Oct 1, 2009

Sinema za Kizazi Kipya cha Tanzania

James Gayo, muongozaji filamu wa Tanzania. Hapa anaongoza upigaji picha wa sinema "The Trip", nje kidogo ya mji wa Kampala-Uganda.

Kuanzia miaka ya 1990 hadi sasa nchi yetu imeshuhudia ongezeko kubwa la utengenezaji na utoaji wa sinema (za kizazi kipya) kila kukicha hali ambayo inaambatana na uwepo wa malalamiko mengi kutoka kwa viongozi, wasomi na wadau wa sekta ya filamu kuwa sinema nyingi kati ya hizi zinazotolewa zinakosa ubora na hazikidhi matakwa ya jamii kwa kuwa ni mbovu.


Ingawa kuna ukweli katika hoja hizo, lakini kinachoshangaza ni kwamba wasemaji na wakosoaji hao huishia kulalamika na kukosoa tu kwenye vyombo vya habari kuhusu uduni wa sinema zetu (kuna waziri aliwahi kuziita sinema hizi mchafukoge) lakini hatuzioni jitihada zozote zinazoambatana na utafiti wa kina ambao ungeweza kutoa majibu ya kwa nini kazi hizi ni mbovu.

Wanapaswa kuelekeza njia nzuri ya namna ya kufanya (kutoa mifano hai) ili sinema zetu ziweze kufikia viwango wanavyovikusudia kuliko kulalamika tu kwenye vyombo vya habari kitu ambacho hakiwezi kusaidia.
Nijuavyo, sinema bora hupimwa kwa vigezo kama vitano (bila kujali kama imetengenezwa Hollywood, Bollywood au Maneromango); Mwongozo Mzuri (Good Script), Waigizaji Wazuri (Good Actors/Actresses), Muongozaji Mzuri (Good Director), Wapigapicha Wazuri (Good Cinematographers), na Mhariri Mzuri (Good Editor).

Katika hali hiyo wachambuzi wa masuala ya filamu wanapaswa kuzichambua kazi zetu na kutuelekeza cha kufanya kwa kutumia mambo hayo matano huku wakiambatanisha mifano hai ili tuweze kujua ni wapi panapohitaji nguvu ya ziada. Lakini kusema tu bila kuwekeza nguvu ya ziada katika kutatua tatizo hakusaidii kuikuza sekta hii kwani kila mtu anaweza kusema.

Binafsi bado nina mashaka kuhusu mbinu wanazotumia wakosoaji wa sinema za Kitanzania, na kama kweli kuna tafiti ambazo wamekuwa wakizifanya basi zitakuwa za juujuu tu. Sikuamini siku moja nilipomsikia kiongozi mmoja (alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo wakati huo) akizisifu sana sinema za Kinaijeria huku akitutaka tuige mifano yao kwa ajili ya kuboresha sinema zetu!

Sekta ya filamu ni sekta pana sana na inayojitegemea kwa kila idara, si sawa na soka au sanaa nyingine; kwa mfano kwenye soka unaweza kukuta timu mbovu lakini ikawa na mchezaji mmoja tu mzuri sana (namba 6 au 8) anayehaha uwanja mzima huku akiwapanga wenzake na hatimaye kuipatia timu yao ushindi.

Sekta ya filamu hapa Tanzania imeachwa tu kama mtoto yatima asiye na mlezi na anayejitafutia chakula chake mwenyewe huku akibezwa na wanajamii wanaomzunguka ambao walipaswa kumsaidia. Sisi sote ni mashahidi jinsi kampuni zetu zinavyokimbilia kuwekeza kwenye mashindano ya urembo na kukumbatia tamthilia za nje badala ya kuwekeza katika kuboresha kazi zetu. Inawezekana wanasababu zao za msingi lakini tunadhani hali hii itaisha lini?

Kwa kuzingatia hilo baadhi ya wadau wa sekta hii hapa Bongo wameamua kuanzisha harakati kwa nguvu zote na kuleta umoja kwa wadau ili waweze kuwa na sauti ya pamoja kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea kwenye sekta hii.

Kuanzia sasa tunapaswa tuwe na mjadala mpana kwa wadau wote wa filamu kuhusu masuala muhimu yanayoihusu sekta hii vinginevyo mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi.
Wakati sasa umefika kwa wadau wa filamu kuwekeza nguvu nyingi katika kuhakikisha elimu kwa waandaaji wa filamu za Kitanzania.

Kuna njia tatu za kujifunza: Kusikia, Kuona, na Kusoma. Ni namna gani mtu ataweza kujifunza, hiyo itategemea na nafasi ya mtu ingawa njia ya kusikia haisadii tena kwa kuwa tumeshasikia mengi. Ni wakati sasa kwa wadau na wenye taaluma hii kufanya kwa vitendo katika kuhakikisha sekta hii inakua na si kusubiri vijana wasio na taaluma wala mitaji walioamua kujitoa mhanga wakosee ili tuwe wa kwanza kuwatupia mawe.

Je, ni wangapi walio tayari kujitolea kuwekeza katika kutoa mafunzo na kugharamia warsha kwa watengeneza sinema wa Kitanzania? Hivi mnajua ni waandishi wangapi wa Kitanzania wanaojua namna ya kuandaa mwongozo (Script)? 
Nini kifanyike ili kuwafanya waweze kuandika scripts zinazokubalika? Hilo si suala la watengeneza sinema pekee bali ni jukumu la kila mdau wa sekta ya hii ya sinema hapa nchini.

Uandishi wa script ni taaluma inayojitegemea na inayohitaji ujuzi na elimu ya kutosha, na ingependeza zaidi kama ingeachwa kwa watu maalum (Professionals) waliopata mafunzo.
Kuwa na "Final Cut Pro" au “Adobe Premiere Pro” hakumfanyi mtu kuwa mhariri (Film Editor),
"Adobe Photoshop" haitufanyi tuwe graphic designers, au "Microsoft Word" bado haitoshi kutufanya tujiite Script Writers kama hatukuwezeshwa na kupatiwa mafunzo.

No comments: