli ni kwamba Mzee huyu wa Kimanyema, aliyelowea Morogoro, alijaaliwa vipaji vingi mno.

Alikuwa mtunzi wa hadithi, mwandishi wa script za filamu na makala za televisheni, mtunzi wa riwaya na mashairi, mwandishi wa vitabu vya watoto, na pia alikuwa msimulizi (narrator) mzuri sana kwenye matangazo ya biashara na makala za televisheni, na hata sauti yake pia ilikuwa nzuri na yenye kuvutia.

Mzee Hammie Rajab ameandika vitabu vingi sana vya riwaya na vingine vimetumika mashuleni kwa ajili ya kuwaelimisha wanafunzi wa sekondari na vyuo kama vitabu vya ziada katika somo la fasihi. Ametunga na kuongoza filamu nyingi sana, ambapo nyingine zimetokana na vitabu vyake mwenyewe.

Miongoni mwa vitabu alivyoandika ambavyo bado navikumbuka ni Somo Kaniponza, Gubu la Wifi, Najuta Kuolewa, Sanda ya Jambazi, Ama Zao Ama Zangu, Roho Mkononi, Miujiza ya Mlima Kolelo, Rest in Peace Dear Mother na Ufunguo wa Bandia.

Filamu alizotunga na kuongoza ambazo naweza kuzikumbuka ni Watoto wana Haki, Usawa, Gubu la Wifi, Benki Yako, Miujiza ya Mlima Kolelo, Mama, Kibuyu, Zawadi, Rama, Nawaachieni na Simu ya Kifo.

Hammie Rajab alizaliwa mwaka 1936 mjini Morogoro, akiwa mtoto wa pili katika familia ya marehemu Mzee Rajab Athuman. Jina lake halisi ni Hamisi Rajab Athuman.

Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Msamvu mjini Morogoro, kabla ya kujiunga na Chuo cha Mombasa Institute of Muslim Education (MIOME) nchini Kenya, ambako alisoma kwa miaka mitano na kuhitimu kama fundi makanika kamili.

Baada ya kuhitimu Chuoni, Hammie Rajab alifanyakazi sehemu kadhaa, ikiwemo kampuni ya mafuta (Caltex) mkoani Iringa, Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Kampuni ya Filamu Tanzania (TFC), ambako nako aliacha. Baada ya hapo, akaamua kuingia moja kwa moja katika utunzi wa vitabu vya riwaya:
"Alikuwa na uwezo mkubwa sana na amesoma vitabu vingi mno. Hammie alikuwa anaimudu vyema lugha ya Kiingereza, kwa hiyo haikuwa vigumu kwake kuingia katika ulimwengu wa uandishi vitabu," anasema Kassim Rajab Athuman, maarufu kama Wibbo, ambaye ni mdogo wake Hammie Rajab na rafiki yake mkubwa.

Kutokana na gharama kubwa za uchapaji vitabu, zilizosababishwa na ukosefu wa karatasi na soko lenyewe la vitabu, kwa kuwa Watanzania wengi hawana utamaduni wa kujisomea vitabu; kazi ya uandishi na uchapishaji vitabu haikuwa na manufaa makubwa katika miaka ya themanini.

Waandishi wa vitabu, akiwemo Hammie Rajab walikata tamaa na wengi wao wakageukia shughuli zingine za kuendesha maisha yao. Hammie Rajab aligeukia tena ulimwengu wa filamu, ambao alikuwa na uzoefu wa kutosha tangu enzi za TFC.

Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1985 mpaka 1995, kulikuwa na wimbi kubwa la mageuzi ya vyombo vya habari nchini, ambapo tulishuhudia vyombo vingi binafsi, kama magazeti, radio na televisheni vikianzishwa, jambo ambalo lilikuwa neema kwa watu wenye vipaji kama Hammie Rajab.

Hammie amewafundisha kazi wafanyakazi wengi tu, wa mwanzo kabisa wa televisheni hapa Tanzania, ambao sasa ni watangazaji maarufu wa radio na televisheni. Wengine ni wahariri na watayarishaji wakubwa wa vipindi vya televisheni.

Huyo ndiyo Hammie Rajab! Si rahisi kumueleza katika kurasa chache za gazeti ukammaliza. Katika fani za utangazaji na filamu, itoshe tu kusema kwamba Hammie alikuwa Encyclopedia!
Licha ya kubobea katika tasnia ya filamu na utunzi wa riwaya, Hammie Rajab pia alipata kuwa mwanasoka hodari, aliyewahi kuzichezea klabu mashuhuri za Simba na Yanga katika miaka ya sitini na mwanzoni mwa sabini:

"Hammie alikuwa wa aina yake... hata alipokuwa Msamvu kabla ya kwenda Mombasa, alikuwa mshambuliaji mzuri sana, anayepiga chenga na kuachia mashuti makali," anakumbuka mzee Abdallah Mwinyi Mtama, maarufu kama Kabwela, ambaye alisoma na Hammie Rajab na kucheza naye mpira:

"Nakumbuka katika mechi maalumu ya ufunguzi wa uwanja wa kumbukumbu ya King George wa sita, ambao sasa unaitwa Jamhuri, kulikuwa na mechi kati ya Home Boys na Wanderers"
"Hammie alipiga shuti kali likambabatiza mlinda mlango wa Wanderers, Watt De Souza ambaye alipoteza fahamu na kukimbizwa hospitali. Huyu bwana alikuwa na asili ya Goa, alikuja kuzinduka saa nne usiku hospitali!" anakumbuka Mzee Kabwela.

Kwa mujibu wa Mzee Kabwela, ambaye anamfahamu Hammie Rajab tangu walipokuwa wadogo, anasema alikuwa mchezaji mwenye nidhamu ya hali ya juu na asiyependa ugomvi. Huyo ndiye Hammie Rajab! Kila mtu anamzungumza vizuri, kuanzia ndugu zake, jamaa zake, rafiki zake na hata wasanii wenzake!

Ilikuwa usiku wa April 21, mwaka 2011, katika Hospitali ya Amana jijini Dar es salam, ndipo mkongwe huyu wa tasnia ya filamu hapa nchini, alipoitwa na Mola wake. Mtoto wake mkubwa wa kiume, anayeishi Morogoro, Mshashi Hammie Rajab, ndiye aliyekuwa naye mpaka mauti yalimpofika:

"Mzee hakuhangaika sana, alikuwa na fahamu zake mpaka alipokata roho. Aliniomba nimsomee Aya za Qur'an Tukufu na kumuombea dua. Akanishukuru na kuusia tuishi kwa amani," anasema Mshashi.

Kisha, kwa mujibu wa Mshashi, ndipo Hammie Rajab alipoanza kupata matatizo ya kupumua. Madaktari na wauguzi walijitahidi kuokoa maisha yake kwa kumuwekea mashine ya kusaidia kupumua (respirator) lakini haikufaa kitu. Siku ya Hammie Rajab ilishafika!

Yeye mwenyewe alitabiri kifo chake tangu mchana wa April 21, wakati analazwa pale Amana, hata akaomba aitiwe mtoto wake wa kwanza kutoka Morogoro (Mshashi), ili amuone kwa mara ya mwisho, kwa kuwa asingeweza kufika siku ya pili.

Saa nane na robo usiku, Hammie Rajab alivuta pumzi ndefu ya mwisho, akamgeukia Mshashi kama vile anayetaka kumwambia kitu, akaishia kutabasamu; akashusha pumzi taratibu na kisha akajinyoosha, kama vile aliyetoka usingizini. Baada ya hapo akatulia kabisa! Mwenyezi Mungu alishachukua kiumbe wake! Inna Lillah wa Inna ilayhi Rajuun!

Hammie Rajab ameondoka na bila shaka sote tutamfuata, lakini ametuachia hazina kubwa ya kazi zake za sanaa ambazo daima zitadumu nasi. Mapenzi, huruma, bashasha na ucheshi wake daima vitabaki katika fikra zetu.

Hammie Rajab amezikwa mjini Morogoro katika makaburi ya Kola, April 22 mwaka 2011. Ameacha mjane, watoto na wajukuu. Mbele yako, nyuma yetu baba! Hatutakusahau kamwe! Pumzika kwa amani, Hammie Rajab!

Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kama mwandishi mwandamizi na mhariri wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, anapatikana kwa namba ya simu 0783 650803

No comments: